Kwanini Ethiopia imetishwa sana na ushirikiano kati ya Misri na Somali?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Ushirikiano wa kijeshi kati ya Somalia na Misri unaongeza hasira zaidi katika upembe tete wa Afrika, na umeibua hasira hususan kwa Ethiopia - na kuna wasiwasi kwamba ghadhabu hiyo inaweza kuwa zaidi ya vita vya maneno.

Mvutano huo uliongezeka wiki hii baada ya kuwasili kwa ndege mbili za kijeshi za Misri aina ya C-130 katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kuashiria mwanzo wa makubaliano yaliyotiwa saini mapema mwezi Agosti wakati wa ziara ya rais wa Somalia mjini Cairo.

Mpango huo unahusu wanajeshi 5,000 wa Misri kujiunga na kikosi kipya cha Umoja wa Afrika mwishoni mwa mwaka huu, huku wengine 5,000 wakiripotiwa kupelekwa katika mpango tofauti.

Ethiopia, ambayo imekuwa mshirika muhimu wa Somalia katika vita vyake dhidi ya wanamgambo wenye mafungamano na al-Qaeda na iko katika mzozo na Misri juu ya bwawa kubwa lililojengwa kwenye Mto Nile, ilisema haiwezi "kusimama tu bila kufanya lolote wakati wahusika wengine wanachukua hatua za kuyumbisha eneo hilo".

Waziri wa ulinzi wa Somalia amejibu kwa kusema Ethiopia inapaswa kuacha "kulia" kwa kuwa kila mtu "atavuna kile alichopanda" - akimaanisha uhusiano wao wa kidiplomasia ambao umekuwa ukizorota kwa miezi kadhaa.

Kwa nini Ethiopia na Somalia ziko katika hali ya uhusiano mbaya?

Somalia haijamleta tu adui yake wa Nile Misri katika mkanganyiko huo, lakini pia ilitangaza kwamba vikosi vya Ethiopia havitakuwa sehemu ya kikosi cha AU kuanzia Januari ijayo.

Hii ni baada ya kuanza kwa operesheni ya tatu ya amani ya Umoja wa Afrika kuanza – ya kwanza wanajeshi walipelekwa huko mwaka 2007 baada ya vikosi vya Ethiopia kuvuka mpaka kusaidia kupambana na wanamgambo wa Kiislamu wa al-Shabab, ambao wakati huo walidhibiti mji mkuu wa Somalia.

Kuna wanajeshi 3,000 wa Ethiopia chini ya ujumbe wa sasa wa Umoja wa Afrika, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

Wiki iliyopita, Waziri mkuu wa Somalia pia alisema Ethiopia italazimika kuondoa wanajeshi wake wengine kati ya 5,000 na 7,000 waliowekwa katika maeneo kadhaa chini ya makubaliano tofauti ya nchi mbili - isipokuwa kama itajiondoa katika mkataba wa bandari na Somaliland.

Ethiopia inaona hili kama kukataliwa, kama waziri wake wa mambo ya nje alivyosema, ikizingatiwa jinsi " ambavyo wanajeshi wa Ethiopia wamejitolea" kwa Somalia.

Kuondolewa kwa wanajeshi pia kutaifanya Ethiopia kuwa katika hatari ya kushambuliwa na wapiganaji wa jihadi, Christopher Hockey, mtafiti mwandamizi katika taasisi ya Royal United Services, aliiambia BBC.

Kupelekwa kwa vikosi vya Misri katika mpaka wake wa mashariki pia kutaifanya Ethiopia kuwa na wasiwasi, aliongeza.

Misri inaliona bwawa la Nile la Ethiopia - magharibi mwa nchi hiyo kama tisho ilionya siku zilizopita kwamba itachukua "hatua" ikiwa usalama wake.

Kwa nini Ethiopia na Somalia ziko katika hali ya uhusiano mbaya?

Yote hayo yanatokana na matarajio ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ambaye anataka nchi yake isiyo na bandari kuwa na bandari.

Ethiopia ilipoteza uwezo wake wa kuifikia bahari wakati Eritrea ilipojitenga mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Siku ya Mwaka Mpya, Bw Abiy alitia saini mkataba wenye utata na Jamhuri ya Somaliland iliyojitangazia uhuru wake kukodi sehemu ya kilomita 20 (maili 12) ya pwani yake kwa miaka 50 ili kuanzisha kambi ya jeshi la majini.

Inaweza pia inadhihirisha Ethiopia kuitambua rasmi Jamhuri iliyojitenga –kitu ambacho Somaliland inakipigania kwa bidii.

Somaliland ilijitenga na Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini Mogadishu inaichukulia kama sehemu ya eneo lake - na kuuelezea mkataba huo kama kitendo cha "ukandamizaji".

Somalia inahofia kuwa hatua kama hiyo huenda ikaweka mfano na kuzihimiza nchi nyingine kutambua uhuru wa Somaliland, mchambuzi wa masuala ya kijiografia Jonathan Fenton-Harvey ameiambia BBC.

Aliongeza kuwa nchi jirani ya Djibouti pia ina wasiwasi kuwa inaweza kuathiri uchumi wake unaotegemea bandari, kwa kuwa Ethiopia imekuwa ikiitegemea Djibouti kwa bidhaa zinazoingizwa nchini humo.

Katika jaribio la kupunguza mvutano huo, waziri wa mambo ya nje wa Djibouti ameiambia BBC kuwa nchi yake iko tayari kuipatia Ethiopia "100%" ya ufikiaji wa moja ya bandari zake.

"Itakuwa katika bandari ya Tadjoura iliyopo kilomita 100 kutoka mpaka wa Ethiopia," Mahmoud Ali Youssouf aliiambia BBC Focus on Africa TV.

Haya kusema kweli ni mabadiliko ya hivi karibuni ya usemi wake kwani mwaka jana, mshauri mwandamizi wa rais alisema Djibouti inasita kutoa ruhusa kwa jirani yake kuifikia nandari yake iliyopo kwenye Bahari ya Shamu.

Majaribio ya kutuliza mvutano baina yake na Uturuki yameshindwa, huku Somalia ikisisitiza kuwa haitasita hadi Ethiopia itakapotambua uhuru wake kuihusu Somaliland.

Kwa nini bwawa la Nile lina utata sana?

Misri inaishutumu Ethiopia kwa kutishia usambazaji wake wa maji kwa ujenzi wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (Gerd).

Ujenzi huu ulianza mwaka 2011 kwenye mto Blue Nile katika nyanda za juu za kaskazini magharibi mwa Ethiopia, ambapo asilimia 85 ya maji ya mto Nile yanatiririkia.

Misri imesema Ethiopia iliendelea kujenga mradi huo kwa "kupuuza" maslahi na haki za nchi za matumizi ya maji na usalama wao wa maji.

Pia ilidai kuwa kupunguzwa kwa asilimia 2 ya maji kutoka mto Nile kunaweza kusababisha kupotea kwa karibu hekari 200,000 (hekta 81,000) za ardhi ya umwagiliaji.

Kwa Ethiopia bwawa hilo linaonekana kama njia ya kuleta mapinduzi nchini kwa kuzalisha umeme kwa asilimia 60 ya watu na kutoa umeme wa mara kwa mara kwa wafanyabiashara.

Juhudi za hivi karibuni za kidiplomasia za kutafuta namna bwawa hilo linavyopaswa kufanya kazi - na kubaini ni kiasi gani cha maji kitatiririka kutoka Sudan na Misri ziligonga mwamba mwezi Disemba mwaka jana.

Tunapaswa kuwa na wasiwasi kiasi gani?

Misri inaona makubaliano yake ya kijeshi na Somalia kama "ya kihistoria" - kwa maneno ya Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi na uwezekano wa kupata suluhisho juu ya bwawa hilo mkubwa.

Kwa kweli mzozo wa Nile unaweza kutokea nchini Somalia, anatahadharisha Dr Hassan Khannenje, mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Mikakati ya pembe ya Afrika.

Unaweza kusababisha "mzozo wa kiwango cha chini wa mataifa" kati ya Ethiopia na Misri ikiwa vikosi vyao vitakutana katika mpaka wa Somalia.

Somaliland pia imeonya kuwa kuanzishwa kwa kambi za kijeshi za Misri ndani ya Somalia kunaweza kuyumbisha eneo hilo.

Ethiopia na Somalia tayari zinakabiliana na mzozo wao wa ndani - Ethiopia ikiwa na uasi wa ngazi ya chini katika mikoa kadhaa huku Somalia, ikiwa ikiwa inatoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 30, na bado ina kabiliana na al-Shabab.

Wataalamu wanasema hakuna anayeweza kumudu vita zaidi - na machafuko zaidi yatasababisha ongezeko la wakimbizi zaidi.

Dkt Khannenje ameiambia BBC kwamba iwapo mzozo utazuka, huenda ukaathiri zaidi jiografia ya Bahari ya Shamu kwa kuwavuta wahusika wengine na kuathiri zaidi biashara ya kimataifa.

Angalau meli 17,000 hupitia mfereji wa Suez kila mwaka, ikimaanisha kuwa kuwa 12% ya biashara ya kila mwaka ya kimataifa hupita kupitia Bahari ya Shamu, yenye thamani ya $ 1tn (£ 842bn) ya bidhaa, kulingana na orodha ya meli ya Lloyd.

Kwa sababu hiyo, nchi kama Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Uturuki zimekuwa na nia ya kuanzisha ushirikiano na mataifa ya Afrika kama Somalia inayopakana na Bahari ya Shamu.

Kwa mujibu wa Bw Harvey, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu zina nafasi nzuri ya kupatanisha na kutafuta eneo la kati.

UAE imewekeza sana katika bandari ya Berbera ya Somaliland na ina ushawishi mkubwa kwa Ethiopia kwa sababu ya uwekezaji wake huko.

Macho yote yatakuwa kwenye shinikizo la kidiplomasia linalofuata na Uturuki, ambayo ina uhusiano na Ethiopia na Somalia. Mazungumzo yanatarajiwa kuanza katikati ya mwezi Septemba.

Ripoti ya ziada ya mwandishi wa BBC Ashley Lime, Waihiga Mwaura, Kalkidan Yibeltal na Juneydi Farah.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah