Wanasayansi wagundua Madini ambayo hayajawahi kuonekana duniani huko Somalia

Jiwe kubwa kutoka angani lililoanguka duniani linamiliki aina mbili za madini ambayo hayajawahi kuonekana katika sayari hii , kwa mujibu wa wanasayansi.

Watafiti wa Canada wanasema kwamba jiwe hilo lilipatikana katika eneo la mashambani la Somalia miaka miwili iliopita, lakini wenyeji wanasema kwamba limekaa eneo hilo kwa muda mrefu zaidi.

 Wanaliita jiwe lililoanguka usiku na wanasema limenakiliwa katika mashairi , nyimbo na densi ambazo zilifanyika zaidi ya vizazi vitano vilivyopita. Siku hizi jiwe hilo hutumika kunoa visu.

Madini hayo yaligunduliwa na wanasayansi katika chou kikuu cha Alberta ambao walichunguza kipande cha gramu 70 kutoka kwa jiwe hilo lenye uzito wa tani kumi na tano , ambalo linadaiwa kuwa la tisa kwa ukubwa kuanguka duniani na lina asilimia 90 ya mdini ya chuma na nickel.

Jina ‘elaliite’ linatokana na kupatikana kwa jiwe hilo katika eneo la El Ali nchini Somali na jina elkinstantonite linatokana na jina la mtaalamu wa Nasa Lindy Elkins -Tanton.

"Lindy amefanya kazi kubwa ya jinsi chembe za sayari zinavyoundwa, jinsi hizi cores za nickel za chuma zinavyoundwa.

Kwa hivyo kulikuwa na haja kutaja madini hayo baada ya jina lake na kutambua mchango wake katika sayansi, " " Alisema Prof Chris Herd ambaye anasimamia mkusanyiko wa mawe hayo ya angani wa Chuo Kikuu cha Alberta.

Kipengele cha tatu, ambacho bado hakijatambuliwa kinachambuliwa na watafiti wa chuo kikuu ambao sasa wanatarajia kupata mawe zaidi - sio tu kuona ni nini kingine wanaweza kugundua, bali pia jinsi yanaweza kutumika duniani.

Je meteorites ni nini?

Meteorites ni miamba ya anga ambayo huanguka Duniani .

Chembe chembe za ukubwa wa vumbi zinazoitwa {Vimondo} hushirikisha asilimia 99 ya takriban tani 50 za uchafu ambao huanguka kwenye uso wa Dunia kila siku.

Baadhi ya miamba hiyo, hata hivyo, ni mikubwa kama mawe.

Kimondo kikubwa zaidi kinachopatikana duniani ni kimondo cha Hoba kilichogunduliwa nchini Namibia mwaka wa 1920.

Kimondo hicho cha Hoba kina uzito wa takribani kilo 54,000 (pauni 119,000).

Miamba ya Hoba ni mikubwa sana, na mizito sana, haijawahi kuhamishwa kutoka mahali ilipopatikana! Vimondo vingi vinafanana sana na miamba inayopatikana Duniani, isipokuwa vimondo huwa na sehemu ya nje yenye giza, iliyoungua.

Sehemu hii ya nje hutokana na msuguano kutoka angahewa inavyoyeyusha miamba wakati inapoanguka kuelekea Dunia.

Utaratibu huu unaojulikana kama uondoaji hewa ya joto, unaweza pia kuvipa vimondo sehemu iliyokauka au laini.

Uondoaji wa joto husababisha maumbile haya tofauti kutokana na kemikali tofauti zilizopo kwenye kimondo.

Miamba ya kwanza iligunduliwa lini?

Mwaka 2005, miamba ya kwanza iliyopatikana kwenye sayari nyingine iligunduliwa na Opportunity, moja ya chombo cha NASA cha Mars rover.

Mwaka 2014, chombo dada cha Opportunity, Curiosity, kiligundua miamba ambayo ilikuwa na upana wa mita 2 (futi 7) na kuifanya kuwa mikubwa zaidi kugunduliwa kwenye Mirihi.

 Zaidi ya vimondo 60,000 vimepatikana duniani. Wanasayansi wamegawanya miamba hii katika sehemu kuu tatu: mawe, chuma, na chuma-mawe.

Kila moja ya aina hizi ina vikundi vidogo vingi.