Mgombea aliyeshindwa mara tano na wanaoshinda kwa mara ya kwanza Kenya

Chanzo cha picha, Reuters
Raila Odinga amepinga matokeo ya uchaguzi wa urais akisema kuwa idadi iliyotangazwa Jumatatu ilikuwa ni "batili na hayana uhalali’’.
Kulingana na matokeo rasmi, Bw Odinga alishindwa kwa kura chache nyuma ya Naibu Rais William Ruto.
Bw Odinga alimshutumu mkuu wa tume ya uchaguzi kwa ‘’kutoheshimu katiba ". "Kwa ujumla bila kuficha tunapinga matokeo ya uchaguzi wa urais ," alisema.
Akizungumza mbele ya wafuasi wake katika mji mkuu Nairobi, Bw Odinga alisema hakuna "mshindi aliyechaguliwa kisheria wala rais mteule".
Odinga mwenye umri wa miaka 77-kiongozi wa muda mrefu wa upinzani alikuwa anawania kiti hicho kwa mara ya tano. Alipinga matokeo katika uchaguzi uliopita ikiwa ni pamoja na wa mwaka 2017.
Mara hii, mwenyekiti tume ya uchaguzi Wafula Chebukati alisema alipata 48.8% ya kura katika uchaguzi wa mwaka huu akilinganishwa na Bw Ruto ambaye alipata 50.5%.
Bw Odinga alimshutumu Bw Chebukati kwa "ukiukaji mkubwa wa sheria" akisema timu yake itachukua mkono wa sheria. Aliliita tangazo lake kama kitendo cha "kurudisha nyuma sana " demokrasia ya Kenya ambacho kinaweza kusababisha mzozo wa kisiasa.
Alisema kwamba Bw Chebukati alikwenda kinyume na sheria kwa kutangaza matokeo bila kuungwa mkono na makamishna wenzake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini mshirika wa Bw Ruto, Musalia Mudavadi, alikiambia kipindi cha redio cha BBC Focus kwamba makamishna wanatakiwa kukusanya matokeo lakini sio kuamua matokeo.
Hili ni suala la kisheria ambalo mwisho wake linaweza kuishia mahakamani.
Dakika kadhaa kabla ya Bw Odinga kuzungumza, makamishna wanne kati ya saba waliokataa kuidhinisha matokeo ya uchaguzi Jumatatu, walifanya mkutano na waandishi wa habari kutoa sababu zao.
Walimshutumu Bw Chebukati kwa kuwatenga na kutangaza matokeo ambayo "kwa mahesabu hayana mantiki ".
Juliana Cherera, Makamu mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, alisema kwamba kama ungejumlisha kura kama zilivyotangazwa na kamishna kwa ujumla utapata 100.01%.
Lakini kitengo cha BBC cha uhakiki wa taarifa - BBC Reality Check kinasema mahesabu hayo ni tatizo la kawaida la uwasilishaji na sio la suala la kutiliwa shaka.
Hatahivyo Bw Odinga aliwapongeza makamishna wanne kwa "ushujaa" wao.
"Wengi wa makamishna (wa tume ya uchaguzi ) – waliokabiliana na vitisho na mwenendo wa kukiuka katiba wa Bw Chebukati, tunawashukuru na tunawaomba wasihofie chochole. Wakenya wako nao ," alisema.
Jumatatu, Bw Ruto alielezea upinzani wa makamshna hao kama "sarakasi za pembeni", lakini alisema kuwa ataheshimu mchakato wa kisheria. Pia alitoa wito wa umoja, akisema kuwa alitaka kuwa rais wa wote, na kwa nchi inayoangazia mbele.
Uchaguzi wa wiki iliyopita ulikuwa wa amani kwa kiasi kikubwa. Tume ya uchaguzi ilipongezwa kwa kiasi kikubwa kwa mchakato wa uwazi kwa kutuma matokeo ya uchaguuzi kutoka kwenye vituo zaidi ya 46,000 vya kupigia kura kwenye wavuti wake na kumhimiza kila mtu kufanya hesabu ya kujumlisha kura mwenyewe.
Hatahivyo, ghasia ziliibuka katika kituo cha kuhesabu kura Jumatatu baada ya wafuasi wa Bw Odinga kuituhumu tume ya uchaguzi kuingilia kura na kujaribu kumzuia Bw Chebukati kutangaza matokeo ya mwisho. Takriban maafisa watatu wa uchauzi walijeruhiwa.
Hali ya utulivu imerejea nchini baada ya mchanganyiko wa sherehe na maandamano kufuatia kutangazwa kwa matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais.
Maelfu ya wafuasi, waliokuwa wamevalia mavazi ya rangi ya manjano, rangi ya chama cha Bw Ruto, walimwagika katika mitaa ya mji wa Eldoret katika Rift Valley.
Kinyume chake katika mji wa kaskazini mwa Kenya wa Kisumu, wafuasi wa Bw Odinga walifunga barabara na kuwasha mioto. Matukio sawa na hayo yalishuhudiwa katika miji kadhaa na katika mji mkuu Nairobi.
Kwa ujumla kulikuwa na hali ya afueni kwamba mchakato wa kuhesabu kura umekwisha kwasababu msimu wa uchaguzi mara kwa mara humaanisha kuwa shughuli nyingi huwa ni kama zimesimamishwa.
Lakini watu watakuwa wakifuatilia kwa karibu mipango ya Bw Odinga ya kuwasilisha kesi katika Mahakama ya juu zaidi.













