Hivi ndivyo waarabu wanavyoliteka soka la dunia

Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

arab

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mmiliki wa Manchester City Sheikh Mansour

Fainali za 22 za kombe la dunia la soka zinatarajiwa kuanza wiki chache zijazo nchini Qatar. Zitachezwa kuanzia Novemba 20 hadi Disemba 18 , zikishirikisha timu 32 zitakazocheza jumla ya mechi 64.

Ingawa katika bara la Asia hizi ni fainali za pili kuchezwa huko baada ya ile ya mwaka 2022 iliyochezwa Japan na Korea Kusini, kwa upande wa nchi za kiarabu hii ni mara ya kwanza kuchezwa kwenye ardhi ya waarabu, tangu kuanzishwa kwake miaka 92 iliyopita.

Wadadisi wa mambo wanakadiria kwamba katika kipindi cha miongo miwili ijayo, soka la uarabuni litakuwa na hadhi inayokaribia na soka la Amerika Kusini na Amerika Kaskazini na yenye hadhi inayokaribia soka la Ulaya.

Kombe la dunia la mwaka huu ni sehemu tu ya jitihada za wazi zinazooonekana, lakini tayari waarabu wameshaanza kufanya uwekezaji mkubwa kwenye ligi karibu zote kubwa duniani katika miongo mwili iliyopita.

Uwekezaji wa 'kibabe' kwenye ligi za Ulaya

arab

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mashabiki wa City wakishangilia ubingwa wa England msimu iliopita

Waarabu kwa sasa wanatajwa kama wawekezaji wakubwa na wasio na mashaka kwenye soka duniani.

Klabu kama Paris Saint-Germain (PSG), iliyokuwa inamilikiwa awali na mbunifu wa mavazi wa Ufaransa, Daniel Hechter, kwa sasa inamilikiwa na Qatar Sports Investments. Hawa ndo wababe wa League 1 na soka la Ufaransa.

Mansour bin Zayed bin Sultan Al Nahyan, anamiliki klabu ya manchester City lakini yuko pia katika ligi ya Australia akimilia Melbourne City FC, kule Marekani anamilikia Newyork City Fc, India anamilikia Mumbai FC na nyingine kadhaa.

Newcastle United inamilikiwa na waarabu wa Saudi Arabia kupitia mfuko wake wa "Public Investment Fund (PIF) waliyoinunua kwa thamani ya £300m mwishoni mwa mwaka jana na kuhitimisha miaka 14 ya umiliki wa Mike Ashley.

Vilabu vingine kama Aston Villa kinamilikiwa na Mwarabu wa Misri Nassef Sawiris, Sheffield United mmiliki wake ni kutoka Saudi Arabia (Abdullah bin Mosaad bin Abdulaziz al-Saud), Farhad Moshiri anaimiliki Everton ya EPL, ana asili ya Irani mwenye uraia wa Uingereza na Sheikh Abdullah bin Nasser bin Abdullah Al Ahmed Al Thani mfanyabiashara wa Qatari anamiliki Malaga ya Hispania.

Hii ni mifano michache ya utawala wa taratibnu unaoletwa na waarabu katika ligi za Ulaya. Kinachowasumbua kuwa wababe leo ni fedha, sasa kumekuwa na vilabu vingi vyenye wamiliki wenye fedha, wengi wao ni waarabu walioamua kununua vilabu na kuvimiliki.

Ushawishi katika ligi za Ulaya

PSG

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vigogo wa PSG wakiongozwa na mmiliki wake Nasser Al-Khelaifi (kushoto)
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Soka ni utaalamu na uzoefu. Ni kujifunza na kutenda. Hakuna namna ya mkarto kufikia mafanikio. Waarabu wameingia kwenye ligi za Ulaya kuwekeza kwa malengo ya kibiashara. mafanikio lakini pia kujifunza.

Kila ligi na kila bara wamewekeza fedha za kutosha na kuongeza ushawishi wao kwenye soka la dunia.

PSG kwa sasa inashika nafasi ya 6 duniani kwa klabu inayoingiza mapato mengi, karibu €556m kwa mwaka kwa mujibu wa Deloitte. Tangu waarabu waichukue imekuwa na nguvu, ushwwishi na mafanikio. Na imekuwa ikisajili wachezaji wenye majina makubwa kama Zlatan Ibrahimović, Neymar, Kylian Mbappé na Lionel Messi na kutwa ataji.

Katika Ligi ya England (EPL), Mansour bin Zayed bin Sultan Al Nahyan, mwarabu wa UAE kupitia City Football Group ameitawala ligi hiyo. Klabu yake ya Manchester City, imekuwa ikifanya vizuri kuliko klabu kama Arsenal ama Nottigham Forest ambazo zilikuwa moto wa kuotea mbali wakati wa utawala wao kwenye soka la England miongo miwili iliyopita.

Leo Newcastle United ya England ni moja ya vilabu vinavyoanza kutishia katika ligi kuu ya EPL.

Watafanikiwa kuliteka soka?

Arab

Chanzo cha picha, Getty Images

'Safari ni hatua' anasema Salim Amin, mchambuzi wa soka, anayeishi Ujerumani.

'Hatua yao ya kwanza ni kusoma wanachokifanya Ulaya, kujifunza na kufanya, uzoefu wanaoupata ni mkubwa na kwa sababu wanapesa, watakuja kuwa tishio sana ndani ya miaka 20 ijayo'.

Kinachosemwa na Amin ni hartua yao ya sasa ya kupata uzoefu wa kuendesha klabu kubwa katika ligi kubwa, uzoefu ambao unaambukizwa kwenye vilabu na ligi za nyumbani kwao.

Kwa mfano Mansour bin Zayed bin Sultan Al Nahyan, anayemiliki klabu ya manchester City, uzoefu wa klabu hii anaupeleka kwenye vilabu vyote vilivyo chini yake. Hivyo nchi yake kuwa mnufaika pia.

Hata wamiliki wa Newcastle United na uzoefu wao utaanza kuambukizwa nchini Saudi Arabia. Mohammed bin Salman, mwenyekiti wa PIF, ambao ni wamiliki wapya wa Newcastle United ni kutoka familia ya kifalme na watawala wa taifa hilo. Wana uswahiba na vilabu vingi vya soka nchini humo.

Juenda isiwe na matokeo ya haraka, lakini kwa matokeo ya muda mfupi, kama wataendelea hivi. Waarabu wanaweza kuwa na dunia yao ya soka muda si mrefu sana.