Maandamano yazuka Israel baada ya Netanyahu kumfuta kazi Waziri wa Ulinzi

fv

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Jon Donnison & George Wright
    • Nafasi, BBC News World
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Maandamano yamezuka nchini Israel baada ya Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu kumfuta kazi Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Yoav Gallant.

Netanyahu amesema "mgogoro wa uaminifu" kati ya viongozi hao wawili ndio uliosababisha kuchukua uamuzi huo, akiongeza kuwa imani yake kwa Gallant "imepungua" katika miezi ya hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Nje, Israel Katz ataingia kuchukua nafasi yake.

Kufuatia habari hizo, Gallant alichapisha taarifa kwenye mitandao ya kijamii akisema "usalama wa taifa la Israel ulikuwa na utabaki daima kuwa ndio misheni ya maisha yangu."

Katika siku za nyuma alisema mpango wa kuwarudisha nyumbani waliotekwa nyara na Hamas, unapaswa kupewa kipaumbele hata kama itamaanisha kuingia makubaliano kuhusu vita vya Gaza.

Netanyahu na Gallant kwa muda mrefu wamekuwa na uhusiano wa kikazi wenye mgawanyiko. Katika kipindi cha mwaka uliopita, kumekuwa na ripoti za kuzozana kati ya watu hao wawili kuhusu mkakati wa vita wa Israel.

Waziri huyo wa zamani wa ulinzi pia hajafurahishwa na mipango ya kuendelea kuwaruhusu raia wa Israel wa madhehebu ya Ultra Orthodox kutojumuishwa katika jeshi la Israel.

Tofauti zao

CX

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Picha ya Oktoba mwaka jana inamuonyesha Netanyahu, kushoto, na Gallant wakati wa mkutano na waandishi wa habari

Miezi kadhaa kabla ya kuanza kwa vita huko Gaza, Netanyahu alimfukuza kazi Gallant kutokana na tofauti za kisiasa, kabla ya kumrejesha kazini kufuatia malalamiko makubwa ya umma.

Lakini siku ya Jumanne Netanyahu alisema: "Katikati ya vita, kuliko hata hapo awali, uaminifu kamili unahitajika kati ya waziri mkuu na waziri wa ulinzi."

Alisema ingawa kumekuwa na uaminifu na "kazi yenye matunda" katika miezi ya kwanza ya vita, lakini "katika miezi iliyopita uaminifu huo umepungua."

Netanyahu aliongeza "tofauti kubwa ilikuwepo kati yangu na Gallant katika uendeshaji wa vita."

Haya "yaliambatana na kauli na vitendo vinavyokinzana na maamuzi ya serikali," aliongeza.

Gallant baadaye alitoa taarifa kamili siku ya Jumanne usiku akisema kuondolewa kwake afisini kumetokana na "kutokubaliana katika masuala matatu."

Anaamini hakupaswi kuwepo kwa ubaguzi kujiunga na jeshi, uchunguzi wa kitaifa unahitajika ili kujifunza, na mateka wanapaswa kurudishwa haraka iwezekanavyo.

Akizungumzia mateka, anasema: "Naamini inawezekana kufikia lengo hili. Yanahitajika makubaliano yenye uchungu, ambayo taifa la Israel linaweza kuyabeba na IDF inaweza kuvumilia."

Maandamano yazuka

EDCX

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mara tu baada ya tangazo la Netanyahu, waandamanaji walimiminika mitaani huku wengi wakimtaka Waziri Mkuu ajiuzulu, na kumtaka Waziri mpya wa ulinzi kutoa kipau mbele kwa mpango wa kuwarudisha mateka waliosalia huko Gaza.

Muandamanaji mmoja, Yair Amit, anasema, Netanyahu anaitia hatarini nchi nzima na kumtaka Waziri Mkuu "kujiuzulu kutoka ofisi yake na kuwaacha watu makini kuiongoza Israel."

Baadhi ya waandamanaji waliwasha moto kwenye barabara kuu ya Ayalon na kuzuia magari kuelekea pande zote mbili, kulingana na vyombo vya habari vya Israel.

Kundi linalowakilisha familia za watu waliochukuliwa mateka na Hamas katika shambulio la Oktoba 7 pia limelaani kitendo cha Netanyahu kumfukuza Gallant, na kusema ni mwendelezo wa juhudi za kuharibu makubaliano ya kuachiliwa huru mateka.

Kundi hilo lilitoa wito kwa waziri wa ulinzi anayekuja "kueleza dhamira ya wazi ya kumaliza vita na kutekeleza mpango wa kurejeshwa mara moja kwa wale waliotekwa nyara."

Takribani mateka 100 kati ya 251 waliochukuliwa na Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 hawajulikani walipo kwa zaidi ya mwaka mmoja wa vita hivyo.

Hata hivyo Waziri mpya wa Ulinzi anaonekana kuunga mkono vita zaidi katika suala la mkakati wa kijeshi.

Mshirika mwingine wa Netanyahu, Gideon Sa'ar - ambaye hapo awali hakuwa na wizara maalumu - atakuwa waziri mpya wa mambo ya nje.

Kufutwa kazi kwa Gallant kutaanza baada ya saa 48. Uteuzi wa mawaziri wapya unahitaji idhini ya serikali na kisha Knesset.

Netanyahu alimfukuza Gallant mara ya kwanza Machi 2023 kufuatia kutokubaliana kwao juu ya mipango yenye utata ya kurekebisha mfumo wa mahakama.

Lakini alilazimika kughairi kumfukuza kazi kufuatia maandamano makubwa ya umma katika miji kadhaa nchini Israel - tukio ambalo lilijulikana kama "Usiku wa Gallant."

Mwezi Mei mwaka huu, Gallant alionyesha kuudhika kuliko wazi kwa serikali kushindwa kueleza suala la mpango wa baada ya vita kuhusu Gaza. Gallant alimtaka Netanyahu atangaze hadharani kwamba Israel haina mpango wa kuitawala kiraia na kijeshi Gaza.

Ilikuwa ni ishara adimu mbele ya umma juu ya mgawanyiko ndani ya baraza la mawaziri la vita la Israeli kuhusu mwelekeo wa vita.

"Tangu Oktoba, nimekuwa nikizungumzia suala hili mara kwa mara kwenye baraza la mawaziri," Gallant alisema, "na sijapata jibu.”

Netanyahu alijibu kwa kusema "hayuko tayari kuibadilisha Hamastan kwa Fatahstan," akimaanisha vikundi hasimu vya Palestina Hamas na Fatah.

Kujibu kuondolewa kwa Gallant, wanachama wa vyama vya upinzani vya kisiasa vya Israel waliitisha maandamano ya umma.

Kufutwa kwa Gallant pia kumetokea siku ya uchaguzi wa rais huko Marekani - mfadhili mkuu wa Israel katika vita vyake huko Gaza.

Gallant alionekana kuwa na uhusiano mzuri zaidi na Ikulu ya White House kuliko Netanyahu.

Mwakilishi wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Ikulu ya White House alisema siku ya Jumanne: "Waziri Gallant amekuwa mshirika muhimu katika masuala yote yanayohusiana na ulinzi wa Israel. Kama washirika wa karibu, tutaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na waziri ajaye wa ulinzi wa Israel."

Kuondolewa kwa Gallant pia kunakuja wakati ambapo Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia kupitisha mswada ambao utaendelea kuruhusu raia wa Israel wa Ultra Othrodox kutotumikia jeshi.

Gallant amekuwa mpinzani wa mswada huo.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah