'Inatisha - lakini hata kujifungua ni hivyo tu': Kikosi cha wanawake kinachozisaka ndege zisizo na rubani za Urusi

Chanzo cha picha, BC/James Cheyne
Ni wakati giza linapoingia mjini Bucha ambapo wachawi hutoka, kwa sababu wakati huo ndege zisizo na rubani za Urusi huanza kuvuma.
Wachawi wa Bucha, kama wanavyojiita, ni kitengo cha kujitolea cha ulinzi wa anga kinachoshirikisha wanawake, ambao sasa wanasaidia kulinda anga ya Ukraine huku wanaume wengi zaidi wakipelekwa mstari wa mbele.
Kuna ndege nyingi zisizo na rubani zinazorushwa kutoka Urusi kwa mpigo ili kuuzidi nguvu ulinzi kabla ya shambulio la kombora.
Zamu za usiku huruhusu wanawake kuchanganya kazi zao za kutetea nchi yao na kazi za mchana kama walimu, madaktari - kuna hata mtaalamu wa ujanja.
Wengi wanasema ni njia ya kushinda kutokuwa na uwezo wakati vikosi vya Urusi vilipochukua eneo la Bucha mwanzoni mwa uvamizi.
Hadithi za kutisha za wiki hizo - ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso na utekaji nyara - zilianza kuibuka baada ya vikosi vya Ukraine kukomboa eneo hilo mwishoni mwa Machi 2022.
Mashambulizi ya anga na silaha za zamani
"Nina umri wa miaka 51, nina uzito wa kilo 100, siwezi kukimbia. Nilidhani wangenifukuza, lakini walinichukua!” Valentyna anakumbuka, daktari wa mifugo ambaye alijiandikisha na waendeshaji wa ndege zisizo na rubani msimu huu wa joto na sasa anaitwa Valkyrie.
Anazungumza juu ya marafiki waliopelekwa mstari wa mbele, na wengine ambao wamekufa kwenye mapigano, kama sehemu ya kile kilichomleta katika kazi hii.

Chanzo cha picha, BBC/James Cheyne
“Naweza kufanya kazi hii. Mzigo ni mzito, lakini sisi wanawake tunaweza kuifanya."
Valentyna anatuonyesha na saa chache baadaye tahadhari ya angani inawashwa katika eneo lote.
Kikosi chake kinakimbia kutoka kwenye kituo chao msituni, na tunalifuata lori lao gizani linapoelekea katikati ya uwanja.
Timu ya watu wanne inaruka nje ili kuanza kuweka silaha zao.
Bunduki zao ni za zamani: Maxims mbili zilizotengenezwa mwaka 1939, masanduku ya risasi yaliyowekwa alama na nyota nyekundu kutoka siku za Soviet.
Serhiy, mwanamume pekee kwenye kundi hilo, analazimika kumwaga maji ya chupa kwa mkono ili kupoza joto kali.
.Haya ndiyo yanayopatikana: sare bora ya Ukraine iko mstari wa mbele, na imekuwa ikiwataka washirika wake kuwaongezea.
Lakini silaha za zamani zimetunzwa vizuri na Wachawi wanasema wameangusha drones tatu .

Chanzo cha picha, BBC/James Cheyne
"Jukumu langu ni kuwasikiliza," Valentyna anaeleza. "Ni kazi ngumu. Lakini tunapaswa kukaa makini, [kusikiliza] kwa sauti ya chini.”
Rafiki yake Inna pia yuko katika miaka yake ya mapema ya 50 na yuko kwenye moja ya mazoezi yake ya kwanza.
"Inatisha, ndio. Lakini ndivyo ninavyojifungua, na bado nilifanya hivyo mara tatu, "anacheka, akiniambia ishara yake ya simu ni Cherry:
"Kwa sababu ya gari langu, si nyanya."
Mwalimu huyo wa hisabati, mara kwa mara inambidi kuharakisha kurudi kutoka msituni kufunza darasani.
“Ninaweka nguo zangu kwenye gari. Viatu vyangu. Ninajipaka rangi ya mdomo na kufunza somo hilo na baadaye mimi hurudi katika gari, nabadilisha nguo kwa haraka na naondoka.
"Watu wameondoka, lakini tuko hapa. Wanawake wa Ukraine hawawezi kufanya nini? Tunaweza kufanya kila kitu.”

Chanzo cha picha, BBC/James Cheyne
Mahali fulani kwenye upeo wa macho kuna mwangaza kutoka kwa kikundi kingine, unaozunguka anga kwa hatari juu ya eneo lao la doria.
Hakuna data ya umma juu ya jumla ya idadi ya vitengo vya kujitolea - au ni wanawake wangapi wanaohusika.
Lakini Urusi inapotuma ndege zisizo na rubani zilizojaa vilipuzi karibu kila usiku, husaidia kuunda ngao ya ziada kuzunguka miji mikubwa na miji.
Kutoka kwa kundi la Wachawi waliopo katika uwanja wa vita, Yulia anafuatilia ndege mbili zisizo na rubani kwenye kompyuta yake. Ziko katika eneo jirani, kwa hivyo hakuna hatari yoyote kwa Bucha, lakini bunduki zitaendelea kuwepo hadi tahadhari itakapokamilika.
Hakuna wanaume waliobaki
Kamanda wa wanawake hao waliojitolea ni jitu la miraba mingi, akiwa ametoka eneo la Pokrovsk mashariki mwa Donbas ambako mapigano ni makali zaidi.
"Kuna milipuko, kila mahalai," ndivyo Andriy Verlaty anavyolielezea eneo hilo, kwa tabasamu.
Alikuwa na takriban wanajeshi 200 wanaoendesha vitengo vya ulinzi wa anga katika eneo la Bucha na washika doria wakati wa amri ya kutotoka nje usiku, wengi wao wakiwa hawafai huduma katika kijeshi.
Kisha Ukraine ikabadilisha sheria yake ya kujiunga na jeshi , ikihitaji wanajeshi zaidi wa haraka, na wafanyakazi wengi wa kanali huyo ghafla wakajikuta wakistahiki kuwa mstari wa mbele.

Chanzo cha picha, BBC/James Cheyne
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
" 90% ya watu wangu waliishia jeshini na wengine 10% walijificha, wakitawanyika kama panya. Hatukuwa na mtu yeyote,” Col Verlaty anasema kwa ukali.
"Tulisalia na Wanaume wasio na miguu, au nusu ya fuvu lao la kichwa likiwa halipo."
Alikuwa na chaguo: Kusajili wanaume walio chini ya umri, au kuajiri wanawake.
“Mwanzoni ilikuwa kama mzaha: ‘Tuwachukue wanawake!’ Hakukuwa na imani kubwa kwao, katika vikosi vya kijeshi. Lakini hilo limebadilika kweli,” anasema.
Kurudisha udhibiti
Wachawi hutumia wikendi zao kupitia mafunzo mapana ya kijeshi. Siku tunapotembelea, ni somo lao la kwanza la kuvamia jengo. Wanafanya mazoezi katika magofu ya nyumba ya shamba, wakielekeza bunduki kwenye milango isiyo na kitu kabla ya kupita kwa tahadhari.
Wengine wanaweza kuonekana kuwa na ushawishi zaidi kuliko wengine, lakini kujitolea na kuzingatia kwa wanawake ni wazi - kwa kuwa sababu zao za kufanya hivyo ni za kina na za kibinafsi.
"Nakumbuka hofu. Nakumbuka mayowe ya mtoto wangu mwenyewe,” Valentyna ananiambia, huku akihema kidogo. "Nakumbuka maiti, tulipokuwa tunakimbia."
Familia yake ilitoroka Bucha na kupita vifaru vilivyochomwa, wanajeshi waliokufa na raia.
Katika kituo kimoja cha ukaguzi cha Urusi anasema mwanajeshi mmoja aliwalazimisha kushusha kioo cha dirisha la gari yao kisha wakamuwekea bunduki kichwani mwanawe.
Amejawa na hasira.
Ndiyo maana pia Valentyna anakataa kuacha kuamini ushindi wa Ukraine, licha ya giza ambalo limetanda sehemu kubwa ya nchi yake baada ya karibu siku 1,000 za vita vikubwa.
“Maisha yamebadilika, mipango yetu yote imesambaratika. Lakini niko hapa kusaidia kuharakisha mwisho wa vita hivi. Kama wasichana wetu wanavyosema hapa, haitaisha bila sisi."

Chanzo cha picha, BBC/James Cheyne
Akikanyaga glasi iliyovunjika kwa buti za jeshi, akiwa na bunduki mkononi, meneja wa ofisi Anya ni Mchawi mwingine wa kujitolea.
Sasa ana umri wa miaka 52, anapata mafunzo ya kijeshi kama yanayomwezesha.
"Mwanzo, nilihisi kutokuwa na maana kabisa kwa uwepo wangu. Sikuweza kusaidia mtu mwingine yeyote, wala kujitetea. Nilitaka kujifunza jinsi ya kutumia silaha, ili niweze kutumika”
Kuna mazungumzo mengi na wakufunzi: wanawake wanafurahiya . Lakini baadaye usiku huo, wakiwa msituni, mmoja wao anafunguka zaidi na kutoa hadithi ya kusisimua.
Bucha ilipochukuliwa, majeshi ya Urusi yalianza kwenda nyumba hadi nyumba. Walibaka na kuua. Kisha siku moja, uvumi ukaenea kwamba wavamizi walikuwa wanakuja kuwaua watoto.
“Kwa uamuzi niliochukua siku hiyo, sitawasamehe Warusi kamwe,” mwanamke huyo aeleza.
Sitasema kuhusu maelezo ya kile alichoniambia - uamuzi wa hali ya juu aliochukua – ila wanajeshi wa Urusi hawakuja na hakulazimika kuufanyia kazi. Lakini mwanamke huyu amekuwa akiandamwa na wakati huo tangu wakati huo, na kwa hatia.
Mara ya kwanza alihisi ahueni ni pale alipoanza kujifunza kujilinda yeye mwenyewe, familia yake na nchi yake.
“Kuja hapa kulisaidia sana,” ananiambia kimya kimya. "Kwa sababu sitawahi kukaa kama mwathirika tena na kuogopa."
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












