Simulizi ya jasusi wa Marekani ambaye ndege yake ilidunguliwa juu ya anga ya Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Tarehe 19 Agosti 1960, miaka 65 iliyopita wiki hii, mahakama moja mjini Moscow ilimkabidhi rubani wa Marekani, Francis Gary Powers, kifungo cha miaka 10 baada ya kukamatwa na vikosi vya usalama vya Soviet. BBC iliripoti juu ya kile kilichokuwa janga la kidiplomasia la Vita Baridi.
Francis Gary Powers alikuwa kwenye ujumbe wa CIA wa ujasusi juu ya anga ya Urusi ya Soviet wakati ndege yake ya U-2 ilipopigwa na kombora la kutoka ardhini hadi angani.
"Nilitazama juu, nikatazama nje, na kila kitu kilikuwa rangi ya machungwa, kila mahali," Powers alikumbuka. "Sijui kama ilikuwa ni rangi ya mawingu au anga nzima . Na ninaweza kukumbuka kujiambia, 'Wallahi, nimekipata.'
Kwa kweli, Powers aliweza kuruka kwa parachuti hadi eneo salama, lakini shida zake hazikuishia hapo. Baada ya kukamatwa na kuhojiwa na KGB, alishtakiwa huko Moscow, ambapo familia yake ingeweza kutazama bila msaada. "Alisema alijua kuwa tulikuwepo kwenye kesi yake," mkewe Barbara Powers aliambia BBC. "Hakujua hapo awali. Lakini aliniona nikipungia mkono.
Na alisema hakuweza kustahimili kutazama upande wa sanduku ambalo tulikuwa tumeketi sote, kwa sababu lilimkasirisha sana, na alijua kwamba litatufadhaisha." Mnamo tarehe 19 Agosti 1960, miaka 65 iliyopita wiki hii, Powers alihukumiwa miaka 10 - mitatu katika gereza la Urusi na saba katika kambi ya kazi ngumu.
Kukamatwa kwake na kesi kungekuwa na athari mbaya kwa uhusiano wa Mashariki na Magharibi katika kilele cha Vita Baridi.
Wakati huo Powers alikuwa na umri wa miaka 30. Akiwa mtoto wa mchimbaji wa makaa ya mawe kutoka Kentucky, Marekani, alisomea kemia na biolojia kabla ya kujiunga na Jeshi la Wanahewa la Marekani mwaka 1950.
Mnamo mwaka wa 1956, aliajiriwa na shirika la kijasusi la Marekani CIA kuendesha ndege za U-2 za kijasusi katika maeneo ya adui.
Ndege za kivita za U-2s ziliweza kuruka futi 70,000 (21.3km), mbali na anga ya ulinzi wa Soviet, na bado kamera ya kisasa kwenye ubao iliweza kuchukua picha za kina za silaha za kijeshi chini humo .
Mnamo tarehe 1 Mei 1960, Powers alipaa kutoka Peshawar, Pakistan, akapitia anga ya USSR na kutua Norway.
"Njia iliyopangwa ingetupeleka ndani zaidi ya Urusi kuliko vile tulivyowahi kwenda, huku tukipitia shabaha muhimu ambazo hazijawahi kupigwa picha," aliandika katika kumbukumbu yake, Operesheni Overflight.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini viongozi wa Soviet walikuwa wamegundua ndege za awali za U-2, na walikuwa wamedhamiria kuzizuia kwa gharama yoyote.
Ndege za kivita za MiG-19 zilishambuliwa na makombora ya S-75 Dvina . Saa nne ndani ya misheni hiyo, ndege ya Powers ilipigwa na mojawapo ya makombora hayo karibu na jiji la Urusi la Sverdlovsk (sasa Yekaterinburg).
Moja ya mbawa zake iling'olewa, na ndege ikazunguka na kuangukia mkia wake . Mwana wa Powers, Gary Powers Jr, alisimulia hadithi kwenye podcast ya Historia ya Mashahidi ya BBC.
"Alifikiri juu ya kujitoa kwenye ndege - hilo ndilo jambo la kwanza ambalo marubani wanafunzwa kufanya, - kutoka katika ndege ilioharibiwa. Lakini anatambua kwamba ikiwa atatoka nje, atakata miguu yake wakati wa kutoka.
Chumba cha marubani cha U-2 ni kidogo sana, kimefungwa. Ili kutaka kutoka ni sharti uwe katika hali nzuri ili usipoteze kiungo chako kimoja.
Suluhisho la Powers halikuwa kutumia kiti cha ejector cha ndege: alifungua tu mwavuli na kutoka nje. Lakini mara tu mwavuli ulipofunguliwa, "Mwili wake nusu ulikuwa umejitokeza huku upande mwengine ukisalia katika ndege na ", alisema Gary Jr. Na hakuweza kufikia kitufe cha kujiribu kujitoa ndani ya ndege hiyo ya U-2.
"Bado ameunganishwa na bomba lake la hewa, kwa hivyo yuko hapa, nusu ndani ya ndege, nusu nje ya ndege, akipoteza fahamu wakati ndege ilipokuwa ikianguka "
Kwa namna fulani, Powers alifanikiwa kutoka katika ndege hiyo, na akaruka kwa parachuti kwenye shamba la pamoja nje kidogo ya Sverdlovsk.
Lakini tayari alikuwa ameona gari jeusi likimfuatilia kwenye barabara ya chini alipokuwa akishuka.
Maafisa wa usalama wa serikali walimtia mbaroni. Pia walikuwa na mabaki ya U-2, pamoja na kamera yake.
Tatizo kwa serikali ya Marekani ni kwamba hawakuwa na njia ya kujua kwamba Powers alikuwa hai, na vilevile haikujua iwapo ndege ya U-2 ilikuwa imeangamizwa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa habari iliyodai kuwa Powers alikuwa akiruka juu ya anga ya Uturuki, akisoma mwelekeo wa hali ya hewa wa Nasa, wakati alipopotea kwa bahati mbaya katika anga ya Usovieti.
Simulizi hiyo hiyo ilijumuisha picha za U-2 zilizo na nembo ya Nasa iliyoongezwa kwa haraka.
Lakini badala ya kuweka misheni kuwa siri, jaribio hili la haraka la hila lingeisaidia kuwa aibu kubwa ya umma.
Waziri Mkuu wa USSR, Nikita Khrushchev, aliutangazia ulimwengu kwamba Powers yuko hai na yuko mzima - na kwamba kamera na picha zake zilipatikana zikiwa shwari, ikithibitisha kwamba alikuwa jasusi.
Alilazimika kukiri kwamba alikuwa amesema uwongo, Rais wa Marekani Dwight D Eisenhower alisema kwamba Marekani ilikuwa ndani ya haki yake ya kuendelea kumfuatilia adui yake.
Muda huo ulikuwa mbaya, kwani viongozi wa mataifa hayo mawili walipaswa kuhudhuria mkutano huko Paris pamoja na wakuu wa serikali za Ufaransa na Uingereza.
Huu ulikuwa ni mkutano wa kwanza wa kilele katika kipindi cha miaka mitano kuhudhuriwa na viongozi wa Usovieti na Marekani, na ilitarajiwa kwamba unaweza kuimarisha urafiki katika eneo la Iron Curtain. lakini makabiliano kati ya mataifa hayo yalifanya hilo lisiwezekane.
"Bw Krushchov alitaka Marekani kuomba msamaha kabla ya majadiliano kuanza," iliripoti BBC mnamo Mei 17.
"Pia alisema Marekani inapaswa kuahidi kutokiuka tena anga ya Usovieti na inapaswa kuwaadhibu wote waliohusika na tukio hilo.
Rais Eisenhower alikataa madai hayo, na kuuacha mkutano wa kilele wa amani katika hali ya switofahamu... Pande zote mbili sasa zinalaumiana kwa kushindwa kwa mkutano huo." Power, pia, ilibidi kubeba baadhi ya lawama kwa janga hili la kidiplomasia.
Imetfasiriwa na Seif Abdalla












