Maandamano Tanzania: Marekani kutathmini upya uhusiano wake na taifa hilo

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Marekani imesema kuwa inatathimini upya uhusiano wake na Tanzania kufuatia mauaji ya raia wengi wakati wa uchaguzi mkuu wa hivi karibuni.
Taarifa iliotolewa na ubalozi wa Marekani, imesema kuwa licha ya uhusiano wake wa muda mrefu uliostawi kati yake na taifa hilo, hatua ya hivi karibuni ya taifa hilo imezua wasiwasi mkubwa kuhusu mwelekeo wa uhusiano huo.
Imesema kwamba matukio yanayoendelea kufanywa na serikali ya Tanzania ya kukandamiza uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza , kuwepo kwa vikwazo vya mara kwa mara dhidi ya uwekezaji wa Marekani na ukatili dhidi ya raia kabla na baada ya uchaguzi ni mambo inalolifanya taifa hilo kutathmini upya uhusiano huo.
Taarifa hiyo imesema kwamba vitendo hivyo vinawaweka raia wa Marekani , watalii na maslahi ya Marekani nchini tanzania hatarini na kutishia kudhoofisha ustawi na usalama wa pamoja ambao umekuwa alama ya ushirikiano wetu kwa miongo kadhaa.
Imeongezea kwamba Marekani haiwezi kufumbia macho vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia wetu, au usalama na utulivu wa kanda'
Imehitimisha kwamba mustakbali wa uhusiano wa rasmi wa kibalozi kati ya Marekani na Tanzania utategemea matendo ya taifa hilo.
Taarifa hiyo inajiri siku chache tu baadaya rais Samia kutoa hotuba kali iliyolenga jamii ya kimataifa .
Moja ya sehemu kali zaidi za hotuba hiyo ni pale Rais alipodai mataifa hayo yamekuwa yakitoa maagizo kuhusu jinsi Tanzania inavyopaswa kuendesha mambo yake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alisema Tanzania haiwezi kukubali kudhibitiwa au kuwekewa masharti kwa kisingizio cha misaada au ushirikiano.
Alisisitiza kuwa baadhi ya mashinikizo ya kimataifa yanatokana na tamaa ya kutaka kufaidika na rasilimali za Tanzania, hususan madini adimu ambayo nchi inamiliki.
Kwa mujibu wake, Tanzania imekuwa ikilengwa kwa sababu ya utajiri wake wa kiasili, na iwapo wazawa hawatakuwa waangalifu, rasilimali hizo zinaweza kuwa chanzo cha migogoro ya kisiasa.
"Maumbile yetu na utajiri wetu isiwe laana tukauana sisi kwa sisi kwa kushawishiwa na wanaotolea macho nchi yetu," alisema.
Kwa msisitizo mkali, Rais aliwataka Watanzania kushikamana na kutoacha tofauti za kisiasa au ushawishi kutoka nje kuigawa nchi.
Alisisitiza kuwa hakuna taifa linaloweza kujiendesha kwa amani kama raia wake wanatoa mwanya kwa nguvu za nje kuingilia mambo yao ya ndani.
Baada ya intaneti kuzimwa kwa takriban wiki moja, kufuatia uchaguzi uliokumbwa na ghasia wa Oktoba 29 makumi ya video na picha zilianza kuibuka mtandaoni zikionyesha athari ya matukio ya vurugu.
Maafisa waliovalia sare walionekana kufyatulia risasi umati wa watu, miili ikiwa imetapakaa mitaani, huku mingine ikiwa imerundikana nje ya hospitali.
Ili kubaini ni nini hasa kilichotokea, BBC Verify ilithibitisha baadhi ya video hizo kwa kutumia picha za setalaiti na kulinganisha maeneo.
Kulingana na video hizo waandamanaji walikabiliwa vikali na maafisa wa polisi waliokuwa na silaha ambao walikuwa tayari kukomesha vurugu hizo kwa njia zote, huku wakifyatua mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji.
Katika video nyingi, milio ya risasi iliweza kusikika wakati watu wakitawanyika katika maandamano.















