Je, kuna la kushangilia baada ya mazungumzo ya Trump na Putin?

dx

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Sarah Rainsford
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Baada ya mazungumzo ya simu ya jana kati ya rais Donald Trump wa Marekani na na mwenzake Vladimir Putin wa Urusi, ni wazi kuwa Trump aliyafanya mazungumzo hayo kuwa ni suala kubwa.

Lakini matokeo ya mazungumzo yenyewe yanaonekana kana kwamba kuna machache sana ya kushangilia.

Rais wa Urusi amempa kiongozi huyo wa Marekani sababu ya kudai kwamba kuna maendeleo kuelekea amani nchini Ukraine, bila ya kumfanya ajione amechezewa na Kremlin.

Trump anaweza kuitaja ahadi ya Putin ya kusitisha mashambulizi kwenye miundombinu ya nishati ya Ukraine kwa siku 30 kuwa ni mafanikio. Hilo likitokea, litaleta ahueni kwa raia.

Putin anaamini usitishaji mapigano wa siku 30 utaiondolea Urusi nguvu zake na kuiwezesha Ukraine kujipanga upya.

Lakini mazungumzo hayo hayajazalisha usitishaji vita kamili na usio na masharti, kama ambavyo Marekani ilitaka kutoka kwa Urusi.

Vita vibaya sana ambavyo Trump anasisitiza anaweza kuvifanya visimame, bado vinaendelea.

Na Putin, mtu anayeshukiwa kuwa mhalifu wa kivita na ICC, amepewa nafasi ya kurudi kwenye safu ya juu ya siasa za kimataifa.

Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vimeripoti kuwa mazungumzo ya simu ya marais hao wawili yalidumu kwa zaidi ya saa mbili.

Mazungumzo hayo yalihusisha pia, mazungumzo kuhusu mpira wa magongo wa barafu, ni aina ya mazungumzo ambayo watazamaji huko Urusi watayafurahia.

Urusi kimataifa

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya miaka mitatu ya kutengwa na ulimwengu wa magharibi, na uhusiano baridi wa muda mrefu kabla miaka hiyo, Urusi imerudi kuzungumza moja kwa moja na utawala wa Marekani.

Viongozi hao wawili pia wamejadili amani ya Mashariki ya Kati na "usalama wa kimataifa."

Kabla ya simu hiyo, wengine walijiuliza ikiwa Donald Trump anaweza kuleta shinikizo kwa Urusi.

Hakuna dalili ya kumvunjia heshima Putin kama ile ambayo kiongozi wa Ukraine Volodymyr Zelensky alilazimika kuivumilia katika Ikulu ya Marekani siku kadhaa zilizopita.

Urusi inasema inataka amani. Lakini badala ya kuzima ndege zake zisizo na rubani na kunyamazisha bunduki zake, inazungumzia jinsi usitishaji mapigano ambao haupo utawezaje kufuatiliwa.

Wakati huo huo, inaongeza masharti zaidi yanayolenga kulemaza uwezo wa Kyiv wa kupigana.

Sharti moja ni kwamba mtiririko wa silaha na ujasusi kwenda Ukraine kutoka kwa washirika wake lazima ukome.

Kwa wananchi wa Ukraine, matumaini pekee ni kwamba Marekani haijakubali lolote kati ya masharti hayo.

Wanaweza pia kuona uthibitisho kwamba Urusi haina nia ya kukomesha uvamizi wake.

Ni kweli mazungumzo hayo yataleta nafuu kidogo kwa Ukraine kutokana na mashambulizi katika miundombinu ya nishati.

Kwa diplomasia ya Marekani, mazungumzo hayo yamekatisha tamaa. Na kwa Kremlin yalikuwa ni mazungumzo mazuri.