'Breki' ya kutafakari - mahesabu ya Israeli kabla ya kuingia Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Frank Gardner
- Nafasi, Mwandishi wa BBC wa Masuala ya Usalama
Kwa siku kadhaa sasa, Israel imeashiria kwamba vikosi vyake viko tayari kuingia Gaza kwa lengo la kuwaondoa Hamas kama kikosi cha kijeshi mara moja, kufuatia uvamizi wake kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba.
Zaidi ya askari wa akiba 300,000 wameitwa kwa ajili ya kuimarisha vikosi vya ulinzi vya Israel, IDF. Mashamba, viwanja na kibbutzim katika mpaka wa upande wa Israel na Gaza yamejaa vifaru vya Merkava, mifumo ya mizinga inayojiendesha yenyewe na maelfu ya askari wanaotembea kwa miguu wenye silaha nzito waliovalia mavazi kamili ya kivita.
Jeshi la Wanahewa la Israel na Jeshi la Wanamaji limekuwa likishambulia kila eneo linaloshukiwa kuwa la wapiganaji wa Hamas na kundi la Kipalestina la Islamic Jihad na hifadhi ya silaha huko Gaza, na kuua na kujeruhi idadi kubwa ya raia katika harakati hizo, pamoja na idadi ndogo ya makamanda wa Hamas.
Idadi kubwa ya majeruhi iliyosababishwa na mlipuko wa Jumanne katika hospitali kuu ya Gaza, inayolaumiwa na kukanushwa na pande zote mbili, itazidisha hali ya wasiwasi katika eneo hilo hata zaidi.
Kwa nini Israel haijaanza operesheni yake ya kuingia Gaza kama ilivyotarajiwa?
Kuna sababu kadhaa zinazojitokaza hapa.
Upande Biden
Ziara iliyopangwa kwa haraka ya Rais Joe Biden nchini Israel wiki hii ni dalili ya jinsi Ikulu ya Marekani ilivyo na wasiwasi kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya. Washington inakabiliwa na maswala mawili makubwa: kuongezeka kwa mgogoro wa kibinadamu na hatari ya mzozo huu kuenea katika Mashariki ya Kati.
Rais wa Marekani tayari ameweka wazi upinzani wake dhidi ya Israel kurejea kukalia kimabavu Gaza, ambayo ilijiondoa mwaka 2005. Hili, alisema litakuwa "kosa kubwa".
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Rasmi amekuwa akiizuru Israel kuonyesha uungaji mkono wa kimkakati kwa mshirika wa karibu wa Amerika Mashariki ya Kati na kusikia mipango ya Israel kwa Gaza.
Kwa njia isiyo rasmi, ana uwezekano wa kuhimiza kujizuia kwa serikali kali ya Benjamin Netanyahu. Marekani ingependa kujua ni jinsi gani, ikiwa Israel itaingia Gaza, mpango wa kutoka, na lini.
Matarajio yoyote ya Israeli kuanza uvamizi kamili wa kijeshi huko Gaza wakati ndege ya Airforce One inayombeba rais wa Marekani iko kwenye lami huko Tel Aviv haitakuwa nzuri, kwa Marekani au Israeli.
Katika ziara iliyogubikwa na mlipuko mbaya katika Hospitali ya Al-Ahli Arab huko Gaza, Rais Biden aliunga mkono hadharani usemi wa Israel wa matukio, kwamba roketi ya Wapalestina iliyorushwa vibaya ilisababisha mlipuko huo. Maafisa wa Palestina wanasema shambulizi la anga la Israel lilipiga hospitali hiyo. BBC inajitahidi kuthibitisha kikamilifu idadi ya waliofariki, ambayo inahofiwa kukaribia mamia, pamoja na chanzo cha mlipuko huo.
Upande wa Iran
Katika siku chache zilizopita, Iran imetoa onyo kali kwamba shambulio la Israel dhidi ya Gaza haliwezi kuendelea kufumbiwa macho. Kwa hivyo hiyo inamaanisha nini katika kiuhalisia?
Iran inafadhili, kutoa mafunzo, silaha na kwa kiasi fulani inadhibiti idadi ya wanamgambo wa Kishia katika Mashariki ya Kati. Kwa mbali, yenye nguvu zaidi kati ya hizi ni Hezbollah huko Lebanon, iliyopiga kambi ng'ambo ya mpaka wa kaskazini wa Israel.
Nchi hizo mbili zilipigana vita vya uharibifu na visivyo na mwisho mnamo 2006 ambavyo vilishuhudia vifaru vya kisasa vya vita vya Israel vikitolewa na mahandaki ya kujificha na kuvizia yalivyopangwa vizuri. Tangu wakati huo, Hezbollah imejizatiti tena kwa usaidizi wa Iran na sasa inadhaniwa kuwa na takriban roketi na makombora 150,000, mengi yakiwa ya masafa marefu na yanayoongozwa kwa usahihi.
Kuna tishio bayana hapa kwamba iwapo Israel itaivamia Gaza basi Hezbollah huenda ikafungua mkondo mpya kwenye mpaka wa kaskazini wa Israel, na kuilazimisha kupigana vita katika pande mbili.
Hata hivyo, hakuna uhakika kwamba Hizbollah inataka vita hivi kwa wakati huu, hasa baada ya meli mbili za kubeba silaha za kivita za Jeshi la Wanamaji la Marekani kutia nanga mashariki mwa Mediterania na tayari kuja kusaidia Israel.
Hii itaipa Israel uhakika kwamba shambulio lolote la Hezbollah linaweza kujibiwa na jeshi la anga na la wanamaji la Marekani kama hatu aya kilipiza kisasi. Ni vyema kukumbuka ingawa mwanzoni mwa vita vya mwisho vya Israel na Hezbollah mwaka 2006 wanamgambo hao waliweza kuishambulia meli ya kivita ya Israel nje ya ufuo kwa kutumia moja ya makombora yao ya hali ya juu.
Sababu za kibinadamu
Dhana ya serikali ya Israel ya mgogoro wa kibinadamu inaelekea kubaki nyuma ya dunia nzima linapokuja suala la kuondoa Hamas kutoka Gaza.
Huku idadi ya vifo miongoni mwa raia wa Palestina ikiongezeka kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel, sehemu kubwa ya huruma kimataifa kwa Israel baada ya vitendo vya kinyama na vya umwagaji damu vya Hamas tarehe 7 Oktoba vimegubikwa na miito inayoongezeka ya kusitisha mashambulizi ya anga na kuwalinda raia wa kawaida wa Gaza.
Endapo vikosi vya ardhini vya Israel vitaingia Gaza kwa nguvu, basi idadi ya vifo itaongezeka zaidi.
Wanajeshi wa Israel watakufa pia, kutokana na vita vya kuvizia vya wavamizi na mitego ya kushambulia - mapigano mengi yanaweza hata kutokea chini ya ardhi, katika maili ya vichuguu.
Lakini kuna uwezekano kwamba, kwa mara nyingine tena ni raia ndio watakaoumia zaidi.
Kushindwa vibaya kwa ujasusi
Idara ya ujasusi ya Israel imekuwa na mwezi mbaya.
Shin Bet, shirika la ujasusi la ndani, limekosolewa vikali kwa kushindwa kung'amua kutokea kwa shambulio baya la Hamas. Inadaiwa kuwa na mtandao wa watoa habari na majasusi ndani ya Gaza, wakiwafuatilia makamanda kutoka Hamas na kundi la Islamic Jihad.
Hata hivyo kile kilichotokea asubuhi hiyo ya Jumamosi kilikuwa cha kutisha kusini mwa Israel na kilitajwa kuwa kufeli vibaya kwa vyombo vya kijasusi katika historia ya taifa hilo tangu vita vya Yom Kippur mwaka 1973.
Idara za kijasusi za Israel zimekuwa zikijaribu sana kufanya marekebisho katika kipindi cha siku 10 zilizopita, na kusaidia IDF kutambua majina na maeneo ya mateka pamoja na mahali makamanda wa Hamas wamejificha.
Inawezekana kwamba wameomba muda zaidi wa kukusanya taarifa zaidi ili wakati vikosi vya ardhini vitakapoamua kingia Gaza, basi vielekee moja kwa moja kwenye eneo maalum, badala ya kuzunguka katika magofu na vifusi vya kaskazini mwa Gaza vinavyokabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara, huku lalama zikienelea kutolewa kutoka sehemu duniani.
Wapiganaji wa Kipalestina wa Hamas na Islamic Jihad ambao bado wanafanya kazi baada ya kampeni endelevu ya Israel ya kulipua mabomu watakuwa wamepanga kuvizia na kwa kuwekea mitego wanajeshi wowote wa Israel wanaosonga mbele. Hali hii itakuwa hatari sana katika vichuguu vya chini ya ardhi. Ujasusi wa Israel utakuwa na kibarua kigumu kubaini mahali walipo na kuonya IDF ipasavyo.














