Kwa nini Israel imechelewesha mpango wa kuingia Gaza? - Magazeti ya Israel

NN

Chanzo cha picha, Reuters

Tunaanza ziara yetu ya magazeti ya Israel kwa kuangalia makala ya gazeti la Jerusalem Post iliyoandikwa na Jonah Jeremy yenye anuani "Kwa nini uvamizi wa ardhini wa Gaza umecheleweshwa tangu Ijumaa?"

Mwandishi anasema suala hilo lilionekana wazi siku ya Alhamisi, kwamba uvamizi wa jeshi la Israel huko Gaza ungeanza Ijumaa au Jumamosi.

Jeshi la Israel pia lilitoa makataa kwa Wapalestina kuhama kaskazini mwa Gaza, na makataa haya yaliisha ilipofika saa sita mchana siku ya Ijumaa.

Anaongeza kuwa ngoma za vita zilianza kupigwa mapema Jumapili na Jumatatu, na Jeshi la Anga lilifungua njia kwa kufanya ulipuaji mbaya wa mabomu. Lakini sasa tumefika Jumanne, na ishara zote zinaonyesha uvamizi huo uko mbali, bado haujakaribia.

Nini kilibadilika? Jonah anasema: Inaonekana kuna sababu kadhaa zinazosababisha kuchelewa. Mojawapo ni ile ambayo vyanzo vya habari vililiambia gazeti la Jerusalem Post, ni wasiwasi unaoongezeka kwamba Hezbollah inasubiri wakati ambapo vikosi vingi vya jeshi la Israel viko tayari kusonga mbele Gaza ili kuanza mapambano kamili na Israel upande wa kaskazini.

Vita ni hadaa. Lakini hilo haliwezi kulizuia jeshi la Israel kuivamia Gaza, ingawa huenda likachelewesha uvamizi huo ili kuipima nia ya Hizbullah, pamoja na kuimarisha vikosi vya kaskazini.

Kuhusu sababu nyingine, mwandishi anaeleza pia kuna utambuzi wa kina ndani ya IDF na katika ngazi ya kisiasa, kwamba IDF haijapigana vita kama hivi kwa miongo kadhaa, na kukimbilia kuingia vitani bila maandalizi ili kukidhi kiu ya kulipiza kisasi, linaweza kuwa kosa kubwa.

Mfano mzuri ni uvamizi wa ardhini katika Vita vya Pili vya Lebanon vya 2006, ambavyo vilikuwa vita kamili, ingawa nguvu ya anga ilikuwa sehemu ya mafanikio.

Mwandishi anaamini kuna sababu nyingine za kucheleweshwa, ambayo inaweza kujumuisha shinikizo la Marekani kuzuia vifo vya raia, wasiwasi wa ndani juu ya mateka wa Israel huko Gaza, na kutoa muda zaidi kwa Wapalestina kuhama.

Mwandishi huyo anaeleza licha ya uungwaji mkono mkubwa wa kimataifa ambao Israel imepata, pindi idadi ya majeruhi Gaza inapoongezeka, jambo ambalo huenda likatokea wakati uvamizi huo utakapoanza, kutakuwa na shinikizo kubwa kutoka Marekani na dunia la kusitisha vita.

Bado haijaamuliwa nini kitatokea Gaza baada ya "jeshi la Israel kuupindua utawala wa Hamas." Mwandishi anahitimisha makala yake kwa kusema - ni baada ya vita ndipo tutajua iwapo muda huu wa ziada ulitumiwa kwa busara katika kuandaa mpango wa uvamizi au ilikuwa ni kupoteza muda.

"Mstari mwekundu katika vita vinavyoendelea’’

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika gazeti la Haaretz, ambalo limechapisha makala ya uchambuzi iliyoandikwa na Yossi Verter chini ya anuani: "Wakati Israel inateseka kutokana na mashambulizi ya Hamas, Netanyahu anamlaumu kila mtu isipokuwa yeye mwenyewe."

Mwandishi huyo anasema hadi Jumatatu usiku, siku ya kumi ya vita, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alikuwa mwangalifu asitamke hata neno moja kuashiria kuwajibika kwake kwa kushindwa kuzuia maafa yaliyotokea.

Anaongeza, siku ya Jumatatu, mkuu wa Shin Bet, Ronen Bar, na Mkuu wa Jeshi la Israel, Luteni Jenerali Herzl Halevy, walikubali kulaumika kwa kile kilichotokea, wakati Netanyahu anaendelea kukwepa na kukanusha, akiamini kujidanganya kutampa hifadhi dhidi ya hasira za raia.

"Kuna maswali mengi, na tayari tumeanza uchunguzi," Netanyahu alisema katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa kikao cha majira ya baridi cha Knesset Jumatatu. Lakini mwandishi anaamini mshitakiwa mkuu ni Waziri Mkuu, na hawezi kuchunguza chochote.

Kwa mtazamo wake, Netanyahu ni kiumbe wa kisiasa mwenye roho mbaya, fikra potofu, na ujuzi ana ujuzi mbaya wa kupambana na migogoro.

Anajiandaa kuulaumu uongozi wa kijeshi ambao haukumjulisha wala kumtahadharisha juu ya kilichotokea, hivyo ni kosa la vyombo vya kijeshi na viongozi wao.

Anahitimisha kwa kusema baada ya vita kumalizika, serikali na rais wake - watashikilia viti vyao kwa gharama yoyote – wakati huu utawala wa Marekani umeweka mstari mwekundu kwa Israel: "Hakutakuwa na mgogoro wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza."

"Msaada wenye masharti’’

Tunamalizia ziara yetu katika magazeti ya Israel kwa ripoti katika gazeti la i24 News, yenye anuani "Waziri wa Ulinzi wa Marekani aliiomba Israel isifanye shambulio la mapema dhidi ya Hezbollah."

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti hilo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, alieleza nchi yake itatoa msaada wa anga kwa jeshi la Israel ikiwa Hezbollah ya Lebanon, ambayo utawala wa Marekani inaitaja kuwa "kundi la kigaidi," itafanya mashambulizi dhidi yake. .

Tovuti ya habari ya Israel iliripoti kwamba kwa sharti la Israel kutoanza kuishambulia Hezbollah, Marekani itaipatia Israeli marubani wake na msaada wa anga, lakini ikiwa Hezbollah itaanzisha shambulio kwa Israeli kwanza.

Washington haikuzungumzia kwa uwazi mashambulio ya Hezbollah dhidi ya Israel siku ya Jumapili, ambayo yalisababisha mauaji ya raia wa Israel Mwarabu na afisa wa jeshi la Israel, pamoja na askari wengine wasiopungua wawili katika matukio ya awali tangu kuzuka kwa vita hivi.