"Hamas haiwawakilishi Wapalestina" - magazeti ya Israel

WEDS

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israeli katika kifaru karibu na mpaka na Gaza

Katika magazeti ya Kiebrania (Hebrew) makala katika gazeti la Haaretz ya mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Israel, Itay Mack, inasisitiza ulazima wa kuondolewa kwa Hamas, lakini bila ya kuua idadi kubwa ya raia wa Palestina.

Mack alianza kwa kuandika kwamba jumuiya ya kimataifa "ilifumbia macho jinai za kivita zinazofanywa na Israel katika ardhi inayokaliwa kimabavu ya Palestina, lakini pia ilifumbia macho harakati na malengo ya Hamas."

Mack anaamini Hamas ni “kundi la mauaji ya halaiki lenye misingi ya imani za misimamo mikali.”

Mack anadai Hamas ina dhamira ya "kuwaondoa Wayahudi katika ardhi kati ya Mto Jordan na Bahari ya Mediterania, ama wakubali kuishi katika utawala wa kiimla wa Kiislamu."

Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu anaeleza - itikadi hiyo ni sawa na itikadi ya utawala wa Iran unaounga mkono harakati za Palestina za Hamas na Islamic Jihad pamoja na kundi la Hizbullah nchini Lebanon.

Mack anaamini kauli zenye migongano katika harakati ya Hamas ziliihadaa jumuiya ya kimataifa na kuifanya ifikirie kuwa hadithi ya Hamas inafanana na kisa cha Harakati ya Ukombozi wa Palestina, ambayo viongozi wake tangu miaka ya 1980 waliacha ndoto yao ya zamani ya kuiangamiza Israel na kusaini Mkataba wa amani wa Oslo.

Mwandishi wa makala hiyo aliishutumu Hamas kwa "kuwaangamiza raia" kwa makusudi waliokuwa katika maeneo ambayo vuguvugu hilo lilivamia wiki iliyopita kusini mwa Israel.

Mack anasema jumuiya ya kimataifa lazima itimize wajibu wake chini ya sheria za kimataifa na mikataba inayohusiana na kupambana na ugaidi ili kuzuia Wayahudi na "mauaji mengine ya halaiki na kuuangusha utawala wa Hamas," lakini wakati huo huo raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza hawapaswi kutolewa kafara kwa hilo.

Mwanaharakati huyo ameongeza, kufuatia shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba inaonekana kana kwamba Israel imepata ruhusa kutoka kwa washirika wake wa Magharibi kuanzisha uvamizi wa ardhini katika Ukanda wa Gaza kwa lengo la kuuangusha utawala wa Hamas.

Lakini Israel na jumuiya ya kimataifa wanajua vyema, kutokana na uzoefu wa Vita vya Lebanon mwaka 1982, kwamba raia wengi wanaweza kudhurika.

Mwandishi huyo anaamini, kukosekana kwa uwezekano wa kuondoka haraka kwa raia wote katika Ukanda wa Gaza, uvamizi wowote wa ardhini wa Israel unaweza kusababisha madhara yasiyo na kifani kwa raia wa Palestina.

''Marekani na ulimwengu wamesimama njia panda"

FDC

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Wapalestina wa Gaza wakiomboleza
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika gazeti la The Times of Israel, kuna makala ya mwandishi Sam Litvin - anatoa wito wa kutofautisha kati ya harakati ya Hamas na Palestina.

Sam anaamini "Hamas sio Wapalestina; ni utawala unaotawala katika Ukanda wa Gaza."

Mwandishi anauliza, "Je, ni kweli tunataka kusimama na wale wanaohalalisha ugaidi? "Ikiwa mtu anaweza kuhalalisha ugaidi dhidi ya Israeli, wengine wataweza kuhalalisha ugaidi dhidi ya Marekani, Ufaransa, au nchi nyingine yoyote."

Mwandishi wa makala hiyo anaamini Marekani na dunia zimesimama kwenye njia panda, na utulivu wa kimataifa unategemea kuchagua mwelekeo katika njia panda hii.

Mwandishi huyo anaendelea kusema: “Lazima tuwe wa wazi kwamba kuunga mkono Hamas - na kujaribu kuizuia Israel kufanya kila iwezalo ili kukomesha vita hivi ambavyo Hamas ilianzisha - hakutawasaidia watu wa Palestina, bali kutawaweka ndani ya mzunguko wa vurugu.

Kama vile kushindwa kumshinda Putin nchini Ukraine kungemfanya kiongozi huyo wa Urusi kuendeleza uchokozi wake katika eneo hilo na katika ulimwengu wote wa kidemokrasia.

Sam alimalizia kwa kusema: “Wale waumini wa maadili ya kidemokrasia lazima wajiulize: Je, wanaelekeza uungaji mkono wao kwa nani?’’

“Hatupaswi kusahau vita hivi''

dcs

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mazishi ya kijeshi huko Israel

Gazeti la Yedioth Ahronoth lina makala kuhusu hisia za Waisraeli juu ya vita vinavyopamba moto dhidi ya Hamas tangu tarehe saba Oktoba hii.

Mwandishi Yair Keitan anaandika kwamba alichopenda zaidi kuhusu watu wake wa Israeli ni mzaha.

Yair anasema: “Tunaweza kukabiliana na msiba wowote kwa kufanya mizaha, ambayo wale tu wa karibu ndio wataelewa na kupata faraja.

Lakini “siku ya saba ya Oktoba, na siku zilizofuata, zilikuja kama ukuta wa kutugawanya; hatukucheka tena kuanzia siku hiyo, au wengi wetu hatukuhisi tena kwamba inawezekana kucheka au kuimba tukiendesha gari kama hapo awali.”

Yair anaongeza: “Pamoja na maumivu na mateso, sitaki kusahau yaliyotokea, sitaki picha za wahanga zipotee na majina yao yafutwe. Nataka maumivu hayo yabaki ndani yangu milele ili waathiriwa hawa wapate watu wa kuishi nao.”

Mwandishi anaendelea kusema: “Hatuna picha moja au rekodi moja ya matukio ya Oktoba 7. Badala yake, wengi wetu tuliamka saa 12 na nusu asubuhi ya siku hiyo ili kufungua macho yetu. Tulikutana na matukio ambayo yamebaki kwetu tangu wakati huo na hayajatuacha."

"Hakuna mtu anayeweza kuendelea kama alivyokuwa hapo awali, katika ulimwengu unaoweza kuzalisha uovu huu wa kutisha. Ulimwengu unaojumuisha watu wanaosherehekea jambo hili la kutisha na kusambaza pipi kwa tukio hilo.’’

Mwishoni mwa makala yake anasema: “Baada ya siku chache za kukosa usingizi na kukosa hamu ya kula, macho yatafumba, muda utapita, na siku moja nitajikuta nikiandika kuhusu mechi ya soka na siku moja tutacheka tukitazama sinema ya vichekesho.''