Matukio makubwa katika siku kumi za vita vya Israel na Hamas

fgv

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/SHUTTERSTOCK

Maelezo ya picha, Athari ya mashambulizi ya Israel katika eneo la Khan Yunis, Gaza

Vita kati ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya "Hamas" vimeingia siku yake ya kumi kwa kuzingatia muendelezo wa mashambulizi ya anga, baharini na ardhini yanayotekelezwa na Israel huko Ukanda wa Gaza.

Ni baada ya Hamas na makundi ya Palestina kulipua miji ya Israel kwa makombora, kufanya operesheni za kujipenyeza katika maeneo yanayozunguka Gaza na kukabiliana na wanajeshi wa Israel.

Huu ni mpangilio wa matukio muhimu zaidi yaliyotokea wakati wa siku kumi za vita hivi:

Oktoba 7

jhnb

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israeli wakifanya msako katika miji ya Kusini mwa Israel baada ya uvamzi wa Hamas

Saa 12:30 asubuhi Jumamosi, Oktoba 7, 2023, wakati ving'ora viliposikika kusini na kati mwa Israeli, kutangaza kwamba maeneo hayo yalishambuliwa kwa makombora

Sambamba na hayo, taarifa rasmi ya kwanza kutoka kwa Hamas ilitolewa na kamanda wa Brigedi za Izz al-Din al-Qassam, tawi la kijeshi la harakati ya Hamas, Muhammad al-Deif, alitangaza katika ujumbe uliorekodiwa uzinduzi wa Operesheni "Mafuriko ya Al-Aqsa."

Alisema ulikuwa wakati wa “adui kuelewa kwamba wakati wa sherehe bila kulipa umeisha.” Aliwataka Wapalestina kushambulia makazi ya Israel kwa silaha zote walizonazo.

Zaidi ya saa moja baada ya kuanza kwa operesheni hiyo, jeshi la Israel lilitangaza wanamgambo wa Hamas wameingia katika maeneo ya kusini mwa Israel na kuwataka wakaazi wa mji wa Sderot na miji mingine kusalia majumbani mwao.

Israel ilitangaza vita na kutoa wito wa askari wa akiba ili kukabiliana na mashambulizi ya roketi kutoka Gaza. Pia ilitangaza kuanza kwa operesheni za kukabiliana na Hamas.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Saa 04:47, ndege za kwanza za kivita zilishambulia Ukanda wa Gaza. Saa moja baadaye, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitoa kauli yake ya kwanza kuhusu kile kilichokuwa kikitokea kupitia tweet kwenye jukwaa la "X" - alisema Israel iko katika vita.

Kufikia saa sita mchana, jeshi la Israel lilianza kufanya operesheni za kupambana na Hamas kusini mwa Israel, huku makombora yaliyorushwa kutoka Gaza katika maeneo hayo yakiongezeka na kufikia zaidi ya roketi 1,200.

Hamas ilitoa kanda za video zinazoonyesha operesheni zake dhidi ya maeneo ya jeshi la Israel na mafanikio yake kwa kuwakamata wanajeshi wa Israel.

Video pia zilionyesha utekaji nyara wa raia wa Israel wanaoishi katika miji inayozunguka Gaza na uhamisho wao hadi Ukanda wa Gaza.

Sambamba na hayo, Marekani ilitoa tamko lake la kwanza kupitia Baraza la Usalama la Taifa, likilaani kile ilichokitaja kuwa ni shambulio la kigaidi na kuthibitisha uungaji mkono wa Marekani kwa Israel.

Rais wa Marekani Joe Biden kisha alimpigia Netanyahu kueleza rambirambi zake na kumuunga mkono na baadaye akatangaza katika hotuba yake kwamba uungaji mkono wa Marekani kwa Israel ni "imara na hautetereki.’’

Oktoba 8

rfgv

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Meli ya Kivita ya Marekani ambayo ndio kubwa zaidi duniani katika bahari ya Mediterranean

Serikali ya Israel ilitoa amri ya watu kuhama wale walio katika miji ya Israel inayopakana na Ukanda wa Gaza. Sanjari na jeshi la Israel likaufunga kabisa Ukingo wa Magharibi.

Netanyahu alimteua Meja Jenerali mstaafu Gal Hirsch kuwajibika kwa faili ya wafungwa na Waisraeli waliopotea.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin aliamuru kutumwa kwa shehena ya ndege za "Gerald Ford" mashariki mwa bahari ya Mediterania, katika hatua ambayo Hamas ililaani na kuiona "uchokozi dhidi ya watu wa Palestina."

Oktoba 9

ghb

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/SHUTTERSTOCK

Maelezo ya picha, Israel inaendelea kushambulia Gaza

Siku hii, Hezbollah iliingia kwenye mzozo huo kwa kufanya shambulio la kombora kwenye eneo la jeshi la Israeli kwenye mpaka na Lebanon, ambalo liliuwa afisa wa jeshi la Israeli. Hezbollah ilitangaza tangu mwanzo wa vita kwamba linaunga mkono mashambulizi ya Hamas.

Israel ilijibu kwa kushambulia kwa mabomu maeneo ya karibu ya miji ya Lebanon kwenye mpaka .

Waziri wa Ulinzi wa Israel alitangaza amri ya kukata umeme, maji na kuzuia kuingia kwa chakula na mafuta katika Ukanda wa Gaza. "Tunapambana na binaadamu wanyama," alisema.

Israel ilituma ndege za usafiri za C-130 hadi Ulaya kuwasafirisha wanajeshi waliokuwa likizo na kuwarejesha nchini kushiriki katika vita.

Oktoba 10

gbfv

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/SHUTTERSTOCK

Maelezo ya picha, Hezbollah imeshambulia maeneo ya kijeshi ya Israel karibu na mpaka na Lebanon

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNRWA) lilitangaza kuuawa kwa wafanyakazi wake wanne katika mashambulizi yanayoendelea ya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Jeshi la Israel lilisema lilishambulia maeneo 70 ya Hamas karibu na kitongoji cha Daraj al-Tuffah huko Gaza.

Silaha za kisasa kutoka Marekani ziliwasili Israel siku hiyo pia.

Abdul-Malik al-Houthi, kiongozi wa vuguvugu la Houthi nchini Yemen, alitangaza uingiliaji kati wowote wa Gaza na Marekani utakabiliwa na uingiliaji kati wa Wahouthi.

Oktoba 11

b

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Dada wa mwanajeshi aliyeuwawa katika mapambano na Hamas katika mji wa Be'eri akilia baada ya mazishi huko Jerusalem

Nege za Israel zilizidisha mashambulizi ya mabomu katika maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza, hali iliyopelekea kuharibiwa kwa idadi kubwa ya majengo ya makazi ya watu, yakiwemo majengo ya Chuo Kikuu cha Kiislamu katika mji wa Gaza.

Israel ilitangaza Hamas ilikuwa ikifanya mauaji katika miji iliyoingia, na kusema kuwa miongoni mwa waliofariki ni watoto, kama ilivyotokea katika mji wa Kfar Azza.

Kwa upande mwingine, Wizara ya Afya ya Palestina ilitangaza, idadi ya waliofariki kutokana na mashambulizi ya anga katika Ukanda wa Gaza imefikia watu 1,055 na wengine 5,184 wamejeruhiwa, na zaidi ya 2,600 wamekimbia makazi yao.

Idadi ya vifo nchini Israeli iliongezeka hadi 1,200.

Wakati huo huo, mtambo pekee wa kuzalisha umeme katika Ukanda huo uliacha kufanya kazi baada ya kukosa mafuta kutokana na kizuizi kilichowekwa na Israel.

Katika mpaka wa Lebanon, Hezbollah ilidai kuhusika na mashambulizi ya makombora kwenye maeneo ya kijeshi ya Israel.

Walinzi wa mpaka wa Israel waliwapiga risasi Wapalestina wawili katika eneo la Jerusalem Mashariki na kuwauwa.

Marekani ilifanya mazungumzo na Misri kuhusu kufungua njia ya misaada ya kibinadamu kupitia kivuko cha Rafah kwenye mpaka wa Misri na Ukanda wa Gaza.

Lakini jeshi la Israel lilishambulia kwa bomu kivuko hicho, na kuvuruga juhudi hizi.

Oktoba 12

ghbv

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Shule ya UNRWA ambayo ilikuwa imehifadhi waliokimbia makaazi yao ilishabuliwa huko kaskazini mwa Gaza

Jeshi la Israel lilitangaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa zaidi ya Waisraeli elfu moja wameuawa na kuthibitisha watu 50 ama walitekwa au kupotea.

Vifaa vya kijeshi vya Marekani viliwasili katika kambi ya kijeshi ya Nevatim sanjari na kuwasili kwa meli za kivita mashariki mwa Mediterania.

Australia na Canada zilitangaza mipango ya kuwahamisha raia wao kwa ndege kutoka Israel kupitia Tel Aviv.

Umoja wa Mataifa ulitangaza zaidi ya Wapalestina 260,000 walikimbia makazi yao kutokana na shambulio na kukimbilia katika shule za UNRWA.

Jeshi la Israel lilitangaza kuwa limeshambulia kwa makombora maeneo zaidi ya 200 katika Ukanda wa Gaza.

Jeshi lilidondosha vipeperushi katika maeneo ya kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, likitoa wito kwa wakaazi kuhama makazi yao na kwenda katika maeneo salama kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Ilifanya mashambulio ya mizinga kwenye maeneo ndani ya ardhi ya Syria baada ya kurusha mizinga kadhaa kaskazini mwa Israel.

Israel ilitangaza Ukanda wa Gaza hautapewa maji, umeme na mafuta hadi mateka watakapokombolewa.

Jeshi la Israel likathibitisha mashambulizi katika viwanja vya ndege vya Damascus na Aleppo nchini Syria.

Oktoba 13

b

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Mtoto wa miaka minne alijeruhiwa na mashambulizi ya Israel yaliyouwa watu 14 wa familia yake huko Khan Yunis, Gaza

Umati wa wakaazi wanaoishi kaskazini mwa Ukanda wa Gaza walianza kuhamia kusini baada ya onyo la Israel, ambalo liliwapa makataa ya saa 24 na kuwahakikishia kuwa halitawaleng.

Lakini shambulio la kombora la Israel liligonga baadhi ya magari na lori lililokuwa likiwasafirisha watu kuelekea kusini, katika Mtaa wa Salah al-Din.

Wizara ya Afya ya Palestina ilisema shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 70.

Umoja wa Mataifa uliitaka Israel kuondoa agizo la watu kuondoka, ikionya juu ya janga la kibinadamu. Wito huo huo ulirudiwa na Amnesty International.

Hamas ilitoa wito kwa wakaazi wa maeneo ya kaskazini mwa Gaza, ambao idadi yao ni takriban milioni 1.1, kutotoka makwao na kutoamini ahadi za Israel.

Jeshi la Israel liliendelea na mashambulizi yake huko Gaza, hali iliyopelekea idadi ya vifo katika Ukanda huo kuongezeka ndani ya wiki moja na kufikia watu 1,900 waliokufa na zaidi ya 7,696 kujeruhiwa, kulingana na taarifa za Wizara ya Afya ya Palestina.

Wakati huo huo misaada ya kibinadamu kutoka pande mbalimbali ikiwemo ya Uturuki imewasili katika uwanja wa ndege wa Al-Arish nchini Misri kusubiri kuruhusiwa kuingia katika Ukanda wa Gaza.

Oktoba 14

gbv

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Malori ya misaada ya kibinadaamu yakisubiri mpaka wa Rafah wa Gaza na Israel kufunguliwa

Jeshi la Israel lilitangaza njia mbili salama kwa Wapalestina kuondoka kutoka maeneo ya kaskazini ya Ukanda wa Gaza kuelekea kusini, na kuweka muda wa saa sita kufanya hivyo.

Israel na Misri zilitangaza kivuko cha Rafah kitafunguliwa kwa ajili ya kuondoka wale wenye pasipoti za kigeni kuanzia saa sita mchana Jumamosi hadi 11 tano jioni, kwa saa za ndani.

Marekani iliruhusu kuondoka kwa wafanyakazi wasio wa lazima wanaofanya kazi katika ubalozi wake nchini Israel.

Israel ilitangaza kuna zaidi ya wageni 100 kati ya watu 1,300 waliouawa na Hamas katika shambulio lake.

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya majengo 1,000 yaliharibiwa huko Gaza kutokana na mashambulizi ya Israel.

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina lilitangaza magari yake ya kubebea wagonjwa yalilengwa kwa makusudi na jeshi la Israel.

Israel ilitangaza kuuawa kwa kamanda wa kikosi cha anga cha Hamas, ambaye alihusika katika kupanga shambulio hilo.

Kwa upande wake, UNRWA ilitangaza katika ujumbe wa Twitter kwamba makazi ambayo ilitenga kuwapokea watu waliokimbia makazi yao katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza si salama tena.

Oktoba 15

gbv

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/SHUTTERSTOCK

Maelezo ya picha, Picha ya Waisrael waliopotea au kutekwa na Hamas huko Tel Aviv

Shirika la Habari la Palestina, Wafa, lilisema wanajeshi wa Israel wamewakamata zaidi ya Wapalestina 50 katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Idadi ya watu waliofurushwa kutoka makwao katika Ukanda wa Gaza ndani ya wiki moja ilifikia zaidi ya watu milioni moja.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Abdollahian ambaye alifanya ziara Lebanon na Qatar ametangaza, kama hujuma ya Wazayuni dhidi ya raia wasio na ulinzi na watu wa Gaza itaendelea, hakuna mtu anayeweza kutoa hakikisho la kudhibiti hali hiyo na kuzuia kuenea kwa mzozo huo.

Mapigano, mashambulio ya makombora na mashambulizi ya kukabiliana yaliendelea kati ya Hezbollah na wanajeshi wa Israel kwenye mpaka wa Lebanon na Israel.

Jeshi la Israel limethibitisha kuwepo kwa mateka 126 wa Israel mikononi mwa Hamas huko Gaza na kusema idadi ya vifo miongoni mwa wanajeshi wake imefikia 279.

Israel ilimfahamisha Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa White House, Jake Sullivan kwamba maji yamerejeshwa kwenye mabomba kusini wa Gaza.

Hospitali nne huko Gaza hazikuwa na huduma, na jeshi la Israeli lilitaka watu waondoke katika hospitali 21 kaskazini mwa Gaza, agizo lililokataliwa na tawala za hospitali hizo. Shirika la Afya Ulimwenguni liliitaka Israeli kuondoa amri hiyo.

Kulingana na Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari, waandishi wa habari wasiopungua kumi na wawili waliuawa, wengine wanane walijeruhiwa, na wawili hawajulikani walipo.

Oktoba 16

Meli yenye ndege za kivita za Marekani iliondoka kwenye bandari ya Virginia, ili kutumika kama njia ya kuzuia kundi lolote linalofikiria kushambulia Israel

Rais Biden alisema katika mahojiano na kipindi cha "Dakika 60" kwenye mtandao wa Marekani wa CBS kwamba kuikalia kwa mabavu Gaza "kutakuwa kosa kubwa," na kuongeza: "Nina imani Israel itachukua hatua kwa mujibu wa sheria za vita."

Biden pia alisema Hamas lazima iondolewe na lazima kuwe na njia inayoelekea kuanzishwa kwa taifa la Palestina.

Pande kadhaa zinafanya juhudi za kidiplomasia kufungua kivuko cha Rafah ili kuleta misaada ya kibinadamu katika Ukanda huo na kuruhusu raia wa kigeni kuondoka.

Katika hatua nyingine, Israel iliamua kuwahamisha wakaazi wa maeneo karibu na mpaka na Lebanon kwa kutarajia kupanuka kwa makabiliano yanayoendelea kwenye mpaka wa Lebanon na Hizbullah.

Wizara ya Afya ya Palestina ilisema idadi ya waliouawa kutokana na mashambulizi ya Israel huko Gaza iliongezeka hadi 2,750. Huku mamlaka ya Israel ikisema idadi ya vifo vya Israel kutokana na mashambulizi ya Hamas imefika 1,400.

Jeshi la Israel limesema idadi ya mateka wanaoshikiliwa na Hamas ni watu 199.