Je Marekani inatoa ujumbe gani kupitia msimamo wake kuhusu Israel-Palestina na Ukraine?

fdcv

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky (kushoto) akiwa na Rais wa Marekani, Joe Biden walipokutana Ikulu ya Marekani Septemba 21, 2023

Wakati Marekani imekuwa ikikemea na kusaidia kuweka kumbukumbu juu ya uhalifu wa kivita wa Urusi - kama ilivyokuwa katika mji wa Bucha wa Ukraine - Biden na wajumbe wake wametaja tu hitaji la kuheshimu sheria za kimataifa katika mashambulizi ya sasa ya Israeli.

Umoja wa Mataifa (UN) tayari umeelezea wasiwasi wake kwamba hatua za Israel - kukata maji, nishati, mafuta na chakula kutoka Ukanda wa Gaza na kuamuru kuondoka kwa zaidi ya watu milioni moja kutoka upande mmoja na kwenda upande mwingine - ndani ya saa 24 - itasababisha idadi kubwa ya vifo vya raia na inaweza kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Katika mitandao ya kijamii, mbunge wa chama cha Democratic Alexandria Ocasio-Cortez, nyota wa mrengo wa kushoto katika siasa za Marekani, alikosoa vikali mashambulizi ya Israel.

"Huku ni kuwaadhibu watu wote na ukiukwaji wa sheria za kimataifa. Hatuwezi kuwauwa kwa njaa karibu watoto milioni moja kwa sababu ya vitendo vya kutisha vya Hamas. Ni lazima tuweke mpaka," alimchapisha kwenye akaunti yake ya X, iliyokuwa Twitter.

Naye mbunge mwingine wa chama cha Democratic, Cori Bush, alisema "kuagiza watu milioni 1.1 kuhama eneo hilo ndani ya saa 24 ni jambo lisilowezekana. Kuna watu ambao wamesalia katika hospitali kaskazini mwa Gaza na ambao hawawezi kusafirishwa. Israel lazima ifutilie mbali agizo hilo, iheshimu sheria za kimataifa na kuzuia ukatili dhidi ya watu wa Palestina."

Jambo jingine ni msimamo wa kihistoria wa Marekani kuhusiana na vitongoji vya walowezi wa Israel katika ardhi zinazochukuliwa kuwa za Kipalestina, kama vile Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na sehemu ya mashariki ya Jerusalem. Ingawa Palestina haikuwahi kuwa nchi, kuna maeneo yanayojitawala yanayotambuliwa kama eneo la Palestina.

Ukaliaji wa walowezi wa Kiyahudi katika maeneo haya tayari umezingatiwa kuwa ni kinyume cha sheria na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Marekani inasema kwamba uingiliaji wa Urusi katika ardhi ya Ukraine ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, lakini Marekani imeepuka kulaani makaazi ya Waisraeli yaliyoanzishwa katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wamarekani hawajawahi kupiga kura ya kuunga mkono tamko lolote la Umoja wa Mataifa linalothibitisha uharamu wa makaazi hayo, isipokuwa azimio la mwaka 1980.

Wakati wa utawala wa Jimmy Carter, diplomasia ya Marekani ilitikisika muda mfupi baada ya kupiga kura na kusema kulikuwa na mkanganyiko, lakini msimamo wa Marekani ulikuwa kujizuia kupiga kura.

Marekani haijawahi kujizuia na badala yake hupiga kura ya turufu dhidi ya maazimio ya Umoja wa Mataifa kuikingia kifua Israel dhidi ya ukosoaji au vikwazo.

Kuhusiana na Urusi, Wamarekani walikuwa wafadhili wa maazimio ya kulaani uvamizi wa Putin katika Baraza la Usalama, ambapo Urusi yenyewe ilipiga kura ya turufu kuyakataa.

Hata hivyo, nje ya medani za kimataifa, viongozi wa Marekani hukiri kwamba uvamizi wa Israel ni kinyume cha sheria na hutoa wito wa kutetea kuundwa kwa taifa la Palestina litakaloishi pamoja na Israel.

Hali ilibadilika wakati wa utawala wa Donald Trump. Novemba 2019, Marekani ilitangaza kwamba haizingatii tena makazi ya Israeli kuwa haramu.

Umoja wa Mataifa ulisema "mabadiliko katika nafasi ya kisiasa ya nchi hayabadilishi sheria iliyoanzishwa ya kimataifa wala tafsiri yake na Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Baraza la Usalama."

Machi 2021, utawala wa Biden ulibadilisha tena msimamo huo na kuyatambua makaazi ya walowezi kama haramu.

Mvutano au utata?

dfgcv

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani, Joe Biden (kushoto) akizungumza na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa, New York, Marekani Septemba 20, 2023

Wachambuzi wa kimataifa waliohojiwa na BBC wamegawanyika kati ya kuonyesha mvutano au undumilakuwili wa msimamo wa Marekani kuhusiana na Israel na Ukraine.

"Ni suala gumu. Marekani imedai kuwa makaazi ya Israel ni kikwazo cha amani. Si mara nyingi, lakini angalau katika baadhi ya nyakati, Wamarekani wameruhusu kupitishwa kwa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanayolaani makazi hayo kama ukiukaji wa sheria za kimataifa, kwamba hawakutumia uwezo wao wa kura ya turufu," profesa wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Stanford, Allen Weiner, aliambia BBC.

"Kwa hiyo nisingesema kuna mkanganyiko, lakini ningesema kuna mvutano kwa maana kwamba Marekani iko wazi katika kupinga uvamizi, unyakuzi na ukaliaji wa Urusi katika maeneo ya Ukraine kuliko kile kinachotokea Israel.”

Trita Parsi, makamu wa rais wa Taasisi ya Quincy think-tank na mwandishi wa kitabu cha Losing an Enemy – Obama, Iran and the Triumph of Diplomacy, anasema, ‘msimamo wa Marekani sio tu una mkanganyiko lakini pia ndio mtazamo wa wengi katika nchi ambazo zinashinikizwa na Marekani kulaani Urusi na kuunga mkono Ukraine kama vile Waafrika na Amerika Kusini.’’

"Msimamo wa Marekani dhidi ya Ukraine na Israel unaonyesha hali ya kushangaza ya viwango viwili ambavyo sehemu kubwa ya Kusini mwa dunia tayari inafahamu," Parsi, mwanamataifa wa Uswidi na Iran ambaye amefanya kazi na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika masuala yanayohusiana na Mashariki ya Kati. .

"Tunaona Ukraine msisitizo kwamba uvamizi huu wa Urusi lazima ukome kabisa. Hata hivyo, huko Israeli, "kinyume chake kuna uungwaji mkono fulani wa kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina," anasema Parsi.

Tangu mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia, Israel imepokea rasilimali nyingi zaidi kutoka Marekani. Kati ya mwaka 1946 na 2023, dola za Marekani bilioni 260 (sawa na zaidi ya dola trilioni 1.3) zimepelekwa Israel - kulingana na ripoti ya Bunge la Marekani iliyochapishwa Machi mwaka huu. Zaidi ya nusu ya kiasi hiki kilipelekwa kama msaada wa kijeshi.’’

‘Balozi mmoja wa Brazil anasema kuna mkanganyiko wa dhahiri katika msimamo wa Marekani kati ya Israeli na Ukraine, kulingana na Parsi.

Brazil imekuwa ikijaribu, tangu Hamas iliposhambulia Israel, kuidhinisha tamko la kusitishwa kwa mzozo huo. Kwa upande mmoja, Marekani inaonekana haiko tayari kuidhinisha jambo lolote ambalo.

"Ninaamini kuwa undumilakuwili umeidhoofisha Marekani katika uga wa kimataifa. Urusi tayari imeashiria kutotambua hatua ya Israel ya kulitwaa eneo la Golan (linalozozaniwa la Syria) kama mfano kwamba Marekani inapinga unyakuzi wa Ukraine si kwa msingi wa kanuni, bali kwa msingi wa siasa za kijiografia," anasema Stephen Zunes, profesa wa siasa na mwanzilishi wa Kituo cha Mafunzo ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha San Francisco huko California.

"Ni muhimu sana kwa uaminifu wa Marekani kwamba tuchukue upinzani thabiti wa upanuzi haramu wa Eneo, sio tu wakati unafanywa na nchi ambazo hatuzipendi, kama vile (Vladimir) Putin. Urusi au Iraq ya Saddam (Hussein), lakini hata wakati washirika wetu, kama Israeli, wanaposhiriki katika vitendo kama hivyo."

Kutakuwa na shinikizo?

cv

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/SHUTTERSTOCK

Maelezo ya picha, Marekani imekuwa ikikwepa kulaani makaazi ya walowezi ya Israel huko West Bank na Jerusalem

Wataalamu wanaeleza - wakati mzozo huo unavyoendelea, shinikizo la ndani na la kimataifa juu ya msimamo wa Marekani juu ya uhalifu wa kivita wa Israel huenda ukaongezeka.

"Ni sawa, mataifa mengi yameshtushwa na mashambulizi ya Hamas na yamejiunga na Marekani katika kulaani Hamas bila masharti na kuiunga mkono Israel katika wakati wake wa uhitaji. Lakini ninahofia kutakuwa na vita vya ardhini vibaya katika Ukanda wa Gaza, pamoja na mashambulizi makubwa ya mabomu ambayo yatasababisha vifo vya maelfu ya raia.

Iwapo Marekani itakataa kulaani hilo, nadhani hilo litaumiza sana sura ya Marekani kwa sababu itaonyesha kwamba Marekani sio tu ina undumilakuwili kuhusiana na suala hilo la uvamizi wa maeneo na unyakuzi, lakini pia katika suala la maisha ya raia, na itaonekana ina ubaguzi," anasema Zunes.

‘Kwa mujibu wa sheria ya kimataifa, vitendo vinavyosababisha vifo vingi vya raia, hata katika mashambulizi ya kukabiliana, vinachukuliwa kuwa uhalifu wa kivita,’’ anaeleza profesa wa Stanford.

"Ulimwengu unaihurumia Israeli kwa sababu ya mashambulizi mabaya ambayo imekumbana nayo, lakini nadhani hilo linaweza kubadilika kama kutakuwa na mateso mengi huko Gaza," anasema Weiner.

"Pengine Marekani ina fursa mpya ya kuleta mazungumzo ya amani. Hakuna nchi ambayo ina uwezo wa kuzileta pande zote pamoja kwa jinsi Marekani inavyofanya, hasa kwa sababu ndiyo nchi pekee ambayo ina ushawishi kwa Israel," anasema Weiner.