Jinsi mzozo wa Israel na Hamas unavyoathiri vita vya Ukraine dhidi ya Urusi

Chanzo cha picha, EPA
Mzozo wa kivita kati ya Israel na Hamas, ambao umedumu kwa takriban wiki moja, umeondoa hisia za walimwengu katika uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine. Lakini hatari zaidi kwa Kyiv ni kwamba vita Mashariki ya Kati vinaweza kuchukua rasilimali za washirika wake wa Magharibi.
"Israel inakabiliwa na kitishio. Ufadhili wowote kwa Ukraine lazima uelekezwe haraka kwa Israel,” amesema Seneta wa Missouri, Josh Gawley, kutoka chama cha Republican, Oktoba 9.
Habari kwamba uungaji mkono wa Magharibi kwa Kyiv utapungua kutokana na mzozo wa Israel - utawala wa Joe Biden na Pentagon umekanusha.
"Tunakataa vikali wazo kwamba Marekani haiwezi kuunga mkono kwa wakati mmoja watu wanaopenda uhuru wa Ukraine na kuunga mkono taifa la Israel," alisema msemaji wa masuala ya usalama katika serikali ya Biden, bwana Jake Sullivan.
Mchana wa Oktoba 11, Marekani ilitangaza kutenga mfuko mwingine wa msaada wa kijeshi kwa Ukraine wa dola milioni 200. Siku hiyo hiyo, ndege iliwasili nchini Israel ikiwa na msaada wa kijeshi wa Marekani, silaha ambazo Ikulu ya Marekani iliahidi kutoa kwa ombi la serikali ya Israel baada ya shambulio la Hamas.
"Tunaunga mkono na kushiriki utayari wa Marekani na nchi nyingine zote kusaidia Israel katika matatizo haya," anasema Oksana Markarova, balozi wa sasa wa Ukraine huko Washington.
Lakini swali linabaki: nini kitatokea ikiwa makabiliano ya sasa nchini Israeli yatageuka kuwa mzozo wa muda mrefu kama vita vya Ukraine?
Silaha zitatosha?

Chanzo cha picha, Getty Images
‘Kauli kwamba Israel ina nguvu kubwa sana za kijeshi ni dhana potofu,’ anasema mtaalamu wa masuala ya ulinzi, Ivan Kirichevsky.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Anasema kwa mfano, uzalishaji wa vifaru vya kivita vya Israeli, vya Merkava yenye mfumo wa ulinzi, havikufanya vizuri vifaru hivyo katika uwanja wa mapigano.
Hata mfumo wa ulinzi wa anga wa Iron Dome, ni zao la ushirikiano na wakandarasi wa Marekani. Kwa hivyo, ikiwa ni operesheni ya muda mrefu ya ulinzi wa anga, Israeli inahitaji msaada wa Mrekani na makombora na vifaa, mtaalamu huyo anasema.
Israel kwa sasa inafanya zaidi mashambulizi ya anga kwenye Ukanda wa Gaza. Makombora mbayo ni maendeleo ya Marekani. Aina ya makombora yanayotumiwa Israel ndio pia yanayotumiwa na Ukraine.
Ndege kuu ya Jeshi la Anga la Israeli ni F-16 ya Marekani, Kirichevsky anabainisha. Na hii ndio aina ya ndege ambayo washirika wa Magharibi waliahidi kutoa kwa Kyiv.
“Tunapozungumzia mgogoro wa muda mrefu, suala la kukarabati na kurejesha ndege litaibuka. Licha ya kauli za kuisifu Israel lakini haijui kutengeneza ndege zenyewe.’’
Pia anaeleza uwezekano wa uhaba wa silaha nchini Israeli kwa askari wa akiba laki tatu walioandikishwa jeshini. Hapa unaweza pia kuhitaji msaada wa washirika wako.
‘’Katika miaka ya hivi karibuni jeshi la Israel limepigana tu na "makundi ya wapiganaji wenye silaha duni," Igor Semivolos, mkurugenzi wa Kituo cha Ukraine kwa tafiti za Mashariki ya Kati anasema.
''Ikiwa mzozo huo utaendelea, ikiwa pande zingine, haswa Iran, zitaingia, basi mahitaji ya Israeli ya usaidizi yataongezeka sana. "Ingawa, kwa sasa, ninakadiria uwezekano Iran kuingia moja kwa moja kwenye mzozo ni chini ya 50%," mtaalam huyo anabainisha.
Ili kuzuia nchi au makundi mengine kuingilia mzozo huo, Marekani ilipeleka meli zake za kivita zinazobeba ndege katika Bahari ya Mediterania karibu na mwambao wa Israeli.
Kuna fedha za kutosha?

Chanzo cha picha, EPA
Aina mbalimbali za silaha ambazo Marekani hutoa kwa Ukraine na ambazo inaweza kuzituma Israeli zinalingana," anasema balozi wa zamani wa Ukraine huko Washington, Valeriy Chaly.
Anakiri hali hiyo itakuwa na athari katika mchakato wa kufanya maamuzi ya kifedha nchini Marekani kwa usaidizi wa kijeshi kwa Ukraine na Israel.
Pentagon mnamo Oktoba 9 iliitaka Congress kutoa ufadhili wa ziada ili Marekani iweze kutoa msaada wa kijeshi unaohitajika kwa nchi hizo mbili kwa wakati mmoja.
Hata hivyo, hilo halitafanyika kwa haraka, kwani Baraza la Wawakilishi limevurugika baada ya kutimuliwa kwa Spika Kevin McCarthy Oktoba 3.
"Kilicho muhimu juu ya suala la silaha na uwezo wetu wa kusaidia Waisraeli na Waukraine kwa wakati mmoja, ni ufadhili wa ziada kutoka kwa Congress ili kuongeza uwezo wetu na kuongeza uzalishaji," alisema Waziri wa Jeshi la Marekani Christine Wormuth.
Lakini kulingana na Washington Post, utawala wa Biden unaweza kuchanganya ufadhili kwa Ukraine na Israeli katika ombi moja kwa Congress.
Faida kwa Urusi

Chanzo cha picha, REUTERS
Rais Vladimir Zelensky anadai Urusi ndio ilihusika na shambulio la wanamgambo wa Hamas kwenye makazi ya Waisraeli karibu na Ukanda wa Gaza.
"Urusi, kwa njia moja au nyingine, inaunga mkono operesheni ambazo Hamas inaendesha nchini Israel. Hili ni dhahiri kwa idara zetu za kijasusi,” rais huyo alisema katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa 2.
“Tuna ushahidi Urusi inawezesha operesheni fulani za kigaidi. Hii si mara yake ya kwanza kufanya hivi. Ilifanya huko Syria na Ukraine.’’
Wakati huo huo, chaneli za telegram za Urusi zinazounga mkono vita na wanablogu walianza kusambaza habari kwamba Hamas wanapigana kwa silaha ambazo washirika wa Magharibi walizipeleka Ukraine.
Rais wa zamani wa Urusi, na sasa Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama, Dmitry Medvedev, naye aliandika katika chaneli yake ya Telegraph.
Lakini wote hawakutoa ushahidi na mamlaka ya Israeli ilikanusha habari hii.
Kurugenzi ya Ujasusi ya Wizara ya Ulinzi ya Ukraine ilisema kwamba Urusi tayari imehamishia wanamgambo wa Hamas vifaa vilivyotekwa wakati wa mapigano huko Ukraine, vilivyotengenezwa nchini Marekani na nchi za Ulaya.
"Hatua inayofuata, kulingana na mpango wa Warusi, inapaswa kuwa shutuma za uwongo dhidi ya jeshi la Ukraine kwa madai ya kuuza silaha za Magharibi kwa magaidi," idara hiyo ilisema katika taarifa.
Balozi wa zamani Valery Chaly anasema hii ni operesheni ya kisaikolojia ya Warusi, ambayo imeundwa kwa watazamaji wa Magharibi. Ukraine lazima kukabiliana nayo, kupitia mbinu za kidiplomasia.














