Je, kuna hatari Israel kukabiliana na vita katika pande zote za mipaka?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kusini mwa Lebanon kumeshuhudiwa kuongezeka kwa shughuli za kijeshi sanjari na Vita vya Gaza vikiendelea. Jeshi la Israel na kundi la Hezbollah la Lebanon zimeshambuliana tangu kuanza kwa mashambulizi ya Hamas kwenye maeneo ya Israel nje ya Ukanda wa Gaza, Oktoba 7 mwaka huu.
Hezbollah iliomboleza kuuawa kwa wanachama wake watatu, na Israel ikatangaza kuuawa kwa maafisa watatu wa jeshi wakati wa kurushiana risasi kwenye mpaka na Lebanon.
Jana jioni kulishuhudiwa kurushwa kwa makombora kutoka ardhi ya Syria kwa mara ya kwanza katika vita hivi, kulingana na na maelezo ya Israel.
Kamanda wa Brigedi ya Al-Qassam - tawi la kijeshi la vuguvugu la Hamas - Muhammad Al-Deif, alitoa wito katika taarifa ya kwanza kufuatia kuanza kwa Operesheni ya "Mafuriko ya Al-Aqsa" kwa yeyote anayemiliki bunduki kuitoa.
Alisema: "Enyi ndugu zetu katika mapambano huko Lebanon, Syria, Iraq na Iran, hii ndiyo siku ambayo pande zote zitaungana."
Mazoezi ya Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
Juni mwaka huu, jeshi la Israeli lilifanya mafunzo na mazoezi ya ikiwa makabiliano yatazuka katika eneo zaidi ya moja. Kando na mazoezi haya, Waziri wa Ulinzi wa Israeli, Yoav Galant alitembelea kikosi cha kijeshi cha Kamandi ya Home Front.
Gallant alisema ikiwa vita vipya vitazuka, Israeli itakabiliwa na changamoto ambazo hazijaonekana kwa miaka 75."
Hapo awali alikuwa ameonya katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mwezi Aprili kwamba huenda Israel itashuhudia mizozo katika mpaka zaidi ya mmoja katika siku za usoni.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kisha akawaambia waandishi wa habari: “Huu ndio mwisho wa enzi ya mzozo mmoja mpakani. Tunakabiliwa na enzi mpya ya usalama ambapo kunaweza kuwa na tishio la kweli kwa mipaka yote kwa wakati mmoja.
Jeshi la Israel lilisema: "Vikosi vitafunzwa kukabiliana na changamoto na matukio ya ghafla katika nyanja nyingi kwa wakati mmoja,’ kulingana na gazeti la Times of Israel.
Wajumbe wa baraza la mawaziri la usalama la Israel walishiriki katika mafunzo hayo, wakifanya mikutano katika Kamandi ya Operesheni na kufanya tathmini katika makao makuu ya jeshi.
Gazeti hilo limemnukuu Netanyahu akisema katika moja ya vikao hivyo: “Israel imejizatiti kufanya kazi dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran, dhidi ya mashambulizi ya makombora kwa Taifa la Israel, na dhidi ya uwezekano wa zaidi ya adui mmoja kuja pamoja, haya ni mazoezi ya kupambana na adui zaidi ya mmoja."
Netanyahu alisema: "Tuna uhakika kwamba tunaweza kukabiliana na tishio lolote sisi wenyewe."
Hii si mara ya kwanza kwa jeshi la Israel kufanya mazoezi yanayoiga vita hivi. Vitengo vyake vilifanya mazoezi makubwa mwaka jana, vikizingatia matukio ya ghafla, ya wakati mmoja katika kumbi nyingi za sinema, kulingana na Times of Israel.
"Kitengo cha mraba"

Chanzo cha picha, REUTERS
Neno "kitengo cha mraba" linatumiwa na vyombo vya habari vilivyo karibu na Hezbollah, Hamas, na Islamic Jihad. Limezidi kutumiwa baada ya mkutano wa mwisho wa pande tatu kati ya Hezbollah, Hamas, na Islamic Jihad Septemba 2.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, Nasrallah aliwapokea mjini Beirut kiongozi wa Hamas, Saleh Al-Arouri na Nakhalah, Katibu Mkuu wa Islamic Jihad, kujadili hali ya Palestina, hasa makabiliano ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na kutilia mkazo kuendelea kwa ushirikiano.
Vyombo vya habari vilivyo karibu na Hezbollah na Iran viliutaja mkutano huu kama uthibitisho wa kanuni ya "umoja" miongoni mwa makundi yanayopigana na Israel katika nyanja mbalimbali.
Nazih Mansour, mwakilishi wa zamani wa kambi ya "Upinzani" ambayo inawakilisha Hezbollah katika Bunge la Lebanon, alisema kwenye tovuti ya "Al-Alam" ya Iran - mkutano huo "unaonyesha umoja wao sio wa maneno matupu. ”
Idhaa ya Al-Mayadeen, iliripoti habari ya mkutano wa Katibu Mkuu wa Islamic Jihad, Ziad Nakhalah, na Nasrallah Agosti 2022 huko Beirut chini ya kichwa, "Bwana Nasrallah anampokea Nakhalah na kujadiliana umoja katika medani za vita."
Katika hotuba yake kwa mnasaba wa "Siku ya Jerusalem" mwezi Aprili mwaka huu, Nasrallah alisema: "Matendo ya Israel huko Palestina, Lebanon na Syria yanaweza kuliingiza eneo hilo kwenye vita vikubwa."
Aliongeza, "Vita vyovyote vikubwa vitajumuisha mipaka yote, na maeneo na uwanja utajazwa maelfu ya wapiganaji."
Siku moja baada ya kuanza kwa shambulio la Hamas, kundi la Hezbollah ilitangaza kulipua maeneo ya jeshi la Israeli katika Mashamba ya Shebaa kusini mwa Lebanon.
Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano wa wafuasi siku hiyo, Hashem Safi al-Din, mkuu wa Halmashauri Kuu ya chama, alisema, "Gaza haiko peke yake."
Kuna vita vya Pamoja vinakuja?

Chanzo cha picha, REUTERS
Mbali na pande zinazojulikana za mapigano zinazoongozwa na Hamas kutoka Ukanda wa Gaza na Hezbollah kutoka kusini mwa Lebanon, wachambuzi wanazungumzia pande mpya zinaweza kujumuisha Syria na mikoa ya Ukingo wa Magharibi.
Kituo cha Mafunzo ya Palestina kilichapisha utafiti uliotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Kitaifa ya Israeli, Aprili 2022. Ripoti hiyo inazungumzia juu ya "uwanja wa vita wenye pande nyingi."
Ripoti hiyo ilitaja maeneo ya makabiliano kutoka Jerusalem na Negev, pamoja na ndani ya Israel, Ukingo wa Magharibi, Gaza, na kusini mwa Lebanon.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Udi Dekel, alitoa maoni yake kuhusu ripoti hiyo kwa kusema, "Tishio kubwa zaidi lililopo ni vita ambavyo vinaweza kuzuka kaskazini na mashariki, mbele ya muungano unaoongozwa na Iran, kwa ushiriki wa Hezbollah na Syria na vuguvugu linaloshirikiana na Iran, pamoja na makundi ambavyo yatashambulia kutoka magharibi mwa Iraq."
Hii ni mara ya kwanza kuwepo kwa tishio kuhusu hatua ya Iraq dhidi ya Israel, na kinachomaanishwa hapa ni ushiriki wa makundi yenye silaha yanayoitii Iran.
Haya ndiyo aliyoyasema mwandishi wa Israel Ben Caspit katika makala yake kwenye tovuti ya “Al-Monitor” ya Marekani, akizungumzia kauli za Yoav Gallant kuhusiana na suala hili na kusema:
"Tishio dhidi ya Israel le, sio kama ule uvamizi wa milima ya Golan mnamo 1973 na makombora yaliyofika Bahari ya Galilaya, wala tishio la vikosi vya Misri kuvuka Mfereji wa Suez ili kuweka daraja la kufikia maeneo yanayodhibitiwa na Israeli.”
Caspit aliendelea, akisema kuwa tishio liko katika "silaha kubwa ikijumuisha maelfu ya makombora yaliyohifadhiwa na Hezbollah, Iran, Hamas, Islamic Jihad, na wanamgambo wanaounga mkono Irani huko Syria na Iraq; wote wana lengo moja dhidi ya Israeli."
Ripoti iliyotolewa 2018 na Taasisi ya Mafunzo ya Washington, inaeleza uwezekano wa kutokea kwa vita "kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea - kama matokeo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, ambavyo viliiwezesha Iran kujenga miundombinu ya kijeshi nchini Syria na kupeleka 'kikosi chake cha kigeni' cha Shia katika mipaka ya Israeli."
Ripoti hiyo ilitaja kauli ya kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Ali Jafari, mwezi Novemba 2017, aliposema, "mapambano yanaunganishwa na kila mtu atasimama kwa pamoja, na ikiwa Israel itashambulia upande wowote, upande mwingine wa mbele utakuja kusaidia.”













