Kwa nini Gaza ni tatizo la mara kwa mara kwa Israel?

v

Chanzo cha picha, Reuters

Shambulio hilo lililoanzishwa na vuguvugu la Hamas dhidi ya Israel liliufanya Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na harakati hiyo kurudi tena katikati mwa mzozo wa Palestina na Israel.

Pia ilikumbusha historia ndefu ya mzozo kati ya Israel kwa upande mmoja na vuguvugu la Hamas hasa na makundi mengine ya Wapalestina huko Gaza kwa ujumla.

Kwa hivyo ni nini kinachofanya Gaza kuwa shida ya kudumu kwa Israel?

Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, Gaza ikawa sehemu ya Palestina chini ya Mamlaka ya Uingereza mwaka 1920, na Umoja wa Mataifa ulipotoa mpango wa kugawa ardhi hizo katika mataifa mawili ya Kiarabu na Kiyahudi mwaka 1947, uliiongeza kwa taifa lililopendekezwa la Palestina, lakini majeshi ya Misri yaliingia katika jiji hilo mwaka wa 1948.

Mnamo Februari 1949,Misri na Israel zilitia saini makubaliano ambayo Misri iliuweka mji huo na ukabaki chini ya utawala wa Misri hadi vita vya 1967.

Misri haikunyakua mji na ardhi bali iliyasimamia kupitia kwa gavana wa kijeshi.

Mnamo Novemba 1965, Uingereza, Ufaransa na Israel zilishambulia Misri (uchokozi wa pande tatu, au vita vya 1956, kama inavyojulikana katika Misri na nchi za Kiarabu, au mgogoro wa Suez, kama unavyojulikana Magharibi, au Kampeni ya Sinai, kama inavyojulikana nchini Israeli), na vikosi vya Israel vilidhibiti Gaza na viunga vyake.

Lakini shinikizo la kimataifa hivi karibuni liliilazimisha Israel kujiondoa.

Baada ya Israel kuikalia tena Gaza katika Vita vya Siku Sita mnamo Juni 1967 (inayojulikana kwa Misri na nchi za Kiarabu kama Naksa), jiji hilo lilibaki chini ya utawala wa kijeshi wa Israeli hadi 1994, wakati uhamisho wa taratibu wa mamlaka ya serikali kwa Wapalestina ulipoanza.

Mwaka 2005, Israel ilikamilisha kujiondoa katika Ukanda wa Gaza na kukabidhi udhibiti wa eneo hilo kwa Wapalestina.

Lakini Gaza daima imekuwa ikiwakilisha tatizo na mzigo kwa Israel. Makundi katika Ukanda huo hayajaacha kufanya mashambulizi, na hakuna makubaliano kati ya Mamlaka ya Palestina na Israel ambayo yamezuia mashambulizi haya kutokea.

Mwandishi wa habari kutoka London Ahmed Isfahani anasema: “Tangu mwanzo, Israel ilijaribu kila njia kuitiisha Gaza.

Suluhu la kijeshi halikuzaa matunda, na kuzingirwa na vikwazo vya kiuchumi havikusaidia katika kuwezesha Israel kuidhibiti.”

Al-Qassam Brigedi, tawi la kijeshi la Hamas

Chanzo cha picha, Reuters

Hamas na mapigano yanayoendelea

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Pengine kuanzishwa kwa vuguvugu la Hamas tarehe 6 Disemba 1987 ilikuwa ni hatua ya mabadiliko ambayo ilibadilisha mkondo wa matukio huko Gaza.

Vuguvugu hilo lilitangaza taarifa yake ya kuanzishwa mnamo Desemba 15, 1987, wakati wa intifada ya kwanza yaani (uasi wa Wapalestina dhidi ya utawala wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza).

Wakazi wa Mji wa Gaza walihusika mapema katika uasi wa kwanza ya Wapalestina. Uongozi wa umoja wa kitaifa wa intifada ulikuwa ukisambaza taarifa za kila wiki katika mitaa ya Gaza na ratiba ya mgomo inayoendana na maandamano ya kila siku dhidi ya doria za Israel katika mji huo.

Mwandishi Hassan Abu Haniyeh, mtaalamu aliyebobea katika makundi ya Kiislamu, anasema: “Gaza daima imekuwa na upekee kwamba wengi wa viongozi wa kihistoria, wawe ndani ya mfumo wa harakati za kitaifa au hata harakati za Kiislamu, waliundwa mjini humo.

Wakati wa maandamano, matairi yalichomwa barabarani, na umati wa watu uliwarushia mawe na vinywaji vya Molotov askari wa Israel.

Jeshi la Israel lilijibu kwa mabomu ya machozi na risasi za mpira, lilifunga shule katika mji wa Gaza, likakamata watu, likaweka amri ya kutotoka nje, na kupiga marufuku kusafiri, jambo ambalo Wapalestina waliona kuwa ni adhabu ya pamoja.

Yitzhak Rabin na harakati za kutafuta amani

Rabin aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi katika serikali za muungano wa Labour-Likud kuanzia 1984 hadi 1990, ambapo alijibu vikali uasi wa Wapalestina (Intifadha ya Kwanza), lakini kushindwa kwa sera kali za kukandamiza uasi huo kulimsadikisha Rabin juu ya umuhimu wa kushughulika kisiasa na Wapalestina.

Aliporejea kushika wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 1992, Rabin alisimamisha ujenzi wa vitongoji vipya vya walowezi wa Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, na serikali yake ilifanya mazungumzo ya siri na Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina, na kuhitimisha kutiwa saini kwa Mkataba wa Oslo.

Shirika la Ukombozi wa Palestina (Septemba 1993), ambapo Israeli ilitambua lilikubali kutekeleza hatua kwa hatua utawala mdogo wa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.

Lakini vuguvugu la Hamas liliuchukulia mkataba wa Oslo kama "makubaliano batili na ya kutisha, kwani yaliipa Israel haki ya kutawala asilimia 78 ya ardhi ya Palestina ya kihistoria."

Vuguvugu hilo lilisema kwamba halitatii makubaliano hayo na likatangaza kuendelea na operesheni zake dhidi ya vikosi vya Israel, na kwa haraka likafanya mashambulizi ndani ya Israel, ikiwemo kulipua mabasi na mashambulizi kadhaa ya silaha.

Vyombo vya habari viliripoti wakati huo kwamba Gaza ilianzisha chuki kwa Rabin, ambaye alihisi kuwa ni kikwazo katika njia ya kufikia makubaliano yoyote ya suluhu, na kwamba alisema: "Natumai nitaamka siku moja na kukuta kwamba Gaza imezama. baharini.”

Mwandishi wa habari Ahmed Isfahani anasema: “Gaza kihistoria imewakilisha tatizo kubwa sana kwa Israeli. Licha ya uwezo wake wa kuendelea kukalia, gharama ni kubwa.

Wapiganaji wa Kipalestina wanazidi kuimarika, na msongamano wa watu huko hauleti matokeo mazuri kwa mustakabali wowote wa makazi.

Makubaliano ya Oslo II yalitiwa saini kwanza huko Taba kwenye Peninsula ya Sinai huko Misri na Israeli na Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina mnamo Septemba 24, 1995, na siku nne baadaye mnamo Septemba 28, 1995, na Waziri Mkuu wa Israeli Yitzhak Rabin na Mwenyekiti wa PLO Yasser Arafat na ushuhuda wa Rais wa Marekani Bill Clinton huko Washington, DC.

Makubaliano hayo ya eneo yalizua upinzani mkali miongoni mwa Waisraeli wengi, hasa walowezi katika Ukingo wa Magharibi.

Mnamo Novemba 1995, Rabin alihudhuria mkutano mkubwa wa amani huko Tel Aviv, uliofanyika ili kukusanya uungaji mkono wa makubaliano kati ya Israel na Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina, lakini mkutano huo uliisha kwa msiba Rabin alipouawa na Myahudi mwenye msimamo mkali.

Mwandishi Hassan Abu Haniyeh anasema: "Baada ya kutia saini Makubaliano ya Oslo, Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina iliacha kile kinachojulikana kama mapambano ya silaha na upinzani na kuanza kuelezea kama ugaidi na hivyo kuchukua njia ya amani na Israel, lakini Gaza iliendelea kuwa kitovu cha upinzani, matokeo ya kasi kubwa ya vuguvugu la muqawama, hasa harakati za Hamas na Islamic Jihad."

Kupeana mikono kwa kihistoria kati ya Yasser Arafat na Yitzhak Rabin mbele ya Bill Clinton

Chanzo cha picha, Getty Images

Sharon na kujiondoa kabisa kutoka Ukanda wa Gaza

Mnamo Septemba 27, 2000, kiongozi wa upinzani wa Israel wakati huo Ariel Sharo alitembelea Haram al-Sharif, au Hekalu la Mlima wa Wayahudi, chini ya ulinzi wa askari elfu mbili na vikosi maalum, na kwa idhini ya Waziri Mkuu wa wakati huo Ehud Barak. Ziara hiyo, ambayo Wapalestina waliiona kuwa ya uchochezi, ndiyo cheche iliyoanzisha intifadha ya pili.

Katika kipindi hicho, Hamas ilifanya operesheni kadhaa za ufanisi dhidi ya Israel, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya vikao vya Netanya, na mashambulizi dhidi ya vilabu vya usiku ndani ya Israel, ambayo yalisababisha kifo na kujeruhiwa kwa makumi ya Waisrael.

Israel ilijibu kwa mashambulizi ya anga kwenye Ukanda wa Gaza na kumuua kiongozi wa harakati hiyo, Salah Shehadeh. Mauaji yaliendelea katika miaka iliyofuata, yakimlenga mwanzilishi wa vuguvugu hilo, Sheikh Ahmed Yassin, na kiongozi, Ismail Al-Rantisi.

Lakini chaguo la kijeshi la Sharon, ambaye alikua waziri mkuu mwaka 2001, kwa lengo la kuitoa Hamas na kusimamisha intifadha, lilishindwa.

Hamas ilianza kuchimba mahandaki mapema mwaka 2003 na baadaye kuweza kujenga mtandao wa njia za chini ya ardhi, jambo ambalo lilikuwa tishio kubwa kwa jeshi la Israel, hasa kwa vile halikuweza kuyaangamiza, kwasababu ya kina chake kikubwa chini ya ardhi na ramani zake tata.

Kwa kuzingatia data hizi, chaguo bora kwa Israel ilionekana kuwa kujiondoa kabisa kutoka Gaza, ambayo ilifanyika mnamo 2005.

Nia ya Sharon, katika awamu ya mwisho ya kazi yake, kukubali aina fulani ya taifa la Palestina na kuamuru Israel iondoke Gaza licha ya upinzani kutoka kwa wafuasi wake wengi wa zamani bila shaka inaweza kuonekana kama mabadiliko makubwa, ingawa wakosoaji wengine wameonesha ni zaidi kama fursa ya kimbinu kuliko... kuakisi mabadiliko ya msingi katika mtazamo.

Mwandishi wa habari Ahmed Isfahani anasema: “Fikra za wakati huo ni kwamba kujiondoa Gaza ilikuwa ni hatua ya kimkakati, kwani ingeweza kuhakikisha Gaza inazingirwa kutoka baharini kwa upande mmoja na kutoka kwenye mipaka ya Misri, ambayo ina mikataba ya amani na Israel.

Kwa upande mwingine, pamoja na kuwepo kwa baadhi ya mambo ya ndani huko Gaza ambayo inaweza kushirikiana na Israel na kuratibu nayo kiusalama, na kwa hiyo dau lilikuwa juu ya vipengele viwili:

La kwanza ni uwepo wa Misri wenye ushawishi kutokana na ushirikiano wa kiusalama na kijasusi na Israel, na kipengele cha pili ni uwepo wa makundi yenye mafungamano na Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Lakini inaonekana kwamba hesabu hizo hazikuwepo, kwani Hamas iliweza kupata madaraka. Huko Gaza, baada ya uchaguzi wa wabunge ambapo ilipata ushindi wa kishindo, vipengele vya mamlaka havikuwepo tena katika Ukanda huo.

Hamas ilipata kura nyingi katika uchaguzi wa wabunge katika Ukanda wa Gaza mwaka 2006, ambao ulikataliwa na Marekani na Mamlaka ya Palestina, na walitaka harakati hiyo iachane na upinzani na kuitambua Israel.

Baada ya hapo, makabiliano yalitokea kati ya Hamas na Mamlaka ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, ambayo yalisababisha kufukuzwa kwa wanachama wa Mamlaka hiyo, na harakati hiyo ikachukua udhibiti kamili wa Ukanda wa Gaza.

Mwandishi Hassan Abu Haniyeh anaeleza: “Tangu Hamas ilipochukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza, nguvu zake na nguvu za Jihad ya Kiislamu zimeongezeka.

Pia wamekuwa sehemu ya vuguvugu la kieneo lenye uhusiano na Iran, Hizbullah ya Lebanon na Syria katika kile kinachoitwa mhimili wa upinzani, na hivyo Gaza imekuwa eneo la incubator.

Mnamo 2008, Hamas ilirusha roketi kadhaa kwenye makazi ya karibu ya Israel. Israel ilijibu kwa kuanzisha mashambulizi makubwa kwenye Ukanda wa Gaza, na kusababisha vifo vya Waisraeli 13 na Wapalestina 1,400.

Hamas ilianza kukuza uwezo wake wa makombora, na kuitumia kama silaha ya kuzuia dhidi ya Israel.

Mnamo 2014, Israel ilianzisha operesheni nyingine dhidi ya Ukanda wa Gaza, na Hamas ilijibu kwa makombora. Makabiliano hayo yaliendelea kwa muda wa siku saba na kusababisha vifo vya Waisraeli 73 wakiwemo wanajeshi 67 na zaidi ya Wapalestina elfu mbili.