Iron Dome: Je, mfumo wa ulinzi wa Israel unafanyaje kazi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ghasia nchini Israel na Gaza katika muda wa siku mbili zilizopita zimeleta picha za makabiliano yakiendelea angani.
Jeshi la Israel linasema roketi 3,000 zilirushwa katika muda wa siku mbili zilizopita kutoka Ukanda wa Gaza kuelekea eneo la Israel, pamoja na operesheni kadhaa za kujipenyeza katika ardhi ya Israel.
Makombora matatu kati ya hayo, yaliyorushwa na Kikosi cha Al-Qassam kutoka Ukanda wa Gaza, yaliangukia maeneo mbalimbali katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Lakini takriban asilimia 90 ya makombora haya yalinaswa na mfumo wa ulinzi wa Iron Dome, kulingana na jeshi la Israel.
Iron Dome iliundwa mahsusi kuilinda Israeli dhidi mashambulizi ya masafa mafupi.
Kwanini Israel iliunda Iron Dome?

Chanzo cha picha, AFP
Sababu ya mfumo huu wa ulinzi, inaanzia kwenye vita ambavyo Israel ilipigana na Hezbollah ya Lebanon mwaka 2006, maelfu ya makombora yalirushwa Israel, na kusababisha uharibifu mkubwa, uhamishaji wa watu wengi, na vifo.
Baada ya hapo, Israel ilisema itatengeneza ulinzi wa kujikinga na makombora.
Kampuni ya Israeli ya Rafael Advanced Defence Systems na Israel Aerospace Industries zilianzishwa kwa usaidizi wa Marekani.
Aprili 2010, kampuni ya serikali ya Israeli ya Rafael Advanced Defence Systems Ltd. ilifichua kwamba imetengeneza mfumo iliouita "Iron Dome" ambao unaweza kunasa roketi za masafa mafupi za Katyusha, ambazo Hezbollah iliifyatulia wakati wa vita vya 2006.
Mfumo wa Iron Dome uliwekwa wakati wa majira ya joto ya 2011 karibu na Ukanda wa Gaza, ambapo Hamas ilirusha makumi ya roketi za Katyusha kwa Israeli.
Baadaye mfumo zaidi ulitumwa karibu na miji ya Ashkeloni na Ashdodi, kusini mwa Tel Aviv na karibu na jiji la Netivot, kilomita 20 kutoka mpaka wa Gaza.
Iron Dome hufanya kazi kwa kufuatilia makombora ya masafa mafupi kwa kutumia rada, kisha huchambua eneo kombora litaanguka, kabla ya kutathmini ikiwa kitengo cha kurusha kombora kinapaswa kuyazuia.
Kila mfumo una rada ya kutambua na kufuatilia, mifumo mitatu ya kushambulia, kila mfumo mmoja unabeba makombora ishirini.
Marekani ni mfadhili mkubwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Februari 2019, Jeshi la Marekani lilitangaza mipango ya kununua na kujaribu mfumo wa Iron Dome wa Israeli.
Marekani imetoa msaada mkubwa kwa ajili ya maendeleo na uzalishaji wa mfumo huo, na baadhi ya nyenzo zake zinatoka katika makampuni ya Marekani.
Iron Dome inaelezwa kuwa ni mifumo wa hali ya juu zaidi wa ulinzi duniani, hutumia rada kutambua vitisho na kuviharibu kabla ya kusababisha uharibifu wowote.
Ni vyema kutambua kwamba mfumo huu, ambao ulihitaji mabilioni ya dola kuundwa, unakabiliwa na upinzani kwa sababu ya gharama yake.
Licha ya gharama kubwa, viongozi wa Israel walisema katika ripoti iliyochapishwa na Reuters mwaka 2014 kwamba kuepuka uharibifu wa roketi kwa kutumia Iron Dome, kunapunguza shinikizo la ndani la kutaka kuongezeka kwa mashambulizi ya anga Gaza na kufanya uvamizi wa ardhi.
2014, maafisa wa Israeli walionya juu ya kile walichokiita "utalii wa Iron Dome," wakimaanisha uhakikisho kuhusu utendakazi wa mfumo huo unawafanya Waisraeli wafuatilie makombora badala ya kutafuta pakujificha.
Hamas iliwezaje kuipenya Iron Dome 2021?

Chanzo cha picha, REUTERS
Gazeti la Uingereza The Telegraph lilichapisha ripoti Mei 2021 yenye kichwa: "Jinsi Hamas walivyoupenya ulinzi wa Iron Dome wa Israeli," iliyoandikwa na mwandishi wake wa Mashariki ya Kati, Campbell MacDiarmid, na mwandishi, James Rothwell, kutoka Tel Aviv.
Gazeti hilo lilitaja maswali yanayoikabili jeshi la Israel kuhusu iwapo Iron Dome ilihitaji kuboreshwa, baada ya raia watano wa Israel kuuawa katika mashambulizi ya makombora.
Gazeti lilidokeza kuwa mfumo huo, ambao maafisa wa Israel wanasema una kiwango cha ufanisi cha asilimia 90, tayari umeiokoa Israeli na vifo vingi.
Lakini wachambuzi wa Israel walisema “vyanzo vya kijasusi vilionya kwamba Hamas ilikuwa imeboresha silaha zake na kwamba huenda zingepenya ngao ya Iron Dome,” kulingana na gazeti hilo.
Gazeti hilo lilimnukuu mchambuzi wa masuala ya kijasusi wa gazeti la Jerusalem Post, Yona Jeremy Pope, akisema kuwa, "Iron Dome ina udhaifu wake. Lakini alisisitiza kuwa hii haimaanishi kuwa Iron Dome haifai tena."
Brigedia Jenerali Mstaafu wa Israel, Amir Avivi alisema Iron Dome inafanya kazi kama ilivyokusudiwa: "Mfumo huo uliundwa kwa matukio makubwa zaidi." Aliongeza: "Iron Dome inaweza kushughulikia kiasi kikubwa cha makombora."
Msemaji wa jeshi la Israel Jonathan Conricus alisema, "Idadi ya vifo na majeruhi ingekuwa kubwa zaidi kama si mfumo wa Iron Dome."
Stephen Wagner, mhadhiri wa usalama wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Brunel huko London, anasema, "ingawa utendaji wa Iron Dome ni wa kushangaza. Silaha za Hamas ni rahisi na za bei nafuu na zinaweza kupenya mfumo wa ulinzi ambao mamilioni ya dola yalitumiwa, kwa ufadhili wa Marekani."
Udukuzi

Julai 2014, BBC ilipitia ushahidi uliothibitisha kwamba wadukuzi waliweza kunasa nyaraka kadhaa za siri za kijeshi kutoka kwa makampuni mawili ya serikali ya Israeli ambayo yalitengeneza Iron Dome.
Udukuzi huu uliripotiwa kwa mara ya kwanza kwenye tovuti ya usalama ya Brian Krebs, lakini kampuni zote mbili zilikanusha kuwa mitandao yao ilidukuliwa.
Hata hivyo, timu iliyogundua udukuzi huo iliwezesha BBC kupitia ripoti ya kijasusi iliyoonyesha kuwa mamia ya mafaili yalikuwa yamenakiliwa.
Cyber Engineering ESI ilifuatilia shughuli za wadukuzi katika kipindi cha miezi minane kati ya 2011 na 2012. Ilieleza kuwa taarifa ambazo wadukuzi walikuwa wakizifuata zinahusiana na Iron Dome.
Ripoti ya Cyber Engineering ESI, iliyotayarishwa mwaka wa 2013, ilionyesha kuwa mashambulizi hayo yalitokea kwa kutumia zana kama zile zinazotumiwa na wadukuzi wa China kupenya makampuni ya ulinzi ya Marekani, madai ambayo serikali ya China ilikana kuhusika.












