Mashambulizi ya Hamas Israel:Waathiriwa wa kimataifa wa shambulio dhidi ya Israel

Chanzo cha picha, EPA
Baadhi ya waliouawa wakati wa shambulio la kundi la wapiganaji wa Palestina Hamas dhidi ya Israel wanatoka ng'ambo. Haya ndiyo tunayojua kuhusu waathiriwa kufikia sasa:
Marekani
Raia tisa wa Marekani waliuawa , msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la nchi hiyo amesema.
"Tunatuma rambirambi zetu kwa waathiriwa na familia za wote walioathiriwa, na tunawatakia majeruhi ahueni ya haraka," walisema.
"Tunaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu na kuendelea kuwasiliana na washirika wetu wa Israel, hasa mamlaka za mitaa."
Vitambulisho vya waliouawa bado havijathibitishwa, huku idadi ikijulikana pia kupotea.
Miongoni mwao ni Hersh Golberg-Polin, raia wa Marekani na Israel ambaye hajawasiliana na yeyote tangu Jumamosi asubuhi.
Kulingana na gazeti la Jerusalem Post, alihama kutoka California hadi Israel pamoja na familia yake akiwa na umri wa miaka saba na alikuwa amemaliza huduma yake ya lazima jeshini mwezi wa Aprili.
Akizungumza na CBS, balozi wa Israel nchini Marekani, Michael Herzog, alisema anaelewa kuwa Wamarekani ni miongoni mwa mateka waliochukuliwa, ingawa hakuna idadi kamili ya ni wangapi.
Canada
Shirika la Global Affairs Canada, shirika la serikali ya Canada, limesema linafahamu taarifa za raia mmoja wa Kanada kuuawa na wengine wawili kutoweka.
Ben Mizrachi, kutoka British Columbia, ni miongoni mwao, Habari za CTV ziliripoti.
Bw Mizrachi alihitimu kutoka Shule ya Upili ya King David ya Vancouver miaka mitano iliyopita na amekuwa akihudhuria hafla moja kusini mwa Israeli, shule hiyo ilisema.
Shirika hilo lilisema kuna Wakanada 1,419 waliosajiliwa nchini Israel, na 492 katika maeneo ya Wapalestina ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza - lakini lilibainisha kuwa usajili huu ulikuwa wa hiari na kuna uwezekano ni idadi isiyo kamiliya raia wake.
Waziri Mkuu Justin Trudeau amezungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kutoa "rambirambi zake kubwa".
Kanada imewahimiza raia wake kujiandikisha na Global Affairs Canada na ina nambari ya mawasiliano ya dharura inayopatikana.
Uingereza

Chanzo cha picha, Familia
Afisa mmoja ameambia BBC kuwa zaidi ya raia 10 wa Uingereza wanahofiwa kufariki au kutoweka.
Nathanel Young, Muingereza anayehudumu katika jeshi la Israel, amethibitishwa kuuawa. Raia wengine wawili wa Uingereza - Jake Marlowe na Dan Darlington - wamethibitishwa kupotea.
Bw Marlowe alikuwa akilinda usalama katika tamasha la muziki kusini mwa nchi. Ameripotiwa kupotea.
Bernard Cohen, kutoka Glasgow, pia ametambuliwa na wanafamilia kwenye mitandao ya kijamii kuwa aliuawa katika shambulio hilo.
Shule ya kaskazini mwa London anayosoma Bw Young, ambaye alikuwa na umri wa miaka 20, "imehuzunishwa" na kifo chake, mwalimu mkuu alisema.
Alisoma katika shule moja - Shule ya Kiyahudi ya JFS ya London Kaskazini - kama Bw Marlowe mwenye umri wa miaka 26.
Waziri Mkuu Rishi Sunak alisema amemhakikishia mwenzake wa Israel Benjamin Netanyahu "uungwaji mkono thabiti wa Uingereza huku Israel ikijilinda".
Ufaransa
Mwanamke wa Ufaransa aliuawa na wengine kadhaa hawajulikani walipo, serikali ya Ufaransa ilisema Jumapili.
Mbunge anayewakilisha raia wa Ufaransa ng'ambo, Meyer Habib, alisema Jumatatu kwamba takriban watu wanane wa Ufaransa wameuawa, kukamatwa au kutoweka.
Mateka hao wanaweza kuwa ni pamoja na mwanamume mwenye umri wa miaka 26 kutoka Bordeaux ambaye alikuwa kwenye tamasha la Supernova kusini mwa Israeli , alisema.
Thailand
Raia 12 wa Thailand wameuawa na wengine 11 kutekwa nyara .
Raia wengine wanane wa Thailand wamejeruhiwa katika ghasia hizo tangu Jumamosi, wizara ya mambo ya nje ya Thailand ilisema.
Ilisema ndege za jeshi la anga ziko katika hali ya kusubiri kuwaleta raia wake nyumbani.
Kuna baadhi ya Wathai 30,000 nchini Israeli wanaofanya kazi katika kilimo, wengi karibu na mpaka wa Gaza.
Nepal
Nepal ilisema raia wake 10 wameuawa.
Nchi hiyo ilithibitisha Jumapili kwamba walikuwa wanafunzi ambao walikuwa wameenda Israeli kufanya kazi na kupata ujuzi katika kampuni ya kilimo.
Wanafunzi wa ziada 265 wa Kinepali pia wanafanya kazi katika mashamba mbalimbali, na Wanepali wengine 4,500 wanafanya kazi kama walezi.
Ujerumani
Mwanamke wa Kijerumani-Israel Shani Louk anaaminika kuchukuliwa kutoka kwenye tamasha la Supernova, na haijabainika ikiwa yu hai.
"Binti yangu, Shani Nicole Luke, raia wa Ujerumani, alitekwa nyara pamoja na kundi la watalii," alisema mamake Ricarda Louk, kwenye video kufuatia tukio hilo .

Chanzo cha picha, INSTAGRAM YA SHANI LOUK
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani pia ilisema inaamini Wajerumani walikuwa miongoni mwa wale waliotekwa nyara na Hamas, na kwamba inaamini watu hao pia walikuwa raia wa Israel .
Kambodia
Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hun Manet, amethibitisha kuwa mwanafunzi mmoja ameuawa.
China
Mwanamke wa Kichina aliyezaliwa Beijing anayeitwa Noa Argamani ni miongoni mwa wale waliochukuliwa kutoka kwenye tamasha la Supernova, kulingana na Ubalozi wa Israeli nchini China .
Ubalozi huo umechapisha video ya kile inachodai kuwa utekaji nyara huo.
Brazil
Watu watatu hawajulikani walipo na mmoja kujeruhiwa.
Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ilisema Jumapili kwamba raia watatu wa Brazil-Israeli walitoweka baada ya kuhudhuria tamasha la muziki na wa nne akitibiwa hospitalini.
Paraguay
Serikali ya nchi hiyo ilisema raia wake wawili wamepotea, bila kutoa maelezo zaidi. Kuna ripoti kwenye vyombo vya habari vya kitaifa kwamba wanandoa wameuawa.
Mexico
Waziri wa Mambo ya Nje Alicia Barcena aliandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba raia wawili wa Mexico wamechukuliwa mateka, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Ireland
Kim Danti, mwanamke wa uraia wa Ireland -Israel mwenye umri wa miaka 22, hajulikani aliko.
RTÉ, kituo cha kitaifa wa nchi hiyo, kinaripoti kwamba alionekana mara ya mwisho kwenye tamasha la muziki. Taoiseach Leo Varadkar alisema Ubalozi wa Ireland nchini ulikuwa unashughulikia.
Kuna timu ya kukabiliana na dharura ya Ireland na wananchi wanahimizwa kuwasiliana na ubalozi wa Tel Aviv.
Tanzania
Ubalozi wa Tanzania nchini Israel unajaribu kuwatafuta wanafunzi wawili wa Kitanzania waliokuwa kwenye mafunzo ya biashara.
Balozi Alex Kallua alisema ujumbe wake umekuwa ukiwasiliana na takriban Watanzania 350 kote nchini wengi wao wakiwa wanafunzi.












