Kwanini Poland imeamua kusitisha msaada wa silaha kwa Ukraine?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Poland imekuwa muungaji mkono wa Ukraine – nchi hiyo ilipovamiwa na Urusi. Lakini uhusiano kati ya majirani hao wawili umevurugika kutokana na mauzo ya nafaka nje ya nchi.
Kila kitu kilifanyika hadharani, wakati viongozi wa nchi hizo walipotumia jukwaa la makao makuu ya Umoja wa Mataifa kushambuliana.
Wakati akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa Poland, Andrzej Duda aliuliza, ni kwa namna gani Ukraine inashukuru kwa msaada wa kigeni na kuilinganisha nchi hiyo na mtu anayezama.
"Mtu anayezama ni hatari sana kwa sababu anaweza kukuzamisha na wewe. Anaweza kumzamisha mwokoaji," alisema.
Saa chache baadaye, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliijibu Poland, akisema inatisha kwamba baadhi ya marafiki wa Ukraine huko Ulaya wanaonyesha mshikamano 'katika ukumbi wa kisiasa tu.’
Poland ililaani maoni ya Zelensky na kutangaza kuwa itaacha kusambaza silaha kwa jirani huyo. Uamuzi unaoweza kuwa na madhara makubwa kwa juhudi za kukabiliana na Urusi.
Ni nini kilisababisha mzozo wa nafaka?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Ukraine ni mzalishaji mkubwa wa nafaka na vita hivyo vimesababisha uhaba wa nafaka duniani kote - huku njia za usafirishaji katika Bahari Nyeusi zikiwa zimetatizika kwa kiasi kikubwa.
Ukraine ilibidi kutafuta njia mbadala za ardhini, ambapo kiasi kikubwa cha nafaka kimekwenda Ulaya ya Kati, na kusababisha bei ya nafaka katika nchi za eneo hilo kushuka.
Ili kulinda wakulima wa ndani, Umoja wa Ulaya ulipiga marufuku kwa muda uagizaji wa nafaka katika nchi tano; Bulgaria, Hungary, Poland, Romania na Slovakia.
Marufuku ilipomalizika Septemba 15, umoja huo uliamua kutoirefusha, lakini Hungary, Slovakia na Poland bado ziliendeleza marufuku hiyo.
Ukraine ililipeleka suala hili katika Shirika la Biashara Duniani (WHO), kwani inaamini huu ni ukiukaji wa majukumu ya kimataifa. Lakini Poland ikasema itaendeleza marufuku hiyo.
Tume ya Ulaya inasema nchi moja moja hazina haki ya kuamua sera jumla za biashara. Lakini chama tawala nchini Poland kinataka kuonekana kama kinalinda kilimo cha ndani wakati nchi hiyo ikielekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 15.
Mpango wa nafaka wa Ukraine
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati jeshi la Putin lilipovamia Ukraine Februari 2022, jeshi la wanamaji la Urusi lilizishikilia bandari za Bahari Nyeusi za nchi hiyo, na kuzuia tani milioni 20 za nafaka ambazo zilipaswa kusafirishwa nje ya nchi.
Hii inasababisha bei ya vyakula duniani kuongezeka na kutishia kusababisha uhaba wa chakula katika nchi za Mashariki ya Kati na Afrika, ambazo huagiza chakula kutoka Ukraine.
Julai 2022, makubaliano yaliyosimamiwa na Uturuki na Umoja wa Mataifa - yalitiwa saini kati ya Urusi na Ukraine, kuruhusu meli za mizigo kusafiri kwenye ukanda wa Bahari Nyeusi. Ukanda huo una urefu wa maili 310 na upana wa maili 3.
Mkataba huu ulisaidia Ukraine kuuza nje karibu tani milioni 33 za nafaka. Kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa; makubaliano haya yamepunguza bei ya chakula duniani kwa karibu 20%.
Hata hivyo, tangu Urusi ilipojiondoa katika makubaliano hayo, bei ya nafaka duniani imeongezeka tena, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ya bei ya chakula.
Urusi inasema inaweza kutatua tatizo hilo. Alipokuwa akizungumza na viongozi wa Afrika Julai 2023, Rais Vladimir Putin aliahidi usafirishaji wa nafaka bila malipo kwa nchi sita za Afrika - Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Eritrea, Mali, Somalia na Zimbabwe - katika muda wa miezi minne ijayo.
Mapema mwezi huu, Putin alisema nafaka hizo zitaanza kupelekwa wiki chache zijazo.
Ni silaha gani zinazopelekwa Ukraine?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Poland na Ukraine zilirithi idadi kubwa ya silaha za zama za Soviet baada ya kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti.
Kwa sababu ya historia hiyo. Poland ilitoa silaha zake za zamani kwa Ukraine. Lakini silaha za jeshi la Poland zimepungua kwa takriban theluthi moja kutokana na kuhamishiwa Ukraine.
Nchi hiyo iliipa Ukraine vifaru 320 vya enzi ya Usovieti na ndege 14 za kivita za MiG-29 kama msaada. Na mzozo wa nafaka umefanya msaada wa silaha kwa siku zijazo kutokuwa na uhakika.
Msemaji wa Serikali ya Poland, Piotr Muller alisema itatuma tu shehena ambayo makubaliano tayari yalishafanyika - ikijumuisha usafirishaji ambao kandarasi zimeshatiwa saini na Ukraine.
Nchi gani zinazosambaza silaha kwa Ukraine?
Marekani inaongoza duniani katika juhudi za kuipatia Ukraine silaha - jumla ya misaada yenye thamani ya dola bilioni 46.
Imetoa vifaru, mizinga na virusha roketi, na kusema inaunga mkono uhamisho wa ndege za kisasa za kivita kwenda Ukraine kwa kuruhusu washirika wa Magharibi kusambaza F-16 zilizotengenezwa na Marekani.
Ujerumani, Uingereza, Norway na Denmark ndizo wafadhili wanaofuata wakubwa, huku Poland ikishika nafasi ya sita. Poland imetuma takriban dola bilioni 3.3 za msaada wa kijeshi kwa Ukraine ili kujilinda dhidi ya Urusi.
Imeipatia Ukraine vifaru vya Leopard 2 - na kuitaka Ujerumani kufanya vivyo hivyo - pamoja na kuahidi kuipatia nchi hiyo ndege za kivita na kuwakaribisha zaidi ya wakimbizi milioni 1.5 kutoka Ukraine.












