Jinsi Urusi inavyotengeneza uungwaji mkono Kusini mwa Ulimwengu na namna Ukraine inavyokabiliana na hilo

Urusi

Chanzo cha picha, getty Image

Tangu vita vya Ukraine vilipoanza, wanadiplomasia wanaoiwakilisha Urusi pia walianza kutembelea nchi za Afrika na Amerika ya Kusini wakiwa na wazo la kuongeza ushawishi wa Urusi duniani.

Mnamo 2023, maafisa wa Urusi walitembelea Angola, Burundi, Eritrea, Eswatini, Kenya, Mali, Mauritania, Afrika Kusini na Msumbiji, wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Sergey Lavrov, alitembelea baadhi ya nchi za Amerika Kusini kama vile Brazil, Venezuela, Nicaragua na Cuba.

Wazo lilikuwa ni kuimarisha uhusiano wa nchi hizi na Moscow na kuongeza msaada kwa vita upande wa Urusi huko nchini Ukraine.

Wakati vita hivyo vikiendelea, baadhi ya waangalizi wamebainisha kuwa Urusi inajaribu kusaka uungwaji mkono msimamo wake katika mzozo huo. Na madai ya nchi hiyo kwamba haya ni mapambano dhidi ya nguvu za Magharibi na ukoloni mamboleo yameipa uungwaji mkono.

Kwa upande wake, majaribio ya Ukraine ya kupata ufuasi katika maeneo hayohayo kupigania himaya haionekani kujitokeza kwa njia sawa.

Wachambuzi hawa pia wanahoji kuwa wanaona kile kinachotajwa ni "kurudi kwa Urusi kimataifa" kupitia ushawishi wa kiuchumi na kisiasa, na vile vile utumiaji wa mbinu za upotoshaji wa kidigitali kusambaza simulizi mbalimbali.

Katika miaka ya 2010, upanuzi wa ushawishi wa Urusi ulikuwa na matokeo ya fursa ya kiuchumi, lakini wakati wa vita yake na Ukraine umekuwa wa kimkakati zaidi.

Kuna ushahidi kwamba ushawishi wa Urusi katika baadhi ya nchi za Kiafrika umeongezeka.

Afrika Kusini, kwa mfano, inaonekana kusonga mbele zaidi kutoka kwenye ushawishi wa Magharibi, na kuingia kwenye mkondo wa ushawishi wa China na Urusi.

Lakini hili linawezekana, kwa kiasi, kwa sababu changamoto ya utaratibu wa kiliberali wa sasa inanufaisha ulimwengu wa Kusini, na kuipa nguvu kubwa ya kufanya mazungumzo katika nyanja ya kimataifa na kufikia malengo fulani ya kisiasa.

Urusi

Chanzo cha picha, Getty Image

Hayo yamedhihirika katika mkutano wa hivi karibuni wa BRICS, kundi la nchi zinazoongozwa na Brazil, Russia, Afrika Kusini na China.

Viongozi wa mataifa haya manne wamesita kutoa shutuma za moja kwa moja za vitendo vya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Katika mkutano huo, rais wa Brazil, Lula da Silva, alisema kwamba vita vya Ukraine "vimeonyesha mapungufu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," huku akionyesha nguvu ya kiuchumi ya washirika wa BRICS kama ishara ya umuhimu wake duniani.

Uamuzi wa hivi majuzi wa kujumuisha nchi zingine sita (ikiwemo Argentina, Iran na Falme za Kiarabu) katika umoja huo utaongeza uzito huu na unaweza kuwawezesha wanachama wake kuwa na ushawishi mkubwa katika mpangilio wa sasa wa dunia.

Ukraine inafanya nini kwa hiki inachokifanya Urusi?

Ukraine imejibu hatua za kidiplomasia za Urusi kwa kuongeza balozi zake barani Afrika na kuipa kipaumbele eneo la kusini katika sera yake ya mambo ya nje, lakini hali hii ya "vita" inaweza kuwa ngumu zaidi kwao kuliko inavyoonekana.

Urusi inaendelea kusambaza ujumbe, kupitia mitandao yaa kidijitali, ambayo huimarisha ushawishi wake wa kijiografia na kisiasa.

Zaidi ya hayo, kwa ulimwengu wa kusini, Urusi inachukuliwa kuwa yenye uzito kama wa Magharibi, hasa Marekani.

Urusi

Chanzo cha picha, Getty Image

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini suala muhimu zaidi, Ukraine inaweza kutoa nini kwa ulimwengu wa Kusini?

Ukraine inaweza kupata uungwaji mkono zaidi kutoka kwa nchi za BRICS kwa kuimarisha uhusiano uliopo wa kiuchumi na kushirikisha matatizo yanayosababishwa na Urusi.

Ujenzi wa vituo vipya vya nafaka, vilivyopendekezwa kuhifadhi nafaka kama vile ngano na mahindi, ni mwanzo mzuri.

Hili ni muhimu hasa kutokana na uamuzi wa kuzuia meli za Ukraine zinazobeba nafaka kuondoka kwenye bandari za Bahari Nyeusi, jambo ambalo huenda likasababisha uhaba wa chakula barani Afrika.

Serikali ya Kenya, kwa mfano, ilishutumu uamuzi wa Urusi kama "kuchoma kisu mgongo" kwa nchi za Kiafrika.

Ukraine pia inaweza kuchukua fursa ya kufanana kwa mapambano yake ya kitaifa na uzoefu wa kupambana na ukoloni wa ulimwengu wa kusini: badala ya kuelekeza masimulizi yake dhidi ya Urusi, inaweza kuanza kujenga "kumbukumbu" za pamoja kwa kuzingatia mambo ya kawaida ambayo wamekuwa nayo kama waathiriwa.

Kinachozidi kuwa wazi ni kwamba nchi yoyote ambayo itajaribu kupinga sura ya Urusi kama wakala wa kupinga ubeberu itakabiliwa na vita virefu, haswa ikiwa nchi hizo haziwezi kuvutia kumbukumbu zao chanya za pamoja.