Miaka 65 ya BBC Swahili:Tumbatu- kisiwa cha mbali huko Zanzibar chenye magari machache sana
Na Halima Nyanza
BBC Swahili

Takriban miaka sita iliyopita uwepo wa gari la abira na mizigo ilikuwa ni ndoto, katika kisiwa cha Tumbatu kilichopo kaskazini mwa kisiwa cha Unguja visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu Sensa ya watu na makazi yam waka 2012, kisiwa cha Tumbatu kilikuwa na idadi ya watu elfu 12, lakini kwa sasa inadi ya watu inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia karibu watu elfu 25, ambao gari kwao sasa imekuwa miongoni mwa huduma muhimu.
Bakari Haji Shekha ni mtu wa kwanza kuendesha gari kisiwani cha Tumbatu, anasema miaka minne iliyopita ilikuwa ni maajabu kwa wakazi wa Tumbatu, kwa gari la mizigo na ambalo pia linabeba abiria kuwasili kusiwani humo. Japo hapo hapo awali yaliwahi kuingia magari kwa kazi maalumu. Huku wengi wakikosa kuyashuhudia.
Anasema ilikuwa ni shida kwao kutokana na watu wengi kutaka kupanda na kulishuhudia, huku wengine wakiziba njia mbele, kiasi kwamba kuamua kutafuta ulinzi na pia kulitoa bandarini nyakati za usiku.

Kufika kwa gari katika kisiwa cha tumbatu kumeleta nafuu kwa wagonjwa, wanawake wajawazito na wazee waliokuwa wakitembea umbali mrefu, kufikia huduma na pia uwepo wa gari hilo, kumebadili hali za wakaazi wake hususan kupungua kwa gharama za maisha ikiwemo gharama za ujenzi wa nyumba bora. Kama wanavyoelezea baadahi ya wakazi wa Tumbatu.
Kwa wakazi wa Tumbatu kutoka sehemu moja mpaka nyingine kwao ni bure, gari limekuwa mkombozi pia kwa wanawake wanaojitwika mizigo ya kuni kichwani kutoka porini wanapolikuta njiani.
Kulipia gharama za usafiri inakuja tu pale kwa mtu anapolikodi, ama nyakati na miezi maalumu kama vile siku za sikukuu.

Lakini licha wa kazi wa Tumbatu kunufaika kwa uwepo wa gari, Dereva huyu wa kwanza, imemjaza umaarufu pi na changamoto, ikiwemo kuwa tayari kuhudumia wateja wake saa 24.
Miundo mbinu ya barabara bado ni changamoto katika wilaya ndogo hiyo ya Tumbatu, ambapo barabara zake chache zilizopo hazijafikia kiwango cha lami. Hivyo kuwa kero kwa dereva ambapo humlazimu kuchonga barabara mwenyewe,kufikishamzigo wa mteja wake.

Khatib Habib Ali Ni Katibu tawala wa Wilaya ndogo ya Tumbatu, anasema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika bajeti yake ya mwaka huu, imeidhinisha fedha kwa ajili ya kujengwa kwa barabara ya Lami kisiwani humo.
Mpaka sasa kisiwa hicho cha Tumbatu chenye hadhi ya Wilaya ndogo kina magari matano yanayofanya kazi ya kubeba mizigo na abiria, huku madereva wakiwa sita tu.
















