Ben-Gvir : Waziri wa Israel mwenye utata aliyewekewa vikwazo kimataifa ni nani?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Sandrine Lungumbu
- Nafasi, BBC Global Journalism
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Waziri wa Usalama wa Kitaifa wa mrengo mkali wa kulia wa Israel Itamar Ben-Gvir hajawa mgeni kwenye mabishano katika kipindi chote cha maisha yake mafupi serikalini na kwa miongo kadhaa kabla ya hapo.
Hivi karibuni alizua ghadhabu baada ya kusali katika eneo takatifu linalozozaniwa huko Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu, na kukiuka makubaliano ya miongo kadhaa katika moja ya maeneo nyeti zaidi katika Mashariki ya Kati.
Picha na video za ziara yake kwenye eneo linalojulikana kwa Waislamu kama Haram al-Sharif (Patakatifu pa Patakatifu) na kwa Wayahudi kama Mlima wa Hekalu zinaonesha Ben-Gvir akiongoza maombi ya Kiyahudi huko. Eneo hilo pia linajulikana kama kiwanja cha Msikiti wa al-Aqsa.
Wayahudi wanaruhusiwa kutembelea lakini si kufanya maombi huko.
Ben-Gvir ametembelea eneo hilo mara kadhaa hapo awali lakini hakuwahi kuomba hadharani, kulingana na gazeti la Times of Israel.
Wachambuzi wanasema ziara hiyo ilifanana na ziara ya marehemu Ariel Sharon - wakati huo kiongozi wa upinzani nchini Israel - katika eneo hilohilo miaka 25 iliyopita ambayo inaaminika kuwa ilichochea kile kinachoitwa intifada ya pili ya Palestina (maasi).
Ni njia ya uendeshaji ambayo Ben-Gvir ameitumia hapo awali.
Alitembelea eneo jingine la ghasia kati ya Waisraeli na Wapalestina Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu mwaka 2021, kitongoji cha Wapalestina cha Sheikh Jarrah, ambapo wakazi wengi walitishiwa kufukuzwa kutoka kwenye nyumba zao ili kutoa nafasi kwa walowezi wa Kiyahudi.
Matukio haya ni sehemu ya historia ya Ben-Gvir ya uanaharakati wa uchochezi na wenye utata mkubwa.
Na haishangazi, anasema Dk Leonie Fleischmann, mhadhiri mkuu wa Siasa za Kimataifa na Haki za Kibinadamu katika Chuo Kikuu cha London. "[Wana]patana na kila kitu alichosema hapo awali, historia yake, itikadi yake na imani yake ya kidini. Ana sababu kichwani."
Kwa hiyo, ni kwa jinsi gani mtu ambaye kwa miaka mingi alionekana kufanya kazi katika mipaka ya jamii ya Waisraeli akapata nafasi hiyo yenye ushawishi mkubwa?

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Dk Fleishmann anaainisha mambo mawili makuu: jinsi mfumo wa uchaguzi wa Israeli unavyofanya kazi na hali ya sasa ya Gaza.
Ben-Givr alipewa wadhifa muhimu wa Usalama wa Kitaifa katika baraza la mawaziri la Israel mwaka 2022. Hii ilikuwa baada ya uchaguzi wa wabunge ambapo chama chake cha mrengo wa kulia cha Otzma Yehudit (Jewish Power) kwa ushirikiano na chama kingine cha mrengo mkali wa kulia, Religious Zionism, kilishinda viti 14.
Alipata uungwaji mkono kutoka kwa vijana, Waisraeli wa mrengo wa kulia na kujiunga na muungano unaoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambaye alihitaji kura zake kusalia madarakani, na anaonekana kuwa na nguvu kubwa ya kiitikadi juu ya serikali.
"Gaza imekuwa fursa ya kweli kwa sababu Netanyahu anataka kung'ang'ania madarakani na kufanya hivyo amekuwa akiwapa nguvu zaidi watu wenye ushawishi wanaomuweka madarakani," anasema Dk Fleishmann.
Ben-Gvir alizaliwa mjini Jerusalem katika familia ya urithi wa Iraq mwaka wa 1976, na hakuhudumu katika jeshi la Israel akiwa na umri wa miaka 18. Hili kwa kawaida lingezingatiwa kuwa kikwazo kikubwa cha uchaguzi. Hata hivyo, alisema siku za nyuma kwamba Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) halikumruhusu kujiandikisha kwa sababu ya maoni yake ya kisiasa.
Mwanasheria kwa mafunzo, msimamo mkali wa kiitikadi wa Ben-Gvir ulighushiwa kutokana na kuhusika kwake tangu akiwa mdogo katika vuguvugu la ultra-Orthodox Kach, lililoanzishwa na marehemu Rabbi Meir Kahane ambaye aliuawa huko New York mwaka 1990.
Vuguvugu hilo ndilo kundi pekee la kisiasa la Israel kuteuliwa rasmi kuwa shirika la kigaidi na kupigwa marufuku Israel na Marekani.
Inaunga mkono itikadi za uzalendo na chuki dhidi ya Palestina na mmoja wa wafuasi wake, daktari wa Marekani,Israel Baruch Goldstein, aliwaua Wapalestina 29 katika msikiti mwaka 1994.
Picha ya Goldstein inaripotiwa kwa wingi kuwa ilitundikwa nyumbani kwa Ben-Gvir.
Ben-Gvir mwenyewe ameshtakiwa kwa kuchochea na kufanya vitendo vya unyanyasaji dhidi ya Wapalestina mara nane, ikiwa ni pamoja na kuhukumiwa mwaka 2007 kwa kuchochea chuki za rangi na kusaidia mashirika ya kigaidi.

Chanzo cha picha, Anas Zeyad Fteha / Anadolu via Getty Images
Ben-Gvir believes that Israel is a Jewish nationalist and Zionist state and opposes
Ben-Gvir anaamini kuwa Israel ni taifa la Kiyahudi lenye uzalendo na Wazayuni na inapinga kuanzishwa kwa taifa la Palestina pamoja na Israel.
Katika siku za nyuma, aliunga mkono ghasia zinazofanywa na walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina na akatoa wito wa kufukuzwa kwa lazima kwa raia "wasio waaminifu" wa Kiarabu kutoka nchini humo, kulingana na Times of Israel.
Tangu ajiunge na baraza la mawaziri, mara kwa mara ameitaka Israel kukalia kwa mabavu eneo lote la Ukanda wa Gaza na kuhimiza kile alichokitaja kuwa ni "uhamaji wa hiari" wa Wapalestina kutoka eneo hilo.
Mwezi Juni, Australia, Norway, Canada, New Zealand na Uingereza zilitangaza vikwazo vya pamoja dhidi ya Ben-Gvir pamoja na waziri mwingine wa siasa kali za mrengo wa kulia, Bezalel Smotrich, kwa "uchochezi wa mara kwa mara wa ghasia dhidi ya jamii za Wapalestina" katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Mwezi uliofuata, Uholanzi na Slovenia zilipiga marufuku Ben-Gvir kuingia katika nchi zote mbili zikitaja ukiukwaji wa haki za binadamu wa Israel na hali inayoendelea kuzorota huko Gaza.
Lakini anaendelea kutoa sauti kali kuhusu masuala ya usalama.
Kufuatia shambulizi la makombora la Iran katika hospitali ya Soroka katika mji wa Beersheba nchini Israel mwezi Juni, Ben-Gvir alitoa wito kwa "mtu yeyote anayechukia taifa la Israel" "ashindwe" na utawala nchini Iran "uangamizwe".

Chanzo cha picha, Reuters
Mrengo wa wastani zaidi au zaidi wa kulia?
Tangu hatua yake kuelekea serikali kuu mnamo 2022, Ben-Gvir alionekana kuchukua hatua za kujitambulisha kama mwanasiasa wa kawaida zaidi.
Aliwahi kuyataja maandamano ya Gay Pride kama "machukizo". Sasa, anasema kwamba angekubali ikiwa mmoja wa watoto wake sita angekuwa anajihusisha na mapenzi ya jinsi moja, lakini anashikilia kuwa ndoa nchini Israeli zinapaswa kuwekwa chini ya vikwazo vya dini ya kiorthodox.
Je, hatua hizi ni jaribio la kupanua wigo wake wa usaidizi ndani ya nchi, kwa kuangalia kile kinachokuja baada ya Netanyahu?
Haiwezekani, anasema Dk Fleischmann. "Sidhani kama ni lazima abadili msimamo wake ili kupata uungwaji mkono.
Ben-Gvir alikuwa mchochezi na chuki dhidi ya Palestina kabla ya Gaza. Sasa Waisraeli wamepitia vita na Iran... bado watamtafuta mtu ambaye ataenda kuwalinda katika ulimwengu huu mpya na ukweli mpya."















