Mahangaiko ya Wagaza 'wanaofungwa minyororo na kufunikwa macho' katika hospitali ya Israel

- Author, Joel Guinto
- Nafasi, BBC News
Wahudumu wa afya nchini Israel wameiambia BBC kwamba wafungwa wa Kipalestina kutoka Gaza mara kwa mara hufungwa minyororo kwenye vitanda vya hospitali, hufunikwa macho, wakati mwingine wakiwa uchi na kulazimishwa kuvaa nepi - hali ambayo daktari mmoja alisema ilifikia "mateso".
Mfichuzi wa madhila hayo alieleza kwa kina jinsi taratibu katika hospitali moja ya kijeshi zilivyofanywa "kawaida" bila dawa za kutuliza maumivu, na kusababisha "kiasi kisichokubalika cha maumivu" kwa wafungwa.
Mfichuzi mwingine alisema dawa za kutuliza maumivu zilitumiwa "kwa kuchagua" na "kwa kiwango kidogo sana" wakati wa utaratibu wa matibabu kwa mfungwa wa Gaza katika hospitali ya umma.
Pia alisema wagonjwa mahututi wanaoshikiliwa katika vituo vya kijeshi vya muda wananyimwa matibabu sahihi kwa sababu ya kusita kwa hospitali za umma kuwahamisha na kuwatibu.
Mfungwa mmoja aliyechukuliwa kutoka Gaza kuhojiwa na jeshi la Israel na baadaye kuachiliwa, aliambia BBC mguu wake ulibidi ukatwe kwa sababu alinyimwa matibabu ya jeraha lililoambukizwa.
Daktari mkuu anayefanya kazi ndani ya hospitali ya kijeshi iliyo inayohusishwa na madai hayo alikanusha kuwa kukatwa kwa viungo vyovyote kulitokana na hali hiyo, lakini alielezea pingu na vizuizi vingine vinavyotumiwa na walinzi kama "udhalilishaji".
Jeshi la Israel lilisema wafungwa katika kituo hicho walitendewa "ipasavyo na kwa uangalifu".
Wafichuaji hao wawili ambao BBC ilizungumza nao wote walikuwa katika nafasi za kutathmini matibabu ya wafungwa. Wote wawili waliomba majina yao yasitajwe kwa sababu ya ukubwa wa suala hilo miongoni mwa wenzao.
Maelezo yao yanaungwa mkono na ripoti iliyochapishwa Februari na Madaktari wa Haki za Kibinadamu nchini Israel, ambayo ilisema kuwa jela za kiraia na kijeshi za Israel zimekuwa "kifaa cha kulipiza kisasi" na kwamba haki za binadamu za wafungwa zilikuwa zikikiukwa - hasa haki yao ya afya.

Wasiwasi juu ya matibabu ya wafungwa wagonjwa na waliojeruhiwa umejikita katika hospitali ya kijeshi, katika kambi ya kijeshi ya Sde Teiman kusini mwa Israel.
Hospitali hiyo iliundwa na Wizara ya Afya ya Israel baada ya mashambulizi ya Hamas hasa kuwatibu wafungwa wa Gaza, baada ya baadhi ya hospitali za umma na wafanyakazi kuususia kuwatibu wapiganaji waliokamatwa siku ya mashambulizi ya Hamas.
Tangu wakati huo, vikosi vya Israel vimekusanya idadi kubwa ya watu kutoka Gaza na kuwapeleka katika vituo kama Sde Teiman kwa mahojiano. Wanaoshukiwa kupigania Hamas wanapelekwa katika vituo vya kuwashikilia watu vya Israel; wengine wengi wanaachiliwa huru kurudi Gaza bila malipo.
Jeshi halichapishi maelezo ya wafungwa ambalo linawashikilia.
Kufungwa pingu na kufumbwa macho
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wagonjwa katika hospitali ya Sde Teiman wamefunikwa macho na kufungwa pingu ya mikono na miguu kwenye vitanda vyao, kulingana na matabibu kadhaa wanaohusika na kutibu wagonjwa huko.
Pia wanakazimishwa kuvaa nepi, badala ya kutumia choo.
Kujibu madai hayo jeshi la Israel lilisema kwamba wafungwa katika hospitali ya Sde Teiman kufungwa kwa pingu "ilichunguzwa kibinafsi na kila siku, na inafanywa katika hali ambapo hatari ya usalama inahitaji".
Ilisema kwamba nepi [diapers] zilitumika "kwa wafungwa tu ambao wamepitia taratibu za matibabu ambazo harakati zao ni ndogo".
Lakini mashahidi, ikiwa ni pamoja na daktari mkuu wa kituo hicho, Yoel Donchin, wanasema matumizi ya nepi na pingu ni ya kawaida katika wadi ya hospitali.
"Jeshi linamfanya mgonjwa kuwa tegemezi kwa 100%, kama mtoto mchanga," alisema. "Umefungwa, uko na diapers, unahitaji maji, unahitaji kila kitu - ni hali ngumu".
Dk Donchin alisema hakuna tathmini ya mtu binafsi ya haja ya vizuizi, na kwamba hata wale wagonjwa ambao hawakuweza kutembea - kwa mfano, wale waliokatwa miguu - wamefungwa pingu kitandani. Alitaja tabia hiyo kuwa ya "kijinga".
Mashahidi wawili katika kituo hicho katika wiki za mwanzo za vita vya Gaza walituambia kwamba wagonjwa huko waliwekwa uchi chini ya blanketi.
Daktari mmoja mwenye ujuzi wa hali za huko alisema kufungwa kwa vitanda kwa muda mrefu kungesababisha "mateso makubwa, mateso ya kutisha", akielezea kama "mateso" na kusema wagonjwa wataanza kuhisi maumivu baada ya saa chache.
Wengine wamezungumza juu ya hatari ya uharibifu wa ujasiri wa muda mrefu.

Picha za wafungwa wa Gaza walioachiliwa baada ya kuhojiwa zinaonyesha majeraha na makovu kwenye vifundo vyao vya mikono na miguu.
Mwezi uliopita, gazeti la Israel la Haaretz lilichapisha madai yaliyotolewa na daktari katika tovuti ya Sde Teiman kwamba wafungwa wawili wamekatwa mguu kwa sababu ya majeraha ya pingu.
Madai hayo yalitolewa, gazeti hilo lilisema, katika barua ya kibinafsi iliyotumwa na daktari huyo kwa mawaziri wa serikali na mwanasheria mkuu, ambapo ukataji wa viungo kama hivyo ulielezewa kuwa "kwa bahati mbaya ni tukio la kawaida".
BBC haijaweza kuthibitisha madai haya.
Dkt Donchin alisema kuwa kukatwa viungo hakukuwa matokeo ya moja kwa moja ya kubanwa na kumehusisha mambo mengine - kama vile maambukizi, kisukari au matatizo ya mishipa ya damu.
Miongozo ya matibabu ya Israel inasema kwamba hakuna mgonjwa anayepaswa kuzuiwa isipokuwa kuna sababu maalum ya usalama ya kufanya hivyo, na kwamba kiwango cha chini cha kizuizi kinapaswa kutumika.
Mkuu wa Bodi ya Maadili ya Madaktari nchini, Yossi Walfisch, baada ya kutembelea eneo hilo, alisema wagonjwa wote wana haki ya kutibiwa bila kufungwa minyororo, lakini usalama wa wafanyakazi unashinda mambo mengine ya kimaadili.
"Magaidi hupewa matibabu ifaayo," alisema katika barua iliyochapishwa, "kwa lengo la kupunguza vizuizi na kudumisha usalama wa wafanyikazi wanaotibu."
Raia wengi wa Gaza wanaoshikiliwa na jeshi la Israel wanaachiliwa bila kufunguliwa mashtaka baada ya kuhojiwa.
Dkt Donchin alisema malalamiko kutoka kwa wafanyikazi wa matibabu katika hospitali ya kijeshi ya Sde Teiman yamesababisha mabadiliko, pamoja na kuhamishwa kwa pingu zilizolegea. Alisema alisisitiza walinzi kuondoa vizuizi kabla ya kufanyiwa upasuaji wowote.
"Haipendezi kufanya kazi huko," alisema. "Ninajua ni kinyume cha kanuni za maadili kumtibu mtu aliyefungwa kitandani. Lakini ni sina budi kufanya hivyo, Je, ni bora kuwaacha wafe? sidhani hiilo lina mjadala.”
Lakini ripoti zinaonyesha mitazamo ya wafanyikazi wa matibabu kwa wafungwa inatofautiana sana, katika hospitali za kijeshi na za kiraia.
'Viwango visivyomithilika vya maumivu'
Mfichuzi aliyefanya kazi katika hospitali ya Sde Teiman mnamo Oktoba, muda mfupi baada ya mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel, alielezea visa vya wagonjwa kupewa kiasi cha kutosha cha dawa za kutuliza maumivu, ikiwa ni pamoja na ganzi.
Alisema daktari aliwahi kukataa ombi lake kwamba mgonjwa mzee apewe dawa za kutuliza uchungu walipokuwa wakifungua jeraha la kukatwa kiungo lililoambukizwa hivi majuzi.
“[Mgonjwa] alianza kutetemeka kutokana na maumivu, na kwa hivyo ninasimama na kusema ‘hatuwezi kuendelea, unahitaji kumpa dawa ya kutuliza maumivu’,” alisema.
Daktari alimwambia kuwa amechelewa kuisimamia.
Shahidi alisema taratibu hizo "zilifanyika mara kwa mara bila analgesia" na kusababisha "kiasi kisichokubalika cha maumivu".
Katika tukio jingine, aliombwa na mshukiwa wa mpiganaji wa Hamas kuingilia kati na timu ya upasuaji ili kuongeza viwango vya morphine na anesthetic wakati wa upasuaji wa mara kwa mara.
Ujumbe huo ulipitishwa, lakini mtuhumiwa alipata fahamu tena wakati wa operesheni iliyofuata na alikuwa na maumivu mengi. Shahidi huyo alisema yeye na wenzake walihisi kulikuwa na hali ambayo ilikuwa ni kitendo cha makusudi cha kulipiza kisasi.
Jeshi lilisema katika kujibu madai hayo kwamba unyanyasaji dhidi ya wafungwa "ni marufuku kabisa", na kwamba mara kwa mara huwajulisha vikosi vyake juu ya tabia inayotakiwa kwao. Maelezo yoyote kamili ya vurugu au udhalilishaji yatachunguzwa, ilisema.
Mfichuzi wa pili alisema hali katika Sde Teiman ilikuwa sehemu tu ya tatizo, ambalo lilienea hadi katika hospitali za umma. BBC inamwita "Yoni" ili kulinda utambulisho wake.

Katika siku zilizofuata mashambulizi ya Oktoba 7, alisema, hospitali za kusini mwa Israel zilikabiliwa na changamoto ya kuwatibu wapiganaji waliojeruhiwa na waathiriwa wa waliojeruhiwa, mara nyingi katika idara sawa za dharura.
Wapiganaji wa Hamas wenye silaha walikuwa wametoka kushambulia jamii za Waisraeli kwenye uzio wa mpaka na Gaza, na kuua takriban watu 1,200 na kuwateka nyara wengine 250.
"Mazingira yalikuwa ya hisia kali," Yoni alisema. "Hospitali zilizidiwa kabisa, kisaikolojia na uwezo wa kufanya kazi."
"Kuna matukio ambapo nilisikia wafanyakazi wakijadili kama wafungwa kutoka Gaza wanapaswa kupata dawa za kutuliza maumivu. Au njia za kutekeleza taratibu fulani ambazo zinaweza kugeuza matibabu kuwa adhabu.
Mazungumzo kama haya hayakuwa ya kawaida, alisema, hata kama matukio halisi yalionekana nadra sana.
"Nakumbuka kisa kimoja ambapo dawa za kutuliza maumivu zilitumiwa kwa kuchagua, kwa kiasi kidogo sana, wakati wa utaratibu," aliiambia BBC.
“Mgonjwa hakupata maelezo yoyote ya kilichokuwa kikiendelea. Kwa hivyo, ukiweka pamoja [kwamba] mtu anapitia utaratibu wa kuvamia, ambao unahusisha hata chale, na hajui kuhusu hilo, na amefumbwa macho, basi mstari kati ya matibabu na kushambuliwa unavukwa."
Tuliomba Wizara ya Afya kujibu madai haya, lakini walituelekeza kwa IDF.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












