Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
China inataka nini katika vita vya Israel na Hamas?
Wakati mzozo kati ya Israel na Hamas ukizidi kupamba moto - China imejiweka kama wakala wa amani. Lakini kuna mipaka kwa kile inachoweza kufanya.
Mwanadiplomasia wa China, Wang Yi, alijadili mzozo huo na maafisa wa Washington mwishoni mwa wiki iliyopita wakati kukiwa na hofu ya vita vikubwa zaidi vya kikanda kuibuka. Marekani imeahidi itafanya kazi na China kujaribu kupata muafaka.
Wang pia amezungumza na viongozi wa Israel na Palestina baada ya mjumbe maalumu wa China huko Mashariki ya Kati, kwenda na kukutana na viongozi wa nchi za Kiarabu. Pia, China imekuwa muungaji mkono wa kusitishwa mapigano katika mikutano ya Umoja wa Mataifa.
Kuna matumaini China kutumia uhusiano wake wa karibu na Iran, ambayo inaunga mkono Hamas huko Gaza na Hezbollah nchini Lebanon, ili kupunguza makali ya mzozo. Maafisa wa Marekani wanaonekana kumshinikiza Wang kuitaka Iran itulie, limeripoti gazeti la Financial Times.
China ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Iran, na mapema mwaka huu Beijing ilianzisha upatanishi wa nadra kati ya Iran na Saudi Arabia. Tehran inasema, iko tayari kuimarisha mawasiliano na China ili kutatua mapigano ya Gaza.
China inaweza kuwa msuluhishi?
'Kwa vile serikali ya China imekuwa na uhusiano mzuri kwa pande zote mbili katika mzozo huo, inaweza kuaminika kuleta suluhu,'' alisema Dkt. Dawn Murphy, profesa katika chuo cha National War, kilicho chini ya Idara ya Ulinzi ya Marekani.
China ina uhusiano mzuri na Wapalestina, Waarabu, Uturuki na Iran, alisema. "Marekani ambayo ina uhusiano mzuri na Israel, wanaweza kuwaleta wahusika wote mezani."
Lakini wafuatiliaji wengine wanaeleza - China haina ushawishi mkubwa katika siasa za Mashariki ya Kati.
"China sio nchi yenye ushawishi katika suala hili. Hakuna mtu anayetarajia China kuchangia kuleta suluhu," anasema Jonathan Fulton, mtaalamu wa uhusiano wa China na Mashariki ya Kati kutoka Baraza la Atlantic.
Kauli ya kwanza ya China kuhusu mzozo huo iliikasirisha Israel ambayo ilionyesha "kukatishwa tamaa sana" kwamba China haikuilaani Hamas wala kutaja haki ya Israel kujitetea.
Bado kuna Changamoto
Baada ya hasira juu ya kauli yake ya kwanza, Wang baadaye aliiambia Israel "nchi zote zina haki ya kujilinda" - lakini pia alisema hatua za Israel zimekwenda "zaidi ya wigo wa kujilinda."
China kwa muda mrefu imekuwa ikiiunga mkono waziwazi harakati za Palestina. Inaanzia wakati wa mwanzilishi wa Chama cha Kikomunisti cha China Mao Zedong, ambaye alituma silaha kwa Wapalestina kuunga mkono kile kinachoitwa harakati za "ukombozi wa taifa hilo."
Mao aliilinganisha Israel na Taiwan - zote zikiungwa mkono na Marekani - kama misingi ya ubeberu wa Magharibi.
Lakini miongo kadhaa baadaye, China ilianzisha uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia na Israel, ambapo sasa wana uhusiano wa kibiashara wa mabilioni ya dola.
Ingawa China imeweka wazi kuwa inaendelea kuwaunga mkono Wapalestina. Katika matamshi ya China kuhusu mzozo wa hivi karibuni, Rais Xi Jinping amesisitiza haja ya kuwepo kwa taifa huru la Palestina.
Baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii ya China wamefananisha vitendo vya Israel na unazi kwa kuwashutumu kutekeleza mauaji ya halaiki kwa Wapalestina, jambo ambalo limekemewa na ubalozi wa Ujerumani mjini Beijing.
Kudungwa kisu kwa mwanafamilia wa mfanyakazi wa ubalozi wa Israel mjini Beijing pia kumeongeza hali ya wasiwasi.
Haya yote yanaweza yasiwe na sura nzuri - China inapojaribu kuishawishi serikali ya Israel.
Kwa nini China inahusika?
Sababu moja ni maslahi yake ya kiuchumi Mashariki ya Kati, ambayo yatatatizika ikiwa mzozo huo utaongezeka.
Beijing sasa inategemea sana uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi, na wachambuzi wanakadiria karibu nusu ya hiyo inatoka Ghuba. Nchi za Mashariki ya Kati zimezidi kuwa wadau muhimu katika mradi mkubwa wa miundombinu ya barabara (BRI).
‘Vita hivyo vimezuka wakati ambapo China inajionyesha kuwa mshirika bora wa dunia kuliko Marekani. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, imekuza maono ya dunia inayoongozwa na China huku ikikosoa kile inachokiona kama kushindwa kwa uongozi wa Marekani,’’ anasema Dkt Murphy.
China imejizuia kuishambulia Marekani kwa msaada wake kwa Israel. Lakini gazeti la kijeshi la China PLA Daily liliishutumu Marekani kwa "kuongeza mafuta kwenye moto."
Maneno yale yale ambayo Beijing imeyatumia kuikosoa Washington kwa kuisaidia Kyiv katika vita vya Ukraine. Gazeti la serikali la lugha ya Kiingereza la The Global Times lilichapisha katuni ya Mjomba Sam akiwa na mikono iliyotapakaa damu.
Undumilakuwili wa China?
Ingawa inadhihirisha mshikamano na mataifa yenye Waislamu wengi na kupinga uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina, Beijing bado inashutumiwa kwa ukiukwaji wa haki za binaadamu za Waislamu walio wachache wa Uyghur, na kuwalazimisha kuishi kama jamii za Wachina wengine.
"China inadhani kusema inaunga mkono Palestina itapata uungwaji mkono na nchi za Kiarabu, na hiyo ni mbinu ya undumilakuwili," anasema Dkt. Fulton.
Wang anadai China inatafuta tu amani kwa ajili ya Mashariki ya Kati na "haina maslahi binafsi kuhusu suala la Palestina."
Changamoto itakuwa ni kuushawishi ulimwengu kuwa hilo ni la kweli.