Shambulio la Septemba 11: Jinsi linavyogharimu maisha hadi sasa

f

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Cindy Augustine
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Maradhi yanayohusishwa na vumbi na moshi baada ya kuanguka kwa majengo mawili makubwa ya ghorofa, yamesababisha vifo mara mbili ya mashambulizi yenyewe miaka 23 iliyopita - na matatizo mapya ya kiafya bado yanaibuka.

Baada ya mwezi mzima wa kufanya kazi katika eneo hilo la Ground Zero, Elizabeth Cascio alipata kikohozi ambacho hakikuweza kuondoka. Kisha alianza kuteseka na matatizo ya maumivu katika kichwa.

"Sote tulijua kuwa hewa haikuwa salama - ilikuwa ni kama sumu kwa jinsi nilivyoihisi," anasema Cascio, afisa wa zamani wa matibabu ya dharura katika Idara ya Zimamoto ya New York (FDNY).

Cascio alitumia karibu miezi miwili kutafuta mabaki ya binadamu. Kile ambacho hakujua wakati huo, ni athari kwa afya yake miongo miwili baadaye. Mwaka 2019, alitibiwa saratani ya shingo ya kizazi, ambayo imehusishwa na tukio la Ground Zero.

Alistaafu mwaka 2023. Sasa akiwa na umri wa miaka 61, Cascio bado anafuatiliwa na Mpango wa Afya wa Serikali ya Marekani (WTC), ambao hufuatilia na kutoa matibabu kwa wale walioathiriwa moja kwa moja na mashambulizi ya Septemba 11 huko New York, Pentagon huko Washington, DC, na Shanksville, Pennsylvania.

Ni miaka 23 tangu Cascio afanye kazi katikati ya vumbi, moshi na uchafu wa majengo hayo, na ana hamu ya kuzungumza juu ya matatizo ambayo wamepata watu kama yeye.

Katika baadhi ya maeneo, vumbi na masizi yalifika unene wa zaidi ya nchi nne (sentimita 10) kwenye sehemu ambayo yalikaa. Ingawa mvua kubwa ilisafisha vumbi jingi la nje, ubora wa hewa bado uliathiriwa kwa miezi kadhaa mbeleni.

Idadi ya waliofariki baadaye

sd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakati ghorofa mbili za World Trade Center zilipoporomoka, wingu kubwa la vumbi lilitanda

Ingawa Idara ya Zimamoto ya New York iliwahimiza wafanyikazi wa uokoaji kuvaa mavazi ya kinga na barakoa, wafanyakazi wengi na watu waliojitolea walikwenda bila vifaa vya kupumulia au mavazi ya kinga, wakati wengine walivaa barakoa nyepesi. Wale wanaoishi na kufanya kazi katika eneo hilo waliendelea na maisha yao huku kukiwa na hewa chafu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Miaka 23 baadaye kuna watu 127,567 wamejiandikisha katika Mpango wa Afya wa WTC, kulingana na Kituo cha Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC).

Kufikia Desemba 2023, 6,781 kati ya wale ambao walisajiliwa na mpango huo wamefariki kutokana na magonjwa au saratani inayohusishwa na eneo hilo.

Ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya watu waliokufa wakati wa Septemba 11. Mwezi Septemba 2024, idara ya zima moto na wahudumu wa kwanza walitangaza zaidi ya watu 360 kutoka idara hizo, wamekufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na tukio hilo – ni idadi kubwa kuliko idadi ya zima moto na wahudumu wa afya, 343 ambao walipoteza maisha siku ya tukio lenyewe.

"Watu wengine waliugua baada ya miaka miwili, wengine waliugua baada ya miaka minane, wengine waliugua baada ya miaka 12," anasema John Feal, afisa ambaye alifika Ground Zero usiku wa shambulio hilo.

"Kuna watu ambao walifanya kazi kwa muda wote wa usafishaji katika miezi minane na hawakuwahi kuugua. Lakini sote tulikabiliwa na sumu ambayo hakuna mtu aliyewahi kuiona hapo awali."

Feal alijeruhiwa vibaya siku sita baada ya kuwasili Ground Zero wakati kipande cha chuma kilipoponda mguu wake. Licha ya kufanyiwa upasuaji mara nyingi, bado mguu wake una athari ya chuma hicho. Feal sasa anatumia muda wake mwingi kutetea manufaa ya kiafya kwa waokoaji.

Athari za kiafya

ws

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kiasi kikubwa cha kemikali zenye sumu, metali nzito na vichafuzi vingine vilirushwa angani wakati minara hiyo ilipoungua na kuporomoka (Mikopo: Getty Images)

Miongoni mwa athari za kiafya kwa wale ambao walikumbana na vumbi na moshi la 9/11 ni saratani, kinga za mwili kushambuliana, pumu, magonjwa ya kupumua na matatizo ya kiwewe (PTSD).

Magonjwa adimu kama vile mabaka katika ngozi, yamegunduliwa kwa kiwango cha juu isivyo kawaida kwa maafisa wa zima moto ambao walikumbana na vumbi na moshi la 9/11.

Haikuchukua muda mrefu baada ya shambulio hilo, watoto wa shule nao waliripotiwa kupata visa vipya vya pumu na magonjwa mengine ya kupumua.

Aina mbalimbali za saratani pia zimeripotiwa kati ya watu 37,500 waliojiandikisha katika Mpango wa Afya wa WTC, huku saratani ya ngozi na saratani ya kibofu zikigunduliwa kwa wingi. Aina ya saratani zingine ni pamoja na saratani ya matiti, damu, saratani ya mapafu na saratani ya tezi dume.

Marc Wilkenfeld, ambaye alikuwa mmoja wa madaktari wa kwanza kuwaona manusura na waokoaji waliopata matatizo ya kiafya baada ya 9/11, akiwa sehemu ya timu ya madaktari na watafiti wa afya ya umma, waligundua kuwa watu walioathiriwa na vumbi kutoka eneo hilo pia wanaonyesha dalili za uharibifu wa neva.

Michael O'Connell, aliyekuwa na umri wa miaka 25 wakati wa 9/11 na sasa ana umri wa miaka 48, alifanya kazi ya uokoaji siku chache baada ya mashambulizi, anasema:

"Inachukua muda kwa magonjwa kukua. Kwa muda wa miezi minane tulikuwa tukivuta hewa yenye sumu. Bado tunaugua, na watu wanakufa kutokana na magonjwa miaka 23 baadaye."

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah