Je, demokrasia ya Kimagharibi inaweza kufanya kazi barani Afrika?

Chanzo cha picha, REUTERS
Mwaka 2007, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza Septemba 15 kuwa Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, kama sehemu ya azimio la kuhimiza serikali kuimarisha na kuboresha demokrasia.
Tangu wakati huo, Siku hii inaadhimishwa kila mwaka duniani kote. Hata hivyo, mfumo huu wa utawala unaonekana kushambuliwa katika bara hili kwa wingi wa mapinduzi ya kijeshi. Mapinduzi ya hivi punde zaidi yametokea Gabon, ambapo Rais Ali Bongo Ondimba alipinduliwa na kundi la maafisa wakuu wa jeshi usiku wa Agosti 29 hadi 30, 2023.
Mapinduzi hayo yalifanyika saa chache baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais na Tume ya Uchaguzi ya Gabon, na kumtangaza Ali Bongo Ondimba mshindi kwa asilimia 64.27 ya kura, dhidi ya Albert Ondo Ossa (30.77%), mgombea wa upinzani.
Jeshi lilisema uchaguzi huo "haukuwa wa wazi, wala wa kuaminika na vilevile haukujumuisha watu wote kama matarajio ya watu wa Gabon."
Kuzorota kwa demokrasia

Chanzo cha picha, AFP
Kuheshimu haki za binadamu, kufanya chaguzi wa wazi na wa mara kwa mara ni maadili yanayojumuisha vipengele muhimu vya demokrasia.
Hata hivyo, katika nchi nyingi, chaguzi zimekuwa vyanzo vya uvunjifu wa amani, hasira na mivutano. Ukiukwaji wa vipengele vya uchaguzi ni kikwazo kwa maendeleo ya kidemokrasia, kulingana na mwanasheria na mtaalamu wa masuala ya uchaguzi, Hilaire Kamga.
"Mifumo ya uchaguzi inapokuwa haiaminiki, hupelekea walioteuliwa kutokana na uchaguzi huo kuwa na walakini. Kwa kuzingatia hilo, migogoro inayotokana na chaguzi huongezeka kama inavyoonekana barani Afrika,” anaeleza Kamga.
Wananchi kukosa kuiamini michakato ya uchaguzi na watendaji wa kisiasa katika mfumo wao wa utawala, huchangia uchaguzi kutokuwa wa amani na wa kuaminika.
Wananchi hukosa imani kunatokana na kutofuatwa kwa sheria za uchaguzi, ghilba za mara kwa mara katika mchakato wa uchaguzi kunakofanywa na mamlaka husika.
"Kukosekana kwa imani kupo kwa sababu wale walio madarakani ambao wanaandaa uchaguzi - huuandaa uchaguzi ili kusalia madarakani na kwa hivyo wanafanya kutokee mizozo baadaye," anasema Hilaire Kamga.
Pamoja na mapinduzi ya Agosti 30 nchini Gabon, Afrika ilikumbwa na mapinduzi nane katika kipindi cha miaka mitatu. Mengi yayo yalifanyika katika nchi zinazozungumza Kifaransa.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ili kuhalalisha mapinduzi yao, wapinduaji mara nyingi hutaja sababu za usalama, kushindwa kwa utawala au ukosefu wa demokrasia.
GUINEA
Nchini Guinea, sababu za demokrasia zilitajwa ili kuhalalisha kupinduliwa kwa rais aliyechaguliwa kidemokrasia. Septemba 5, 2021, Rais Alpha Condé alipinduliwa na wanajeshi wakiongozwa na Kanali Mamady Doumbouya - wakati huo alikuwa mkuu wa kikosi maalumu cha jeshi, na kisha akawa rais.
Katika hotuba yake kwenye televisheni ya taifa, Kanali Mamady Doumbouya anakemea dosari za mamlaka zikijumuisha usimamizi mbaya wa fedha, kukithiri siasa katika mambo ya umma, umaskini na ufisadi ulio furutu ada.
BURKINA FASO
Nchini Burkina Faso, Januari 24, 2022, Rais Roch Marc Christian Kaboré alilazimishwa kujiuzulu na jeshi, Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba alitawazwa kuwa rais mwezi Februari.
Septemba 30, Damiba alipinduliwa na jeshi, Kapteni Ibrahim Traoré aliwekwa kama rais wa mpito, aongoze nchi hadi uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Julai 2024.
Sababu iliyotolewa ni kushindwa kwa Rais mteule Roch Marc Christian Kaboré kukabiliana na ukosefu wa usalama uliokithiri.
NIGER
Nchini Niger, Julai 26, 2023, wanajeshi walitangaza wamempindua Rais Mohamed Bazoum.
Jenerali Abdourahamane Tiani, mkuu wa kikosi cha ulinzi wa rais. Amekuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo. Alihalalisha mapinduzi hayo kwa sababu ya kuzorota hali ya usalama wa Niger kulikoathiriwa na ghasia za makundi ya kijihadi.
Mtindo wa demokrasia ya Kimagharibi unaifaa Afrika?

Chanzo cha picha, Getty Image
Mtaalamu wa sera za umma, Mbeninese Joël Atayi Guedegbe anasema, litakuwa kosa kulitazama ongezeko la mapinduzi kama uthibitisho wa kufa kwa demokrasia barani Afrika.
“Demokrasia haijashindwa kwa namna yoyote ile. Ni maisha ya kawaida kwa ujenzi wa taasisi za nchi, ambapo mapinduzi ya kijeshi yakifanyika tunaweza pia kusema kwamba tayari tuko katika demokrasia," anasema Guedegbe.
Dhana ya demokrasia shirikishi inaendelea kushika kasi barani Afrika na duniani kote, lakini kulingana na wataalamu, demokrasia inapaswa kuendana na mazingira ya sasa ya kijamii na kisiasa.
"Ni wakati wa Afrika kufanya ukarabati. Leo hii mifano tuliyonayo ya demokrasia ni ile iliyowekwa baada ya uhuru na inafundishwa katika shule, vyuo vikuu na katika sayansi ya siasa. Kutoka wakati huo hadi sasa, kuna mahali fulani demokrasia inapaswa kuendana na dhana ya asili na misingi ya Afrika,'' anaeleza Guedegbe.
"Kwa mtazamo huu, ikiwa mtindo kutoka nje umewekwa kwa zaidi ya miaka sitini, labda ni wakati wa Waafrika kufikiria upya ugatuzi wa mamlaka kwa kutumia mifano ya usimamizi wa jamii zao - huku tukichukua kile kinachovutia katika demokrasia ya Magharibi,'' anaeleza Guedegbe.
Zaidi ya miaka sitini baada ya uhuru, Afrika iko katika njia panda. Mtindo wa sasa wa demokrasia ya Magharibi unazidi kupingwa na mipaka yake kufichuliwa. Bara hili linajikuta katika hali inayolihitaji kuchagua kati ya mfumo wake mpya wa kisiasa na utawala au kuendelea na mfumo wa kimagharibi.
Swali muhimu ni; Je, inafaa kubumi mtindo wa kidemokrasia wa Kiafrika? Kulingana na Joël Atayi Guedegbe, "tunapaswa kuwa makini na mtindo wa aina mmoja."












