Huu ndiyo muarobaini wa matatizo ya umeme Tanzania?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 7

Tanzania inazalisha umeme takribani Megawati 3500 kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya umeme, wakati mahitaji yake yakiwa chini ya Megawati 2000. Kwa hesabu rahisi nchi hiyo inaziada ya kutosha ya umeme ambayo inaweza kutosheleza nchi kama Rwanda au Burundi. Lakini suala la kukatika kwa umeme limekuwepo kwa muda sasa, licha ya jitihada kubwa ya serikali.

Kwa mfano mradi wa bwawa la mwalimu Nyerere (JNHPP) pekee unazalisha zaidi ya nusu ya umeme unaoingia kwenye gridi ya taifa. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), Gissimo Nyamohanga, alisema mpaka kufikia mwezi huu wa Machi, bwawa hilo litakuwa linaingiza Megawati 2,115 kwenye gridi ya taifa. Ni moja ya miradi mikubwa ya umeme Afrika ambayo imeifanya Tanzania kuwa na umeme mwingi wa kujtosheleza.

Pamoja na ziada na uhakika wa uwepo wa mradi mkubwa kama JHPP, wengi walitarajia mjadala kuhusu umeme uegemee zaidi kwenye kushuka kwa bei kwa watumiaji na bei ya uuzaji nje na sio matatizo ya upatikanaji wake nchini humo.

Maeneo kadhaa yamekuwa na changamoto ya umeme na nchi hiyo kutangaza hivi karibuni kwamba itanunua umeme kutoka Ethiopia kwa ajili ya mikoa ya kanda ya Kaskazini, kumeibua mjadala mkali, wengi wakihoji, kwanini umeme ukatike? na kwa nini umeme utoke Ethiopia, maelfu ya maili kuja Tanzania na sio kutoka JNHPP huko Rufiji ama sehemu yoyote nchini ambapo ni karibu?

Tatizo la kukatika kwa umeme

samia

Chanzo cha picha, Samia

Maelezo ya picha, Rais Samia amekuwa akisisitiza uwekezaji mkubwa kwenye miundo mbinu ya umeme

'Umeme unakatikakatika maeneo ya kaskazini huku, lakini serikali yenu, inachukua hatua ya kununua umeme nje, maalumu kwa mikoa ya Kaskazini, ili umeme upatikane masaa 24, bila kukatikakatika', ilikuwa kauli ya Rais Samia Suluhu, hivi karibuni alipokuwa akizindua mradi wa maji Same -Mwanga – Korogwe.

Suala la kukatika kwa umeme, limekuwa tatizo sugu na la muda mrefu linalotofautina tu kiwango cha ukatikaji, muda wa ukatikaji na mahali ama maeneo ya ukatikaji.

Kukatika huku, kunakoonekana kwa kawaida, kunaweza kuathiri shughuli za kawaidia za wananchi, wanaotegemea nishati hiyo katika maisha yao ya kila siku.

Kuna wakati mbunge wa viti maalumu, Jesca Kishoa, aliwasilisha takwimu bungeni za kukatika kwa umeme mara 2,844 kwa mwaka mmoja, akirejea ripoti ya Mamlaka ya udhiniti wa nishati na maji (EWURA) ya mwaka 2018. Uchakavu wa miundombinu ni moja ya sababu inayotajwa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Msemaji wa serikali, Gerson Msigwa anakiri kuwepo kwa tatizo hilo, ingawa kwa sasa anaelezea limepungua kwa kiasi kikubwa, "kwa sasa kelele za kukatika kwa umeme zimepungua lakini tunaendelea kuboresha (kuhakikisha kuondoa tatizo) kupitia mradi wa gridi imara", aliviambia vyombo vya habari hivi karibuni.

Mradi anaoutaja ni moja ya miradi mingi ya kuboresha miundombinu ya umeme, inayotekelezwa nchini humo, kwa ajili kuhakikisha uzalishaji wake, usambazaji wake na upatikanaji wake ni wa uhakika.

Kwa kauli ya viongozi wa serikali karibu wote, wanataja miundo mbinu kama sehemu muhimu ya kuhakikisha tatizo la umeme nchini humo linakoma.

'Changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini inatokana na uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme', ilikuwa kauli ya Naibu Waziri wa Nishati, Mhe, Judith Kapinga, aliyoitoa bungeni aliposisitiza kuhusu kuimarisha miundo mbinu. Je huo ndio muarobaini wa matatizo ya umeme Tanzania?

Safari ya 'milele' ya miundo mbinu

a

Chanzo cha picha, Maelezo

Maelezo ya picha, Bwawa la Mwalimu Nyerere(JNHPP) ni moja ya vyanzo vikuu vya umeme Tanzania

Wataalamu wa nishati hii, wanataja aina nne ya miundo mbinu katika sekta ya umeme inavyohusika katika uzalishaji, usafirishaji, na usambazaji wa nishati hiyo Miundo mbinu hii haiepukiki, ni ya 'milele' kuhakikisha safari yake ya kuzalishwa, kusafirishwa na kumfikia mtumiaji.

Aina ya kwanza ni Miundombinu ya kufua au uzalishaji wa umeme inayohusisha mitambo ya umeme wa maji (Hydropower plants), jua (Solar power plants), upepo (Wind power plants), makaa ya mawe (Coal power plants), nyuklia (Nuclear power plants) na mitambo ya umeme wa gesi asilia (Natural gas power plants).

Baada ya kuzalishwa, umeme husafirishwa kwa umbali mrefu kwa kutumia miundo mbinu inayojumuisha nyaya za umeme wa msongo wa juu (High Voltage Transmission Lines), nguzo kubwa za umeme (Transmission Towers/Pylons), pamoja na Vituo vya kupoza na kuongeza nguvu ya umeme (Substations & Transformers)

Umeme husambazwa kutoka kwenye vituo vya kupoza hadi kwa watumiaji kupitia miundo mbinu inayojumuisha, nyaya za msongo wa kati na chini (Medium & Low Voltage Power Lines), nguzo ndogo za umeme (Utility Poles) na Transfoma zinazowekwa mitaani (Distribution Transformers).

Na miundombinu ya matumizi ya Umeme inahusiana na vifaa vinavyotumiwa na watumiaji wa mwisho ambavo ni nyaya za majumbani na viwandani, vifaa vya kupima matumizi ya umeme (Meters & Smart Meters) na mitambo ya kuhifadhi umeme kama betri kubwa (Energy Storage Systems)

Kwa ujumla, miundombinu hii yote inafanya kazi pamoja kuhakikisha kuwa umeme unapatikana kwa ufanisi na salama kwa watumiaji.

Hakuna shaka, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha miundo mbinu ya umeme nchini humo, ikiwekeza matrilioni ya shilingi kwenye eneo hilo.

Kuanzia miundombinu ya mradi wa Bwala la Mwalimu Nyerere (JNHPP) iliyotumia shilingi trilioni 6.6, bwawa linalochangia asilimia karibu 65 ya umeme kwenye gridi ya taifa, mpaka mita zinazotumiwa majumbani ama viwandani.

Mwaka wa fedha uliopita pekee serikali ilitumia shilingi bilioni 109.8, kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme. Na kila mwaka inatenga bajeti kubwa.

Unaweza pia kusoma

Ununuzi nje au Gridi imara?

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Miundombinu imara na isiyo chakavu inasaidia uhakika mkubwa wa umeme

Ujenzi na uboreshaji wa miundo mbinu ya umeme ni safari ya 'milele'. Itajengwa kila mwaka na itaboreshwa kila mwaka. Kama sasa inavyofanyika kwenye kuboresha gridi ya taifa. Haiepukiki, lakini je ndo mwarobaini wa matatizo ya umeme Tanzania?

Gridi ya taifa, ni mradi wa kuboresha miundo mbinu, kuanzisha vyanzo vipya ya kufua umeme na kuunganisha mikoa ya pembezoni mwa nchi.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa vituo vya kupokea na kupozea umeme vya Chalinze- Msongo Kilovoti 400 na Nyakanazi 400. Miundo mbinu ya kuunganisha gridi ya Taifa, Afrika mashariki na gridi ya ukanda wa kusini mwa Afrika, pamoja na mradi wa Tanzania-Zambia msongo wa kilovoti 400 (TAZA) unatekelezwa ili kuunganisha Iringa, Mbeya, Tunduma mpaka Sumbawanga, urefu wa kilometa 664.

Kwa muktadha wa kauli ya msemaji wa Serikali , Msigwa, itachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kero ya kukatika kwa umeme lakini lini itakamilika? ili kutamatisha tatizo la kukatika kwa umeme?

Hakuna jibu la moja kwa moja, lakini Msigwa anasema kufikia mwaka 2030, kila nyumba Tanzania itafikiwa na nishati hiyo.

Kama alivyogusia Rais Samia, Tanzania iko katika hatua za mwisho kusaini mikataba ya kununua umeme wa megawati 100 kutoka Ethiopia ili kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme. Hiki kitakuwa moja ya chanzo cha kuimarisha upatikanaji wake, hasa maeneo ya Kaskazini, ambayo ni ya uchumi wa kitalii, kutokana na uwepo wa mlima Kilimanjaro na hifadhi ya mbuga kadhaa za wanyama.

s

Chanzo cha picha, maelezo

Maelezo ya picha, Naibu Katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na madini Tanzania, Felchesmi Mramba,

Wataalamu wanataja kuwa na vyanzo tofauti vya umeme ni njia kubwa inayoweza kupunguza tatizo hilo. Vyanzo vya kuuzalisha kama maji, gesi, makaa ya mawe, upepo na jua lakini pia kuwa na ameneo tofauti ya upatikanaji wa umeme ndani ya nchi na hata nje ya nchi.

'tuwe na vyanzo tofauti tofauti, tusiwe (tusitegeme) na chanzo kimoja, tunapokuwa na vyanzo vingi vingi, chanzo kimoja kinapopata shida, kingine kinaingilia (kinaokoa jahazi)', anasema mhandisi Costa Rubagumya , mtaalamu wa masuala ya uzalishaji umeme Tanzania.

Mtaalamu wa masuala ya nishati, kutoka Kenya,Theo Njoroge anaunga mkono suala la Tanzania kununua umeme Ethiopia kusaidia kukatika kwa umeme maeneo ya Kaskazini kwa sababu ya unafuu wa bei na uwepo wa miundombinu iliyo tayari.

'Umeme unaotoka Ethiopia ni nafuu kuliko umeme unaozalishwa Tanzania, (kwa sababu) nchi ya Ethiopia ina bwawa kubwa zaidi la maji linaloweza kuzalisha umeme Megawati 7,000', anasema Njoroge

Hilo linaungwa mkono na Felchesmi Mramba, Naibu Katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na madini Tanzania, alipotoa ufafanuzi kwanini Tanzania iagize umeme nje na sio kutumia umeme wa ziada iliyo nao?

"Umeme wa Ethiopia tunanunua kwa senti ya Marekani 0.077, wakati tuna vyanzo vingi ambavyo vinazalisha kwa gharama ya juu zaidi, hivyo hii ni nafuu kwetu'.

Ethiopia moja ya wazalishaji wakubwa wa umeme wa bei nafuu Afrika, ikiungana nchi ya Sudan na Libya.

Upotevu wa umeme, ambao serikali umetaja kusababisha hasara ya shilingi bilioni 32 kila mwaka, ni jambo la kuzingatiwa. Mmoja wa viongozi waaandamizi wa Shirika la Umeme nchini humo (TANESCO), Pakaya Mtamakaya, aliwahi kuripoti uwepo wa upotevu wa umeme wa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka, kutokana na umeme wenye kilovoti ndogo kusafirishwa umbali mrefu.

Pengine hatua hii ya kununua umeme Ethiopia ambao utachukuliwa kwneye gridi ya taifa Kenya kuingia Namanga, Tanzania, itapunguza upotevu na kuongeza upatikanaji wake.

Lakini Matumizi ya umeme yamekuwa yakiongezeka kila mwaka. Kwa mfano mwaka 2023/2024, matumizi ya umeme yaliongezeka kwa asilimia 16, kwa mujibu wa TANESCO. Ongezeko hili, litahitaji tena miundo mbinu ama ya usambazaji au usafirishaji, usimamizi na bajeti. Kwa hiyo huenda safari ya kukomesha kukatika kwa umeme bado ikaendelea kuwa mjadala wa muda mrefu.