Je, kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi husababisha mshtuko wa moyo?

g

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Nandini Vellaswamy
    • Nafasi, BBC Tamil
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Utafiti mkubwa kuhusu uhusiano kati ya uvimbe kwenye kizazi (uterine fibroids) na magonjwa ya moyo yanayohusiana na mishipa ya damu (ASCVD) kwa wanawake, uliochapishwa Desemba mwaka jana kwenye Jarida la American Heart Association, umeonyesha matokeo ya kushtua.

Utafiti huu ulifanywa kwa wanawake zaidi ya milioni 2.7, ikiwa ni pamoja na wanawake milioni 4.5 wenye uvimbe huo na milioni 2.25 wasio nao. Wastani wa umri wao ulikuwa miaka 41.

Taasisi kadhaa zilishirikiana kwenye utafiti huu uliochukua muongo mmoja, na matokeo yalionyesha kwamba wanawake wenye vimelea vya uterasi Fibroids wana hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa ya moyo ikilinganishwa na wanawake wasio navyo.

Utafiti pia unaonyesha kwamba hatari hii inahusu magonjwa yote makuu ya moyo, yakiwemo:

  • Ugonjwa wa arteri za moyo
  • Magonjwa ya mishipa ya ubongo

Aidha, hatari hii inaweza kuathiri wanawake wa rika zote na makundi yote.

Hivyo basi, vimelea vya uterasi vinaweza kuwa ishara ya mapema ya hatari ya magonjwa ya moyo kwa wanawake.

Wataalamu wa matibabu wanaelezea uvimbe kwenye kizazi yaani Fibroids ni nini na jinsi unavyohusiana na ugonjwa wa moyo.

Je, vimelea vya uterasi ni nini?

Madaktari wanasema kwamba watu wenye uvimbe kwa mfuko wa kizazi yaani fibroids hupata maumivu yaliyoongezeka wakati wa hedhi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Madaktari wanasema kwamba watu wenye uvimbe kwa mfuko wa kizazi yaani fibroids hupata maumivu yaliyoongezeka wakati wa hedhi.

Vimelea vya uterasi ni uvimbe unaokua kutoka kwenye misuli ya uterasi. Vimelea hivi vinaweza kuwepo bila kuonyesha dalili yoyote, anasema daktari wa uzazi Shanti Ravindranath.

"Vimelea hivi hupatikana tu pale unapofanya vipimo vya matibabu. Hii siyo kusema kwamba ni hatari, lakini tatizo hili linaonekana kwa wanawake wengi zaidi. Homoni mbili, estrojeni na progesteroni, zina jukumu muhimu katika ukuaji wake," anafafanua.

Vimelea hivi vinaweza kutokea kwa umri wowote, lakini ni vya kawaida zaidi kabla ya miaka 40, hasa wakati wa ukomo wa hedhi na kabla ya ukomo wa hedhi.

"Huenda huonyeshi dalili yoyote kabla ya ukomo wa hedhi, lakini baadaye dalili zinaweza kujitokeza," anasema Dkt. Shanti.

Uhusiano kati ya vimelea vya uterasi na magonjwa ya moyo

"Vimelea hivi hutoa kemikali zinazosababisha uvimbe na mwitikio wa uchochezi. Kemikali hizi pia zinaweza kuchangia magonjwa ya moyo," anafafanua Dkt. Shanti.

"Kadri homoni ya estrojeni inavyotolewa mwilini, inasaidia kuzuia magonjwa ya moyo. Lakini viwango vya estrojeni hupungua baada ya ukomo wa hedhi.Si kila mwanamke anayeingia ukomo wa hedhi hupata magonjwa ya moyo, lakini mara nyingi huonekana kwa wanawake waliyoingia kipindi hiki," anasema Dkt. Shanti.

Dkt. K.S. Ganesan, profesa wa masuala ya moyo aliyestaafu, anaongeza:

"Kwa kawaida, viwango vya estrojeni hupungua wakati wa ukomo wa hedhi, jambo linaloongeza hatari ya magonjwa ya moyo. Hali hii inahusu wanawake wenye au wasio na uterasi."

Dalili za kawaida za vimelea vya uterasi ni kama vile:

  • Kutokwa na damu kwa wingi wakati wa hedhi
  • Maumivu makali ya hedhi
  • Utasa
  • Kupata haja ndogo mara kwa mara

Umri wa kuathiriwa na sababu

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Dkt. Shanti anasema ni vigumu kusema kwa uhakika ni nini husababisha vimelea hivi, lakini baadhi ya hatari ni:

  • Uzito kupita kiasi
  • Kuavya mimba
  • Kuingia katika ukomo wa hedhi au kuchelewa sana

''Vimelea hubadilika ukubwa wakati wa mimba na hupungua baada ya kujifungua au ukomo wa hedhi'', Dkt. Shanti anaeleza.

Jinsi ya kuzuia

Dkt. Shanti anashauri njia kadhaa za kupunguza hatari:

  • Kudumisha uzito mwili unaofaa kwa urefu
  • Kuacha uvutaji sigara
  • Kupunguza mfadhaiko
  • Kufuata mtindo wa maisha wenye afya
  • Kupata usingizi wa kutosha
  • Kufanya vipimo vinavyofaa, ikiwemo ultrasound ili kubaini ukubwa na mahali pa uvimbe na kupata matibabu sahihi

"Uzito kupita kiasi kwa wanawake umeongezeka nchini India. Hivyo basi, kuna haja ya kufanya utafiti maalumu kuhusiana na uhusiano kati ya vimelea vya uterasi na magonjwa ya moyo," anasema Dkt. Shanti.

Kulingana na utafiti wa Lancet uliochapishwa mwaka wa 2025, inakadiriwa kuwa kufikia 2050, karibu Wahindi milioni 450 nchini wanaweza kuwa wanene.

Jinsi ya kuzuia ugonjwa wa moyo kwa wanawake?

Madaktari wanasema kuwa mnene kupita kiasi ni sababu kuu ya kuwa na uvimbe kwenye mfuko wa kizazi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Madaktari wanasema kuwa mnene kupita kiasi ni sababu kuu ya kuwa na uvimbe kwenye mfuko wa kizazi.

"Hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanawake wanaougua ugonjwa wa moyo. Kuna tofauti katika dalili na matibabu ya ugonjwa wa moyo kwa wanawake. Hili ni eneo la kipekee ambalo linahitaji utafiti wa kina," alisema profesa mstaafu wa magonjwa ya moyo K.S. Ganesan.

Dkt. Ganesan anasema:

Hatari ya magonjwa ya moyo huongezeka wakati wa ukomo wa hedhi unapoanza.

Wanawake wengi huanza kupata magonjwa ya moyo bila dalili.

Wanawake waliyoingia ukomo wa hedhi wanapaswa kuwa makini.

"Wanawake wana mishipa midogo kuliko wanaume, hivyo kama kuna kuongezeka kwa kuganda kwa damu (hypercoagulation), wana hatari ya kushambuliwa na moyo mara moja," anaonya.

Vipimo vinavyopendekezwa kwa wanawake wenye umri wa zaidi ya 40:

  • Kipimo cha homoni
  • Kipimo cha jumla cha kuchunguza kiwango cha mafuta mwilini (lipid profile)
  • Uchunguzi wa vinasaba (genetic study)
  • Kipimo cha jumla cha kuchunguza kuganda kwa damu (coagulation profile)
  • Kipimo cha Homocysteine

Wanapopatikana matatizo yoyote, dawa au hatua za kuzuia zinapendekezwa. Pia anashauri kutembea angalau saa moja kila siku.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi