Miungano ya kisiasa 'iliyowaponza' na 'kuwaneemesha' wanasiasa Kenya
Na Dinah Gahamanyi
BBC Swahili

Chanzo cha picha, Martha Karua/Twitter
Wakati Rais William Ruto akiapishwa rasmi kuwa Rais wa tano wa Kenya na hivyo kuiongoza kenya kwa muhula wa miaka mitano ijayo bila shaka kuna wanasiasa wanaotabasamu, huku wengine wakijiuliza, ni upi mwelekeo wao wa kisisasa baada ya miungano yao kushinda au kushindwa katika uchaguzi huu.
Bw Ruto amekuwa rais baada ya Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya kuidhinisha ushindi wake katika uchaguzi wa tarehe 9 Septemba, kufuatia aliyekuwa mgombea wa Muungano wa Azimio La Umoja Raila Odinga kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.
'Balaa' la Azimio La Umoja au One Kenya Alliance

Chanzo cha picha, Kalonzo Musyoka/Twitter
Licha ya kinara wa Muungano wa Azimio La Umoja , kiongozi mkongwe wa upinzani Raila Odinga kupata pigo la kushindwa katika jaribio lake la tano la kuwania urais, kushindwa kwake kumewaacha njia panda viongozi wengine hususan wakongwe waliojiunga na Muungano wake.
Wengi waliahidiwa uteuzi wa viti mbali mbali kuanzia uwaziri hadi uongozi wa taasisi kubwa za kiserikali, lakini hilo limesalia kuwa ndoto.
Katika mipangilio ya Azimio, Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka alikuwa ameahidiwa wadhifa wa kinara wa mawaziri.
Kwa kuona mambo yameenda mrama, Bw Kalonzo alichukua karatasi za kuomba kazi ya spika wa bunge la kitaifa.
Magavana wanaoondoka Hassan Joho (Mombasa) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) walikuwa pia wameahidiwa nafasi za uwaziri kama Azimio ingeshinda urais.
Bw Joho aliahidiwa cheo cha waziri wa ardhi huku Bw Oparanya akitengewa wizara ya fedha.
Mbali na hao, kuna wanasiasa ambao waliamua kutowania nyadhifa zozote wakiahidiwa watateuliwa kwenye serikali ya Bw Odinga.
Wanajumuisha Suleiman Shahbal, ambaye alitaka kuwania ugavana Mombasa, Kenneth Marende aliyeweka kando azma yake ya kuwania ugavana wa Vihiga na mwenyekiti wa ODM, John Mbadi, aliyekubali kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Homa Bay.

Chanzo cha picha, Charity /Twitter
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aliyekuwa gavana wa Kitui, Charity Ngilu naye aliamua kutotetea kiti chake.
Bw Marende aliahidiwa wadhifa wa Spika wa Seneti huku Bw Mbadi na Bi Chege wakiwa miongoni mwa waliopendekezwa kuwa wabunge maalumu.
Mawaziri katika serikali ya Rais Kenyatta waliotarajia kuteuliwa katika serikali ya Bw Odinga ni James Macharia (Uchukuzi), Joe Mucheru (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano), Keriako Tobiko (Mazingira), Ukur Yatani (Fedha), Mutahi Kagwe (Afya) na Fred Matiang’i (Usalama).
Wengine ni Eugene Wamalwa (Ulinzi), Peter Munya (Kilimo) na Raphael Tuju. Wengine waliokuwa wakitegea vyeo vya juu katika serikali ya Azimio ni waliokuwa magavana Nderitu Muriithi (Laikipia), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet), Mwangi wa Iria (Murang’a) na James Ongwae wa Kisii.
Ushindi wa Bw Ruto pia ni pigo kwa mabwanyenye na viongozi wa mashirika ya kijamii ambao waliunga mkono Azimio akiwemo Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli, na aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth.
Vilevile, mamia ya wanasiasa ambao wamejijenga kisiasa kwa msingi wa kumuunga mkono Bw Odinga kila wakati wa uchaguzi huenda wakalazimika kuunda mikakati upya.
Hii ni kutokana na kuwa, akiwa na umri wa miaka 77 sasa, uwezekano wa Bw Odinga kuwania urais tena ifikapo 2027 ni finyu kwa mujibu wa wadadisi wa kisiasa.
‘’Neema'' ya Muungano wa Kenya Kwanza’’ .

Chanzo cha picha, Musalia Mudavadi/Twitter
Ushindi wa Rais Mteule William Ruto ni neema kwa viongozi hususan wale waliounda muungano naye, ambao sasa wanatarajia kupata sehemu ya ‘’mkate’’ wa ushindi wa Bw Ruto.
Bila shaka chini ya muungano wa Kenya Kwanza Bw Mudavadi na Wetang’ula ‘’wamefufuka’’ kisiasa baada ya vyama vyao kufifia kwa kuzama ndani ya Muungano NASA ulioshindwa katika uchaguzi wa mwaka 2017, na hivyo kuviacha vyama hivyo viking’ang’ana kupata nyadhifa za juu za uongozi.
Katika juhudi za kupata wingi wa kura kutoka maeneo ya magharibi mwa Kenya na mashariki mwa Kenya Bw Ruto ambaye alikuwa katika chama cha United Democratic Alliance (UDA), alifanikiwa kuwavuta katika Muungano huo Wanasiasa wakongwe Bwana Musalia Mudavadi wa chama cha Amani Kenya alliance na mwenzake kutoka chama cha Ford-Kenya Moses Wetang’ula ambao waliukimbia Muungano wa Azimio la Umoja wa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Muungano huu haukuja bila ahadi. Wawili hao walihakikishiwa na Bw Ruto kupata 30 ya nyadhifa za serikali.
Kwa kuleta idadi kubwa ya wapiga kura ndani ya Muungano wa Kenya Kwanza Mudavadi aliahidiwa kupata Waziri mkuu, na kwa upande wa Wetang’ula apewe nafasi ya kiti cha Spika wa Bunge la taifa ambacho tayari amekipata.
Kwa pamoja waliunda muungano wa Kenya Kwanza, uamuzi ambao huenda wasiwahi kuujutia.















