Dini – nguvu nyuma ya rais mpya wa Kenya
Na Evelyne Musambi BBC News, Nairobi

Chanzo cha picha, DP OFFICE
William Ruto, ambaye anaapishwa kama rais mpya wa Kenya leo Jumanne, ndiye rais wa kwanza wa kiinjilisti nchini humo na huenda akaweka dini katika mstari wa mbele akiwa madarakani baada ya kutekeleza jukumu muhimu katika ushindi wake wa uchaguzi.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 55 haoni haya kukiri hadharani imani yake na amekuwa akizungumzia masuala kama vile haki za mashoga na uavyaji mimba, ambayo huenda yakaibuka wakati wa uongozi wake.
Bw Ruto anapenda kunukuu maandiko, kusali na hata kulia hadharani. Wakati wa kampeni, wapinzani wake walimdhihaki kwa kumpa jina la "naibu Yesu" – jina ambalo wafuasi wake walilikumbatia .
Hatua yake ya kwanza baada ya Mahakama ya Juu kuidhinisha ushindi wake katika uchaguzi wa mwezi uliopita ilikuwa kupiga magoti na kusali pamoja na mkewe Rachel na viongozi wengine waliokuwa chumbani humo.
BwRuto na mkewe hata wamejenga kanisa katika makazi yao rasmi mtaano Karen katika jiji kuu la Nairobi.
Kiongozi wa Waislamu pia alisali katika boma hilo baada ya uamuzi huo, akionyesha kwamba licha ya imani kubwa ya Bw Ruto ya Kikristo, ana mpango wa kuwa kiongozi wa watu wa dini zote. Jamii mbalimbali za kidini za Kenya kwa ujumla huishi pamoja kwa amani na rais mpya pia anafurahia kuungwa mkono na Waislamu wengi.

Chanzo cha picha, DP OFFICE
Askofu David Oginde wa Muungano wa Kiinjilisti wa Kenya alisema anatumai kuwa serikali ya Bw Ruto "itasimamia maadili na kuheshimu ukweli kwamba Kenya ni jamii ya kidini".
Kenya ni nchi ya waumini, huku hata Jaji Mkuu Martha Koome akihusisha uamuzi wa Mahakama ya Juu iliyothibitisha ushindi wa Ruto kama "kazi ya Mungu" - badala ya mahakama yenyewe.
Akiwa naibu rais, ushawishi wake wa kidini kwa Rais anayemaliza muda wake Uhuru Kenyatta - Mkatoliki - pia ulidhihirika wakati wa muhula wao wa kwanza, haswa wakati wa harakati zao za kusafisha majina yao katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kutokana na mashtaka yanayohusiana na ghasia zilizozuka baada ya mzozo mkali kuhusu uchaguzi wa 2007.
Wawili hao mara kwa mara walihudhuria makanisa ya kiinjilisti kusali, walipojaribu kuepuka kushtakiwa - jambo ambalo walifanikisha wakati upande wa mashtaka ulipoondoa mashtaka dhidi ya Bw Kenyatta mwaka wa 2014 na majaji wakatupilia mbali kesi dhidi ya Bw Ruto 2016.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sifa za kidini za kampeni yake ziliimarishwa na mke mpya wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Dorcas, mfanyakazi wa benki aliyestaafu ambaye sasa ni mhubiri .
Asilimia 85 ya Wakenya ni Wakristo - 33% Waprotestanti, 21% Wakatoliki, 20% Wakristo wainjilisti na 7% wanafuata makanisa ya Kiafrika - wakati karibu 11% ni Waislamu, kulingana na sensa ya mwisho, mwaka wa 2019. Idadi ndogo ya watu wanafuata kanuni za imani nyingine lakini ni wachache sana wanaokiri kuwa hawaamini kuna Mungu au hata kuamini kwamba hakuna Mungu.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Macharia Munene aliambia BBC kwamba rufaa ya Bw Ruto kwa Wakristo kote katika madhehebu yote ndiyo iliyochangia ushindi wake katika uchaguzi.
"Mpinzani wake Raila Odinga alifanya dosari alipozungumza kuhusu Ukristo kuwa juhudi za kuwavuruga watu bongo na mkewe Ida alipozungumza kuhusu kudhibiti makanisa. Kauli hizo zote zilimpendelea Ruto kwa njia ya kura," Bw Munene alisema.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Herman Manyora alisema hatashangaa iwapo Bw Ruto atawateua viongozi wa kidini katika nyadhifa serikalini, kwani wamechangia pakubwa katika kusaidia kampeni yake.
"Kama vile wakati wa utawala wa Rais Moi, kuna uwezekano kwa ibada za kanisa kuangaziwa sana katika habari kuu za Jumapili," Bw Manyora aliongeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Bw Ruto anatarajiwa kuchukua msimamo mkali kuhusu haki za wapenzi wa jinsia moja. Mnamo mwaka wa 2015, kabla ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Marekani John Kerry, aliambia waumini jijini Nairobi kwamba "Kenya ni jamhuri inayomwabudu Mungu. Hakuna nafasi ya wapenzi wa jinsia moja nchini Kenya".
Katika mahojiano na CNN kufuatia ushindi wake wa uchaguzi alisema "hakutaka kuunda mlima kutoka kwa molekuli" lakini, muhimu zaidi, aliongeza: "Wakati [haki za wapenzi wa jinsia moja] linakuwa suala kubwa kwa watu wa Kenya, watu wa Kenya watafanya uamuzi."
Bw Manyora alisema mtihani mkubwa kwa serikali utakuja iwapo kutakuwa na jaribio la kisheria la kutambua haki za wapenzi wa jinsia moja. Mnamo mwaka wa 2019, Mahakama Kuu ilitoa uamuzi dhidi ya wanaharakati ambao walikuwa wanataka kubatilisha sheria inayopiga marufuku ngono ya wapenzi wa jinsia moja, hata hivyo wanaharakati waliapa kuendelea na kampeni yao.
"Sheria ya adhabu inayoharamisha mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha katiba. Huyu hapa mtu anayedai kuwa Mkristo sana. Watu wanamwita 'naibu Yesu' na tuseme uamuzi wa mahakama unapingana na mawazo yake kuhusu hilo, itapendeza sana kutazama majibu ya Bw Ruto.’ Bw Manyora aliambia BBC.
Bw Ruto pia anajulikana kwa maoni yake ya kihafidhina kuhusu uavyaji mimba, akipinga - kwa kuungwa mkono na kanisa - kifungu cha katiba cha sasa kinachoruhusu ikiwa kuna hatari kwa afya ya mama.
Hivyo uwezekano wa serikali yake kulegeza sheria za utoaji mimba ni mdogo, hata hivyo chini ya katiba ya sasa, ana uwezo mdogo wa kuzibana, bila kujali imani yake binafsi.
Bw Ruto pia ana uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa Waislamu, wengi wao wakikubaliana naye kuhusu masuala kama vile haki za wapenzi wa jinsia moja na uavyaji mimba.
Alipata msukumo mkubwa baada ya uchaguzi, wakati United Democratic Movement (UDM) - ambayo ina makumi ya viongozi wa Kiislamu ndani ya safu zake - ilipoacha muungano wa Bw Odinga, na kuweka uzito wake nyuma ya Bw Ruto kusaidia kupata wabunge wengi baada ya uchaguzi .
Hata hivyo, Bw Manyora anaonya kwamba anapaswa kufahamu hisia za Waislamu: "Atawatuliza Waislamu kwa kuwaleta viongozi wao karibu naye lakini asipopunguza Ukristo wake, atawaudhi baadhi ya Waislamu."

Chanzo cha picha, Getty Images
Askofu Oginde alisema iwapo Bw Ruto atawateua viongozi wa kidini katika nyadhifa za serikali, basi imani zote zinafaa kuwakilishwa.
"Tutamuunga mkono, kutoa mwongozo pale tunapoweza na kwa hakika tutamuombea. Tunaomba kwamba atadhihirisha uongozi wa Kimungu," askofu aliongeza.
Mafanikio ya Bw Ruto katika uchaguzi yalitokana zaidi na ukweli kwamba alijionyesha kama "Hustler" , akipambana na jaribio la familia mbili za kisiasa - Odingas na Kenyattas - kung'ang'ania mamlaka.
Aliahidi mbinu ya kukuuza uchumi kutokea "chini kwenda juu " ili kukabiliana na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, na kuboresha maisha ya watu maskini.
Bw Manyora alisema rais mpya wa Kenya sasa atalazimika kutimiza ahadi zake.
“Ukristo ni mbinu inayotumiwa na viongozi wengi duniani kupata madaraka na wanapoingia madarakani mambo hubadilika,” alisema.















