Je, rais anayeondoka wa Kenya atakumbukwa vipi?

Na Peter Mwangangi BBC News, Nairobi

th

Chanzo cha picha, IKULU YA RAIS KENYA

Mwanafunzi mmoja alipomuuliza Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta mwaka wa 2018 kuhusu jinsi ambavyo angependa kukumbukwa atakapoondoka madarakani, alionekana kupatwa ghafla na swali hilo, kabla ya kutaja mambo mawili.

"Moja ni kwamba nitakuwa nimeacha jamii iliyoungana, yenye mshikamano. Na pili, kwamba tutakuwa tumeshinda vita dhidi ya ufisadi," alisema huku akishangiliwa.

Je, anapojiandaa kuachia ngazi baada ya mihula miwili, na kukabidhi madaraka mshirika wake wa zamani aliyegeuka kuwa mpinzani wake , William Ruto, je, amefikia malengo haya na mengine?

Hatua muhimu zaidi kuelekea umoja wa kitaifa ilikuwa Machi 2018 alipopeana mkono na kiongozi wa upinzani na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kama ishara ya mapatano yao ya kisiasa.

"Kupeana mkono" kwa sasa maarufu kama ‘Handshake’ kulimaliza miezi kadhaa ya sintofahamu na machafuko kufuatia uchaguzi ambao ulibatilishwa na Mahakama ya Juu 2017, na uchaguzi wa marudio ulisusiwa na Bw Odinga, ambaye aliendesha sherehe yake ya kuapishwa ya katika mji mkuu Nairobi.

Lakini mapatano ya Kenyatta na Odinga hayakupokelewa vyema na Naibu Rais William Ruto, ambaye alidai kwamba yalivuruga ajenda yao madhubuti ya kuimarisha usalama wa chakula, kufikia huduma ya afya kwa wote, kujenga nyumba za gharama nafuu zaidi, na kukuza sekta ya viwanda.

Hili hatimaye lilisababisha wawili hao kutofautiana, huku Bw Kenyatta akiondoa uungaji mkono wake kwa Bw Ruto na badala yake kumuunga mkono mpinzani wake, Bw Odinga, kuwania urais katika uchaguzi wa Agosti.

Mvutano kati ya Bw Kenyatta na naibu wake umeendelea hata baada ya uchaguzi. Bado hajatoa pongezi hadharani kwa Bw Ruto kwa ushindi wake, ingawa amesema atafanikisha mabadiliko ya mamlaka kwa njia ya amani .

TH

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Salamu hii ya maridhiano ilibadilisha hali ya kisiasa ya Kenya
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Huenda umoja ambao Bw Kenyatta alitafuta haukutokea jinsi ambavyo angetaka, lakini wachunguzi wa mambo wanasema ulikuwa muhimu kwa nchi ambayo imejaribu kujiepusha na ghasia zilizoenea kati ya makabila ambayo yalizuka kufuatia uchaguzi wa 2007 uliozozaniwa, ambapo Watu 1,200 walikufa na maelfu ya wengine walilazimika kukimbia makazi yao.

Huku uchaguzi uliokuwa umekamilika hivi punde kufanyika kwa amani, wadadisi wanaamini kuwa Bw Kenyatta alifanikisha azma yake ya kuleta umoja na kujenga jamii yenye mshikamano, licha ya mgombea wake Bw Odinga kushindwa.

"Kusalimiana kwa mikono kulizua hisia ya ushirikishwaji kwa sababu kama kungekuwa na kitu chochote ambacho kingegawanya nchi hii na kuitupa katiba kaburi la sahau , [ilikuwa] wazo zima la baadhi ya watu kuhisi kutengwa - wazo kwamba serikali ni ya sehemu fulani ya watu au jamii,” anasema Egare Kabaji, profesa wa mawasiliano ya fasihi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST).

Makubaliano haya, hata hivyo, yaliacha ombwe kwa upinzani.

"Iliongeza mkanganyiko juu ya nani alikuwa serikalini na nani hakuwepo," anasema Nerima Wako-Ojiwa, mchambuzi wa kisiasa na mkuu wa Siasa Place, ambayo husaidia vijana kujihusisha na siasa.

Ukosefu wa upinzani mkali wa kuangalia ubadhirifu wa serikali huenda ulichangia katika kushindwa kwa Bw Kenyatta kukomesha ufisadi na ufujaji wa rasilimali za umma.

Alipokuwa akimpigia debe Bw Odinga, alikiri kwamba amekuwa mpole katika kushughulika na wafisadi. Mnamo 2021, alisema nchi ilikuwa ikipoteza takriban shilingi bilioni 2 za Kenya ($17m; £14m) kila siku kutokana na ufisadi.

"Kwangu mimi, swali la wazi ni: 'Naam, kama ulijua hilo, kwa nini hukufanya kitu kuhusu hilo?' Kuna kesi nyingi mahakamani, lakini zinaonekana kwenda kinyume," anasema Nikhil Hira, mtaalam wa kodi katika Kody Africa.

TH

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Reli ya Standard Gauge ilielezewa kuwa mradi mkubwa wa miundo msingi nchini Kenya tangu uhuru

Utawala wa Bw Kenyatta uliwekeza pakubwa katika miundombinu kote nchini na miradi inayoanzia mabwawa makubwa, viwanja vya michezo, viunganishi vya umeme, reli na barabara kama vile Barabara ya Nairobi Expressway.

Uwekezaji huu uliwezekana kwa kukopa kwa wingi, lakini maswali yameibuka kuhusu gharama zilizotumika, thamani ya fedha na mapato ya uwekezaji kwa wananchi.

Kwa mfano, Reli ya Kisasa ya Standard Gauge (SGR) iliyojengwa na China kutoka mji wa pwani wa Mombasa hadi Nairobi iligharimu mlipa ushuru $3.2bn (£2.8bn), ambayo wachambuzi wanahoji kuwa ilikuwa ya bei kubwa ikilinganishwa na miradi kama hiyo iliyotekelezwa na majirani wa Kenya ,Tanzania na Ethiopia.

Ukopaji huo ulisukuma deni la umma nchini kufikia viwango vya juu, ambavyo nchi italazimika kulipa kwa miaka ijayo.

Mwishoni mwa 2021, deni la nchi lilifikia $72.6bn, sawa na 68% ya Pato la Taifa, ikilinganishwa na 38% ya Pato la Taifa wakati Bw Kenyatta alipokuwa rais 2013.

th

Wakati waangalizi wakikubaliana kuwa nchi hiyo inahitaji miundombinu mipya ili kuharakisha ustawi wa uchumi wa nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi wa Afrika Mashariki, wameibua wasiwasi kuhusu ubadhirifu wa fedha.

"Wakati hakuna ubaya kuwa na deni, suala ni jinsi gani tunaitumia?" Anasema Bw Hira.

Kando na mijadala ya sera, wengine watakosa utu ‘wepesi’ wa Bw Kenyatta, haswa anapotangamana na watu katika shughuli zisizo rasmi, ambapo angekuwa "halisi".

Angepigwa picha akitembea kwa starehe barabarani jijini Nairobi huku usalama wake ukifuatwa kwa mbali, akila nyama choma katika soko lililozungukwa na watu wa eneo hilo na viongozi, au akihudhuria mashindano ya gofu ambapo alitangamana kwa uhuru na washiriki.

Pia "aliharibu" Ikulu, kwa kuifungua kwa watu wengi wakiwemo watoto na watu mashuhuri kutembelea na kutazama pande zote. Hapo awali, ilikuwa hifadhi ya kipekee ya wale walio madarakani.

Pia mara nyingi alikuwa hajitambui wakati akitoa hotuba na kuwapa umma dokezo la kile kinachotokea nyuma ya pazia.

Bi Wako-Ojiwa anasema jambo hilo linaweza kuwa la kupendeza, ingawa linaweza pia kusababisha kuvurugika alipochelewa kwa mikutano

th

Chanzo cha picha, AFP

Mnamo 2013, Bw Kenyatta aliahidi kuwanunulia watoto wote wa shule kompyuta za mkononi na vipakatalishi ili kuwasaidia kuwapa ujuzi wa kidijitali. Lakini mpango huo haukutekelezwa baada ya awamu ya majaribio, huku vifaa vilivyotolewa kwa baadhi ya shule vikikosa kutumika na vingine kuibwa kwa kukosa vyumba vya kuhifadhia.

Waangalizi katika sekta ya elimu walilaumu kushindwa kwa mradi huu kutokana na ukosefu wa mafunzo kwa walimu na usambazaji duni wa umeme, miongoni mwa masuala mengine.

"Tuliishauri Serikali badala yake ijenge maabara za kompyuta katika shule zote na ziwekewe, na hilo lingepatikana kwa urahisi sana, lakini kwa namna fulani waliofanya maamuzi hawakuwasikiliza baadhi yetu. Na hiyo ilikuwa ni bahati mbaya sana," anasema Bw. Kabaji. 

Hata hivyo, utawala wake uliweza kurekebisha mtaala wa kitaifa.

Ingawa kulikuwa na ukosoaji wa mabadiliko hayo, mfumo huo mpya unanuiwa kuibua uwezo wa ubunifu wa wanafunzi kwa kuwapa ujuzi watakaohitaji kupata kazi, badala ya kuzingatia kufaulu mitihani tu.

Na wakati mpango kabambe wa kusambaza huduma za afya kwa wote nchini haujatekelezwa kikamilifu, uwezo wa vitanda vya hospitali umeboreshwa kwa kiasi kikubwa na hospitali mpya kujengwa.

Mbali na mandhari ya ndani, kimataifa, hadhi ya Kenya imeimarika katika muongo uliopita.

Ilichukua urais wa zamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo iligonga vichwa vya habari mnamo Februari 2022 baada ya kulaani Urusi kwa uamuzi wake wa kutuma wanajeshi Ukraine. Katika taarifa ambayo ilisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii, balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa, Martin Kimani, alilinganisha uzoefu wa Afrika wa ukoloni na mzozo wa Urusi na Ukraine.

"Tunaelewa kuwa watu waliotenganishwa wanaweza kuangalia kwa shauku kupita mipakani wakitumai kuunganishwa tena lakini Kenya inakataa tamaa kama hiyo ya kuandamwa kwa nguvu," alisema Bw Kimani. 

Nchi nyingine nyingi za Kiafrika ziliamua kujizuia, badala ya kuchukua upande katika mzozo wa Russia na Ukraine.

Bw Kenyatta pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), anayeshughulikia kutatua mizozo nchini Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo aliteuliwa kuwa mpatanishi wa kundi hilo.

Hata hivyo, Anthony Francis Mveyange, mkuu wa Ushirikiano wa Utafiti wa Kijamii na Utawala wa Kiafrika (PASGR), anasema haikuwa sahihi kutekeleza makubaliano ya kibiashara baina ya Marekani na Uingereza, badala ya kufanya mazungumzo kupitia EAC.

"Hii inaweza kuathiri jinsi Kenya inavyohusiana na mataifa katika kambi za kanda ambako ni mwanachama," Dkt Mveyange anasema.

Kwa ujumla, Kenya ilikabiliwa na changamoto zisizotarajiwa wakati wa utawala wa Bw Kenyatta kama vile mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu mjini Nairobi na kwingineko, janga la Covid-19 na kupanda kwa gharama ya maisha kwa kiasi fulani kulikosababishwa na vita vya Urusi na Ukraine.

Huku Bw Kenyatta akikabidhi hatamu za uongozi, changamoto kwa serikali ijayo itakuwa sio tu kutekeleza baadhi ya ahadi kubwa walizotoa kwa wapiga kura wakati wa kampeni, bali pia kushughulikia baadhi ya mahitaji muhimu yanayowakabili wananchi.

Hizi ni pamoja na ukosefu mkubwa wa ajira na kupanda kwa gharama ya maisha, huku mfumuko wa bei ukipanda hadi rekodi ya juu ya 8.5% mwezi Agosti. 

th