Fahamu urithi unaoachwa na Uhuru Kenyatta kwa Wakenya
Na Asha Juma
BBC Swahili,Nairobi

Chanzo cha picha, STATE HOUSE KENYA
Uhuru Kenyatta alipoingia madarakani kwa awamu ya pili mwaka 2017, nchi ilikuwa imegawanyika sana kwa misingi ya kikabila na kikanda na kukawa na tathmini nyingi tu ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kwamba kama angeshindwa kufikia maridhiano na mpinzani wake mkuu Raila Odinga, basi huenda angekuwa na kibarua kigumu si haba.
Ikumbukwe kwamba hayo yote yalikuwa yametokana na matokeo ya urais wa uchaguzi huo, ambapo Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi lakini Bw Odinga akapinga matokeo.
Na hata baada ya kuelekea kwenye Mahakama ya Juu Zaidi na kuamuriwa kwamba uchaguzi urudiwe, bado Bw Odinga alishindwa.
Na ili kuweka mambo sawa, kukawa na makubaliano ya maridhiano yaliyojulikana kama Building Bridges Initiative (BBI), maarufu kama ‘’Handshake” yaliyofanyika Machi 9, 2018.
Maridhiano hayo yalifurahiwa na wengi ndani ya nchi na hata kimataifa na kuchukuliwa kama ya kihistoria kukiwa na matumaini kwamba ingerudisha utulivu lakini matokeo yake ikawa ni mpasuko mkubwa katika chama cha Jubilee baada ya Naibu Rais William Ruto kuichukulia hatua hiyo kama njama ya kutaka kumuondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2022.
Uhuru na Raila walikanusha madai hayo wakati huo - lakini Ruto alianza kampeni ya kukata na shoka iliyolenga familia za Kenyatta, Moi na Odinga kama ‘’familia za kitajiri’’ zilizotaka kutawala Kenya milele.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini cha kushangaza ni kwamba muda mfupi baada ya hapo, hali ilibadilika na ikaanza kujitokeza kama uhasama.
Ukweli ni kwamba huu ulikuwa mradi wa Rais Uhuru Kenyatta pengine suala ambalo watu wanaweza kujiuliza leo hii ni kwamba, je, wale waliokuwa wanamuunga mkono wakati huo, walikuwa tayari na mradi huo?
Na pengine kuna wale ambao kwa upeo wao, wanaweza kusema kwamba BBI ndio ilikuwa chanzo cha masaibu ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.
Na kama mchezo mchezo, ukawa mwanzo wa msuguano haswa wa kisiasa na naibu wake kiasi cha hata kuvunjika kwa Muungano wa Jubilee chama ambacho kilikuwa na jukumu muhimu katika kuwaingiza madarakani Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto.
Kilichofuata ikawa ni kurushiana cheche za maneno kati ya rais na naibu wake kila mmoja akimtupia mwingine kidole cha lawama kutokana na kuzorota kwa ukuruba wa kisiasa kwa wawili hao na kuonekana hata hadharani.
Mfano, katika harakati za kutaka kubadilisha katiba ambako kulikuwa kunaungwa mkono na rais, naibu alipinga hatua hiyo na kuitaja kama ulaghai mkubwa mno ambao haujawahi kufanyika nchini kenya.
Na kadiri mvutano wao ulivyokuwa unaendelea, ndivyo hali ilivyoendelea kuwa mbaya na ikafikia wakati Rais Uhuru Kenyatta akaonesha wazi kumuunga mkono kinara wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga katika uchaguzi uliofanyika Agosti 9, 2022 wala sio naibu wake William Ruto.
Tangu walipoanza kwenda njia mbili tofauti, William Ruto naye alikuwa akikosoa Muungano wa chama cha Jubilee uliowaingiza madarakani.
Changamoto zilizojitokeza serikalini alidai kwamba Rais Uhuru Kenyatta ndiye aliye madarakani, na anayeendesha kila jambo kwa hiyo yeye hastahili kulaumiwa kwa kufeli kwa serikali katika masuala kadhaa kama vile kudorora kwa uchumi kunakokumba Wakenya na kuongezeka kwa gharama ya maisha.
Upande mwingine Rais Uhuru Kenyatta alikuwa akimlaumu naibu wake kwa kutotekeleza majukumu yake na badala yake kutembea kila pembe ya Kenya kupiga kelele badala ya kuhudumia Wakenya.
Hali ilivyokuwa katika jamii ya Wakikuyu

Chanzo cha picha, Getty Images
Hatua ya Uhuru Kenyatta kumuunga mkono Raila Odinga ilichukuliwa vipi na jamii yake ya Wakikuyu?
Jamii ya Wakikuyu yenye utajiri wa kura nchini Kenya, imekuwa na maoni tofauti kuhusu hatua ya rais anayemaliza muda wake Uhuru Kenyatta kumuunga mkono aliyekuwa mpinzani wake Raila Odinga, badala ya naibu wake William Ruto.
Rais Uhuru Kenyatta alichukuliwa kwa muda mrefu kama kinara wa kisiasa wa jamii hiyo, huku wazee wake wakimtaja kwa fahari kuwa mwana wao.
Lakini wakati BBC ilipozuru jimbo la Nyeri - ambalo lipo katika eneo la Mlima Kenya ilibainika kuwa uaminifu wake umepata pigo kutokana na uamuzi wake wa kumuidhinisha Bw Odinga katika kile alichokitaja kuwa jaribio la kubuni umoja wa kitaifa baada ya miongo kadhaa ya chuki za kisiasa.Na hilo limedhihirika kupitia matokeo ya uchaguzi uliokamilik ambapo wenyeji wenhi walimpigia kura William Ruto-hata katika kituo cha kupigia kura cha rais Kenyatta ,katika kaunti ya Kiambu .
Wakili Wahome Gikonyo alihisi kuwa Bw. Kenyatta 'amemsaliti' Bw Ruto, ambaye alimsaidia kushinda uchaguzi dhidi ya Bw Odinga katika uchaguzi uliopita.
"Ruto alifanya kazi ya punda mwaka 2013 na 2017. Kama sio yeye Uhuru hangelikuwa rais. Je hiyo ndiyo njia ya kumlipa rafiki?" Bw Gikonyo alisema alipokuwa akizungumza na BBC katika afisi yake iliyopo makao makuu ya kaunti hiyo, eneo la Nyeri.
Baadhi ya wakazi, kama Mchungaji Hannah Kanyithere, alihisi Bw Kenyatta hangejihusisha na kinyang'anyiro cha kumtafuta mrithi wake.
Wakati wa muhula wa pili wa urais (2017-2022), serikali ya Uhuru na Ruto imeangazia mkakati wa kiuchumi katika vipengele vinne maarufu kama Ajenda 4.
Nazo zilikuwa ni usalama wa chakula, nyumba za bei nafuu, huduma za afya kwa wote, uzalishaji na ubunifu wa fursa za ajira.
Kupitia hilo, serikali ilitaka kutekeleza miradi na sera zinazolenga kuharakisha ukuaji wa uchumi na kubadilisha maisha ya wananchi.
Hata hivyo, serikali ya Uhuru imekumbwa na changamoto si haba licha ya kwamba ilikuwa na mikakati ya kufanikisha uchumi wakati utawala wake unaanza. Changamoto hizo ni pamoja na:
Ukosefu wa ajira

Kulingana na taarifa ya BBC, theluthi moja ya Wakenya zaidi ya milioni 52 wana umri wa kati ya miaka 18 na 35. Wengi wao hawana kazi licha ya kuwa na ujuzi wa kujikimu wenyewe na familia.
Biashara nyingi katika sekta muhimu kama vile viwanda na kilimo zimetatizika kutokana na gharama ya juu ya uzalishaji, na kusababisha kuachishwa kazi kwa watu wengi.
Hali hiyo imechochewa zaidi na janga la Covid-19.
Mgogoro wa deni la umma

Hali ya deni la Kenya ni mojawapo ya sababu ambazo zimelaumiwa kwa nyakati ngumu za kiuchumi zilizopo sasa hivi.
Deni la nchi lilifikia $72.6 bilioni (Ksh8.2 trilioni) mwishoni mwa mwaka jana, huku kila Mkenya akidaiwa $1,470, kutoka $499 mwaka wa 2013 Uhuru Kenyatta alipoingia mamlakani.
Rais Kenyatta amekopa $56.7 bilioni (Ksh6.41 trilioni) ikilinganishwa na $13.5 bilioni za Kibaki (Ksh1.17 trilioni) na Moi'$8 bilioni (Ksh629.6 bilioni) muhula wa kwanza wa Kenyatta ofisini unachangia asilimia 44 ya pesa za utawala wake alizokuwa amekopa mwishoni mwa mwaka jana.
Wachambuzi wanasema kuwa fedha zilizokopwa zimetumika zaidi na miradi ya miundombinu inayohitaji mtaji ambayo haijachangia mapato ya haraka na uboreshaji wa maisha ya wananchi.
Gharama kubwa ya maisha

Chanzo cha picha, BUSINESS DAILY/TWITTER
Uchaguzi umefanyika wakati ambapo Kenya inapitia nyakati ngumu sana za kiuchumi.
Mwezi Juni mwaka huu, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 7.9 ikilinganishwa na asilimia 6.3 wakati huo huo mwaka jana.
Hii ilikuwa ni asilimia ya juu zaidi nchini kuwahi kurekodi tangu Agosti 2017 wakati ilikuwa asilimia 8, inaonyesha takwimu kutoka Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya.

Bei za vyakula na bidhaa nyingine za kimsingi zimepanda kwa kiasi kikubwa.
Baadhi ya vyakula vya msingi ambavyo bei yake ni kubwa zaidi ni pamoja na mafuta ya kupikia, unga wa ngano, unga wa mahindi, maziwa, na mkate.
Serikali ya Uhuru imetoa ruzuku katika unga wa mahindi wiki mbili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu lakini wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia kutopatikana kwa bidhaa hiyo ya unga huo wa mahindi ambao ulisemekana bei yake imepungua kwa muda.
Na pia ruzuku hiyo imefikia ukomo wake ikiwa na maana kwamba wananchi wanarejea kununua bidhaa hiyo kwa bei ile ile ya kwanza ambayo imeongezeka kweli.
Afya
Inasemekana kuwa asilimia 20 ya watu wako katika mpango wa Kitaifa wa Bima ya Afya (NHIF) huku 1% wanaweza kulipia huduma za afya za kibinafsi.
Kufikia sasa haijawa lazima kujiunga na NHIF lakini hilo linatarajiwa kubadilika kufikia mwisho wa mwaka huu, ikiwa rais mpya na serikali yake – wataendeleza mipango ya utawala wa Uhuru Kenyatta anayeoondoka.
Uanachama wa NHIF ni sehemu ambayo inalipwa na wengi kutokana na walio kwenye ajira katika sekta rasmi.
Ada ya shilingi 500 ya Kenya ($4.20; £3.50) ya kila mwezi inagharimu matibabu ya hospitali kwa wanachama na wategemezi wao - ingawa dawa zinagharimu zaidi.
Licha ya mpango huo wa kufanya uanachama kuwa wa lazima, serikali haijaeleza jinsi itakavyokuwa nafuu kwa wengi ambao mishahara yao ni midogo.
Mpango wa Rais mteule William Ruto, ni kuwa na sera zitakazoshughulikia tatizo la afya.
Na katika kampeni zake aliahidi kupunguza mchango wa kila mwezi wa NHIF kutoka shilingi 500 ya Kenya ($4.20; £3.50) hadi shilingi 300 ($2.50) kwa kila kaya.
Upande mwingine wa shilingi
Hata hivyo, serikali ya Uhuru Kenyatta inayomaliza muda wake inajivunia miradi ya miundombinu katika sekta kama vile barabara na miradi ya maji.
Mifano ni pamoja na reli ya SGR ,Barabara ya Nairobi Expressway jijini Nairobi na mitandao ya barabara nyingi kote nchini .
Barabara bora zinatarajiwa kupunguza muda wa usafiri kupeleka bidhaa sokoni huku kukiwa na matumaini ya upatikanaji wa maji safi pindi miradi hiyo mingi itakapokamilika .

- MATAYARISHO:Uchaguzi Kenya 2022: Je Kenya iko tayari kwa uchaguzi mkuu?
- YA MSINGI:Uchaguzi Kenya 2022: Kwa nini uchaguzi wa Kenya mwaka huu ni muhimu?
- MIUNGANO:Uchaguzi Kenya 2022: Musalia Mudavadi kujiunga na naibu rais William Ruto itabadilisha siasa za Kenya?
- UNAYOFAA KUJUA:Uchaguzi Kenya 2022: Je Naibu wa rais wa Kenya William Ruto anakabiliwa na changamoto gani katika kumteua naibu wake wa rais?
- UCHAMBUZI:Uchaguzi wa Kenya 2022: Je hatua ya Rais Kenyatta kumuunga mkono Raila Odinga itamsaidia au kumharibia?
- WASIFU:William Ruto: Muuza kuku aliyepanda ngazi hadi kuwa naibu wa rais wa Kenya
- RAILA ODINGA:Uchaguzi Kenya 2022: Siwezi kuwa kibaraka wa mtu yeyote-Raila Odinga













