Matokeo ya Uchaguzi Kenya 2022: Fahamu kiasi cha fedha anazolipwa rais mstaafu wa Kenya anapostaafu

Rais Uhuru Kenyatta akiwasilia raia

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Kenya

Maelezo ya picha, Rais Uhuru Kenyatta akiwasilia raia
    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili

Waswahili wanasema hayawi hayawi huwa, hatimaye uchaguzi mkuu wa Kenya umefanyika na naibu Rais William Ruto ametangazwa mshindi na Tume ya Uchaguzi IEBC licha ya mvutano uliokuwepo kati ya makamishna wa tume hiyo.

Makamishna wanne wa IEBC kati ya saba waliopo walipinga matokeo hayo yaliyotolewa na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati wakidai kwamba licha ya zoezi hilo kuendeshwa vizuri, awamu ya mwisho ya shughuli hiyo ilikumbwa na kiza kikuu.

Hatahivyo Ruto sasa anatarajiwa kumrithi rais Uhuru kenyatta kama rais wa tano wa taifa la Kenya tangu taifa hili lijipatie Uhuru iwapo mpinzani wake Raila Amollo Odinga hatokwenda mahakamani kupinga matokeo hayo.

Na baada ya William Ruto kutangazwa kuwa rais mteule, Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kumkabidhi mrithi wake mamlaka na kuendelea na maisha yake ya kustaafu.

th

Kabla ya kustaafu kwake , kamati ya makabidhano ya mamlaka ilifanya kikao chake siku ya Ijumaa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Joseph Kinyua, alipokuwa akihutubia wanahabari kutoka , alisema tarehe ya kuapishwa kwa rais mteule itatangazwa kuwa siku ya mapumziko

Alisema kwamba mamlaka ya kamati hiyo yataanza kufanya kazi mara tu tume ya uchaguzi itamtangaza rasmi rais mteule.

Lakini baada ya kuhudumu kwa mihula miwili, Je maisha ya rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta yatakuwaje.

Mafao ya rais anayeondoka madarakani

th

Rais Uhuru Kenyatta ambaye anatarajiwa kuondoka madarakani atakabidhiwa marupurupu mengi ya kustaafu, ikiwa ni pamoja na kundi la magari ya kifahari, ofisi ya kibinafsi iliyo na samani kamili na wafanyakazi kadhaa baadaye mwaka huu.

Sheria inampatia wasaidizi wawili wa kibinafsi, makarani wawili, wajumbe wanne, madareva wanne pamoja na walinzi wanne katika ofisi yake mpya na wafanyakazi wanne wa nyumbani chini ya mfumo unaosimamiwa na walipa kodi. Wafanyakazi hao watatolewa na serikali.

.
Maelezo ya picha, Gari aina ya Buggatti

Vilevile wafanyakazi hao watashirikisha makatibu wa habari na maafisa wa usalama watakaolipwa na serikali. Rais Kenyatta pia atakabidhiwa magari manne ikiwemo magari mawili aina ya limousine na magari mawili aina ya sport ambayo hubadilishwa kila baada ya miaka minne.

Marupurupu

Pia atakabidhiwa marupurupu ya kila mwezi ya shilingi 300,000 , marupurupu ya mafuta ya ksh.200,000, marupupuru ya burudani ya ksh. 300,000 na marupurupu mengine ya ksh 300,000 yatakayolipa kodi ya maji na umeme pamoja na bima ya afya.

Mbali na hayo rais Uhuru Kenyatta pia atakabidhiwa ofisi yenye samani iliokamilika , takrima ya mwaka mmoja kwa kila muhula aliohudumu mbali na pensheni ya kila mwezi ya asilimia 80 ya mshahara wake aliopata katika mwezi wake wa mwisho. Mshahara rasmi wa rais ni ksh. Milioni 1.44.

.
Maelezo ya picha, Rais Uhuru Kenyatta atakuwa na uwezo kusafiri katika maeneo mbali mbali kujivinjari na familia yake

Bima ya afya ya rais anayeondoka madarakani inamruhusu kupata matibabu nyumbani na ughaibuni. Bima hiyo pia inamshirikisha mkewe Margeret Kenyatta.

Mafao ya kustaafu ya marais wastaafu yamezingatiwa sana, haswa katika miaka michache iliyopita wakati mgao uliongezeka kwa kiasi kikubwa, licha ya serikali kusisitiza kuwa imeweka hatua za kubana matumizi ili kukabiliana na mishahara mikubwa ya wafanayakazi wa umma .

.
.