Mfahamu Spika mpya wa Bunge la Kenya Moses Wetangula

Chanzo cha picha, kbc
Kiongozi wa chama cha Ford-Kenya, Moses Wetangula, ametangazwa kuwa spika wa bunge la Kenya baada ya mgombeaji wa Azimio la Umoja, Kenneth Marende, kujiondoa katika awamu ya pili ya kinyang'anyiro hicho.
Tangazo hilo liliwasilishwa kwa katibu wa bunge na Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed.
Wetangula alimshinda Kenneth Marende wa muungano wa Azimio la Umoja katika awamu ya kwanza ya kinyang'anyiro cha Spika wa Bunge la Kitaifa.
Katika kura hiyo Seneta huyo wa zamani wa Bungoma alipata kura 215 dhidi ya 130 za Marende.
Alikuwa anahitaji zaidi ya kura 230, theluthi mbili ya kura zilizopigwa ili kushinda kiti hicho katika raundi ya kwanza .
Lakini Je Moses Wetangula ni nani haswa?
Jina kamili la Wetangula ni Moses Masika Wetangula. Alizaliwa tarehe 13 Septemba 1956 katika Tarafa ya Nalondo, Kaunti ya Bungoma.
Moses ni mwanasiasa wa Kenya. Alichaguliwa katika Seneti ya Kenya mnamo 2013, akiwakilisha Kaunti ya Bungoma, na kuwa Kiongozi wa Wachache katika Seneti.
Elimu
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wetangula alisomea Shule ya Msingi ya Nalondo, kisha akajiunga na Shule ya Sekondari ya Teremi na Shule ya Friends Kamusinga kwa elimu ya A-Level kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi, ambako alifuzu na shahada ya Sheria (LLB).
Wetangula baadaye aliteuliwa kuwa Hakimu Mkuu na Idara ya Mahakama. Baadaye alipandishwa cheo kama Hakimu wa Wilaya mwaka 1983.
Wetangula kisha aliacha kazi yake na kufuata sheria za kibinafsi kupitia kampuni yake ya mawakili, Wetangula & Company Advocates.
Siasa
Mnamo 1993, Wetangula aliingia katika siasa za kitaifa alipoteuliwa kuwa Mbunge na chama cha KANU ambako alihudumu hadi 1997. Alichaguliwa kama Mbunge wa Sirisia mwaka wa 2002 ambapo alifanikiwa kushinda kiti chake cha kwanza cha kisiasa.
Umaarufu wake hatahivyo uliongezeka alipohudumu katika wizara ya Mambo ya Nje. Baada ya jukumu lake katika kampeni za Rais wa zamani Mwai Kibaki katika uchaguzi wa 2007, Wetangula aliteuliwa katika nafasi hiyo ya juu mwaka wa 2008.
Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi huo yalipingwa na chama cha Orange Democratic Movement (ODM) ambacho kilisababisha mazungumzo ya kuzipatanisha pande hizo mbili.
Alikuwa Kiongozi wa Wachache katika Seneti
Baada ya kushinda uchaguzi katika bunge la Seneti, Wetangula alichaguliwa kuhudumu kama Kiongozi wa Wachache wa Muungano wa CORD.
Mnamo Machi 2018, Wetangula alitimuliwa kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika Seneti na nafasi yake kuchukuliwa na James Orengo.













