Mfahamu Spika mpya wa seneti Kenya Amason Jefwa Kingi

TH

Chanzo cha picha, AGENCIES

Amason Kingi wa muungano wa Kenya Kwanza amechaguliwa kuwa spika wa bunge la seneti nchini Kenya .

Kingi ambaye alihudumu kama gavana wa Kaunti ya Kilifi kwa mihula miwili alipata kura 46 na alipendekezwa kugimbea nafasi hiyo na mrengo wa rais mteule William Ruto .

Ni mwanasiasa aliyejiinua mwenyewe ambaye aliingia katika bunge kwa mara ya kwanza mnamo 2007 kama mbunge wa Magarini.

Alijipatia umaarufu wake baada ya kupiga marufuku sherehe zote za muziki za kijamii katika Kaunti ya Kilifi.

Je Amason Jefwa Kingi ni nani?

Amason Kingi alizaliwa Malindi, Kaunti ya Kilifi eneo la Pwani .

Elimu

Amason Jeffah Kingi alianza safari yake ya masomo katika shule ya msingi ya Magarini. Baadaye alijiunga na shule ya wavulana ya Alliance ambapo alimaliza masomo yake ya sekondari.

Kisha akaelekea Chuo Kikuu cha Nairobi ambako alifuzu na shahada ya Sheria.

Siasa

Amason Jeffah Kingi alijiunga na siasa mwaka wa 2007.

Wakati huo alifanikiwa kuchaguliwa kuwakilisha eneo bunge la Magarini kama Mbunge.

Awali kabla ya kuwa gavana Amason Kingi aliwahi kuwa waziri wa Uvuvi. Sasa atakuwa spika wa tatu wa seneti tangu bunge hilo kurejeshwa katika katiba mpya ya mwaka wa 2010.Maspika wengine waliomtangulia ni Ekwe Ethuro na Ken Lusaka.Lusaka sasa ni gavana wa kaunti ya Bungoma