Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yanatoa taswira gani kwa siasa za Tanzania?

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaendelea kupanga safu ya uongozi wake. Miongoni mwa teuzi kubwa zilizokwisha fanyika. Ni uteuzi wa Mabalozi wapya Mei 23, 2021. Juni, 2021 kulifanyika uteuzi wa wakuu wa wilaya.
Shughuli imeendelea kwa kufanyika uteuzi uliobadilisha kidogo sura ya Baraza la Mawaziri siku ya jana. Mawaziri wanne wamepewa majukumu, wawili wakiwa wanawake na wawili wanaume. Pia kumefanyika uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Haya ni mabadiliko madogo ya pili ya baraza hilo tangu kifo cha Rais John Pombe Magufuli March 17, 2021. Mabadiliko ya kwanza yalifanyika Machi, 2021 Ikulu ya Chamwino, Dodoma wakati wa hafla ya kumuapisha makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango.
Uwiano huu wa kijinsia katika uteuzi wa Mawaziri wa sasa, unaakisi pakubwa ahadi ya Rais Samia ya kuleta usawa wa kijinsia katika nafasi za kiungozi. Ingawa safari bado inaweza kuwa ni ndefu kufikia usawa wa hamsini kwa hamsini.
Zanzibar yakumbukwa
Msomi wa mawasiliano ya Teknolojia ya Habari na mwanasiasa Profesa. Makame Mnyaa Mbarawa, ameteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi. Akichukua nafasi ya Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Ukosoaji makubwa ulisikika wakati wa uteuzi wa Baraza la Mawaziri chini ya Hayati John Pombe Magufuli, Disemba 2020; baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba wa mwaka huo. Ukosoaji ulitokana na kukosekana Waziri kamili kutoka upande wa Zanzibar.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ipo kwa misingi ya Muungano wa nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar. Hivyo, naamini Serikali inaundwa ina wajibu wa kuwa na Baraza la Mawaziri lenye kuakisi sura ya Muungano.

Chanzo cha picha, Twitter
Kuteuliwa kwa Profesa Mbarawa, ambaye Mbunge wa Mkoani, Pemba na amewahi kuhudumu kama Waziri wa Maji pia Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika awamu zilizopita. Ni hatua moja mbele kuelekea kuwa na Baraza la Mawaziri lenye mawaziri kutokea visiwani. Hii inatokana na ukweli kwamba kabla ya uteuzi wa Mbarawa, hapakuwepo waziri kamili kutoka Zanzibar.
Kilikuwa ni kitendawili kilichokosa jawabu hadi leo; juu ya kipi kiliusukuma utawala wa Magufuli kutotoa nafasi ya Waziri kama ilivyozoeleka katika tawala zilizopita. Na kuifanya Zanzibar kutokuwa na Waziri hata katika Wizara ambazo zinashughulika na masuala ya Muungano.
Eneo lisilomridhisha Rais
Moja ya eneo ambalo Rais Samia amekuwa akirudia kauli za ukosoaji, ni kutoridhishwa na mifumo ya upatikanaji haki, kuazia katika Jeshi la Polisi na namna baadhi ya kesi zinavyoshughulikiwa.
Ni mara kadhaa amenukuliwa akihoji namna washitakiwa wanavyokaa muda mrefu rumande, ubambikaji wa kesi. Pia amewahi kugusia kadhia ya matumizi ya nguvu kupita kiasi ya Jeshi la Polisi.
Kwa kuzingatia majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, baadhi yakiwa ni kuishauri Serikali juu ya mambo ya kisheria na kuzishauri idara na taasisi zingine:
Uteuzi wa Dkt. Eliezer Feleshi, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akipokea kijiti kutoka kwa Prof. Adelardus Kilangi; zinaweza kuwa ni juhudi za kujaribu kufanya mageuzi anayoyataka Rais katika mifumo ya upatikaji wa haki kwa watuhumiwa.
Kusahau yaliyopita na kuganga yajayo
Mbunge wa Bumbuli kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, (CCM), January Makamba ameteuliwa kuwa Waziri wa Nishati, hivyo kuchukua nafasi ya Dkt. Medard Kalemani.
Wakati wa Rais Magufuli, Makamba aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Kisha akatumbuliwa mnamo Julai 2019.

Maisha yake ya kisiasa yalikumbwa na mkosi baada ya kuwa katika kundi la vigogo wa chama tawala waliotuhumiwa kuanzisha zengwe dhidi ya Magufuli. Kwa kile kilichoonekana kutoridhika na namna Rais huyo alivyokuwa akiendesha nchi.
Hadithi ya zengwe lile ni ndefu. Lakini iliishia kwa wengi wao katika kundi hilo kumuomba radhi Magufuli na chama kikatoa onyo kali baada ya mambo yao kugundulika.
Kurudishwa kwa January Makamba katika serikali, ni ujumbe kuwa Magufuli aliwasamehe kwa dhati tofauti iliyotokea imezikwa na kusahauliwa kwa kanuni ya kuacha yaliyopita na kuganga yajayo.
Historia yaandikwa
Rais Samia ameihamishia Idara ya Habari katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kwa maana hiyo Wizara mpya itafahamika kama Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Wizara hii itashikwa na mwanamke Dkt. Ashatu Kijaji anayechukua nafasi ya Dkt. Faustine Ndugulile. Atakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Wizara hii iliyopanguliwa na kupangwa kivingine.
Changamoto kubwa inayomkabili ni uhuru wa vyombo vya habari dhidi makucha ya Serikali yake. Tanzania imekuwa na historia mbaya ya kuandama vyombo vya habari. Wakati huu ikiwa tayari imeyafungia magazeti mawili ndani ya mwezi mmoja.

Chanzo cha picha, Dkt. Kijaji/Twitter
Lililo kubwa zaidi hasa ni uteuzi wa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, DKt. Stergomena Tax, akimrithi Elias John Kwandikwa aliyefariki Agosti 3, 2021.
Licha ya Tanzania kuwa na wanawake wanaofahamika bayana katika historia ya siasa zake na mapambano ya uhuru. Wizara ya Ulinzi haikuwahi kushikwa na mwanamke tangu uhuru kutoka kwa mkoloni.
Hivi karibuni Dkt. Stergomena Tax aliteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania. Uteuzi umekuja baada ya kumaliza muda wake akiwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika - SADC hivyo kuzua tetesi kuwa kungekuwepo mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri.

Chanzo cha picha, Dkt. Stergomena Tax/Twitter
Malengo yoyote ya kisiasa au kiutawala juu ya teuzi hizi yatafichuka katika utendaji wa walioteuliwa. Namna Rais Samia anavyozichanga karata zake katika baraza la Mawaziri baada ya kifo cha Magufuli, ni wazi kuwa anazichanga kwa kupangua viti ingawa wakaliaji ni walewale.












