Vyama vya korosho vyadaiwa kulipa wakulima hewa

Serikali nchini Tanzania kuchunguza madai ya ubadhirifu na rushwa ya mabilioni katika ununuzi wa korosho msimu uliopita.Mwaka jana serikali iliingilia kati biashara ya korosho kufuatia mvutano wa bei kati ya wakulima na wafanyabiashara. Vyama vya msingi vilikuwa moja ya taasisi za serikali zilizohusika kufanikisha biashara ya korosho msimu uliopita.
Mwaka jana serikali hiyo iliweka bei elekezi za korosho kwa kupitia vyama vya ushirika kati ya wakulima na wafanyabiashara.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema hata fedha zilizotolewa siku za hivi karibuni kiasi cha shilingi Bilioni 40 kukamilisha malipo kwa wakulima hazijakamilisha kazi iliyokusudiwa.
Wapo wakulima wengi ambao bado wanalalamika kutokulipwa malipo yao.
Hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya Tanzania kukubali hadharani mapungufu baada ya kujiingiza katika biashara ya korosho msimu uliopita
Hasunga alitoa mfano wa chama kimoja cha msingi cha Pwani, SangaSanga Amcos ambacho alidai kilidanganya kwamba kilinunua kilo laki mbili na kumi na nane za korosho ilhali uhakiki ulibaini chama hicho kilinunua kilo 212 tu
Aliongeza vyama vingine vimeonekana kufanya malipo hewa na kudanganya juu ya madaraja ya korosho waliyonunua ili waongeze bei waliyotakiwa kulipa
Tume imepewa hadi tarehe 15 Januari kuwa imekamilisha jukumu lake.
Kujiingiza kwa serikali kwenye biashara ya korosho mwaka jan kulisababisha kupanda kwa bei ya korosho katika soko la dunia na kuvuruga uzalishaji wa biashara ya korosho nchini
Pamoja na mabadiliko mengine, msimu wa mwaka huu serikali imeacha soko huria kupanga bei ya biashara ya korosho

Waziri mkuu amtoa madarakani
Mara baada ya uamuzi wa uchunguzi wa fedha za korosho kupotea, waziri mkuu wa taifa hilo Kassim Majaliwa amemtaka kaimu mkuu wa mkoa wa Ruvuma, kusini mwa Tanzania kumuondoa mkurugenzi wa bodi ya korosho katika wadhifa wake.
Waziri mkuu amedai kufurahishwa na zoezi la mnada wa korosho ambalo linaendelea lakini hajafurahia kusikia kuwa kiasi cha shilingi milioni 40 za kitanzania ambazo rais alituma ili wakulima walipwe hawajalipwa wakati ilifahamika kuwa zimeshalipwa.
"Nataka ufuatile ujue hizo fedha zimekwama wapi...?''
Malalamiko ya wakulima hapo awali?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakulima walisema kuwa bei za korosho zilizopangwa na wafanyabiashara hazikidhi gharama za uzalishaji kwa kuwa upatikanaji wa pembejeo ni mgumu, hivyo zao lao haliwalipi.
''Hatujaweza kupata mtetezi wa moja kwa moja na hatua zinazochukuliwa na serikali zinaishia njiani na utekelezaji unakuwa mdogo, hatujajua Rais anakwama wapi au katika mapambano haya yuko peke yake''. Anaeleza mkulima wa korosho mkoani Mtwara Hamisi Athumani Minjale maarufu Jaba.
''Tunaingia kwenye msimu mpya kwa hali ngumu kwa kuwa wakulima wengi hawajalipwa, ukiingia kwenye ghala yangu nina zaidi ya tani 19 bado ninahitaji pesa za kuendesha shughuli za kilimo, hivyo biashara hii tunaifanya kigumugumu''. Anaeleza Minjale.
Kwa mujibu wa soko la bidhaa hiyo nchini Uingereza, bei ilipanda kwa 10% mpaka dola 3.8 za marekani kwa kilo, kutokana na masuala ya usafirishaji wa korosho kutoka Tanzania.
Mwezi Juni 2019, Waziri wa fedha na mipango, Dokta Philip Mpango aliliambia bunge kuwa mauzo ya korosho kwa ujumla katika soko la kimataifa yalishuka kwa zaidi ya 60%.
Naye waziri wa kilimo Japhet Asunga, aliviambia vyombo vya habari kuwa Tanzania inatarajia kuongeza uzalishaji wa korosho kwa 33.5% msimu huu.
Asunga alisema tani 300,000 za korosho zinatarajiwa kuzalishwa, kutoka tani 225,000 za msimu wa mwaka 2018/2019.
Tanzania ni mfanyabiashara muhimu katika soko la korosho duniani. Zao la korosho huzalishwa kwa wingi nchini Tanzania, likifuatiwa na chai, kahawa na katani.













