Wakulima wa korosho walalamika bado hawajalipwa, changamoto za ununuzi zaendelea Tanzania

Mkulima wa Korosho
Maelezo ya picha, Wakulima wa korosho wamekuwa wakikumbwa na changamoto mara kadhaa

Mwaka jana, serikali, iliingilia kati sakata la bei na kuamua kununua korosho yote iliyopo sokoni moja kwa moja kwa bei ya juu kidogo tofauti na iliyopangwa na wafanya biashara.

Lakini, miezi mitatu baadae, baadhi ya wakulima bado hawajalipwa huku wengine wakirudishiwa korosho zao kwa madai ya kuwa chini ya kiwango.

Korosho, ambayo miaka yote imekuwa ni dhahabu ya kusini, ni zao ambalo linaongoza nchini Tanzania kuingizia fedha za kigeni.

Hata hivyo, wakulima wa zao hili wamekuwa wakikumbwa na changamoto mara kadhaa.

Wafanyabiashara walisababisha mgogo mwaka jana mwezi Novemba pindi walipotaka kununua bidhaa hiyo kwa bei ambayo haina tija kwa mkulima.

Katika jitihada za kutatua mgogoro huo, serikali iliingilia kati na kuamua kununua korosho zaidi ya tani laki mbili kwa bei iliyodaiwa kuwa na maslahi kwa wakulima.

Lakini miezi 3 baadae, wakulima wanaendelea kulalamikia malipo yao.

Hamisi Mwinjale
Maelezo ya picha, Hamisi Mwinjale ni mkulima wa Korosho anasema malipo ya korosho sio mazuri

Hamisi Mwinjale, ni mkulima wa korosho, "Malipo ya korosho sio mazuri. hali sio nzuri kwasababu tumewasilisha katika ghala lakini mpaka sasa hakujakuwa na uthibitisho wowote. Tumeathirika pakubwa.''

Tatizo kubwa linaonekana ni ucheleweshwaji wa uhakiki wa majina ya wakulima na ubora wa korosho.

Wakulima wanadai, mchakato huo hauendi kwa kasi inayotakiwa huku serikali ikidai baadhi ya korosho ziko chini ya kiwango.

Waziri wa kilimo Josephat Asunga ameelezea yanayozingatiwa katika ununuzi wa korosho hizo, "Korosho tunazonunua zingawanywa kwa makundi matatu, kuna gedi ya kwanza, gredi ya pili na ya tatu ambayo huwa tunasema ni zisizofaa.

Kwa sasa tayari tumeshanunua za gredi ya kwanza, kilo kwa shilingi 3200 shillings, tunanunua gredi ya pili kwa shilingi 2600 kwa kilo, na kwa gredi ya tatu hatuzinunui, kwasababu iwapo ni chafu, na hifikii viwango vinavyostahili, tutazinunuaje?"

korosho

Chanzo cha picha, ISSOUF SANOGO

Kwa upande wake, serikali inasema, tayari ishalipa wale wenye korosho chini ya kilo 1000, huku wenye kilo zaidi ya elfu moja bado uhakiki unaendelea.

Mgogoro huu, umekuwa na athari kubwa.

Mpaka sasa, uandikishwaji wa watoto shuleni kwa mwaka mpya wa masomo, umeshuka kwa asilimia ishirini kwa sababu baadhi ya wazazi wanadai wameshindwa kumudu gharama.

"Nimepeleka kilo 1302 za korosho, zote zimerudishwa bila ya sababu. Limeniathiri pakubwa, siwezi hata kuwapeleka watoto wangu shule,' anasema Mohammed Champunga, mkulima wa korosho.

Maelezo ya video, Jeshi la Tanzania limeanza rasmi operesheni ya kuratibu ununuzi wa korosho

Tangu kuingia madarakani mwaka 2015, rais John Magufuli ambae alipewa jina la TingaTinga, amekuwa akichukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanaamini kwamba, kwa mgogoro kama huu kupata utatuzi, ni vyema kushirikisha wataalamu.

'Tulitarajia wanauchumi wangeongoza katika kutoa muelekeo wa kiuchumi wakati mawakili walitakiwa kuunda sheria na kuchora mpaka wa kulinda mawazo hayo. lakini tumeona katika mpangilio huu, mtazamao wa kihseria umongoza mtazamao wa kiuchumi.

Na ndio sababu imekuwa vigumu mno kufikiria kwa mtazamo wa soko la kimataifa, na nafasi ya korosho katika soko la dunia' anasema mwanauchumi Bravis Kayozya, kutoka nchini Tanzania.

Lakini jitihada za kutatua mgogoro huu, hazitaonekana hadi hapo wakulima wakulima watakapolipwa fedha zao.