Sakata la Korosho: Waziri wa Kilimo Charles Tizeba, Waziri wa Biashara Charles Mwijage watimuliwa kazi

Chanzo cha picha, AFP
Sakata la korosho nchini Tanzania limechukua sura mpya mara baada ya Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwatimua mawaziri wawili katika baraza lake.
Waziri wa Kilimo Charles Tizeba na Waziri wa Biashara Charles Mwijage watimuliwa kazi hii leo tarehe 10 Novemba, 2018 mara baada ya rais kuwahakikishia wananchi kuwa serikali itanunua korosho kwa bei elekezi ya shilingi 3000 ya Tanzania.
Mzozo wa korosho ulianza mara baada ya wakulima kugomea bei mpya kati ya Sh1,900 mpaka Sh2,700 kwa kilo ikiwa ni anguko la kutoka wastani wa Sh 4,000 kwa kilo msimu uliopita.
Tarehe 28 Oktoba 2018, Rais Magufuli alifanya kikao na wanunuzi wakuu wa zao hilo na kuwaeleza kuwa serikali inaunga mkono msimamo wa wakulima.
Magufuli alienda mbali kwa kusema serikali yake ipo radhi kuzinunua korosho zote kwa bei inayowafaa wakulima na kuziuza katika masoko ya kimataifa nchini Marekani na Uchina.
"…nipo tayari hata kutumia majeshi yetu kununua korosho na tutatafuta masoko ya uhakika ili tuuze kwa bei nzuri" amesisitiza Rais Magufuli.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao walikubali kununua korosho kwa bei isiyopungua shilingi 3,000. Huku serikali pia ikikubali kuondosha baadhi ya tozo na vikwazo vitakavyopelekea wafanyabiashara kushusha bei.
Pamoja na makubaliano hayo na wafanyabiashara, leo hii rais Magufuli amekagua magari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyoandaliwa kwa ajili ya kubeba korosho za wakulima endapo wanunuzi binafsi hawatatii maagizo ya Serikali ifikapo Jumatatu tarehe 12 Novemba, 2018 saa 10:00 Jioni.
Jana serikali ya Tanzania kupitia waziri mkuu Khassim Majaliwa ilitishia kuwafutia leseni watakaokaidi utaratibu uliopangwa wa bei ya korosho.
Vilevile serikali hiyo ilisema itachukua hatua ya kutumia JWTZ na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kununua korosho zote za wakulima kwa bei ya zaidi ya shilingi 3,000 kwa kilo na hatakuepo mnunuzi yeyote binafsi atakayeruhusiwa kununua korosho.

Rais Magufuli amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuteua Mawaziri wawili na Naibu Mawaziri wanne leo tarehe 10 Novemba, 2018 .
Rais Magufuli amemteua Japhet Ngailonga Hasunga kuwa Waziri wa Kilimo, Hasunga alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, na anachukua nafasi ya Dkt. Charles John Tizeba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Joseph George Kakunda kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Kabla ya uteuzi huo Mhe. Kakunda alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), na anachukua nafasi ya Charles John Mwijage ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Tatu, Rais Magufuli amemteua Constantine John Kanyasu kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Kanyasu anachukua nafasi ya Hasunga ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo.
Nne, Rais Magufuli amemteua Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Kabla ya uteuzi huo Dkt. Mwanjelwa alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Rais Magufuli amemteua Mwita Mwikwabe Waitara kuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI.
Waitara anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Kakunda ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Rais Magufuli amemteua Innocent Lugha Bashungwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo. Bashungwa anachukua nafasi ya Dkt. Mwanjelwa ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Rais Magufuli ametengua pia uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Mama Anna Margareth Abdallah na kuivunja bodi hiyo kuanzia leo tarehe 10 Novemba, 2018.
Uteuzi wa viongozi hawa umeanza leo tarehe 10 Novemba, 2018 na wateule wote wataapishwa Jumatatu tarehe 12 Novemba, 2018 saa 3:00 asubuhi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.












