Rais Magufuli: 'Serikali itanunua korosho zote na fedha za kununulia zipo'

Chanzo cha picha, AFP
Leo rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekagua magari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyoandaliwa kwa ajili ya kubeba korosho za wakulima endapo wanunuzi binafsi hawatatii maagizo ya Serikali ifikapo Jumatatu tarehe 12 Novemba, 2018 saa 10:00 Jioni.
Rais Magufuli amefanya ukaguzi huo katika Kambi ya Jeshi ya Twalipo, Kikosi cha Usafirishaji cha 95KJ Mgulani Jijini Dar es Salaam ambapo magari 75 yenye uwezo wa kubeba tani 1,500 kwa mpigo yameandaliwa kwa ajili ya kubeba korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na Tanga.
Akizungumza na Maafisa na Askari wa JWTZ waliokuwepo wakati wa ukaguzi huo, Rais Magufuli amesema endapo wanunuzi binafsi hawatatii maagizo ya Serikali ya kununua korosho za wakulima kwa bei isiyopungua shilingi 3,000 kwa kilo sambamba na kutii agizo lililotolewa jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Aidha serikali itachukua hatua ya kutumia JWTZ na Bodi ya Mazao mchanganyiko kununua korosho zote za wakulima kwa bei ya zaidi ya shilingi 3,000 kwa kilo na hatakuepo mnunuzi yeyote binafsi atakayeruhusiwa kununua korosho.

Chanzo cha picha, USHIRIKA
Rais Magufuli amebainisha pi kuwa baada ya kununua korosho, Serikali itatafuta soko na korosho nyingine zitabanguliwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
"Nataka kuwahakikishia wakulima wa korosho Serikali ipo na itaendelea kuwapigania, ikifika Jumatatu saa 10:00 jioni, hawa wanunuzi binafsi hawajajitokeza na kueleza watanunua tani ngapi, Serikali itanunua korosho zote na fedha za kununulia zipo" amesema Rais Magufuli.

Serikali ya Tanzania imedai kulazimika kuchukua hatua hizi baada ya wanunuzi binafsi kufanya mgomo wa kununua korosho kwa kusuasua licha ya kufanya nao mazungumzo na kufikia makubaliano tarehe 28 Oktoba, 2018 Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo Serikali iliungana na msimamo wa wakulima wa korosho wa kukataa bei ya kati ya shilingi 1,900 hadi 2,700 kwa kilo, na hivyo kukubaliana kuwa korosho zitanunuliwa kwa bei isiyopungua shilingi 3,000 kwa kilo.
Mpaka sasa kati ya kampuni 37 zilizoomba kununua korosho ni kampuni 14 tu ndizo zimejitokeza na ununuzi unafanyika kwa kusuasua.
Takribani tani 210,000 za korosho zipo mkoa wa Lindi na Mtwara huku kuna maghala yanayoweza kuhifadhi zaidi ya tani 90,000 jijini Dar es salaam.

"Na kutokana na jambo hili, sasa JWTZ kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ianze kufikiria kuanzisha kiwanda kikubwa cha kubangua korosho, hata kama itakuwa ni kwa Serikali kutoa fedha za kujenga kiwanda hicho, tuanze kuachana na uuzaji wa korosho ghafi, huo ni utumwa, tuwe na viwanda vyetu na vijana wetu wapate ajira" amesisitiza Rais Magufuli.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Mabeyo amesema JWTZ imetayarisha magari ya uwezo tofauti 75 yenye uwezo wa kubeba jumla ya tani 1,500 kwa mpigo na kwamba tani nyingine 500 zitabebwa na meli ya kijeshi ambayo inaweza kutia nanga mahali popote katika ufukwe wa bahari.












