Kuongezeka uzito ni changamoto inayowakabili wanawake wengi wanapotoka kujifungua

Watu wengi huwa wanapenda kuweka picha zenye muonekano mzuri kwenye mitandao ya kijamii.
Na kufanikisha hilo huwa wanafanya jitihada za ziada ili kuendelea kutunza miili yao.
Lakini kwa upande wao mama waliotoka kujifungua changamoto huwa ni kubwa zaidi kwa sababu kipindi anapopata mtoto mwili wake huwa unabadilika pia kwa kuongezeka.
Hali ambayo inawafanya wanawake wengi kutamani kupungua uzito mara baada ya kujifungua.
Japo huwa ni jambo rahisi kwa baadhi, lakini wengi wao huwa wanapitia wakati mgumu.
Unaweza kusoma pia :
Doreen Umutesi, ni mama kutoka Rwanda yeye anasema hakuwa na tatizo lolote wakati alipokua na mimba ya mwanawe.
" Nimejaliwa na mtoto mvulana ana mwaka mmoja na miezi mitatu. Wakati wote wa ujauzito wangu, sikuwa na tatizo lolote. Kwangu ilikuwa kama kipindi cha kawaida maishani.
Wakati ambao naweza kusema nilipata ugumu ni wakati wa kujifungua nilipata uchungu sana".
Baada ya Doreen kijifungua mtoto wao salama na kurejea nyumbani, umbo lake lilianza kubadilika kwa kuongezeka uzito kila kukicha.
"Wakati wa ujauzito niliongeza uzani, lakini hiyo ilikua kawaida. Lakini punde baada ya kujifungua kila baada ya wiki mbili nilikuwa naongezeka uzito. Nilianza kunenepa, na nguo zangu zikawa hazinitoshi tena.
Wakati nilipojifungua uzito wangu ulikua kama Kilo 102 na pointi saba. Mwanangu alipofikisha miezi minane, uzito wangu ulifika kilo 120.
Kabla ya ujauzito nilikuwa na uzito wa kilo 85 na nilishauriwa kutoongeza uzani zaidi ya kilo 90, kisha nilijikuta nna kilo 120, hali hiyo ilinshtua sana."

Baadhi ya tafiti zinaonyesha kwamba inachukua kama miezi tisa kwa mwanamke kurejelea umbile lake la awali baada ya kujifungua mtoto.
Lakini kwa upande wake Doreen, imemchukua zaidi ya mwaka mmoja kutafakari jinsi ya kupunguza uzani wake unaoendelea kuongezeka.
Baada ya muda alipata ushauri kutoka kwa mama mwenzake kwa jina Amanda, na kumueleza kuhusu mazoezi yanayoweza kumsaidia kupungua.
Alimuelekeza pia kuhusu ukumbi wa kufanyia mazoezi uliopo mjinii Kigali na Doreen unaotolewa mafunzo na bi. Claire Munesi.

Katika ukumbi huo wanawake wameamua lazima wapunguze uzito wao.
Claire ambaye ni mama wa miaka thelathini na nne amekua akiwasaidia wanawake kupunguza uzito kwa kufanya mazoezi haswa baada ya kujifungua.
Binafsi Claire alikua na uzani wa kilo sabini na mbili kabla ya kupata mimba. Alipokaribia kujifungua alikuwa na uzito wa kilo mia moja na nane..
Punde baada ya kujifungua alichukua picha yake ya zamani na kuanza hatua za kupunguza uzito aliopata baada ya kujifungua.
"Baada ya wiki mbili, nilianza mazoezi... pamoja na kutembea kwa kwa muda wa nusu saa, nilitumia kipindi cha miezi mitatu ambacho wanawake hupumzika baada ya kujifungua kuhakikisha narejesha umbile langu la kawaida."
Lakini anasema kuwa jambo la muhimu zaidi ambalo alilizingatia ni kuwa makini sana lishe yake na kunywa maji mengi.
Baada ya juhudi zote hizo Claire aliweza kupunguza uzito wa kilo 28 kwa kipindi cha miezi sita, baada ya kujifungua mwanae wa kiume.
Wataalamu wa afya mara nyingi huwashauri wanawake kutofanya mazoezi hadi pale watakapohudhuria uchunguzi wa kwanza baada ya kujifungua.
DR. Butoyi Alphonce mtaalamu wa afya ya uzazi mjini Kigali.
" Wakati mwanamke anapojifungua kwa njia ya kawaida ni sawa wakianza mazoezi baada ya wiki moja hadi wiki tatu. Lakini hali ni tofauti kwa wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji.
Ni muhimu kwao kuhakikisha kwamba wamepona kidonda, baada ya mwezi anaweza kuanza kutembea kwa muda wa nusu saa, kuogelea, japo siyo kwa nguvu sana."

Doreen ana malengo ya kupunguza uzito wake kwa kilo 30 ifikapo mwisho mwezi decemba.
Kando ya kufanya mazoezi, Doreen pia ameanza kuwa makini sana na lishe yake aliyoshauriwa na Claire..
Wanawake wanaweza kupata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa lishe, ili kufahamu vyakula wanavyostahili kula kila siku.
Lazima vyakula viwe na madini ya Protini, Vitamini na vile vyenye kuongeza nguvu.
Sio lazima kuacha kula vyakula vya nguvu kama ngano, wali, hivyo ni muhimu ni kula kiwango kidogo tu.
"Mimi hula vyakula vya wanga kwa kiasi tu.Huwa siweki sukari kwenye chai au kahawa. Nakula mboga za majani nyingi, matunda ,juisi na maji.
DR. Butoyi anashauri kuhusu lishe kwa wanawake wanaonyonyesha .
" Kwa wanawake ambao wananyonyesha , hawahitaji kula kiasi cha kushindwa hata kutembea. Naona jamii nyingi hapa Afrika wanawake hupenda kula kupita kiasi, wanakula zaidi ya mara nne kwa siku."













