Mfanyakazi wa ndani wa Uganda nchini Syria hatarajiwi kunyongwa
Balozi wa Syria nchini Uganda Dkt. Tamouh Moustafa anasema mfanyakazi wa ndani kutoka Uganda anayetuhumiwa kumuua mwajiri wake nchini Syria hana uwezekano wa kunyongwa.
Moustafa alikuwa akizungumza na gazeti la Daily Monitor la Uganda alipoelezea kwamba tukio hilo lilitokana na mawasiliano yasiyofaa yaliyosababishwa na ujuzi mdogo wa lugha ya Kiingereza wa mwathiriwa na ujuzi mdogo wa Vicky wa Kiarabu.
Mapema wiki hii, ripoti zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zilidai kwamba Vicky Ajok alipangwa kunyongwa nchini Syria mnamo tarehe 28 Februari, baada ya kukiri na kupatikana na hatia ya kumuua mwajiri wake, Huda Shaarawi, mnamo tarehe 29 Januari katika mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus.
"Mwathiriwa alimwambia (Vicky) asiguse chakula chake au friji yake. Alitumia neno 'sumu,' ambalo halikuwa neno sahihi.
Alichotaka kusema ni kwamba 'umeambukizwa na unaweza kuniambukiza.' Hilo ndilo mwathiriwa alilokusudia kumwambia msichana huyo," Moustafa alisema.
Aliongeza kuwa Vicky aliposikia neno "sumu," hakuelewa vizuri. "Msichana alikuwa mgonjwa, na aliposikia neno 'sumu' , na unajua hapa Uganda neno hili la sumu ni la kawaida sana kusikia , kwa hivyo alipofikiria kwamba 'bibi huyu kizee amenipa sumu, ambayo ina maana kwamba nitakufa hivi karibuni, kwa hivyo tutakufa pamoja'. Hilo ndilo lililomtokea," Moustafa alifafanua.
Balozi huyo alisema Syria sasa ina mfumo wa kisheria ulio wazi, akiongeza kwamba hakuna shinikizo linalotolewa kwa msichana huyo. "Nchini Syria, adhabu ya kuua inaweza kuwa kifo, hiyo ni kweli, lakini si hivyo tu. Sio kila mauaji, na si mara moja. Kesi lazima ipitie hatua nyingi kabla haijafikia hatua hiyo," Moustafa aliambia Daily Monitor.
Aliendelea kusema kwamba utekelezaji hautatekelezwa Jumamosi, akiongeza kwamba huenda usifanyike kabisa. Mwanadiplomasia huyo alisema kuna mambo kadhaa katika kesi hiyo ambayo yanaweza kumsaidia Vicky kuepuka adhabu ya kifo.
Akizungumza na BBC nyumbani kwao katika kijiji cha Paidwe, kaskazini mwa Uganda, baba yake Vicky, Kitara Simon, alitoa wito kwa serikali na jamii ya Waluo nchini Uganda na nje ya nchi kuingilia kati suala hilo na kuokoa maisha ya binti yake.
"Ninatoa wito kwa serikali, na jamii ya Waluo wanaoishi nje ya nchi na hapa, kuungana na kunisaidia kumrudisha binti yangu nyumbani, binti yangu hana hatia.
Kwa ufahamu wangu tangu alipokua hapa, najua hawezi kufanya hivyo," alisema Simon. Kesi ya Vicky imevutia umakini mkubwa, ikirudia kesi za zamani zilizowahusisha wafanyakazi wa ndani wa Kiafrika katika Mashariki ya Kati, ambao wengi wao wameripoti unyanyasaji wa kimwili na kingono, pamoja na kutolipwa mishahara.