AFCON 2025: Sahau 16 bora, haya ni mafanikio mengine 5 ya Tanzania

Muda wa kusoma: Dakika 7

Kwa mara ya kwanza katika historia yake ya ushiriki wa AFCON, Tanzania (Taifa Stars imevuka hatua ya makundi na kuingia 16 bora. Hilo peke yake tayari ni habari kubwa. Lakini kwa macho ya uchambuzi wa kina, kufuzu huku ni sehemu ndogo tu ya simulizi pana zaidi kuhusu mabadiliko ya Taifa Stars katika soka la Afrika.

Kwa miaka mingi, Tanzania imekuwa ikipewa nafasi ya "mshiriki" badala ya "mshindani" kwenye mashindano makubwa. Ilikuwa timu inayokuja kujifunza, kukutana na wakubwa, kisha kuondoka mapema. AFCON 2025 imebadilisha kabisa taswira hiyo. Sio tu kwa matokeo, bali kwa namna timu imecheza, imehimili presha, na imejijengea utambulisho mpya.

Kundi C lilikuwa gumu, Nigeria yenye historia na ubora wa kudumu, Tunisia iliyozoea hatua za mtoano, na Uganda jirani anayefahamiana vyema na Tanzania kwa mazingira ya soka la Afrika Mashariki.

Ndani ya muktadha huo, Tanzania haikuonekana kama timu ya kuleta ushindani, bali kama mshiriki anayekuja kujifunza na kujiandaa kwa ajili ya michuano ijayo, lakini akapata mabao bila ushindi, akakusanya alama kwa sare mbili, na hatimaye akafuzu 16 bora kupitia nafasi ya mshindi wa tatu bora wa kundi C. Ilishindwa kufanya hivyo mwaka 1980, 2019 na 2023.

Lakini hata baada ya shangwe za kufuzu 16 bora hilo ni muhimu na jambo moja tu, lakini kuna masuala kadhaa zaidi ya mafanikio yanayostahili kuangaliwa. Kwa kuondoa hisia na kuangalia takwimu, historia na mwelekeo wa timu, AFCON 2025 imeacha alama tano muhimu zinazothibitisha kuwa Taifa Stars ipo kwenye njia ya mabadiliko ya kweli.

1. Nafasi ya tatu kwa mara ya kwanza katika kundi

Kwa mara ya kwanza, Tanzania imemaliza kundi katika nafasi ya tatu. Kihistoria, hili ni jambo kubwa zaidi kuliko linavyoonekana.

Mwaka 1980, Tanzania ilimaliza ya mwisho kwa alama moja. Mwaka 2019, ilimaliza ya mwisho bila alama. Mwaka 2023, tena ilijikuta mkiani kwa alama mbili. AFCON 2025 imevunja mfululizo huo wa kumaliza mkiani, na kuonyesha kuwa Taifa Stars sasa inaweza kushindana kwa alama, si kwa heshima pekee.

Nafasi hii ya tatu pia imeleta Tanzania kwenye mjadala wa kisasa wa AFCON, mfumo wa ''best third-placed teams'', timu zinazoshika nafasi ya tatu na kusonga mbele. Mataifa kama Benin na hata Ivory Coast, mabingwa watetezi wa zamani, waliwahi kutumia njia hii kufika hatua za juu. Tanzania sasa ipo kwenye ramani hiyo ya kimkakati ya mashindano haya.

Zaidi ya hilo, kumaliza ya tatu kunamaanisha kuwa Taifa Stars haikubahatisha, bali ilifanya kazi ya kukusanya alama kwa juhudi. Sare dhidi ya Uganda na Tunisia, pamoja na ushindani dhidi ya Nigeria, zimejenga picha ya timu inayojua inalinda nini na inapigania nini katika kila dakika 90.

2. Kufunga bao katika kila mechi

Tanzania imefunga mabao matatu kwenye AFCON 2025, mafanikio ambayo hayajawahi kutokea tangu mwaka 1980. Wakati huo, Taifa Stars ilifunga mabao matatu katika mechi tatu, ilipofungwa 3–1 na Nigeria, 2–1 na Misri, na kutoka sare ya 1–1 dhidi ya Ivory Coast.

Baada ya hapo, hali ilizidi kuwa ngumu. AFCON 2019 ilipata mabao mawili pekee ikipigwa na majirani zao kenya 3–2 na kupoteza kwa Algeria na Senegal. AFCON 2023 ilikuwa ya maumivu zaidi. Ilipata bao moja tu dhidi ya Zambia, mechi zingine ilipata kipigo cha 3–0 kutoka Morocco na sare tasa dhidi ya DR Congo.

AFCON 2025 imebadilisha simulizi hii. Taifa Stars imefunga katika kila mechi ya kundi, ikionyesha maendeleo ya wazi katika eneo ambalo kwa miaka mingi lilikuwa tatizo kubwa, nalo ni ushambuliaji na ujasiri mbele ya lango.

2. Kufungwa mechi moja tu kwenye michezo mitano ya AFCON

Mbali na historia ya kufuzu na kufunga bao katika kila mechi , Tanzania imeonyesha dalili muhimu za kukua kiushindani katika ngazi ya juu ya soka la Afrika. Katika michezo mitano ya fainali za AFCON iliyochezwa tangu michuano ya 2023 hadi sasa, Taifa Stars imepoteza mechi moja tu, kipigo hicho kikiwa ni dhidi ya Nigeria cha 2-1 wiki iliyopita, moja ya vigogo wa soka la Afrika. Huu ni mwelekeo tofauti kabisa ukilinganisha na taswira ya awali ya Tanzania kama timu iliyokuwa ikipoteza kwa urahisi katika hatua za makundi.

Katika kipindi hicho, Tanzania imetoka sare dhidi ya DR Congo na Zambia kwenye AFCON 2023, kisha mwaka huu ikaendelea kushika kasi kwa sare dhidi ya Uganda na Tunisia. Matokeo haya yanaonyesha uthabiti wa kimfumo, uwezo wa kusoma mechi, na nidhamu ya kiuchezaji dhidi ya wapinzani wenye uzoefu mkubwa wa mashindano haya makubwa zaidi ya Afrika. Kwa mara ya kwanza, Taifa Stars haionekani tena kama mshiriki wa kujaza nafasi kwenye kundi, bali mpinzani anayeweza kuzuia na kushindana.

Aidha katika michezo hiyo mitano, Tanzania imefunga mabao manne na kufungwa mabao manne, uwiano unaoonyesha usawa wa ushindani badala ya pengo kubwa la ubora. Mara nyingi kwa Stars ilikuwa mabao ya kufungwa yanakuwa mara mbili au zaidi kuliko yale ya kufunga.

3. Zawadi nono ya kifedha

Zaidi ya mafanikio ya kiwanjani, AFCON 2025 imekuwa chanzo muhimu cha faida ya kifedha kwa Tanzania na wachezaji wake. Kwa kufuzu hatua ya 16 bora, Taifa Stars imejihakikishia zawadi ya dola za Marekani 800,000, sawa na karibu shilingi bilioni 2 za Tanzania, kulingana na mfumo wa zawadi wa CAF. Ni mojawapo ya fedha kubwa zaidi kuwahi kupatikana katika historia ya timu ya taifa, na ishara ya namna mafanikio ya ushindani yanavyoweza kuzaa thamani halisi nje ya uwanja.

Katika muktadha huo wa mafanikio, safari ya Tanzania imeongezewa uzito na motisha ya ndani kupitia mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan unaojulikana kama "goli la mama." Katika mechi dhidi ya Nigeria na Uganda, kila bao lililofungwa na Taifa Stars lilizawadiwa shilingi milioni 100 za kitanzania, karibu dola 40,000 kwa kila goli. Bao la kusawazisha dhidi ya Tunisia ambalo ndilo lililohakikisha nafasi ya 16 bora lilipata motisha kubwa zaidi ya shilingi milioni 200 (karibu dola 80,000), fedha ambazo kwa mujibu wa Naibu Waziri wa michezo, Paul makonda zinawekwa moja kwa moja kwenye akaunti za wachezaji kama kutambua thamani ya mchango wao.

4. Soka la kimataifa, silaha mpya ya ushindani

Mchango wa wachezaji wa Taifa Stars wanaocheza soka la ushindani nje ya nchi umeonekana wazi kwenye AFCON 2025. Kati ya wachezaji 28 walioteuliwa, wanane wanacheza soka la kimataifa: Mbwana Samatta (Le Havre, Ufaransa), Kelvin John (Aalborg BK, Denmark), Simon Msuva (Al-Talaba, Iraq), Charles M'Mombwa (Floriana FC, Malta), Haji Mnoga (Salford City, England), Novatus Dismas (Göztepe, Uturuki), Tarryn Allouche (Rochdale AFC, England) na Alphonse Mkabule (Shamakhi, Azerbaijan).

Dhidi ya Nigeria, sita walianza kikosi cha kwanza, huku Kelvin John na Haji Mnoga wakiingia kipindi cha pili, maana yake wanane wote walipata dakika za kucheza. Dhidi ya Uganda, sita walianza tena, na Samatta pamoja na M'Mombwa wakaingia kipindi cha pili, wote wakihusika katika sare ya 1–1. Katika mchezo wa mwisho wa kundi dhidi ya Tunisia, wachezaji watano wa kimataifa walianza, wawili wakaingia kipindi cha pili, huku Kelvin John pekee akiwa hajacheza.

Kwa ujumla, mchango wa kundi hili umeonekana katika utulivu wa uchezaji, nidhamu ya kimbinu na uwezo wa kushindana dhidi ya wapinzani wakubwa. Kama ilivyo kwa timu za Afrika Kaskazini na Magharibi, Tanzania imeanza kunufaika na uzoefu wa wachezaji wanaocheza nje, silaha mpya iliyochangia moja kwa moja kufuzu kwa Taifa Stars hatua ya 16 bora. Haya ni mafanikio makubwa kuwa na wachezaji wanaocheza nje na kusaidia taifa lao.

5. Kufunga kila AFCON na Msuva akiweka rekodi

Tanzania imefunga bao kila AFCON kuanzia ile ya kwanza ya mwaka 1980 mpaka ya sasa. hilo sio jambo dogo. Imewahi kukutana katika mashindano haya na vigogo wa soka la Afrika kama Nigeria, Ivory Coast, Tunisia, Senegal, Misri na hata Zambia ya miaka hiyo na bado Stars ikafanikiwa kuona nyavu. Pia Simon Msuva ameendelea kuwa mhimili wa Taifa Stars. Kwa kufunga kwenye AFCON 2025, amefunga katika AFCON tatu mfululizo, mwaka 2019, 2023 na 202, rekodi nadra kwa mchezaji wa Tanzania.

Bao hilo pia limemfikisha kwenye jumla ya mabao 25 ya kimataifa, akifungana na Mrisho Ngasa kama wafungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa. Hii ni hadithi ya uthabiti, nidhamu na mchango wa muda mrefu katika kizazi tofauti cha Taifa Stars. ni mafanikio makubwa kuwa na mchezaji aliyefunga katika michuano matatu mfululilizo. Wako wachezaji wengi wakubwa Afrika na wanaocheza ulsaya ambao hawana mafanikio haya.

Lakini mchango wa Msuva anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Al-Talaba, Iraq,hauishii kwenye mabao pekee. Ni kiongozi asiye na kelele, anayetoa uzoefu wake kwa wachezaji chipukizi ndani ya kikosi. Katika mashindano haya, amekuwa kiungo kati ya vizazi vipya akijua shinikizo la AFCON na pia matarajio mapya ya timu.

Katika soka la kimataifa, mafanikio ya timu mara nyingi hujengwa juu ya wachezaji wachache wenye uthabiti wa muda mrefu. Kwa Tanzania, Msuva anaendelea kuwa mfano wa aina hiyo, mchezaji anayejenga historia yake binafsi sambamba na historia ya taifa.