Urusi ina haki ya kutumia silaha za nyuklia itakapotishiwa usalama wake - Putin

Kauli hii imekuja mwezi mmoja tangu Kremlin kuidhinisha mabadiliko ya kanuni mpya ambazo nchi hiyo itazizingatia juu ya utumiaji wa silaha zake.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & RashidAbdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

    Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu, tukutane kesho.

  2. Marekani yapiga marufuku droni katika baadhi ya miji ya New Jersey

    dx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka ya usafiri wa anga ya Marekani (FAA) imepiga marufuku matumizi ya ndege zisizo na rubani katika miji 22 ya New Jersey hadi tarehe 17 Januari, ili kuruhusu serikali kutumia "nguvu" dhidi ya ndege zisizo na rubani ambazo ni "tishio la usalama.”

    Hatua hiyo inajiri baada ya wiki kadhaa za kuonekana kwa ndege zisizo na rubani kote New Jersey na majimbo mengine, na kusababisha wasiwasi kwa wakaazi na kuzua nadharia kadhaa kuhusu ushiriki wa nguvu za kigeni.

    Serikali haijatoa majibu ya uhakika, lakini Rais Joe Biden alisema kuonekana kwa ndege zisizo na rubani "hakuna jambo baya."

    Agizo hilo linasema ndege isiyo na rubani inapaswa kufanya kazi chini ya futi 400, urefu wa juu zaidi kwa shughuli za burudani za ndege zisizo na rubani kwa mujibu wa sheria.

    FAA inasema mashirika machache, kama vile taasisi za usalama na misheni za kukabiliana na majanga, hayajajumuishwa katika vikwazo hivyo.

    Baadhi ya shughuli za kibiashara za ndege zisizo na rubani zitaruhusiwa chini ya vizuizi, lakini waendeshaji watahitaji kuwa na kibali halali cha kazi.

    Kwa wiki kadhaa, Wamarekani wamekuwa wakiripoti ndege zisizo na rubani zikiruka karibu na kambi za jeshi la Marekani, karibu na ukanda wa pwani na karibu na katika miundombinu mengine.

    Pentagon imekanusha madai ya mbunge mmoja wa New Jersey kwamba ndege hizo zisizo na rubani zilitoka katika ndege au meli ya Iran, na afisa wa FBI alisema hayo ni madai yaliyotiwa chumvi.

  3. Urusi ilipaswa kuivamia Ukraine mapema zadi - Putin

    c

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Urusi ilipaswa kufanya uvamizi nchini Ukraine mapema zaidi na kujiandaa vyema kwa vita.

    Katika mkutano wake na waandishi wa habari wa mwisho wa mwaka siku ya Alhamisi, Putin amesema kulipaswa kuwepo na "maandalizi ya kimfumo" kwa uvamizi wa 2022, ambao yeye anasema ni "operesheni maalumu ya kijeshi."

    Urusi iliiteka Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014 na vikosi vinavyoiunga mkono Urusi vilianza mapigano mashariki mwa Ukraine, lakini ni baada ya miaka minane ndipo Putin alijaribu kuiteka Kyiv kwa uvamizi ulioanza 2022.

  4. Macron atua Mayotte kupeleka msaada wa chakula na vifaa vya matibabu

    dc

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewasili Mayotte katika kisiwa cha Bahari ya Hindi ambacho ni milki ya Ufaransa baada ya kukumbwa na uharibifu kutokana na Kimbunga Chido.

    Macron alitua Mayotte siku ya Alhamisi asubuhi na kusema ameleta tani nne za chakula na shehena ya vifaa vya matibabu.

    Takribani watu 31 wameripotiwa kufariki, huku maelfu wakiwa bado hawajulikani walipo baada ya kimbunga hicho kukumba visiwa hivyo vidogo siku ya Jumamosi.

    Hapo awali, seneta wa Ufaransa wa Mayotte, Salama Ramia aliambia BBC chakula cha dharura ndicho kinachopaswa kupewa kipaumbele.

    "Duka moja au mawili yamefunguliwa lakini si kila mtu ana pesa za kununua chakula, na hata maduka yanaanza kuwa matupu, hivyo chakula kinahitajika."

    Nusu ya eneo hilo halina umeme.

    Mayotte ni mojawapo ya sehemu maskini zaidi nchini Ufaransa, huku wakazi wake wengi wakiishi katika miji ya vibanda.

    Utawala wa Macron umekosolewa kwa kutotoa kipaumbele kwa Mayotte kwa miaka kadhaa.

    Ni nyumbani kwa wahamiaji 100,000 wanaotafuta hifadhi Ufaransa na wanaishi katika makazi yasiyo rasmi, wanaaminika kuwa miongoni mwa walioathirika zaidi na kimbunga hicho.

    Chido - dhoruba mbaya zaidi kuwahi kukumba visiwa hivyo katika kipindi cha miaka 90 - ilileta kasi ya upepo ya zaidi ya kilomita 225 kwa saa siku ya Jumamosi.

    Baada ya dhoruba ya Mayotte, dhoruba hiyo imepiga bara la Afrika, na kuua watu wasiopungua 45 nchini Msumbiji na 13 nchini Malawi.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Mwakilishi wa Uganda nchini RDC atakiwa kutoa 'ufafanuzi' juu ya maneno ya Generali Muhoozi

    df

    Chanzo cha picha, RDC Affaires Étrangères / X

    Maelezo ya picha, Balozi mdogo wa Uganda nchini DRC, Matata Twaha Magara (kushoto), akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Thérèse Kayikwamba Wagner

    Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imemuita mwakilishi wa muda wa balozi wa Uganda nchini humo na kumtaka atoe maelezo kuhusu kauli iliyotolewa na mkuu wa majeshi ya Uganda na mtoto wa rais wa nchi hiyo Generali Muhoozi Kainerugaba.

    Tangazo la serikali ya DRC linasema kuwa jana Jumatano Waziri wa Mambo ya Nje Thérèse Kayikwamba alimpokea ofisini kwake Matata Twaha Magara, mwakilishi wa muda wa balozi wa Uganda na kumtaka atoe "maelezo kuhusu maneno ya Muhoozi Kainerugaba."

    Kamanda mkuu wa jeshi la Uganda, hivi karibuni alizungumza kuhusu Rais [Félix] Tshisekedi."

    Serikali ya Congo pia imesema Waziri Kayikwamba alimwomba Magara "tafsiri ya serikali juu ya mamlaka ya Uganda" kwa maneno hayo na "hali ya uhusiano kati ya nchi hizi mbili."

    Haijulikani ni nini hasa Jenerali Kainerugaba alichokisema sema kilichochochea ombi la Congo la kutaka ufafanuzi.

    Si mara ya kwanza kwa Jenerali Kaineruigaba kutoa matamshi na maandishi kwenye mitandao ya kijamii ambayo hulazimika kuomba msamaha.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Human Rights Watch yaituhumu Israel kwa kufanya vitendo vya mauaji ya kimbari Gaza

    po

    Chanzo cha picha, EPA-EFE

    Maelezo ya picha, HRW iliishutumu Israel kwa kuharibu miundombinu ya maji kimakusudi

    Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linaishutumu Israel kwa kufanya "vitendo vya mauaji ya kimbari" huko Gaza kwa kuwanyima kwa makusudi raia wa Palestina maji ya kutosha.

    Linasema hatua za Israel ni pamoja na kuharibu miundombinu ya maji na mifereji ya maji kwa makusudi.

    Shirika hilo linasema hayo yanaweza yamesababisha maelfu ya vifo, ambavyo pia ni sawa na "kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kuwaangamiza."

    Israel imeikataa ripoti ya HRW na kusema ni "propaganda." Na kuongeza kuwa, "ripoti hii imejaa uongo ambao ni wa kutisha.”

    Ripoti yenye kurasa 179 inasema "tangu Oktoba 2023, serikali ya Israel imezuia kwa makusudi Wapalestina kupata kiasi cha kutosha cha maji kinachohitajika kwa ajili ya kuishi katika Ukanda wa Gaza."

    Inasema Israel iliharibu miundombinu kimakusudi, ikiwa ni pamoja na paneli za jua zinazowezesha mitambo ya kusafisha, kuhifadhi maji, na ghala la vipuri, huku pia ikizuia mafuta ya jenereta kuingia.

    Inasema Israel pia ilikata umeme, ikashambulia wafanyakazi wa ukarabati na kuzuia vifaa kuingia Gaza kwa ajili ya ukarabati.

    Mkurugenzi mtendaji wa HRW Tirana Hassan anasema, "ni sera ya makusudi ya kawanyima haki, ambayo imesababisha vifo vya maelfu ya watu kutokana na upungufu wa maji mwilini na magonjwa na ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na kitendo cha mauaji ya kimbari."

    Ripoti hiyo inatokana na mahojiano na makumi ya Wapalestina kutoka Gaza, wakiwemo maafisa wa mamlaka ya maji, wataalamu wa usafi wa mazingira na wafanyakazi wa afya, pamoja na picha za satelaiti kutoka Oktoba 2023 hadi Septemba 2024.

    Israel ilianzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi huko Gaza baada ya Hamas kuishambulia Israel tarehe 7 Oktoba 2023, na kuua takriban watu 1,200 na kuwachukua mateka wengine 251.

    Takriban watu 45,129 wameuawa huko Gaza tangu kuanza kwa mashambulizi hayo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

    Ripoti ya HRW ni ya hivi punde katika msururu wa shutuma za makundi ya kutetea haki za binadamu kwamba Israel inatekeleza mauaji ya kimbari Gaza.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Vifo kutokana na unywaji wa pombe vyaongezeka Uingereza

    c

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Takwimu za serikali zinaonyesha, vifo vinavyosababishwa na unywaji wa pombe nchini Uingereza vimeongezeka katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

    Zaidi ya watu 8,200 wamefariki kwa sababu ya pombe mwaka 2023 – ni ongezeko la 42% kutoka 2019 - huku Kaskazini Mashariki ikiwa na viwango vya juu zaidi.

    Wakati wa janga uviko 19, vifo vilivyosababishwa na pombe viliongezeka kote Uingereza. Wanywaji wakubwa wa pombe walikuwa wakinywa zaidi.

    Baada ya baa kufungwa, watu wengi walianza kununua pombe kwenye kutoka madukani na kunywa nyumbani.

    Vifo vingi ni miongoni mwa wanaume, ambao wanakufa kabla ya umri wa miaka 75 - kutokana na ugonjwa wa ini unaohusiana na pombe, huku uchunguzi ukionesha umri wa miaka 55-74, "ndio kundi kubwa la wanywaji wa pombe.”

    Muungano wa unywaji pombe salama (AHA), ambao unawakilisha mashirika 60 yanayofanya kazi kupunguza madhara yanayosababishwa na pombe, unatabiri kuwa kutakuwa na ongezeka la vifo kutokana na pombe na kuwepo mzigo mkubwa kwa mfumo wa afya na jamii.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Waziri wa zamani wa ulinzi afungwa jela kwa ufisadi Guinea

    trfgcv

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Guinea imekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu 2021

    Mahakama nchini Guinea imemhukumu aliyekuwa waziri wa ulinzi kifungo cha miaka mitano jela kwa makosa ya rushwa, utajiri wa haramu, ubadhirifu na utakatishaji fedha.

    Mohamed Diane aliwahi kuwa waziri wa ulinzi kati ya 2015 na 2021 chini ya Rais Alpha Condé, kabla ya jeshi kunyakua mamlaka.

    Pia ametakiwa kulipa faini ya dola za kimarekani milioni 58.5, na akaunti zake za benki na mali katika mji mkuu Conakry na mji wa mashariki wa Kankan pia zitachukuliwa na serikali.

    Hakimu amesema mali hizo zinapaswa kutaifishwa kwani asili yake haiwezi kuthibitishwa.

    Diane amekuwa kizuizini tangu Mei 2022 wakati utawala wa kijeshi ulipoanzisha kampeni dhidi ya ufisadi nchini humo.

    Baada ya kuchukua madaraka, utawala wa kijeshi uliweka mapambano dhidi ya rushwa kuwa mojawapo ya vipaumbele vyake muhimu katika taifa hilo maskini la Afrika Magharibi na kuanzisha mahakama ya kupambana na rushwa.

    Kufikia mwisho wa 2022, viongozi hao wa kijeshi walitaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu 180, wakiwemo mawaziri wa zamani na maafisa wengine wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

    Wakati huo serikali ya kijeshi ilikuwa tayari imefungua kesi dhidi ya Rais wa zamani Condé.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Watoto wafariki katika mkanyagano Nigeria

    tg
    Maelezo ya picha, Tukio hilo lilitangazwa kuwa la bure, likavutia idadi kubwa ya watu

    Watoto kadhaa wamefariki katika tamasha moja katika mji wa Ibadan kusini-magharibi mwa Nigeria, huku wengine wengi wamelazwa hospitalini.

    Idadi kamili ya waliojeruhiwa haijulikani.

    Tukio hilo lilitangazwa kuwa bila kiingilio na kuvuta umati mkubwa wa watu lakini watu wengi walijitokeza na kusababisha tafrani wakati wakihangaika kupata nafasi ya kuingia.

    Wakazi wanasema watoto wapatao 5,000 walikusanyika katika ukumbi huo na mkanyagano ulitokea pale waandalizi wakuu walipofika kuanza hafla hiyo.

    Serikali ya jimbo la Oyo imesema waathiriwa wamepelekwa hospitalini kote Ibadan kwa matibabu baada ya mkanyagano huo uliotokea katika Shule ya Upili ya Kiislamu ya Basorun.

    Serikali imewataka wazazi ambao wana wasiwasi kuhusu waliko watoto wao kuangalia katika hospitali za jiji hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Nchi za Magharibi hazina uwezo wa kuzishinda silaha za Urusi - Putin

    vc

    Chanzo cha picha, Reuters

    Katika mkutano wa kila mwaka na vyombo vya habari, Rais wa Urusi, Vladimir Putin alipoulizwa juu ya kombora jipya la Urusi lililoshambulia Ukraine, amesema teknolojia za Magharibi hazina nafasi ya kulizuia.

    Putin amesema, “chagua eneo lolote Kyiv, kisha lete mifumo ya ulinzi ya nchi za Magharibi na uone ikiwa yana uwezo wa kulizuia.”

    Siku ya nyuma Putin alisema kombora lililoshambulia Ukraine mwezi uliopita, linasafiri kwa kasi ya kilomita 2.5 hadi 3 kwa sekunde (mara 10 ya kasi ya sauti), na kuongeza kuwa “kwa sasa hakuna njia ya kuizuia silaha hiyo.”

    Katika hatua nyingine, Putin anasema hajazungumza na Rais mteule wa Marekani Donald Trump kwa zaidi ya miaka minne na hana uhakika ni lini atakutana au kuzungumza naye.

    Lkaini amesema yuko tayari kukutana naye. "Niko tayari kukutana naye ikiwa anataka," anasema.

    Wawili hao walikutana mara ya mwisho katika mkutano wa kilele wa G20 nchini Japan mwaka 2019, ambapo walifanya mazungumzo kando ya mkutano huo.

  11. Urusi ina haki ya kutumia silaha za nyuklia itakapotishiwa usalama wake - Putin

    cv

    Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

    Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema iwapo nchi nyingine zitaleta tishio kwa Urusi, anaamini Urusi ina haki ya kutumia silaha za nyuklia dhidi yao.

    Katika mkutano wake wa kila mwaka na vyombo vya habari, amesema, "tunazungumza kuhusu vitisho vya kijeshi vinavyoibuka, kama vile kuibuka kwa mifumo ya kupambana na makombora."

    Kauli hii imekuja mwezi mmoja tangu Kremlin kuidhinisha mabadiliko ya kanuni mpya ambazo nchi hiyo itazizingatia juu ya utumiaji wa silaha zake.

    Kanuni mpya zinasema shambulio kutoka kwa taifa lisilo la nyuklia, ikiwa litafanyika chini ya usaidizi wa nchi yenye nguvu za nyuklia, litachukuliwa kama shambulio la pamoja dhidi ya Urusi.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Wanaume 50 wahukumiwa katika kesi ya ubakaji wa mwanamke mmoja Ufaransa

    dfc

    Chanzo cha picha, CLEMENT MAHOUDEAU/AFP

    Maelezo ya picha, Gisèle Pelicot

    Dominique Pelicot amepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kumpa dawa za kulevya mke wake wa zamani, Gisele Pelicot na kumbaka na kuwaalika wanaume kadhaa kumbaka kwa takriban muongo mmoja.

    Pelicot amekiri kuwaalika makumi ya wanaume aliowasiliana nao mtandaoni kujamiiana Gisèle katika kitanda chake nyumbani huku akiwa amepoteza fahamu wala hajitambui.

    Mahakama huko Ufaransa imewapata wanaume 47 na hatia ya ubakaji, wawili na hatia ya kujaribu kubaka, na wawili na hatia ya unyanyasaji wa kingono.

    Mzee huyo mwenye umri wa miaka 72 alishtakiwa na wanaume 50, ambao wengi wao walijaribu kukanusha mashtaka ya ubakaji. Miongoni mwao ni wazima moto, madereva wa lori, askari, walinzi, mwandishi wa habari na DJ.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Israel yashambulia maeneo ya Wahouthi nchini Yemen baada ya shambulio la kombora

    df

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Jeshi la Israel limesema limelenga miundombinu ya nishati katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa

    Israel imesema ndege zake za kivita zimeifanya mfululizo wa mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi nchini Yemen ambayo ni ya vuguvugu la Houthi linaloungwa mkono na Iran.

    Msemaji wa jeshi la Israel amesema shabaha hizo ni pamoja na bandari za Bahari ya Shamu na miundombinu ya nishati katika mji mkuu Sanaa.

    Televisheni ya Al Masirah inayoongozwa na Wahouthi iliripoti kuwa watu saba wameuawa katika bandari ya Salif na wawili katika kituo cha mafuta cha Ras Issa, ambavyo vyote viko katika mkoa wa Hudaydah.

    Mashambulizi hayo yametokea chini ya saa mbili baada ya kombora lililorushwa kutoka Yemen kuzuiwa katikati mwa Israel. Shule na magari kadhaa yaliharibiwa huko Ramat Gan kwenye ukingo wa Tel Aviv.

    Waasi wa Houthi walianza kuishambulia Israel na meli za kimataifa muda mfupi baada ya kuanza vita vya Gaza mwezi Oktoba 2023, wakisema wanafanya hivyo kutoa mshikamano kwa Wapalestina.

    Jeshi la Israel linasema mamia ya makombora na ndege zisizo na rubani zimerushwa nchini humo kutoka Yemen, ambazo nyingi zimenaswa.

  14. Japani: Wasiotenga takataka inavyotakikana kuaibishwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kwa wasiojua, kutenga takataka inaweza kuwa mchakato mgumu nchini Japani - nchi ambayo inajivunia mojawapo ya sheria kali zaidi za utupaji takataka.

    Lakini katika jiji la Fukushima, mambo yanakaribia kuwa magumu zaidi.

    Kuanzia mwezi Machi, serikali ya jiji itapitia mifuko ya takataka ambayo inakiuka kanuni - kama vile ambayo taka hazijatengwa kwa usahihi, au ambayo taka zao ni nyingi kupita kiasi - na wakati mwingine itawatambulisha wamiliki wa taka hizo hadharani.

    Kanuni hizo mpya, zilizopitishwa katika mkutano wa manispaa siku ya Jumanne, zinawadia huku kukiwa na msukumo wa muda mrefu wa Japani kuimarisha mfumo wake wa usimamizi wa takataka.

  15. Mwanaume akiri kuendesha 'kituo cha polisi' cha siri cha China Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamume mmoja nchini Marekani amekiri kosa la kusaidia kuendesha kile kilichotajwa kuwa kituo cha polisi cha siri cha kwanza kujulikana mjini New York kwa niaba ya serikali ya China.

    Waendesha mashtaka wanasema Chen na mshtakiwa mwenzake Lu Jianwang walifungua na kuendesha kituo hicho katika kitongoji cha Manhattan mapema 2022 kwa niaba ya Wizara ya Usalama wa Umma ya China.

    Takriban vituo 100 vya aina hiyo vimeripotiwa duniani kote katika nchi 53, huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakiishutumu China kwa kutumia vituo hivyo kuwatishia na kuwafuatilia raia wa China walio nje ya nchi.

    Lakini China imekanusha kuwa ni vituo vya polisi, ikisema ni "vituo vya kutoa huduma" za utawala kwa raia wa ng'ambo.

    Watu hao ambao wote ni raia wa Marekani, walikamatwa mwezi Aprili mwaka jana.

    Siku ya Jumatano, Chen, 60, alikiri kuwa na hatia ya kula njama kama wakala wa China, na anakabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela atakapohukumiwa mwaka ujao.

    Soma zaidi:

  16. Wanajeshi 100 wa Korea Kaskazini wauawa katka vita vya Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Takriban wanajeshi 100 wa Korea Kaskazini wameuawa katika mapigano katika vita vya Ukraine tangu waingie kwenye mapigano upande wa Urusi mapema mwezi huu, mbunge wa Korea Kusini amesema.

    Lee Sung-kwon, akizungumza na waandishi wa habari baada ya bunge kupewa taarifa na Idara ya Kitaifa ya Ujasusi ya nchi hiyo, alisema wengine 1,000 wamejeruhiwa.

    Alisema waliopoteza maisha ni pamoja na maafisa wa ngazi za juu, na inaweza kuelezewa na wanajeshi hao kutofahamu eneo hilo, na vita vya ndege zisizo na rubani.

    Ripoti za kwanza za majeruhi wa Korea Kaskazini zilikuja mapema wiki hii. Iliibuka mwezi Oktoba kwamba Kaskazini ilikuwa imetuma wanajeshi 10,000 kusaidia juhudi za vita vya Urusi.

    Siku ya Jumatatu msemaji wa Pentagon ya Marekani alisema Wakorea Kaskazini waliuawa, bila kutaja idadi, na siku moja baadaye afisa wa Marekani ambaye hakutajwa jina alisema kuwa kulikuwa na "mia kadhaa" waliouawa au kujeruhiwa.

    BBC haijathibitisha madai hayo kwa uhuru.

    Wanajeshi wa Korea Kaskazini, ambao hakuna hata mmoja wao aliye na uzoefu, wanaaminika kuwa walitumia wiki zao za kwanza nchini Urusi katika mafunzo na kisha katika majukumu ya usaidizi.

    Majeruhi hao wanadhaniwa kutokea katika eneo la Kursk nchini Urusi, ambako wanajeshi wa Ukraine wanalinda eneo dogo lililotekwa wakati wa uvamizi wa ghafla mwezi Agosti.

    Jumamosi iliyopita, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Urusi imeanza kutumia "idadi kubwa" ya Wakorea Kaskazini katika mashambulio yake huko Kursk.

    Hawafikiriwi kuwa wametumwa nchini Ukraine kwenyewe, ambapo wanajeshi wa Urusi wamekuwa wakisonga mbele katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo katika miezi ya hivi karibuni.

  17. Majaji kutoa uamuzi katika kesi ya ubakaji iliyomgeuza mwanamke, 72, kuwa shujaa

    .

    Chanzo cha picha, CLEMENT MAHOUDEAU/AFP

    Majaji katika mji wa Avignon nchini Ufaransa watatoa uamuzi kwa wanaume 51 siku ya Alhamisi katika kesi ya ubakaji ambayo imemfanya mwanamke mwenye umri wa miaka 72 kuwa shujaa.

    Kwa takriban muongo mmoja, Gisèle Pelicot alitiliwa dawa na mume wake wa zamani Dominique, ambaye kisha aliwaalika wanaume kadhaa aliokuwa amewasajili mtandaoni kufanya ngono na aliyekuwa mke wake kitandani nyumbani kwao huku akiwa amepoteza fahamu na hajitambui.

    Ulikuwa uamuzi wake kuondoa kinga ya kutojitambulisha na kuweka kesi hii hadharani - kwa maneno yake, "mabadilishano ya aibu" kutoka kwa mwathiriwa hadi mbakaji.

    Ingawa anakubali mashtaka dhidi yake, wanaume wengine wengi walioshtakiwa wanakana walichofanya ni ubakaji.

    Waendesha mashtaka wameomba kifungo jela kuanzia miaka minne hadi ishirini, kifungo cha juu zaidi kwa shtaka la ubakaji uliokithiri.

    Mmoja wa washtakiwa, ambaye amekiri mashtaka, amesema kesi hiyo iliendeshwa haraka na "kushindwa kufanyika kwa usawa".

    Soma zaidi:

  18. Picha ya ramani ya Google yasaidia polisi kufungua kesi ya mauaji

    .

    Chanzo cha picha, Google Maps Streetview

    Picha ya ramani ya Google ya mwanamume akipakia begi kubwa jeupe la plastiki kwenye buti ya gari lake imesaidia kutegua kitendawili katika kisa cha mauaji kwenye mji wa kaskazini mwa Uhispania, polisi wanasema.

    Programu ya Google inaruhusu watumiaji kuona picha za mitaa kote ulimwenguni.

    Ilinasa wakati ambapo mwili wa mwathiriwa ulikuwa unadaiwa kuondolewa.

    Watu wawili walikamatwa mwezi uliopita, wakituhumiwa kuhusika na kutoweka na mauaji ya mtu Oktoba mwaka jana.

    Mabaki yake yaliyokatwakatwa yalipatikana kwenye kaburi wiki iliyopita.

    Mnamo tarehe 12 Novemba mwaka huu, polisi walimkamata mwanamke anayesemekana kuwa mpenzi wa mtu aliyepotea na mwanamume anayesemekana kuwa mpenzi wake wa zamani.

    Mapema mwezi huu, kiwiliwili kilichooza sana kipatikana baada ya mhusika kuchimba na kuufukua mwili katika makaburi ya karibu.

    Washtakiwa wamerudishwa rumande na upelelezi unaendelea.

  19. Arsenal 3-2 Crystal Palace: Sasa kilichosalia ni Arteta kukabiliana na 'kikwazo kigumu zaidi'

    ,

    Chanzo cha picha, Getty Images

    The Gunners wameishinda Crystal Palace jana Jumatano na kutinga nusu fainali ya Kombe la Carabao, huku wakipania kushinda kombe la kwanza kuu tangu kubeba Kombe la FA katika msimu wa kwanza wa kunolewa na Mikel Arteta.

    Gabriel Jesus alifunga mabao matatu, bao lake la kwanza kwenye Uwanja wa Emirates kwa zaidi ya mwaka mmoja, dhidi ya Eagles na kuwaacha wakiwa sare katika michuano miwili waliocheza ugenini tangu ushindi wa 2020.

    Hii ni nusu fainali ya pili ya Arteta ya nyumbani tangu kombe hilo - ingawa pia walifika nusu fainali ya Ligi ya Europa mnamo 2021.

    Siku ya Ijumaa, Arteta - kocha wa tatu kwa muda mrefu zaidi katika Ligi ya Primia na wa nne katika kandanda ya Uingereza - atakuwa ameiongoza Arsenal kwa miaka mitano.

    Tunatazama kwa undani utawala wake Arsenal na jinsi, licha ya ukosefu wa mataji, wamebadilika kutoka kuwa wenye kuyumbyumba hadi moja wa washambuliaji wakubwa zaidi katika Ligi ya Primia.

    Sasa, kinachokosekana tu ni usahihi katika hatua hiyo ya mwisho.

    Mtaalamu wa kandanda wa Uhispania Guillem Balague anaamini, kama "mmoja wa watu wenye fikra za kina za mchezo", Arteta tayari ameonyesha uwezo wa kuwapeleka Gunners mbele zaidi.

    Alisema: "Hakuna anayetilia shaka kwamba Arsenal kwa mara nyingine ni klabu iliyoingia kwenye nafasi nne za juu ambayo bado inahitaji marekebisho kidogo ili kuwawezesha kushindania ubingwa na kuongeza moja ya Kombe la FA na mataji mawili ya Community Shields walioshinda kwa sasa.

    "Nina hakika kwamba Arteta amefikiria juu yake na ana maono ya kuleta mabadiliko muhimu."

    Maoni ya mashabiki kwa Arteta

    Scott: Kabla ya Arteta kuwasili, nilikuwa kwenye hatihati ya kuacha kuwaunga mkono kwa sababu nilihisi kama Arsenal niliyokua nikiipenda imetoweka. Mikel ameijenga upya klabu, ametufanya kuwa imara, amewapa vijana nafasi na kuonyesha matokeo na alifanya maamuzi magumu.

    Savs: Arsenal wametoka mbali sana katika kipindi cha miaka mitano. Na hii ilikuwa baada ya zaidi ya miaka mitano ya kushuka taratibu. Ulinganisho mara nyingi hufanywa na baada ya Sir Alex Ferguson Manchester United

    Kwa mtazamo huu, Arteta amefanya kazi nzuri sana. Hata hivyo, sasa imewadia hatua ngumu zaidi ya mwisho - kushinda mataji. Apewe muda na nafasi ya kufanya hivyo. Lakini hii lazima iwe msimu huu au ujao. Endelea kuwa na imani…Endelea kuamini.

    Soma zaidi:

  20. Urusi inaondoa vifaa vyake katika kambi zake za kijeshi Syria - picha za satelaiti zaonyesha

    .

    Urusi inaondoa kwa kiasi kikubwa vifaa vyake vya kijeshi nchini Syria, kuashiria maandalizi ya kujiondoa kwa kiasi fulani, wachambuzi wanasema.

    Picha za satelaiti zinaonyesha mkusanyiko wa magari ya kijeshi katika bandari inayodhibitiwa na Urusi na kambi ya wanajeshi wa anga magharibi mwa Syria.

    Ndege za usafiri pia zimeonekana kuwasili na kuondoka nchini humo katika siku za hivi karibuni.

    BBC Verify pia imeweka kijiografia video zinazoonyesha safu nyingi za lori za kijeshi za Urusi zikielekea kaskazini kwenye vituo vya kijeshi.

    Taasisi ya Utafiti wa Vita inapendekeza hii inaonyesha maandalizi ya kupunguzwa au kuondoka kabisa kwa vikosi vya Urusi nchini humo.

    Taasisi hiyo yenye makao yake makuu mjini Washington imeongeza kuwa, kuhamisha magari ya kijeshi katika kambi zake huenda ikawa hatua ya tahadhari wakati Moscow ikijadiliana na serikali mpya mjini Damascus.

    BBC Verify iliripoti wiki iliyopita jinsi meli za kivita za Urusi zilivyoondoka kwenye bandari ya Tartous, huku wachambuzi wakipendekeza kwamba zilikuwa zikiwekwa katika maji ya kimataifa kwa wakati huo.

    Meli hizo hazijarudi - lakini zaidi ya magari 100 ya kijeshi yamewasili katika kambi hiyo siku za hivi karibuni, picha za satelaiti zinaonyesha.

    "Urusi sasa inaondoa vitengo na vifaa vya kijeshi ambavyo viliwekwa katika karibu ngome mia moja kote nchini humo kabla ya kuanguka kwa utawala wa Assad," amesema Anton Mardasov, mwanazuoni katika mpango wa Taasisi ya Mashariki ya Kati nchini Syria.

    Soma zaidi: