'Mimi ni mbakaji', mume akiri katika kesi ya ubakaji Ufaransa

Gisèle Pelicot akiwasili katika mahakama ya Avignon siku ya Jumanne

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Gisèle Pelicot awasili katika mahakama ya Avignon siku ya Jumanne
Muda wa kusoma: Dakika 3

Tahadhari: Taarifa hii ina maelezo ya kusikitisha kuanzia mwanzo.

Dominique Pelicot, mwanamume mwenye umri wa miaka 71 anayekabiliwa na mashtakiwa kwa kumtilia mke wake dawa za kulevya ili alale na kuwalipa makumi ya wanaume kumdhulumu kwa zaidi ya miaka 10, amekiri mashtaka yote dhidi yake katika ushahidi wake wa kwanza tangu kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa tarehe 2 Septemba.

Akiwashiria washtakiwa wenzake 50 ambao wanadaiwa kumbaka mke wake wa zamani Gisèle, Bw Pelicot alisema: "Mimi ni mbakaji kama wengine katika chumba hiki."

"Wote walijua, hawawezi kupinga hilo," alisema.

Kuhusu mke wake wa zamani, alisema: "Hakustahili kufanyiwa uovu huo."

"Nilifurahishwa naye sana," aliambia mahakama.

Gisèle, ambaye alipewa nafasi ya kujibu muda mfupi baadaye, alisema: "Ni vigumu kwangu kusikiliza hili. Kwa miaka 50, niliishi na mwanamume ambaye sikuwahi kufikiria angeweza kufanya hivyo. Nilimwamini kwa roho moja."

Soma pia:

Bw Pelicot, ambaye ni baba na babu, aliambia mahakama kuhusu matukio ya kiwewe cha utotoni na kusema alidhulumiwa na muuguzi wa kiume alipokuwa na umri wa miaka tisa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alipoulizwa kuhusu ndoa yake na Gisèle, Bw Pelicot alisema alifikiria kujitoa uhai alipogundua kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi. Alisema alitaka kugongesha gari lake kwenye eneo lenye miti mingi, lakini alikosa ujasiri. "afadhali ningefanya hivyo," aliongeza kusema.

Bw Pelicot pia aliangazia hisia zake kwa Gisèle, ambaye alisema "alikuwa na wazimu lakini... nilimpenda sana, na bado ninampenda."

"Nilimpenda vyema kwa miaka 40 na vibaya kwa miaka 10," aliongeza, akimaanisha muongo ambao alimtumia dawa za kulevya na kumdhulumu.

Pia aliulizwa kuhusu maelfu ya video alizonasa za wanaume wakimdhulumu mkewe aliyekuwa hana fahamu. Haya yalipatikana na wachunguzi na yalisaidia sana kuwasaka wanaume 50 ambao sasa wanatuhumiwa kwa ubakaji.

Bw Pelicot alikiri kuwa alikuwa amewarekodi wanaume hao kwa ajili ya "kujifurahisha," lakini pia "anashukuru leo kupitia [video] hiyo imesaidia kuwapata watu walioshiriki katika uhalifu huo".

Ingawa hakuna kamera zinazoruhusiwa mahakamani, kesi iko wazi kwa umma kwa ombi la Gisèle Pelicot, ambaye aliondoa haki yake ya kutotajwa jina mwanzoni mwa kesi. Timu yake ya wanasheria ilisema kufanya hadharani kesi hiyo kutaelekeza "aibu" kwa mshtakiwa.

Bw Pelicot, ambaye anasadikiwa kuugua ugonjwa wa figo, hakuwepo mahakamani kwa takriban wiki moja. Amepagiwa kutoa ushuhuda wake siku nzima, ingawa ataruhusiwa kupumzika ya mara kwa mara.

xx

Chanzo cha picha, EPA

Katika vikao vya awali vya kesi hiyo, Bi Gisèle alisema alikuwa na hofu kwamba anaugua maradhi ya Alzheimer hali ambayo ilimfanya kupoteza uzani na kumbukumbu. Haya kwa hakika yalikuwa ni madhara ya dawa ambazo mumewe alikuwa akimpa.

"Nilijaribu kuacha, lakini uraibu wangu ulikuwa na nguvu zaidi, hamu ya kufanya vitendo hivyo ilikuwa inaongezeka," alisema.

"Nilikuwa najaribu kumtuliza, nilisaliti uaminifu wake. Nilipaswa kuacha mapema, kwa kweli sikupaswa kufanya hivyo kabisa."

Bw Pelicot pia anadaiwa kumpa dawa za kulevya na kumdhulumu bintiye, Caroline, baada ya picha zake za nusu uchi kupatikana kwenye kompyuta yake ndogo.

Hapo awali alikanusha hilo na Jumanne pia alisema hajawahi kuwagusa wajukuu zake. "Ninaweza kutazama familia yangu machoni na kuwaambia kuwa hakuna kitu kingine kilichotokea," alisema.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi