Je, kwa nini wafanyakazi wengi wa China wanalengwa na kuuawa duniani kote?

Chanzo cha picha, Getty Images
Oktoba 6, raia wawili wa China waliuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika shambulio la bomu la kujitoa muhanga nje ya uwanja wa ndege wa Karachi nchini Pakistan. Jeshi la Ukombozi la Balochistan (BLA) limedai kuhusika na shambulio hilo, ikiwa ni mfululizo wa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa China nchini Pakistan na nchi nyingine katika miaka ya hivi karibuni.
Zaidi ya wafanyakazi nusu milioni wa China wameajiriwa katika miradi ya maendeleo duniani kote, mara nyingi katika maeneo yenye utulivu wa kisiasa, na wengi wameuawa au kutekwa nyara.
Ni mara ngapi wafanyakazi wa China wameshambuliwa nchini Pakistan?

Chanzo cha picha, Getty Images
Raia wawili wa China waliouawa katika shambulio la Oktoba 6 walikuwa sehemu ya msafara wa watu waliokuwa wakisaidia kujenga mitambo ya umeme katika mji wa Port Qasim, karibu na Karachi.
Wafanyakazi hao waliuawa wakati bomu lilipolipuka katika gari karibu na uwanja wa ndege wa mji huo. Watu wengine 10 walijeruhiwa.
Jeshi la BLA, ambalo linadai uhuru kwa watu wa Baloch, lilisema "limeulenga msafara wa wahandisi wa ngazi ya juu wa China na wawekezaji" wanaowasili kutoka uwanja wa ndege katika kile ilichokiita shambulio la kujitoa muhanga.
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif ameliita shambulio hilo "kitendo cha kikatili". Wizara ya mambo ya nje imesema kuwa waliotekeleza shambulio hilo "wataadhibiwa".
Raia hao wawili wa China waliouawa walikuwa wakifanya kazi katika eneo la ujenzi katika mji wa Port Qasim katika jimbo la Sindh nchini Pakistan.
Mwezi Machi, BLA pia lilikiri kuishambulia kambi ya jeshi la majini karibu na bandari ya Gwadar huko Balochistan, ambayo imetengenezwa na makampuni ya China.
Wanamgambo hao pia walikiri kuwaua wasomi watatu wa China na dereva wao wa Pakistani mnamo mwezi Aprili 2022, katika shambulio la kujitoa muhanga karibu na Taasisi ya Confucius inayoendeshwa na China katika chuo kikuu cha Karachi.
BLA liinadai kuwa watu wa Baloch hawajapokea sehemu sawa ya utajiri unaotokana na uwekezaji wa kigeni katika jimbo au kutoka kwa uchimbaji wa madini (kama vile mafuta) na makampuni ya kigeni katika mkoa huo.
Ni watu wangapi wa China wanaofanya kazi nje ya nchi na kwa nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Takriban raia 568,000 wa China wanafanya kazi nje ya nchi katika miradi inayoendeshwa na makampuni ya China kote duniani, kwa mujibu wa takwimu za wizara ya biashara ya China kufikia mwaka 2022.
Wengi wa wafanyakazi hawa wanahusika katika miradi chini ya Mpango wa China wa Ukanda Mmoja na Njia Moja (BRI), unaojulikana kama Road Initiative (BRI).
China imewekeza kiasi cha dola trilioni 1 katika BRI kuendeleza miradi kama vile barabara na reli, bandari na mitambo ya umeme.
Lengo ni kujenga njia mpya za mauzo ya nje ya China na kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya China na mataifa yote ambayo yamejitolea kushiriki katika mradi huu.
Pakistan ni nyumbani kwa moja ya miradi mikubwa ya BRI: Ushoroba wa kiuchumi wa Chin na Pakistan. Mpango huo unajumuisha mfululizo wa njia za barabara na reli kutoka mpaka wa magharibi wa China kupitia Pakistan hadi bandari ya Gwadar kwenye Bahari ya Arabia.
Kama ilivyo Pakistan, nchi nyingi za Afrika, kama vile Kenya, Ethiopia na Senegal, zimekopa mabilioni ya dola kutoka China ili kujenga miundombinu bora ya usafiri na nishati.
Wakazi wa nchi zinazowahifadhi mara nyingi hulalamika kuwa kampuni zinazoendesha miradi ya maendeleo huwapa kazi chache na kuajiri raia wa China.
"Watu wa ndani katika nchi za Afrika hawafurahii hali hii," Profesa Steve Tsang, kutoka Taasisi ya SOAS China katika taasisi ya mafunzo ya Kiafrika katika Chuo Kikuu cha London, aliiambia BBC.
Anaongeza kuwa "makampuni huajiri wafanyakazi wengi wa Kichina na mtu hupata hisia kwamba wanatumia Waafrika tu kwa kazi zilizo na hali ngumu zaidi."
"China inadai uwekezaji wake nje ya nchi una manufaa kwa wote," mchambuzi Alex Vines wa taasisi ya Royal Institute of International Affairs, inayojulikana kama Chatham House, mjini London, aliiambia BBC.
"Lakini ilitoa ajira kwa wafanyakazi wa China kutatua tatizo la ukosefu wa ajira nchini China," Vines aliongeza.
Je, ni hatari kiasi gani kwa raia wa China kufanya kazi nje ya nchi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Uwekezaji wa China nje ya nchi umesababisha raia wake kufanya kazi katika baadhi ya nchi hatari zaidi duniani, ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya migogoro.
Pakistan, kwa mfano, imeorodheshwa kati ya nchi zenye utulivu wa kisiasa, kulingana na orodha ya Benki ya Dunia.
Mwandishi wa BBC World Service mjini Karachi, Riaz Sohail, anaripoti kuwa kumekuwa na mashambulizi 16 yanayohusishwa na miradi ya maendeleo ya China nchini Pakistan, ambapo raia 12 wa China wameuawa na wengine 16 kujeruhiwa.
Hii ni pamoja na mauaji yaliyotokea mwezi Machi 2024 ya wahandisi watano wa Kichina wanaofanya kazi kwenye bwawa la umeme la Dasu katika mkoa wa Bisham wa Khyber Pakhtunkhwa, eneo tete sana kaskazini magharibi mwa nchi.
Mnamo mwezi Novemba 2018, watu wenye silaha waliwaua watu wasiopungua wanne katika shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa China mjini Karachi.
Barani Afrika, kumekuwa na mashambulizi kadhaa dhidi ya wafanyakazi wa China wanaofanya kazi katika migodi ya dhahabu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, eneo ambalo ghasia za kisiasa zinazofanywa na makundi ya wanamgambo wenye silaha zimeenea.
Mnamo mwezi Julai 2024, raia sita wa China na askari wawili wa Kongo waliuawa kwa kupigwa risasi katika mgodi wa dhahabu kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, sehemu inayomilikiwa na kampuni ya China, shirika la habari la Reuters liliripoti wakati huo.
Wahusika wa shambulio hilo wanaaminika kuwa wanachama wa kundi la wanamgambo linalojulikana kama Congo Development Cooperative, moja ya makundi kadhaa yenye silaha yanayopigania udhibiti wa ardhi na maliasili katika eneo hilo.
Mnamo Januari 2022, watu wenye silaha wa Nigeria waliripotiwa kuwateka nyara wafanyakazi watatu wa Kichina katika Jimbo la Niger, katika eneo la ujenzi wa bwawa linalojengwa na kampuni inayomilikiwa na serikali ya China Sinohydro.
Makundi yenye silaha barani Afrika na Kusini Mashariki mwa Asia mara nyingi yanapata faida kuwateka nyara raia wa China kwasababu wanatarajia makampuni kulipa kikombozi kikubwa ili waachiliwe, kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Peterson ya Uchumi wa Kimataifa (PIEE).
Nchini Afghanistan, wakati wa kati ya miongo miwili ya ukosefu wa mamlaka kwa Taleban na kurejesha madaraka, mara nyingi Wataleban waliwateka nyara wafanyakazi wa kigeni wa China na kuwashikilia kwa ajili ya kupata kikombozi.
Je, China inajaribu vipi kuwalinda wafanyakazi wa kigeni?
Hadi sasa, serikali ya China na makampuni yameshughulikia mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa nje kwa "kulipa fkikombozi ili kuwezesha kuachiliwa kwao, kushinikiza mamlaka za nchi mwenyeji kutoa usalama bora, na kusafirisha teknolojia ya ufuatiliaji kusaidia kutambua na kuzuia watu wenye msimamo mkali," PIEE inasema.
China pia inatoa mafunzo kwa wanajeshi wa nchi wenyeji ili kutoa usalama bora, na makampuni ya China yanazidi kuajiri makampuni binafsi ya usalama ili kujilinda dhidi ya washambuliaji wa kujitoa muhanga, wafyatuaji risasi na watekaji nyara.
"Lakini kuna mipaka ya kile ambacho Beijing inaweza kutarajia kutoka kwa nchi zinazowahifadhi," ripoti ya PIEE ilisema, na kuongeza kuwa : "Uwekezaji wa moja kwa moja wa China nje ya nchi umeelekezwa kwa nchi zilizo na utawala dhaifu wa sheria."
Kufuatia shambulio la hivi karibuni nchini Pakistan, ubalozi wa China nchini humo umewakumbusha raia wake na makampuni ya China yaliyopo nchini humo kuwa macho na "kufanya kila wawezalo kuchukua hatua za kiusalama."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla












