Kumzuia Putin ni nafuu kuliko mapambano ya silaha duniani, Zelensky asema
Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Ukraine ameonya kwamba bila hatua kali za washirika "Putin ataendelea kuendeleza vita mbele zaidi na zaidi", na akasema "Ukraine ni ya kwanza tu".
Rais wa Ukraine alikosoa udhaifu wa taasisi za kimataifa kwa kushindwa kuizuia Urusi.
Alisema kuwa "kumzuia Putin sasa ni bora zaidi" kuliko nchi zinazojaribu kujikinga na Urusi baadaye
Kuhusu AI na silaha kama vile ndege zisizo na rubani, alisema:
"Sasa tunaishi katika mbio mbaya zaidi ya silaha katika historia ya wanadamu", akiongeza kuwa sheria za kimataifa kuhusu akili mnemba zinahitaji kuwekwa.
Zelensky alisema alikuwa na "mkutano mzuri" na Donald Trump siku ya Jumanne na kuwa anathamini uungwaji mkono wa Marekani, "mwishowe, amani inategemea sisi sote."
Tunachokifahamu kufikia sasa kuhusu kinyang'anyiro cha urais wa Malawi
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Huu hapa ni muhtasari wa kile ambacho kimekuwa kikitokea nchini Malawi huku taifa hilo likisubiri kwa hamu kutangazwa rasmi kwa matokeo ya uchaguzi wa urais:
Rais Lazarus Chakwera amekubali kushindwa katika hotuba yake ya moja kwa moja kwa taifa.
Anasema aliyekuwa Rais Peter Mutharika amechukua uongozi "usioweza kushindwa", na amempigia simu kumpongeza.
Mutharika alitawala Malawi kuanzia 2014 hadi 2020, aliposhindwa na Chakwera.
Benki zote na maduka mengi katika mji mkuu Lilongwe yamefungwa kwa siku hiyo kwani kulikuwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa maandamano, lakini Malawi imesalia kuwa na amani, huku Chakwera akiahidi kukabidhi madaŕaka.
Tume ya uchaguzi inasema bado inakagua matokeo kabla ya kutangaza rasmi.
Awali Chakwera alitoa wasiwasi wa kutokea "machafuko", na alisema alitarajia tume kuyashughulikia, hata kama ameshindwa.
Dawa mpya ya kupambana na Virusi vya Ukimwi kupatikana kwa bei nafuu
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Dawa mpya ya kuzuia HIV itapatikana kwa gharama ya chini katika zaidi ya nchi 100 za kipato cha chini ndani ya miaka miwili, hatua inayotarajiwa kuwapa mamilioni ya watu fursa ya matibabu na uwezekano wa kuleta ulimwengu karibu na kumaliza janga la UKIMWI.
Dawa hiyo, iitwayo Lenacapavir na inayotolewa kwa njia ya sindano, inatazamiwa kuanza kutumika mapema mwishoni mwa mwaka huu, kwa gharama ya $28,000 (£20,000) kwa kila mtu kila mwaka.
Lakini tangazo la Jumatano linaahidi kupunguza bei hiyo hadi $40 pekee, karibu 0.1% ya gharama ya awali.
Toleo la bei ya chini litatolewa mwaka wa 2027 katika nchi 120 za kipato cha chini na cha kati.
Wanasayansi wanasema dawa hiyo huzuia virusi visijizalishe ndani ya seli.
Mpango huo wa kihistoria wa kutoa dawa za kupunguza makali ya virusi kwa watu wenye virusi vya Ukimwi katika nchi zinazoendelea ulisimamiwa na Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton baada ya mazungumzo na makampuni ya dawa.
Makubaliano hayo yaliyotangazwa Jumatano yalifikiwa kati ya Wakfu wa Clinton kwa ushirikiano na Gates Foundation na makundi mengine, ikiwa ni pamoja na taasisi ya utafiti ya Afrika Kusini, Wits RHI.
Rais Chakwera amekubali kushindwa, na kuliambia taifa la Malawi kuwa anafanya hivyo kwa kuheshimu nia yao ya kutaka mabadiliko ya serikali.
Rais Chakwera akihutubia taifa kabla ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa leo mchana.
Matokeo ya awali yanaonesha mpinzani wake, Rais wa zamani Peter Mutharika ameongoza vyema, akijizolea karibu asilimia 66 ya kura zilizohesabiwa kufikia Jumanne. Chakwera alikuwa amepata 24%.
Katika hotuba yake, Chakwera alitambua matokeo ya kura za awali, jambo ambalo lilionyesha mpinzani wake Peter Mutharika alikuwa ameongoza kwa kiasi kikubwa.
"Ninajua kwamba kwa wengi wenu mliopiga kura, matokeo haya ni taswira ya nia yenu ya pamoja ya kuwa na mabadiliko ya serikali na hivyo ni sawa kukubali kushindwa kutokana na kuheshimu matakwa yenu kama raia," aliwaambia Wamalawi.
Chakwera anasema amempigia simu Mutharika kumpongeza kwa "ushindi wake wa kihistoria".
Alithibitisha kuwa alifika mahakamani jana kujaribu kuzuia matokeo yasitangazwe lakini akasema anakubali uamuzi wa mahakama kwamba tume ya uchaguzi lazima iendelee na kutangaza matokeo.
Chakwera pia alisema: "Wamalawi, kama mko upande wa kushindwa au kushinda, tafadhali muwe na amani."
Je, kweli Trump ‘amemaliza vita saba vilivyokuwa vigumu kuisha’?
Chanzo cha picha, EPA
Rais Trump ameorodhesha "vita" anazodai zimemalizika kuwa ni kati ya: Israel na Iran, Pakistan na India, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Thailand na Cambodia, Armenia na Azerbaijan, Misri na Ethiopia na Serbia na Kosovo. Idadi ya "vita" hivi ilidumu kwa siku chache na haijulikani ikiwa baadhi ya mikataba ya amani itadumu.
Wakati Trump alidai "mazungumzo yaliyopatanishwa na Marekani" yalimaliza mzozo wa siku nne kati ya India na Pakistan, serikali ya New Delhi ilichukua jukumu la Marekani.
Mwezi Juni, Marekani ilishambulia maeneo ya nyuklia nchini Iran - hatua inayoonekana kumaliza uhasama wa siku 12 na Israel, lakini wataalamu wanasema hakujawa na makubaliano ya amani ya kudumu.
Ndege zisizo na rubani zaishambulia boti ya misaada ya Gaza katika maji ya Ugiriki
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Watu wakikusanyika karibu na boti kadhaa zinazobeba misaada kwenda Gaza kwenye kisiwa cha Ugiriki cha Syros mnamo tarehe 14 Septemba.
Meli aina ya Flotilla iliyobeba msaada katika Ukanda wa Gaza imeripotiwa kushambuliwa na ndege zisizo na rubani katika maji ya Ugiriki.
Wanaharakati wanaoandaa msaada huo walisema kulikuwa na milipuko na mawasiliano yao yalitatizwa.
Boti hizo hapo awali zilikuwa zimetoka katika bandari ya Uhispania na zilitangaza nia yao ya kuvunja kizuizi cha jeshi la wanamaji la Israeli katika Ukanda wa Gaza.
Sambamba na tukio hili, vifaru vya Israel vimeripotiwa kuingia katikati mwa Mji wa Gaza.
Mashambulizi ya pande zote ya Israel katika mji wa Gaza yamezidisha mzozo wa kibinadamu huko.
Siku ya Jumanne, Rais wa Marekani Donald Trump alikutana na viongozi wa Waarabu na Waislamu katika Umoja wa Mataifa kujadili usitishaji vita huko Gaza, kuachiliwa kwa mateka na utawala wa baada ya vita huko Gaza.
Chombo cha habari cha Imarati kilisema mazungumzo hayo yalilenga katika kumaliza vita, ingawa maelezo ya mpango huo wa Washington bado hayako wazi.
Jana - Septemba 23 - Marais wa Uturuki na Brazil waliikosoa vikali Israel katika hotuba zao kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
"Mashambulizi ya kigaidi ya Hamas hayana uhalali wowote, lakini hakuna chochote kinachohalalisha mauaji ya kimbari huko Gaza," Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, alisema mbele ya Rais wa Marekani Donald Trump katika Umoja wa Mataifa.
Mwandishi wa habari wa Australia aliyefukuzwa kazi kwa ujumbe kuhusu Gaza alipwa $150,000
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kufukuzwa kwa Antoinette Lattouf kulizua wimbi la hasira ya umma
Shirika la utangazaji la taifa la Australia limeagizwa kulipa A$150,000 (£73,435.50, $99,200) kama adhabu kwa kumfukuza kinyume cha haki mtangazaji kutokana na chapisho la mtandao wa kijamii kuhusu vita vya Gaza.
Shirika la Utangazaji la Australia (ABC) lilimwondoa mtangazaji wa redio Antoinette Lattouf hewani mnamo Desemba 2023 kwa sababu ya maoni yake ya kisiasa na baada ya ushawishi kutoka kwa vikundi vinavyounga mkono Israeli, Mahakama ya Shirikisho ilipata mapema mwaka huu.
Lattouf tayari ametunukiwa fidia ya A$70,000, lakini Jumatano Jaji Darryl Rangiah alisema kiasi "kikubwa" cha ziada kilihitajika ili kuhakikisha ABC inajifunza somo lake.
Mtangazaji huyo ameomba msamaha hadharani kwa Lattouf, akisema pia iliwafelisha wafanyikazi wake na watazamaji.
Kufukuzwa kwa Lattouf kulizua wimbi la hasira ya umma na kuzua taharuki katika shirika la ABC - na kuibua maswali juu ya uhuru wake na kuibua wasiwasi kuhusu jinsi inavyosaidia wafanyikazi, hasa wale ambao wana utamaduni tofauti.
"ABC ilidhalilisha umma wa Australia vibaya iliposalimisha haki za mfanyakazi wake ... ili kutuliza kikundi cha watetezi," Jaji Rangiah alisema Jumatano.
Macron kukutana na Masoud Pezeshkian kujadili mpango wa nyuklia wa Iran
Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema atakutana leo na mwenzake
wa Iran Masoud Pezeshkian kujadili mpango wa kinyuklia wa Iran miongoni mwa
masuala mengine.
Akihutubia mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa unaofanyika New
York, Bwana Macron ameonya kuwa vikwazo vikali vya Umoja wa Mataifa huenda
vikarejeshwa kama Iran haitaruhusu shirika la kudhibiti matumizi ya silaha za
kinyuklia kufanya kazi.
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian
Viongozi wa Ulaya walikutana na waziri wa mambo ya kigeni hapo jana lakini hakukupigwa juhudi zozote.
Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesisitiza nchi hiyo haitashinikizwa kuachana na mpango wake wa kinyuklia.
Iran ina mpaka Jumamosi hii kufikia makubaliano na mataifa yenye nguvu ya Ulaya la sivyo irejeshewe vikwazo vilivyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa vilivyoondolewa baada ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015.
Rais wa Somali aiambia BBC amenusurika majaribio kadhaa ya Al-shabab yaliyolenga kumuua
Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Omalia Hassan Sheikh Mohamud amefichua kwamba sasa
yeye ni shabaha kuu ya al-Shabaab, kikundi cha Kiislamu chenye mafungamano na
Al-Qaeda.
Katika mahojiano
marefu ya kipekee na BBC, alisema alikuwa amenusurika majaribio kadhaa ya
mauaji na kikundi hicho.
"Kwa miaka miwili iliyopita,
al-Shabaab wamenijaribu mara tano, kwa sababu wanaamini mabadiliko ambayo
wanaweza kuzima vita dhidi yao ni kumuua rais. Miji mingi imekombolewa kutoka kwa al-Shabaab
lakini bado inafanya kazi katika maeneo ya vijijini. Al-Shabaab ni dhaifu
ikilinganishwa na maisha yao ya zamani."
Somalia inakabiliwa na vitisho vya usalama kutoka kwa
al-Shabaab na ISIS, licha ya uingiliaji kati wa kijeshi wa vikosi vya Umoja wa
Afrika na Marekani.
Wachambuzi wanasema kuwa mafanikio ya hivi karibuni ya
al-Shabaab katika Somalia ya kati na kusini yanaonyesha kwamba kundi hilo bado
ni tishio kubwa.
Pia alithibitisha uwepo wa vikosi vya Jubaland nchini Kenya.
"Wamevuka
kwenda Kenya, na wako huko Mandera. Hatujafurahishwa na hilo, na tumeshiriki
wasiwasi wetu na serikali ya Kenya, na waliahidi kwamba watachukua hatua, na
tutaenda pamoja na kufanyia kazi usalama wa eneo la mpaka."
Wakati
akizungumzia masuala ya kikanda rais aliapa kuendeleza kupelekwa kwa wanajeshi
wa Misri nchini mwake, licha ya wasiwasi kwamba inaweza kuongeza mvutano na
nchi jirani ya Ethiopia.
Alipuuzilia mbali ripoti za uwezekano wa makabiliano kati
ya walinda amani wa Misri na Ethiopia katika ardhi ya Somalia. Somalia
inajiandaa kuwapokea walinda amani wa Misri wakati wa kukaribisha vikosi vya
Ethiopia.
Kuna wasiwasi
kwamba nchi zote mbili zinaweza kupanua mpasuko wao juu ya Bwawa la Grand
Ethiopian Renaissance hadi Somalia. Alisisitiza kuwa nchi yake haitakuwa uwanja
wa vita vya wakala.
Mwanaume apatikana na hatia ya kujaribu kumuua Trump Florida
Chanzo cha picha, Reuters
Ryan Routh
amepatikana na hatia ya kujaribu kumuua Rais Donald Trump kwenye uwanja wa gofu
wa Florida Septemba mwaka jana.
Mahakama ilimpata
Routh, 59, na hatia ya mashtaka yote, ikiwa ni pamoja na jaribio la mauaji ya
mgombea mkuu wa urais na makosa kadhaa ya kutumia silaha.
Tukio hilo
lilitokea tarehe 15 Septemba 2024 wakati Trump, ambaye wakati huo alikuwa
mgombea urais, alikuwa akicheza gofu kwenye uwanja anaoumilik uliopo katikaufukwe wa West Palm Beach,
takriban dakika 15 kutoka kwa makazi yake ya Mar-a-Lago.
Routh alijaribu kujidhuru baada ya hukumu kusomwa, kulingana na mshirika wa BBC wa Marekani, CBS News. Inasemekana alijaribu kujichoma kisu kwa kutumia kalamu kabla ya Wanajeshi wa Marekani kuingilia kati.
Katika chapisho la mtandao wa kijamii mara baada ya hukumu hiyo, Trump alishukuru vyombo vya sheria na shahidi ambaye alitoa taarifa zilizofanikisha kukamatwa kwa Routh.
Trump alisema kuhusu Routh: "Huyu alikuwa mtu muovu mwenye nia mbaya, na walimkamata. Wakati mkubwa sana kwa HAKI NCHINI AMERIKA!".
Mwanasheria mkuu wa serikali Pamela Bondi alisema: "Jaribio hili la kumuua halikuwa tu shambulio kwa rais wetu, bali ni dharau kwa taifa letu."
Idadi ya majeruhi wa shambulio la Israel Mjini Gaza yawalemea madaktari
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Baadhi ya Wapalestina waliouawa wakati wa mashambulizi ya Israel katika mji wa Gaza wanazikwa katika uwanja wa hospitali ya al-Shifa.
Madaktari katika hospitali moja ya mwisho ya Jiji la Gaza
wanasema wamelemewa na majeruhi kutokana na mashambulizi ya Israel na wanalazimika
kufanya oparesheni katika mazingira machafu na hakuna dawa za ganzi.
Daktari mmoja wa Australia anayejitolea katika hospitali ya
al-Shifa aliambia BBC kwamba kila siku kulikuwa na tukio la majeruhi wengi,
huku mwingine akielezea jinsi mtoto mchanga alivyookolewa kutoka kwa mwili wa
mwanamke mjamzito ambaye alikuwa amekatwa kichwa.
Vikosi vya Israel kwa sasa viko umbali wa mita 500 tu kutoka
hospitali huku wakipanua mashambulizi yao ya ardhini ili kuliteka kikamilifu
Jiji la Gaza, ambalo jeshi la Israel linaiita Hamas "ngome kuu".
Walioshuhudia wanasema vifaru vinaingia katikati mwa jiji
kutoka kusini na kaskazini-magharibi.
Mashambulio ya anga na mizinga ya Israel, mashambulio ya
ndege zisizo na rubani na ulipuaji wa magari yanayoendeshwa kwa mbali yakiwa na
vilipuzi yanaendelea kuwafukuza makumi ya maelfu ya Wapalestina kutoka makwao
kila siku.
Trump asema Ukraine inaweza kuyakomboa maeneo yake yote yaliyotekwa na Urusi
Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Kyiv inaweza
"kushinda Ukraine yote na kuirejesha katika hali yake awali", na
hivyo kuashiria mabadiliko makubwa katika msimamo wake kuhusu vita na Urusi.
Katika chapisho kwenye jukwaa lake la la kijamii, Truth Social , amesema Ukraine inaweza
kurudisha "mipaka ya asili kutoka mahali ambapo vita hivi vilianza"
kwa msaada wa Ulaya na Nato, kutokana na shinikizo kwa uchumi wa Urusi.
Maoni yake yamekuja baada ya mazungumzo na Rais wa Ukraine
Volodymyr Zelensky, yaliyofanyika baada ya Trump kulihutubia Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Jumanne.
Trump amerudia kuelezea nia yake ya kumaliza vita, lakini
hapo awali alionya kwamba mchakato huo unaweza kuhusisha Ukraine kutoa eneo
fulani, matokeo ambayo Zelensky amekuwa akiyakataa mara kwa mara.