Waziri Mkuu wa Israeli akataa ukosoaji wa vita vya Gaza na wanajeshi wa akiba
Jeshi linasema litawafuta kazi wanajeshi wa akiba ambao walitaka kurudishwa kwa mateka wapewe kipaumbele badala ya kupigana na Hamas.
Muhtasari
- Mwanamke ajifungua mtoto asiyemfahamu baada ya kiinitete kuchanganywa
- Waziri Mkuu wa Israeli akataa ukosoaji wa vita vya Gaza na wanajeshi wa akiba
- Polisi yazuia mkutano wa Chadema yapiga mabomu ya machozi kutawanya wafuasi
- Zimbabwe yafanya malipo ya kwanza ya fidia kwa wakulima wazungu juu ya kunyakua ardhi
- Sanaa na Siasa: Kwanini maigizo ya 'Echoes of War' yaibua hisia Kenya
- Mabadilishano ya wafungwa ya Marekani na Urusi: Aliyefungwa jela kwa kusaidia Ukraine aachiliwa
- Mahakama ya Kimataifa ya The Hague inaanza kusikiza kesi ya Sudan dhidi ya UAE
- Marekani yawafungulia mashtaka raia wake waliotuhumiwa kufanya jaribio la mapinduzi DRC
- Sudan kusini: Joto la kisiasa lapanda baada ya wanachama wa muungano wa upinzani kutofautiana Sudan Kusini
- Uchunguzi wa mate unagundua saratani ya tezi dume mapema - Utafiti
- Trump aiwekea vikwazo Iran huku wakitarajiwa kufanya mazungumzo ya nyuklia
- Uokozi katika ukumbi wa burudani waendelea Jamhuri ya Dominican huku 184 wakifariki
- Marekani yasitisha ushuru wa juu zaidi kwa nchi nyingi lakini yazidisha dhidi ya China
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Asha Juma
Mwanamke ajifungua mtoto asiyemfahamu baada ya kiinitete kuchanganywa

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamke mmoja nchini Australia amejifungua mtoto wa mtu asiyemfahamu bila kujua, baada ya kliniki yake ya uzazi kuingiza kwa bahati mbaya viinitete vya mwanamke mwingine ndani ya chake.
Mchanganyiko huo katika kliniki ya kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi ya Monash IVF huko Brisbane, Queensland umesemekana kuwa makosa ya kibinadamu, vyombo vya habari vya Australia vinaripoti.
"Kwa niaba ya Monash IVF, nataka kusema ninasikitika sana kwa kile kilichotokea," Mkurugenzi Mtendaji Mkuu Michael Knaap alisema, akiongeza kwamba kila mtu katika kliniki ya uzazi "alihuzunishwa" na kosa hilo.
Mwaka jana, kliniki hiyo hiyo ililipa A$56m (£26.8m) kwa mamia ya wagonjwa ambao viinitete vyao viliharibiwa licha ya kuwa na uwezo wa kutungisha mimba.
Kulingana na msemaji wa Monash IVF, wafanyikazi walifahamu tatizo hilo mnamo mwezi Februari wakati wazazi waliozaa walipoagizwa kuhamisha viinitete vyao vilivyobaki vilivyogandishwa hadi kliniki nyingine.
"Badala ya kupata idadi inayotarajiwa ya viinitete, kiinitete cha ziada kilibaki kwenye hifadhi," msemaji huyo alinukuliwa akisema na ABC.
Monash amethibitisha kwamba kiinitete kutoka kwa mgonjwa mwingine kiliyeyushwa kimakosa na kuhamishiwa kwa mtu tofauti, na kusababisha kuzaliwa kwa mtoto.
Kliniki imeanzisha uchunguzi na tukio hilo limeripotiwa kwa vyombo vya udhibiti.
Soma zaidi:
Waziri Mkuu wa Israeli akataa ukosoaji wa vita vya Gaza na wanajeshi wa akiba

Chanzo cha picha, EPA
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekataa ukosoaji wa vita vya Gaza na baadhi ya wanajeshi wa akiba wa jeshi la anga, na kutaja tukio hilo kuwa "lisiloweza kusameheka".
Jeshi la Israeli lilisema kuwa litawafuta kazi wanajeshi wa akiba waliokuwa wametia saini barua ya kutaka kurejeshwa kwa mateka wa Israeli kupewa kipaumbele badala ya kupigana na Hamas.
Barua hiyo pia inasema mapigano ya sasa yamechochewa kisiasa na yatasababisha vifo vya mateka, wanajeshi wa Israeli na raia wasio na hatia.
Jeshi lilisema haliwezi kuruhusu wanajeshi wa akiba wanaohudumu kushiriki maandamano ya kisiasa.
Israeli ilianza tena kampeni yake ya angani na ardhini huko Gaza mwezi uliopita, ikisema kwamba shinikizo la kijeshi litailazimisha Hamas kuwaachilia mateka ambao bado inawashikilia.
Jeshi la anga la Israeli, ambalo limetumika sana huko Gaza katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, linategemea sana marubani wa jeshi la akiba.
Idadi kubwa ya waliotia saini barua hiyo ambao ni 970 iliyochapishwa katika magazeti ya Israeli Alhamisi asubuhi wamestaafu. Lakini inaripotiwa kuwa kadhaa bado ni wafanyikazi.
Barua hiyo haitoi wito wa kukataa kuhudumu, lakini inadai "kurejeshwa kwa mateka wote hata kama itamaanisha ni kwa gharama ya kusitisha uhasama".
Jeshi la Israeli lilianzisha kampeni ya kuiangamiza Hamas kujibu shambulizi la kuvuka mpaka ambalo halijawahi kutokea tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Zaidi ya watu 50,880 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo.
Soma zaidi:
Polisi yazuia mkutano wa Chadema yapiga mabomu ya machozi kutawanya wafuasi

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapema Leo Polisi walipiga mabomu ya machozi na kuwatawanya wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema huku wakizua viongozi wa chama hicho kufanya mkutano na waandishi wa habari.
Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kushikiliwa kwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, John Heche, Mjumbe wa Kamati kuu, Godbless Lema, Mwenyekliti wa chama hecho kanda ya Kusini, Aden Mayala na Mkurugenzi wa Mawasiliano na uenezi, Brenda Rupia, waliokuwa wazungumze na wanahabari.
Hayo yanakuja siku moja, baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu kukamatwa baada ya kumaliza mkutano wa hadhara mkoani Ruvuma, kusini mwa Tanzania.
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limethibitisha kumshikilia kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Chadema Tundu Lissu kwa tuhuma za uchochozi.
Taarifa ya jana ya chama hicho inadai kutofanyiwa haki na jeshi hilo, ikiwemo kuzuiwa kufanya mkutano na kutawanishwa kwa nguvu.
Awali kupitia mtandao wa kijamii wa x, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche aliandika kuwa wamezuiwa kufanya mkutano wa waandishi wa habari ambao ulipangwa kufanyika katika ofisi za chama zilizopo Mfaranyaki, Songea.
Heche pia alisema, wafuasi wao pia walitawanywa kwa mabomu ya machozi yaliyopigwa na jeshi la polisi.
Wakati hayo yakiendelea watetezi mbalimbali wa haki za binadamu wameitaka Serikali ya Tanzania kufuata misingi ya haki.
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kupitia kwa Rais wake, Wakili Boniface Mwabukusi kimesema kinafuatilia kujua nini kimepelekea Lissu kukamatwa.
Wakili Mwabukusi anukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akisema, “Nguvu illyotumiwa na Polisi dhidi ya Raia wasiokuwa na silaha yeyote siyo tu matumizi mabaya ya sheria bali ni hali inayoashiria kutokuwajibika na kukosekana kwa ustahimilivu wa kisiasa katika taifa letu.”
"Kulikuwa na namna nyingi za kiueledi ambazo zingeweza kufanyika bila rabsha wala risasi au mabomu ya machozi, Lissu sio tu kwamba ni Mwanachama na Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani huyu pía ni Mwanachama hai wa TLS na ana haki kwa mujibu wa sheria,” alisema wakili huyo.
BBC imezungumza na baadhi ya wafuasi wa chama hicho ambao wamedai kuwa kinachoendelea hakiwapunguzii nguvu kuelekea uchaguzi.Mmoja wa wafuasi hao alisema, “Tunalishangaa jeshi la polisi kusumbua chama chetu wakati tunafanya mikutano kwa amani. Chama dola, CCM kinalitumia jeshi hilo vibaya na sioni kama watatuzuia kwenye siasa hizi kuelekea uchaguzi mkuu.”
'Wakati hayo yakiendelea, Chadema hivi karibuni imekuwa ikifanya na mikutano ya hadhara wakishinikiza kuwepo kwa mabadiliko ya sera na taratibu za chaguzi kabla ya kufanyika uchaguzi.
Chama hicho kimeweka shinikizo kieleza kuwa hakutakuwa na uchaguzi iwapo mabadiliko hayo hayatafanyika.
Zimbabwe yafanya malipo ya kwanza ya fidia kwa wakulima wazungu juu ya kunyakua ardhi

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Zimbabwe imetangaza malipo ya awali ya $3m (£2.3m) kwa wakulima wazungu ambao mashamba yao yalitwaliwa chini ya mpango wa serikali wenye utata zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Ni malipo ya kwanza kufanywa chini ya makubaliano ya fidia ya mwaka 2020 yaliyotiwa saini kati ya serikali na wakulima wazungu wa ndani ambapo Zimbabwe ilijitolea kulipa $3.5bn (£2.6bn) kwa mashamba yaliyonyakuliwa.
Maelfu ya wakulima wazungu walilazimishwa kutoka katika ardhi yao, mara nyingi kwa jeuri, kati ya mwaka 2000 na 2001.
Unyakuzi huo ulikusudiwa kurekebisha unyakuzi wa ardhi enzi za ukoloni lakini ulichangia kuzorota kwa uchumi wa nchi hiyo na kuharibu uhusiano na nchi za Magharibi.
Malipo hayo yaliyotangazwa Jumatano ni ya wakulima 378 wa kwanza, kati ya 740 waliokuwa wamiliki wa mashamba ambao fidia yao ilikuwa imeidhinishwa.
Mnamo mwaka 1980, Zimbabwe ilipata uhuru, na kumaliza miongo kadhaa ya utawala wa wazungu wachache. Wakati huo, sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba zaidi ilikuwa ikimilikiwa na wakulima wazungu takriban 4,000.
Mageuzi ya aŕdhi yalilenga katika kugawa upya aŕdhi inayomilikiwa na wazungu kwa wakulima weusi, kufuatia seŕa za enzi za ukoloni wakati maelfu ya wakulima weusi walilazimishwa kutoka katika aŕdhi yao na maeneo yenye rutuba zaidi nchini humo yalitengwa kwa ajili ya watu weupe.
Mnamo mwaka wa 2000, Rais wa wakati huo Robert Mugabe aliunga mkono uvamizi wa ardhi uliofanywa na mseto wa vikosi vya serikali na vikundi vya kujihami, na hivyo kuzua shutuma za kimataifa.
Rais Emmerson Mnangagwa, ambaye alichukua nafasi ya Mugabe katika mapinduzi ya mwaka 2017, ametaka kutatua mzozo huo ili kurejesha uhusiano na serikali za Magharibi.
Soma zaidi:
Sanaa na Siasa: Kwanini maigizo ya ‘Echoes of War’ yaibua hisia Kenya

Chanzo cha picha, Facebook
Maelezo ya picha, Jalada ya tamthilia inayoibua hisia mseto Kenya Wanafunzi wa shule ya upili ya wasichana ya Butere nchini Kenya wamesusia hafla ya maigizo yanayoendelea katika shule ya Lions jijini Nairobi.
Wanafunzi hao wamedinda kuigiza tamthilia ya "Echoes of War" baada ya umma kuzuiwa kuhudhuria hafla hiyo, wakiimba wimbo wa taifa na kuondoka jukwaani.
Walifika kufuatia agizo la mahakama kuu ya Nyamira iliyoidhinisha mchezo huu kuigizwa baada ya wasichana hao kutakiwa waende likizo ilhali walipaswa kuhudhuria tamasha hizo za maigizo.
Kulingana na wakili wa shule hiyo Ken Echesa aliyekuwa amehudhuria ameapa kurejea mahakamani kumshtaki Mkurugenzi wa wizara ya elimu ukanda wa magharibi bwana Abiero kwa kutofuata agizo la mahakama kikamilifu.
Kulingana na Eugene Wamalwa aliyekuwa waziri wa ulinzi na wakili wa mwandishi wa igizo hilo, Cleophas Malala amesema kuwa Malala amezuiliwa eneo la Eldama Ravine tangu jana usiku.
Hata hivyo ameachiliwa na wakati wowote atakuwa akihutubia wanahabari.
Haya yakijiri maafisa wa polisi wametupa vitoa machozi katika shule moja walimoweka makaazi wanafunzi wa Butere ilikuwatawanya baada yakudinda kuigiza tamthilia yao kama ilivyotarajiwa.
Maudhui ya tamthilia ni yepi?
Tamthilia ya Echoes of War inaangazia mapambano ya vijana kuhusu uhuru wa kiraia, utawala na haki ya kijamii. Maudhui yake yanachora taswira ya taifa la Kenya linalopona kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe huku vijana wakitarajiwa kuwa nguvu kubwa katika ujenzi wa taifa.
Hisia zinazoendelea kuibuliwa
Kupitia ukurusa wa X chama cha ODM kimesuta vikali serikali kwa kuingilia ubunifu wa wanafunzi katika maigizo ya shuleni.
‘’Funzo kubwa kutoka kwayo ni kwamba hata sauti za watoto wa shule zina umuhimu, na kwa kweli hazina hatia, sauti zao zinahitajika katika kuendesha mjadala wa kitaifa. Hakika tunaifananisha na igizo maarufu la Afrika Kusini la Sarafina’’ ODM ilisema.
Naye Mwenyekiti wa chama cha KANU, Gideon Moi, amekashifu serikali kwa kuwanyima wanafunzi hao fursa ya kutumia kipaji chao.
Wakati huo huo, Amnesty International Kenya imelaani vikali hatua za polisi kuvuruga kwa nguvu onesho la tamthilia na kutaka Tume ya IPOA kuchunguza kwa uwazi na haraka vitendo vya polisi waliohusika, na kuhakikisha uwajibikaji.
Vipi fasihi ilijumuishwa katika mtaala wa elimu Kenya?
Mnamo mwaka wa 2010, Wizara ya Elimu ilianzisha sera ya mageuzi iliyojulikana kama “Demokrasia katika Elimu,” ikiwa na dhamira ya kuimarisha ushirikishwaji wa wanafunzi katika masuala ya usimamizi wa shule na kukuza mazingira ya mawasiliano ya wazi kati ya walimu, wanafunzi, na wadau wengine wa elimu.
Miongoni mwa vipengele muhimu vya sera hii ni:
• Kuanzishwa kwa baraza la wanafunzi katika shule, kama jukwaa la majadiliano ya wazi kati ya uongozi wa shule na wanafunzi.
• Uwekaji wa masanduku ya maoni ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kueleza mawazo yao kwa njia ya faragha na huru.
• Marekebisho kupitia Sheria ya Elimu ya Msingi ya mwaka 2013, yaliyojumuisha wawakilishi wa wanafunzi na walimu katika Bodi za Usimamizi za shule, hatua iliyolenga kuimarisha ushirikiano wa pande zote.
• Kufutwa rasmi kwa adhabu ya viboko, kama hatua ya kulinda haki za wanafunzi na kukuza mbinu mbadala za nidhamu.
• Kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa wanafunzi moja kwa moja na wanafunzi wenyewe, hatua iliyolenga kukuza maadili ya uongozi na uwajibikaji miongoni mwa vijana.
Kwa miaka mingi nchini Kenya, wanafunzi pia wamekuwa wakifundishwa kazi za fasihi zinazochambua kwa kina hali ya jamii.
Miongoni mwa kazi hizo ni Betrayal in the City, Masaibu ya Ndugu Jero, Damu Nyeusi, Mashetani, Kifo Kisimani, na Mstahiki Meya.
Kazi hizi za kifasihi zimekuwa zikiibua mijadala kuhusu maovu ya kijamii, ukandamizaji wa haki, na changamoto za kiuongozi katika jamii.

‘’Sanaa ni kioo cha Jamii’’
Sanaa, hususan michezo ya kuigiza, imekuwa daima kioo cha jamii.
Hata hivyo, wanaharakati wameibua hisia katika tukio la hivi majuzi lililohusisha kuingiliwa kwa mchezo wa kuigiza wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere na kuzua maswali kuhusu nafasi ya sanaa katika kueleza ukweli wa kijamii.
Mchezo huo ambao ulikuwa na fursa ya kuelimisha na kuamsha fikra, ulizimwa katika mazingira yenye utata, na hivyo kuvuta hisia za umma na kuibua mjadala mpana kuhusu uhuru wa kisanii nchini Kenya.
Mabadilishano ya wafungwa ya Marekani na Urusi: Aliyefungwa jela kwa kusaidia Ukraine aachiliwa

Chanzo cha picha, Reuters
Raia wa Urusi mwenye asili ya Marekani ameachiliwa huru katika mabadilishano ya wafungwa kati ya Moscow na Washington.
Ballerina Ksenia Karelina, mkazi wa Los Angeles, alikuwa gerezani nchini Urusi kwa zaidi ya mwaka mmoja, baada ya kukamatwa katika jiji la Yekaterinburg mapema 2024.
Alipatikana na hatia ya uhaini kwa kutoa pesa kwa shirika la misaada lenye makao yake makuu nchini Marekani linalotoa msaada wa kibinadamu kwa Ukraine na alihukumiwa kifungo cha miaka 12.
Kwa kubadilishana, Marekani iliripotiwa kumwachilia Arthur Petrov, raia mwenye uraia mara mbili wa Ujerumani-Urusi aliyekamatwa Cyprus mwaka wa 2023. Alishtakiwa kwa kusafirisha vifaa vidogo vya kielektroniki kwenda Urusi kwa watengenezaji wanaofanya kazi na jeshi la Urusi kinyume cha sheria.
Mabadilishano ya wafungwa yalifanyika Abu Dhabi asubuhi ya Alhamisi.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio alithibitisha kuwa Bi Karelina alikuwa "kwenye ndege akirejea nyumbani Marekani."
Aliongeza kuwa "amezuiliwa kimakosa na Urusi kwa zaidi ya mwaka mmoja".
Ni mara ya pili kubadilishana wafungwa kati ya Urusi na Marekani katika muda wa chini ya miezi miwili.
Mnamo Februari, raia wa Urusi Alexander Vinnik - ambaye alifungwa katika jela ya Marekani kwa mashtaka ya utakatishaji fedha - aliachiliwa kwa kubadilishana na kuachiliwa kwa mwalimu wa shule wa Marekani Marc Fogel.
Pia unaweza kusoma:
Mahakama ya Kimataifa ya Haki huko The Hague (ICJ) inaanza kusikiza kesi ya Sudan dhidi ya UAE

Chanzo cha picha, Reuters
Mahakama ya Kimataifa ya Haki huko The Hague imeanza kusikiliza kesi ya Sudan dhidi ya UAE kwa tuhuma za kuunga mkono vikosi vya Rapid Support Forces ambayo imekuwa ikipigana nayo tangu katikati ya Aprili 2023.
Mahakama hiyo imepanga vikao viwili ambavyo vitazingatia ombi la Sudan la hatua za dharura kuchukuliwa dhidi ya UAE, ambayo inasema imekiuka Makubaliano ya Kimbari kuhusu watu wa Masalit, haswa huko Darfur Magharibi.
Katika ombi lake kwa ICJ, Sudan inadai RSF imekuwa na hatia ya "mauaji ya kimbari, ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia, uhamishaji wa lazima, na ukiukaji wa haki za binadamu."
Inadai: "Vitendo vyote kama hivyo vimetekelezwa na kuwezeshwa na msaada wa moja kwa moja kwa waasi wa RSF na nchi ya Falme za Kiarabu.
Sudan pia imewasilisha malalamiko dhidi ya taifa hilo la Ghuba katika Baraza la Usalama la UN.
Hata hivyo, UAE, imetupilia mbali madai hayo. Waziri wake wa Mambo ya nje, Anwar Gargash, katika ujumbe kwenye mtandao wa X, alisema "kipaumbele cha Sudan kinapaswa kuwa kusitisha mapigano katika vita hii ya upuuzi na ya uharibifu - na kushughulikia janga kubwa la kibinadamu ambalo limejitokeza."
Mnamo mwezi Januari, Marekani iliamua kwa kauli moja kwamba vikosi vya Rapid Support Force (RSF) - vilijihusisha katika vita vya kikatili dhidi ya vikosi vya jeshi la Sudan tangu 2023 - walikuwa na hatia ya mauaji ya kimbari na kuamuru vikwazo dhidi ya Kamanda Mohammed Hamdan Dagalo.
Soma zaidi:
Hujambo msomaji wetu. Karibu katika awamu ya pili ya matangazo ya moja kwa moja. Mimi ni wako Asha Juma.
Marekani yawafungulia mashtaka raia wake waliotuhumiwa kufanya jaribio la mapinduzi DRC

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Raia wa Marekani waliohukumiwa kwa kuhusika katika mapinduzi yaliyofeli nchini DRC Wizara ya Sheria ya Marekani imewafungulia mashtaka raia wanne wa Marekani kwa kuhusika kwao katika jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya watatu kati yao kurejeshwa mikononi mwa mamlaka za Marekani wiki hii.
Marcel Malanga, Tyler Thompson, na Benjamin Zalman-Polun walikuwa tayari wamehukumiwa nchini DRC kwa kuhusika katika jaribio hilo lililofeli la mapinduzi lililotokea Mei 2024, ambapo watu waliokuwa na silaha walivamia makazi ya maafisa waandamizi wa serikali na kwa muda mfupi walikalia ofisi ya urais jijini Kinshasa.
Watatu hao waliachiliwa huru Jumanne katika makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya mshauri mkuu wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu masuala ya Afrika, Massad Boulos, nchini DRC.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, washukiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kutumia silaha za maangamizi, kulipua majengo ya serikali, na kupanga kuua au kuwateka nyara watu katika nchi ya kigeni.
“Washukiwa walipanga kwa makusudi, walichunguza maeneo ya mashambulizi, na waliwataja waathiriwa waliolengwa katika shambulio la kijeshi, wakiwa na nia ya kuua watu wengine, wakiwemo maafisa wa ngazi za juu serikalini,” ilisema taarifa hiyo.
“Walihamasisha na kuwaajiri watu wengine kujiunga na mpango huo kama wapiganaji wa jeshi la waasi, na katika baadhi ya matukio, walitoa malipo ya kifedha kama kishawishi.”
Malanga, Thompson, na Zalman-Polun walikuwa miongoni mwa watu 37 waliohukumiwa na mahakama ya kijeshi ya DRC mnamo mwezi Septemba, wakipatikana na hatia ya kula njama ya kihalifu, ugaidi, na makosa mengine, na wote wakahukumiwa adhabu ya kifo.
Hata hivyo, mchakato wa kuwaachilia huru ulihusishwa na mazungumzo yanayoendelea kati ya Marekani na Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, kuhusu uwekezaji katika sekta ya madini.
Watu hao watatu walikana mashtaka yote na walikata rufaa dhidi ya hukumu hiyo bila mafanikio.
Wiki iliyopita, Rais Tshisekedi alipunguza adhabu yao hadi kifungo cha maisha, kabla ya kuwakabidhi kwa mamlaka za Marekani.
Soma pia:
Sudan Kusini: Joto la kisiasa lapanda baada ya wanachama wa muungano wa upinzani kutofautiana

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Riek Machar amekuwa hasimu wa rais Salva Kiir kwa miaka Muungano mkuu wa upinzani nchini Sudan Kusini umeonekana kugawanyika, hali inayozidisha mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini humo.
Kiongozi wa chama cha upinzani SPLM-IO , Dkt. Riek Machar, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini kufuatia makubaliano ya amani yaliyolenga kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir, aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani mwezi uliopita.
Hapo jana, kundi la viongozi waandamizi wa SPLM-IO lilitangaza nia ya kumteua Stephen Par Kuol kuwa kiongozi wa mpito hadi pale Dkt. Machar atakapokuwa huru.
"Tulichofanya ni kutatua mgogoro huu wa uongozi ambao umesababishwa na mgogoro unaotokana na kuwekwa kizuizini kwa mwenyekiti wetu na kutoroka kwa viongozi wetu wengine kama naibu mwenyekiti na katibu mkuu," alisema Par.
Hata hivyo, hatua hiyo ilipingwa na baadhi ya wajumbe wa chama hicho, huku Par Kuol akilazimika kujitetea dhidi ya madai kwamba alikuwa anatekeleza mapinduzi ya kisiasa ndani ya chama.
Ikiwa ni wiki mbili tangu Machar awekwe kifungo cha nyumbani Par sasa ametoa wito kiongozi huyo na wanachama wengine wakuu wa SPLM-IO ambao walizuiliwa kufuatia ghasia mbaya kaskazini mwa nchi waachiliwe huru.
"Kitendo hiki cha kuwekwa kizuizini kinadhoofisha kanuni za amani na mazungumzo muhimu kwa ukombozi wa taifa letu," alisema.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukionya kuwa Sudan Kusini iko kwenye ukingo wa kurejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kufuatia kuongezeka kwa mzozo kati ya Machar na rais ambao umeendelea kwa wiki kadhaa.
Viongozi hao wawili walikubaliana mnamo Agosti 2018 kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoua karibu watu 400,000.
Lakini katika kipindi cha miaka saba iliyopita uhusiano wao umezidi kuwa mbaya huku kukiwa na mivutano ya kikabila na ghasia za hapa na pale.
Soma pia:
Uchunguzi wa mate unagundua saratani ya tezi dume mapema - Utafiti

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kwa PSA, uchunguzi wa njia ya haja kubwa ni moja ya hatua zilizopendekezwa kwa uchunguzi wa saratani ya tezi dume Kupimwa mate kunaweza kusaidia “kubadili mkondo” wa saratani ya tezi dume, kwa mujibu wa wanasayansi nchini Uingereza.
Vipimo hivyo huchambua vinasaba (DNA) vya wanaume ili kubaini wale waliozaliwa wakiwa na hatari kubwa ya kuugua saratani ya tezi dume.
Kwa kuwalenga wanaume hao kufanyiwa vipimo vya kutoa sampuli ya mate ili kupimwa kwa maabara na uchunguzi wa MRI, wanasayansi wameweza kugundua baadhi ya aina hatari za saratani ambazo zingepuuzwa pasipo dalili za wazi.
Hata hivyo, jaribio hilo bado halijathibitishwa kuwa lina uwezo wa kuokoa maisha, na wataalamu wanatahadharisha kuwa huenda ikachukua miaka kadhaa kabla ya vipimo kama hivyo kuanza kutumika kwa kawaida katika huduma za afya.
Kila mwaka, takriban wanaume 12,000 hufariki kutokana na saratani ya tezi dume nchini Uingereza.
Wito wa kuanzishwa kwa uchunguzi wa mara kwa mara kwa wanaume wenye afya njema – maarufu kama upimaji wa saratani – umekuwa mkubwa zaidi, hasa baada ya bingwa wa baiskeli wa Olimpiki, Sir Chris Hoy, kutangaza kuwa ana saratani ya hatua ya mwisho ya tezi dume.
Hapo awali, upimaji wa kawaida ulitupiliwa mbali kutokana na kasoro za kipimo kilichopo sasa, ambacho hupima viwango vya protini maalum ya tezi dume (PSA) kwenye damu.
Profesa Dusko Ilic wa Chuo Kikuu cha King’s College London amesema matokeo ya utafiti huo ni ya “kuahidi”, lakini jaribio hilo linaongeza ugunduzi wa saratani kwa kiasi kidogo tu linapotumiwa pamoja na viashiria vya hatari vilivyopo kama umri, viwango vya PSA na uchunguzi wa MRI.
Aidha, Profesa Ilic ameongeza kuwa bado hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa jaribio hilo linaongeza muda wa kuishi au kuboresha maisha ya wagonjwa, hivyo kuna haja ya kufanya tafiti zaidi.
Utafiti huo kwa sasa umejikita kwa watu wa asili ya Ulaya pekee, na juhudi zinaendelea kulibadilisha ili liweze kutumika kwa watu kutoka asili nyingine.
Inasadikiwa kuwa wanaume wenye asili ya Kiafrika wako katika hatari mara mbili zaidi ya kuugua saratani ya tezi dume.
Timu ya watafiti pia imeeleza kuwa kuna maswali yanayohitaji kujibiwa kuhusu ufanisi wa gharama, madhara yanayoweza kujitokeza, na muda muafaka wa kuchambua hatari hiyo.
Jaribio la mate sasa limeingizwa katika utafiti mkubwa unaoitwa Transform, unaolenga kubaini mbinu bora ya kuanzisha mpango wa upimaji wa saratani ya tezi dume nchini Uingereza.
Pia unaweza kusoma:
Trump aiwekea vikwazo Iran huku wakitarajiwa kufanya mazungumzo ya nyuklia

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais Donald Trump Marekani imeiwekea vikwazo Iran, siku chache tu baada ya Rais Donald Trump kutangaza watafanya mazungumzo na Iran kuhusu mpango wake wa kinyuklia.
Hatua hiyo inaonekana kulenga kuishinikiza Iran kuelekea mazungumzo yaliyopangwa kufanyika Jumamosi hii huko Oman.
Hapo jana, Bwana Trump alirejelea vitisho vyake kuwa uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi upo iwapo Iran haitakomesha mpango wake wa kinyuklia na kuongeza Israel itakuwa na mchango mkubwa kuhusiana na Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alithibitisha kuwa mkutano huo utafanyika huko Oman tarehe 12 Aprili lakini hautakuwa wa moja kwa moja na Marekani.
Kupunguza uwezo wa Iran katika uzalishaji wa silaha za kinyuklia kumekuwa ni lengo kuu la sera za kigeni za Marekani na washirika wake kwa miongo kadhaa.
Katika mwaka 2015, Rais Barack Obama alifanikisha makubaliano na Iran, ambayo ilikubali kupunguza shughuli zake za kinyuklia na kuruhusu wakaguzi wa kimataifa ili kuhakikisha vifaa vinatumika kwa madhumuni ya kiraia pekee, na sio kwa ajili ya uzalishaji wa silaha.
Hata hivyo, mwaka 2016, Trump alijiondoa kutoka kwa makubaliano hayo, akielezea kushinikiza kurekebisha makubaliano hayo.
Katika miaka iliyofuata, Iran ilikiuka masharti ya makubaliano hayo, na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limeonya kuwa Iran imejilimbikizia hifadhi kubwa za urani ya kutajirika, ambayo inaweza kutumika kutengeneza mabomu ya kinyuklia.
Israel, kwa upande wake, inaona kuwa kuzuia Iran kupata silaha za kinyuklia ni jambo muhimu sana kwa usalama wake wa muda mrefu.
Inaripotiwa kwamba imekuwa ikifikiria kushambulia vituo vya uzalishaji vya Iran katika miezi ya hivi karibuni. Mwaka jana, Israel ilisema kuwa ilishambulia tovuti ya kinyuklia ya Iran kwa kulipiza kisasi kwa shambulizi la makombora kutoka Iran dhidi ya Israel.
Makubaliano haya yanaashiria safari ndefu na ngumu katika juhudi za kimataifa za kudhibiti silaha za kinyuklia za Iran.
Kila upande unalenga kuonyesha msimamo wake, huku mamilioni ya watu wakiwa wameshika pumzi, wakisubiri kuona kama tahadhari za kisiasa na kidiplomasia zitafanikiwa au kama mlango wa vita utalipuka.
Marekani imeiwekea vikwazo serikali ya Iran tangu mwaka 1979, wakati ubalozi wa Marekani mjini Tehran ulipotekwa na maafisa kushikiliwa mateka.
Marekani ilianza kuweka vikwazo kwa mpango wa nyuklia wa Iran mwaka 1992.
Sasa imeweka vikwazo vingi zaidi dhidi ya Iran kuliko dhidi ya nchi nyingine yoyote.
Marekani imepiga marufuku makampuni yake kufanya biashara na Iran.
Pia unaweza kusoma:
Uokozi katika ukumbi wa burudani waendelea Jamhuri ya Dominican huku 184 wakifariki

Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa wa uokozi katika Jamhuri ya Dominican sasa wanaelekeza nguvu katika kutafuta miili na sio tena kuokoa walioangukiwa na paa la ukumbi wa burudani siku mbili zilizopita wakati wa tamasha la muziki.
Miili 124 imetolewa kutoka klabu ya Jet Set. Kwa muda wa siku mbili familia zimekusanyika nje ya mabaki ya klabu ya Jet Set huko Santo Domingo, zikihangaikia taarifa kuhusu jamaa zao waliopotea na kushiriki picha na polisi ili kusaidia katika utambuzi.
Maafisa hao wa uokozi wanasaidiwa na timu ya Israel na Mexico ambao wanatumia vifaa vya hali ya juu kujaribu kupata mtu yeyote ambaye bado yuko hai.
Madai yameanza kuibuka kiini cha anguko la paa hilo ambalo limeua watu 184.
Wengi wananyooshea kidole cha lawama tukio la moto lililotokea katika klabu hiyo ya burudani miaka miwili iliyopita.
Wengine wanahofia kuwa moto huo ulidhoofisha nguzo za jengo hilo na kuhofia kuwa huenda ukarabati uiofanywa baada ya mkasa haukuafiki viwango hitajika.
Mmiliki wa klabu ya Jet Set, Antonio Espaillat, alitoa ujumbe wa video kupitia mitandao ya kijamii kutoa rambirambi zake na zile za "familia yote ya Jet Set", kwa jamaa za waathiriwa.
Pia alisisitiza kuwa yeye na timu yake walikuwa wakishirikiana "kwa uwazi na mamlaka" juu ya janga hilo.
Msanii maarufu Rubby Perez aliyekuwa akitumbuiza ni miongoni mwa waliofariki.
Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yasitisha nyongeza ya ushuru lakini haijaisaza China

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump Rais Donald Trump ametangaza kusitisha kwa siku 90 nyongeza ya ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka mataifa mengine huku akikosa kuilegezea China.
Katika mabadiliko makubwa ya sera, saa chache baada ya ushuru dhidi ya takriban washirika 60 wa biashara wa Marekani kuanza, Trump alisema alikuwa akiidhinisha "kupunguzwa kwa ushuru wa asilimia 10%" wakati mazungumzo yakiendelea.
Hata hivyo aliongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa kutoka China hadi asilimia 125%, akiishutumu Beijing kwa "ukosefu wa heshima" baada ya kulipiza kisasi kwa kusema kuwa ingetoza ushuru wa 84% kwa bidhaa za Marekani.
"Itafika wakati China igundue kuwa siku za kuvuna kutoka kwa Marekani na nchi zingine sio endelevu au kukubalika," anasema Trump.
Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisisitiza kuwa mabadiliko ya sera hayajaathiriwa na anguko la kimataifa la kiuchumi, lakini mwandamizi wa chama cha Democrat Chuck Schumer alisema uamuzi huo unaonyesha Trump "anayumba na kurudi nyuma".
Akihojiwa na waandishi wa habari kuhusu athari za kujibizana na China kibiashara, Bwana Trump amesema anaamini watafikia makubaliano na kiongozi wa China.
"Nadhani Rais Xi ni mtu anayefahamu fika anachokifanya.Ni mwerevu,anaipenda nchi yake,hilo nafahamu vyema,namjua vizuri na nadhani atataka kufikia makubaliano,nadhani hilo litafanyika.Tutapata simu wakati fulani na kutaafikiana,litakuwa jambo jema kwa na kwetu na litakuwa jambo jema kwa ulimwengu na ubinadamu", anasema Trump.
Hata hivyo, uamuzi huu mpya wa Trump haujaathiri tangazo la awali a ushuru ambao unaendelea kutekelezwa tangu tarehe 2 mwezi Aprili.
Hizi ni pamoja na asilimia 25% ya ushuru wa kuagiza kwa magari na vipuri vya magari vinavyoingia Marekani, na ushuru zaidi wa 25% kwa bidhaa zote za chuma na alumini.
Ushuru wa kimataifa wa Trump umesababisha msukosuko mkubwa zaidi wa biashara ambao hujawahi kutokea katika miongo kadhaa.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja
