'Ugumba ulinifanya nijihisi mwenye hatia'

Chanzo cha picha, Andrea Byrne / Y Lolfa
- Author, Rosie Mercer
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mtangazaji wa habari Andrea Byrne amesema alihofia mumewe angekuwa "afadhali" bila uwepo wake katika safari ya miaka saba ya wanandoa hao kutokuwa na uwezo wa kupata mtoto.
Byrne, 45, ambaye ameolewa na mchezaji wa zamani wa raga wa Wales Lee Byrne, 44, amewasilisha habari za Welsh na mtandao katika kituo cha ITV tangu 2008.
“Unajihisi kuwa mwenye kasoro,” anasema Byrne, akikumbuka wakati alipoambiwa na madaktari kwamba yhuenda hangeweza kubeba mimba yake mwenyewe.
"Nakumbuka hisia hizo zikinizonga nikifikiria jinsi mwenza wangu [Lee] angekuwa bora bila uwepo wangu."
Wanandoa hao walimzaa binti yao Jemima, ambaye "alikiuka sayansi" kwa kuzaliwa kupitia njia asilia, mnamo 2019.
"Ninajawa na hisia ninaposimulia hadithi yangu, kwamba huenda ukafikiria labda ilikuwa jambo rahisi kusema kwa sababu hatimaye tulifanikiwa kupata mtoto," alisema Byrne.
"Lakini bado ninahisi kuna haja ya kuzungumzia hili, kwa sababu najua jinsi tulivyokuwa wapweke wakati wa safari hiyo."

Chanzo cha picha, Andrea Byrne / Y Lolfa
Baada ya kufunga ndoa Siku ya Mwaka Mpya mnamo 2012, Byrne anasema yeye na mumewe walianza mpango wa kupata ujauzito moja kwa moja.
"Sote tulikuwa mwanzoni mwa miaka yetu ya 30," alisema. "Sikuwa na sababu yoyote ya kufikiria kungekuwa na chochote cha kuhofia."
Baada ya muda, walienda kwenye kliniki ya uzazi kwa ajili ya vipimo.
Uchunguzi wa ultrasound ulifichua suala la unene wa ukuta wa tumbo la uzazi la Byrne, ambalo alilielezea katika kitabu chake kipya Desperate Rants and Magic Pants kama "kasoro ya nadra isiyoweza kurekebishwa".
"Ni habari ambayo hukutarajia kusikia," Byrne aliambia BBC.

Chanzo cha picha, Andrea Byrne / Y Lolfa
Taarifa hizo zilifuatiwa na miaka kadhaa ya majaribio na taratibu za kimatibabu, ikiwa ni pamoja na upandikiza mimba, ama kwa kimombo In Vitro Fertilization (IVF).
"Kusema ukweli, siwezi hata kukumbuka idadi ya mizunguko hiyo," alisema.
"Pia tulijaribu vitu vingi tofauti kando na IVF, vitu ambavyo tulishauriwa vinaweza kufanya kazi kutoka kwa wataalam tofauti.
"Pia tulipata vipimo chanya ya mimba tukadhani tulikuwa wajawazito, lakini kwa bahati mbaya hatukufanikiwa.
"Kwa hivyo ilipitia kipindi kigumu cha panda shuka za hisia."
'Nenda tu ukatafute mtu mwingine'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Byrne alisema miaka ya kujaribu kupata ujauzito pia uliathiri uhusiano wake na mumewe.
"Nadhani tulivuka kizingiti hicho sababu yake, lakini wakati huo ulikuwa ngumu sana," alisema.
"Kuna kipindi tulijiuliza jinsi tutakavyoishi pamoja," aliongeza Byrne, "kwa sababu ni vigumu sana kihisia".
"Nakumbuka niliwahi kumwambia Lee, na alikuwa akipingana nami, kwa sababu nilikuwa nikisema 'jamani naomba utafute mtu mwingine, mtu mwingine ambaye anaweza kufanya hivi kwa urahisi zaidi, nenda tu utafute mwanamke mwingine'.
"Na angeniambia 'mke wangu, tuko pamoja katika hili'."
Madaktari hatimaye waliwaambia wanandoa hao tumaini lao pekee lilikuwa kubebewa mimba na, mnamo 2018, walianza kutafakari uwezekano wa kupata mwanamke atakayebeba mimba kwa niaba yao nchini Marekani.
Katika kitabu chake, Byrne anaeleza jinsi alivyofahamu dakika chache kabla ya kuwasilisha habari za jioni kwamba hakuna hata kiini-tete ambacho walitarajia kutumia kwa ajili ya mtu mwingine kuwabebea mimbo ambacho kingeweza kuishi.
Aliandika: "Najiangalia kwenye kioo jinsi machozi yanavyonilenga, nikijihisi mnyonge, kupumua kwa dhiki, nikitembea nje ya chumba cha mavazi, na kuweka tabasamu na kutembea kupitia chumba cha habari chenye shughuli nyingi, na kwenda kwenye studio."

Chanzo cha picha, Andrea Byrne / Y Lolfa
Byrne alisema wakati huo alihisi kama mwisho wa mapambano.
"Tulijadiliana baada ya hapo na kuamua tuendelee na maisha mengine pamoja," alisema.
"Najawa na hisia sana nikikumbuka hilo, kwa sababu nilijihisi mwenye hatia sana kwa kutoweza kufanya kile ambacho kila mwanamke angeweza kufanya."
Lakini miezi michache baadaye, cha kushangaza ni kwamba Byrne alipata mimba kwa njia ya kawaida.
"Tulishangaa sana, hatukuamini tumefanikiwa kupata ujauzito kwa kweli," alisema Byrne.
"Hatukuwa na matumaini kwasababu walisema sikuwa na uwezo wa kubeba ujauzito.
"Kwa hivyo mtoto wetu [Jemima] alikaidi kila mtu, ushauri wote wa matibabu tuliopewa, alikuja na kusema 'hapana, nitazaliwa'."

Chanzo cha picha, Andrea Byrne / Y Lolfa
Byrne, ambaye pia anaandaa podcast ya uzazi inayofahamika kama Making Babies, alisema wazo la kuandika kitabu chake lilikuwa la "kihisia."
"Najua ni neno dogo lakini linatoa mwanga kidogo pia, nadhani," alisema.
Kitabu hiki kinajumuisha sura zinazoangazia safari ya uzazi ya watu wengine mashuhuri ambao wamesimulia hali yao kwenye podcast ya Byrne, akiwemo mtangazaji Gabby Logan na mcheshi Geoff Norcott.
"Ninamtazama Jemima kila siku na ninashukuru sana," alisema Byrne.
"Nina furaha kwamba ninaweza kutumia jukwaa langu kuwapa matumaini watu wanaojihisi kutengwa kwa kutokuwa na uwezo wa kupata ujauzito."
Alipoulizwa kama alikuwa na ushauri wowote kwa wengine wanaokabiliwa na ugumba, Byrne alisema anatamani angekuwa mwema kwake.
"Nadhani ni rahisi sana kujihukumu unapopata habari mbaya, unajipata ukifikiria hatua 10 mbele," alisema.
"Na bila kujua unaishia kufuta uwezekano wa kitu chochote kutokea kimiujiza, ni rahisi sana kujipata katika hali hiyo kwa sababu umepoteza matumaini.
"Hakuna anayejua kitakachotokea hatua katika safari ya kutafuta ujauzito, kwa hivyo jaribu tu kushughulikia kile kinachotokea wakati huo. Natamani ningezingatia hilo zaidi.
"Pia ni vyema kutuliza hisia wakati wa mchakato huo. Tenga muda wa kufurahia maisha kwani kuna mengi ya kufurahia na kumshukuru Mungu kwayo kama vile uhai.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












